JAMBOLEO
Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Matata Sheba mkazi wa Tungi Manispaa ya Morogoro amenyofolewa sehemu za siri na kuliwa na mambo wakati akioga mtoni.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Diwani wa kata ya Tungi, Deogratius Mzeru alisema Sheba alikwenda mtoni kuoga gafla alitokea mamba na kumg’ata.
Alisema wakati Sheba akijaribu kujiokoa kwa kupiga kelele za kuomba msaada alifanikiwa kutoka kwenye maji wakiwa wanavutana na mamba na kelele zilipozidi zilimshtua mamba na kumg’ata korodani na kurudi majini.
“Juzi jioni wakati Shebe anaoga mara alitokea mamba anayeishi katika mto huo na kutaka kummeza lakini katika purukushani alifanikiwa kutoka nje ya maji lakini alikuwa ameng’atwa sehemu zake za siri ” Mzeru.
Alisema baada ya taarifa hizo kumfikia aliamua kutafuta usafiri wa kumpeleka hospitali ambapo hali yake ilikuwa mbaya.
Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro Rita Lyamuya alisema hali ya mgonjwa imekuwa ikiimarika ingawa bado ana maumivu.
MWANANCHI
Serikali imetishia kuanza kutekeleza sheria inayodhibiti asasi za kijamii na kidini, ikizitaka taasisi hizo kuacha mara moja kutoa matamko yanayolenga kuwashawishi waumini wao waikatae Katiba Inayopendekezwa na pia kuwapangia nini cha kufanya katika Uchaguzi Mkuu ujao na kusema watakaobainika watachukuliwa hatua kali.
Katika kuzipiga ‘kufuri’ taasisi hizo, Serikali imesema kuanzia Aprili 20 itazifuta taasisi zote zilizosajiliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ambazo havifuati matakwa ya kisheria ya kuwasilisha taarifa zao za mwaka za ukaguzi wa hesabu na kulipa ada za kisheria.
Hata hivyo, viongozi wa dini ya Kikristo na Kiislamu waliozungumza na gazeti hili jana kuhusu kauli hiyo, wamesema taasisi zao zinawakilisha watu, na hivyo zina haki ya kikatiba na kisheria kupinga jambo lolote zitakaloona linakwenda kinyume na maslahi ya Taifa na kwamba ziko tayari kukaguliwa.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe alisema jana kuwa kazi hiyo ya kupitia usajili wa vyama hivyo itaanza kwa vyama vilivyopo jijini Dar es Salaam, baadaye kuendelea nchi nzima.
Vyama vyote vitakavyofutiwa usajili vitawekwa katika tovuti ya wizara hiyo na havitaruhusiwa kuendelea na shughuli zake.
“Matukio ya aina hii yanapofanyika yanaashiria kuvuruga amani na utulivu nchini. Kazi ya Serikali ni kuhakikisha usalama wa watu wote unaimarishwa ili shughuli zote za kisiasa, kidini, kijamii na kiuchumi, zinatekelezwa kwa misingi ya kisheria,” Chikawe.
Uamuzi huo umekuja wakati Jukwaa la Wakristo likiwa limetoa tamko la kuwataka waumini wake kujiandikisha kwa wingi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, kuisoma Katiba Inayopendekezwa na kujitokeza kuikataa kwa kupiga kura ya hapana.
Jukwaa hilo, linaloundwa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) na Umoja wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT), linadai kuwa Serikali imewaahidi Waislamu kuwapa Mahakama ya Kadhi ili waipigie Katiba Inayopendekezwa kura ya ndiyo. Jambo ambalo limesema litasababisha mgawanyiko.
Mbali na jukwaa hilo, pia Jumuiya na Taasisi za Kiislamu liliwataka waumini wake kuikataa Katiba Inayopendekezwa iwapo Serikali itashindwa kuwasilisha bungeni muswada wa Mahakama ya Kadhi ili chombo hicho kitambulike kisheria.
Muswada huo uliondolewa baada ya kuibuka kwa mvutano mkali katika mkutano wa 19 wa Bunge uliomalizika Aprili Mosi, mwaka huu.
Katika siku za hivi karibuni viongozi mbalimbali wa dini wamekuwa wakitaja wazi sifa na hata majina ya watu wanaopaswa kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu ujao, na wakati fulani vikundi vya wachungaji na masheikh kwa nyakati tofauti vilienda nyumbani kwa kada wa CCM, Edward Lowassa mjini Dodoma kumshawishi atangaze nia ya kugombea urais.
“Kauli za viongozi wa dini kuhusu masuala ya Katiba au Uchaguzi Mkuu ujao zinakiuka sheria za usajili wa taasisi zao. Viongozi ambao tayari wameshatoa matamko ya aina hiyo tunawapa onyo kwa sasa, wasirudie tena,” Chikawe.
Alisema waumini wana haki ya kuamini mafundisho ya dini zao, lakini wanapaswa kutekeleza masuala yao ya kisiasa na kijamii kwa utashi wao bila ya kushawishiwa na mtu yeyote, kama sheria za nchi zinavyotaka.
MWANANCHI
Huenda Watanzania wanaougua magonjwa ya moyo wakaepuka kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu baada ya tiba ya kuzibua mishipa ya moyo iliyoziba kufanyika kwa mara ya kwanza nchini.
Asilimia kubwa ya Watanzania wamepoteza maisha kutokana na magonjwa ya moyo yanayosababishwa na mtindo wa maisha ikiwamo mshtuko wa moyo na kuharibika kwa valvu za moyo.
Akizungumza wakati timu ya madaktari ikiendelea na tiba hiyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jana, Mkuu wa Idara ya Tiba na Upasuaji wa Moyo, Prof. Mohamed Janabi alisema hayo ni mapinduzi makubwa na yenye tija katika sekta ya afya.
“Tanzania imeandika historia ya pekee na huenda kasi ya kupeleka wagonjwa nje ya nchi ikapungua kwa kiasi kikubwa kwa sababu wale wote wenye matatizo haya watapatiwa tiba hapa hapa,” .
Idara ya Tiba na Upasuaji itashirikiana na wataalamu kutoka Marekani na India kuhakikisha wanafanya uchunguzi, kutoa tiba kwa wagonjwa wa moyo na kufundisha madaktari wa nchini.
Akielezea jinsi matibabu yanavyofanyika, Profesa Janabi ambaye pia ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya Moyo alisema, tiba hiyo inatumia kifaa maalumu kiitwacho ‘stent’ ambacho huingizwa hadi kwenye moyo na kuzibua mishipa ya damu iliyoziba.
Alieleza kuwa, mtambo maalumu uitwao ‘Cath Lab’ huingizwa mwilini mwa mgonjwa na kusaidia kuona iwapo kuna tatizo la moyo kabla ya kuweka kifaa hicho cha kuzibua mishipa ya kusambaza damu kwenye moyo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hussein Kidanto alisema, ujio wa tiba hiyo una manufaa makubwa kwani Watanzania.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo kutoka Kituo cha Afya cha Virginia, Marekani, Peter O’Brien alisema, fursa ya kuwafunda madaktari wa Kitanzania ni ya muhimu kwake kwani inampa ujuzi zaidi hata kujifunza jinsi nchi nyingine zinavyotoa tiba ya moyo.
MWANANCHI
Imebainika kuwa wakati Bunge la Kumi likiwa limebakiza mkutano mmoja tu wa bajeti kuhitimisha ngwe yake ya miaka mitano, wapo baadhi ya wabunge ambao hawajauliza swali la msingi, la nyongeza wala kuchangia chochote.
Kwa mujibu wa tovuti ya Bunge inayoonyesha idadi ya maswali yaliyoulizwa na michango ya kila mbunge, wapo wabunge wawili ambao hawajawahi kuuliza wala kuchangia chochote tangu Bunge hilo, lenye wabunge 358, lilipoanza Uchaguzi Mkuu uliopita hadi sasa.
Vilevile, tovuti hiyo inabainisha majina ya wabunge waliofanya vizuri zaidi katika kila eneo, yaani maswali ya msingi, ya nyongeza na michango waliyotoa katika mijadala mbalimbali.
Katika orodha hiyo, Spika Anne Makinda, ambaye pia ni mbunge wa Njombe Kusini, ndiye anayeonekana kinara kwa kuchangia mara 2,055 pale anapoongoza Bunge na kuuliza swali moja huku naibu wake, Job Ndugai akiwa amechangia mara 1,350 bila kuuliza swali hata moja.
Kiwango cha michango ya wabunge kimeelezwa na baadhi ya wasomi kuwa inategemea mambo mengi, ikiwamo mbunge kuwa sehemu ya Serikali na hivyo kushindwa kuihoji, uwezo wake kielimu na msimamo wake kiitikadi.
“Wabunge wengine tunaona ni wafanyabiashara ambao hawana elimu. Walishinda kwenye uchaguzi kutokana na fedha zao lakini hawana uelewa wa mambo..
Alisema orodha ya wabunge 10 waliochangia sana na wengine 10 waliochangia mara chache, haihusishi kiti cha spika, wenyeviti wa Bunge na mawaziri.
Wabunge 10 wenye michango michache
Nambari moja inashikwa na wabunge wawili ambao pia ni viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ambao ni mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, Mohamed Said Mohamed (CCM) ambaye ni mwakilishi wa Mpendae na Naibu Waziri wa Kilimo na Maliasili, pamoja na mbunge wa Kitope (CCM), Balozi Seif Ali Iddi ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Anayefuatia ni mbunge wa Babati Mjini, Kisyeri Chambiri (CCM) ambaye amechangia mara nne lakini hakuwahi kuuliza swali lolote.
Katika orodha hiyo wabunge waliochangia mara tano bila kuuliza maswali yoyote ni Dk Mohamed Seif Khatibu (Uzini – CCM), Edward Lowassa , Shawana Hassan (Dole – CCM). Mbunge wa Kalenga, Godfrey Mgimwa aliuliza maswali matatu ya nyongeza na kuchangia mara mbili.
Mwingine ni Ali Haji Juma wa (Chaani – CCM) aliyechangia mara nne, akauliza swali moja la msingi na moja la nyongeza.
MWANANCHI
Jumuiya ya Umoja wa Ulaya EU imeachia Serikali shilingi bilioni 107 kati ya trilioni 1 za bajeti zilizoshikiliwa kwa muda kutokana na sakata la ufisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Taarifa iliyotolewa jana na mkuu wa kitengo cha siasa na habari cha EU, Luena Reale alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya wahisani wa maendeleo kukubaliana kuziachia kabla ya mwaka wa fedha 2014/15 kuisha.
“EU imeridhishwa na hatua za Serikali ya Tanzania na taasisi nyingine zilizoshiriki katika kushughulikia suala la Escrow’ ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Mwaka jana baada ya sakata hilo kupamba moto, jumuiya ya wahisani wa maendeleo waliitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya waliohusika.
Mwenyekiti wa wahisani hao ambao ni ambao ni balozi wa Finland Sininka Antila alitangaza uamuzi huo wa kusitisha fedha hizo mwaka jana, akisema wataziachia pindi ripoti ya uchunguzi itakapotolewa na CAG na hatua kuchukuliwa.
NIPASHE
Wanafunzi sita wa shule ya msingi, wamefariki dunia kwa kupigwa na radi na wengine 15 wamejeruhiwa miongoni mwao vibaya kufuatia mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali na radi kunyesha katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji jana.
Tukio hilo lilitokea jana saa 5:00 asubuhi katika Shule ya Msingi Kibirizi iliyopo kwenye manispaa hiyo.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni, Dk. Fadhili Kibaya, alisema alipokea maiti za watu wanane zikiwamo za wanafunzi sita wa Shule ya Msingi Kibirizi na moja ya mwalimu wao jana saa 6:00 mchana.
Alisema maiti nyingine ni ya mwanaume mkazi wa Bangwe katika manispaa hiyo. Alisema mbali ya maiti, pia alipokea majeruhi 15.
Aidha, alisema wengine watano wako kwenye chumba cha uangalizi maalum (ICU) na wengine walitibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani kwao.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Shule ya Msingi Kibirizi, Emmanuel Wilbert, alisema mwalimu aliyefariki dunia alitoka darasa la tatu na kuingia ofisi ya walimu na kukaa akiendelea na shughuli zake kama kawaida.
Wilbert alisema baada ya muda mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali na radi huku walimu wengine wakiwa madarasani wakiendelea na vipindi, ilipiga radi iliyosababisha kifo cha mwalimu na wanafunzi hao waliokuwa madarasani.
Alisema baada ya tukio hilo, wanafunzi na walimu walikimbia ovyo na mwalimu mwingine Merina Serilo, alipigwa na radi na kujeruhiwa.
NIPASHE
Asasi zisizo za kiserikali 53 zimemwandikia Rais Jakaya Kikwete, barua ya kumuomba asisaini Sheria ya Takwimu ya 2015 na Sheria ya Makosa ya Mtandaoni zilizopitishwa na Bunge hivi karibuni ili kuruhusu kufanyiwa marekebisho kwanza.
Kwa majibu wa barua hiyo iliyosainiwa na asasi 53 na mtandao wa asasi za kiraia ambayo zinataka sheria hizo zirudishwe bungeni kuondoa vifungu vinavyokwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 na haki za binadamu kwa ujumla.
“Tunashauri kabla ya kutia saini sheria hizi upate muda wa kusikiliza kilio cha jamii juu ya ubaya wa sheria hizi kwa mustakabali wa taifa.
Sheria hizi zikipitishwa katika utawala wako zitatia doa dhamira yako nzuri ya kuongeza wigo na uhuru wa habari na ushiriki wa wadau katika maendeleo ya kitaifa,” alisema.
Barua hiyo imeeleza sababu za kumtaka Rais kutosaini sheria hizo kuwa ni, malengo ya Sheria ya Takwimu siyo tu kuratibu takwimu za kitaifa, bali umetoa madaraka makubwa kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kama kitovu cha utoaji wa takwimu nchini.
“Maana yake ni kwamba taasisi zote za serikali, mashirika binafsi, taasisi za elimu ya juu, vyuo vikuu na taasisi za utafiti hazitakuwa na uhuru wa kutoa matokeo ya tafiti wanazozifanya bila ya kibali au ridhaa ya NBS” ilisema barua hiyo.
NIPASHE
Wanafunzi wa vitivo vya Sayansi ya Afya wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Kampala-tawi la Dar es Salaam (KIU), wamegoma kuendelea na masomo baada ya kubaini kuwa kozi wanazosoma katika chuo hicho hazijasajiliwa katika bodi mbalimbali kama taratibu na sheria zinazoelekeza.
Walianza mgomo huo tangu Ijumaa iliyopita baada ya kugundua kuwa kozi wanazofundishwa hazijasajiliwa katika Bodi ya Mafamasia, Bodi ya Maabara na Baraza na Madaktari.
Walisema jana chuoni hapo kuwa wamekuwa wakiendelea na masomo bila kugundua kama kozi wanazochukua hazijasajiliwa katika bodi hiyo huku uongozi wa chuo ukikaa kimya.
Waziri wa Afya wa Serikali ya Wanafunzi (KIUSO), Kenedy Murunya, alisema walibaini kuwa kozi wanazosoma hazijasajiliwa baada ya kwenda katika ofisi za bodi na kuelezwa kuwa hazijasajiliwa.
Wanafunzi waliokumbwa na tatizo hilo ni wale wanaochukua Shahada za maabara, udaktari na upasuaji.
“Wanafunzi walipokwenda Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) waliambiwa kuwa tume imeshafanya asilimia 50 ya usajili wa chuo hicho na asilimia 50 nyingine zilizobaki zinatakiwa zishughulikiwe na bodi husika za usajili,” alisema.
Alisema Septemba, 2014 walikwenda Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa lengo la kumuona Waziri, Dk. Shukuru Kawambwa, lakini hawakumuona hivyo kumwandikia barua ili awape majibu ambayo hadi sasa hawajapatiwa.
Alisema wanaendelea kulipa ada kubwa japokuwa serikali ilikiagiza chuo hicho kushusha ada cha kushangaza Baraza la KIU ambalo lipo Uganda lilikataa maagizo ya serikali.
Alisema wanafunzi wa udaktari mwaka wa pili wanalipa Sh. milioni 8 wakati wa mwaka kwanza wanatozwa Sh. milioni 6.7, maabara sh. milioni 4.8, Famasia milioni 5.4 huku wa mwaka wakilipa sh. milioni 3.8.
MTANZANIA
Jeshi la Polisi nchini, limesema Watanzania 866 wamefariki dunia katika kipindi cha miezi mitatu, kutokana na ajali za barabarani.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga alisema kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, ajali 2,116 zimetokea katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema katika ajali hizo, watu 866 wamepoteza maisha na wengine 2,363 kujeruhiwa, ambao baadhi yao wamepata ulemavu.
Hata hivyo nje na kipindi hicho, ajali nyingine zilizotokea kuanzia Machi 11 hadi April 12, mwaka huu zimesababisha vifo vya watu wengine 103 na hivyo kufanya idadi ya watu walipoteza maisha katika kipindi cha miezi mine kuwa 969.
Akizungumzia sababu za ajali hizo, Kamanda Mpinga alisema ni mwendo kasi usiozingatia alama za barabarani na kufutika kwa baadhi ya michoro barabarani.
Alisema sababu nyingine, ni baadhi ya wamiliki wa vyombo vya moto kuhamasisha mwendo kasi kwa madereva wao, abiria kushabikia na baadhi ya wadau wa usalama barabarani kutowajibika ipasavyo.
Kamanda Mpinga, alisema uzembe wa madereva, ubovu wa barabara na uoni hafifu kwa baadhi ya madereva ni miongoni mwa sababu zinazochangia ajali nyingi kutokea..
Kuhusu hatua, Kamanda Mpinga, alisema madereva wote waliosababisha ajali za hivi karibuni watachukuliwa hatua, ikiwa ni pamoja na kunyang’anywa leseni zao.
MTANZANIA
Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), linatarajia kuitisha mgomo wa wafanyakazi nchi nzima, endapo Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) haitaondoa kanuni mpya ambayo inaruhusu watumishi watakaostaafu kwa hiari yao kukatwa asilimia 18 ya mafao yao.
Kanuni hiyo mpya itaanza kutumika Julai mwaka huu ambapo watumishi watakaostaafu kwa hiari watalazimika kukatwa kiasi hicho.
Ili kuhakikisha suala hilo linashughulikiwa ndani ya muda mwafaka, TUCTA imeazimia kuitisha mkutano mkuu unaotarajiwa kufanyika Aprili 23 na 24, mwaka huu ili kujadili suala hilo.
Rais wa shirikisho hilo, Gratian Mukoba alisema kanuni hiyo ni kandamizi na inawanyima haki watumishi kwa sababu kulipwa mafao ni haki ya mtumishi aliyestaafu, ingawa pia wakati wanajadili kuipitisha hawakushirikishwa.
“Tutawahamasisha watumishi kugoma nchi nzima ili kuishinikiza SSRA kubadili kanuni hii kwa sababu ni kandamizi kwa mtumishi.
“Bila ya kufanya hivi, Serikali itaendelea kutunga kanuni nyingine ambazo zinaweza kutoa nafasi kwa watumishi kuendelea kufanya kazi hadi miaka 70 ili wakifariki kabla ya muda huo wawe wamepoteza mafao yao, kutokana na hali hii, hatutakubali na tunataka iondolewe mara moja,” Mukoba.
Alisema kutokana na hali hiyo, shirikisho hilo linasubiri majibu ya barua hiyo na endapo hawasikilizwa watafanya mgomo huo.
MTANZANIA
Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, Januari Makamba ametajwa kuwa mwanasiasa bora kijana na taasisi ya Tanzania Awards International, jijini Dar es Salaam juzi.
Makamba ameshika nafasi hiyo akiwapita wanasiasa wengine vijana ambao ni pamoja na Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, Naibu Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba, Wabunge Vick Kamata, Esther Bulaya, David Kafulila na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Mboni Mhita.
Katika tuzo za mwanasiasa mtu mzima ushindi umechukuliwa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na katika kundi hilo, Profesa Muhongo alishindanishwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, Waziri Sheria na Katiba, Dk. Asha Rose Migiro na Waziri wa Nchi Katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano, Samia Suluhu.
Wengine ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Liberata Mulamula.
Tuzo ya jamii ilichukuliwa na Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi.
Waliopewa tuzo za heshima katika jamii ni Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere na Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela.
Si Makamba, Profesa Muhongo wala Mengi waliohudhuria shughuli hiyo badala yake waliwakilishwa na ndugu zao.
Akitoa ufafanuzi wa tuzo hizo, Mratibu wa Taasisi hiyo, Amani Mwaipaja alisema zilikuwa katika vipengele vitano ambavyo ni tuzo ya jamii 2015, tuzo za jamii ya heshima, tuzo jamii katika haki za binadamu, tuzo ya mwanasiasa kijana na tuzo ya mwanasiasa mzee.
“Tumeangalia vigezo kadhaa ikiwa pamoja na uadilidu, uaminifu, utii katika sheria, kuwa na maono, mikakati na mipango,” Mwaipaja.
millardayo.com ndio sehemu yako kuzipata story zote mtu wangu, unaweza kuwa karibu zaidi na mimi kwa kujiunga kwenye Facebook, Twitter na Instagram pia zitakufikia zote mtu wangu, jiunge hapa >>>twitter Insta Facebook