Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ilisema kuwa serikali yake kwa kauli moja imekataa azimio lililotolewa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linalounga mkono kuifanya Palestina kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa.
Ofisi ya Netanyahu ilisema kuwa azimio hilo halitatumika kama msingi wa mazungumzo ya siku zijazo, halitabadilisha hali ya maeneo yanayozozaniwa, na halitatoa haki yoyote kwa Mamlaka ya Palestina (PA).
Waziri Mkuu wa Israel aliongeza kuwa serikali yake haitaruhusu “taifa la kigaidi” kuanzishwa.
Aliongeza kuwa Israel haitatoa zawadi yoyote kwa Palestina baada ya matukio ya tarehe 7 Oktoba mwaka jana.
Tarehe 10 Mei, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio linalolitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufikiria upya kuruhusu Palestina kuwa mwanachama kamili wa chombo hicho cha kimataifa. Palestina kwa sasa ni nchi isiyokuwa mwanachama.