NIPASHE
Mkazi wa Ilala Sharifu Shamba, jijini Dar es Salaam, anatuhumiwa kumuua rafiki yake kisha kumfukia kwenye shimo alilochimba na kulisakafia uani kwenye nyumba aliyokuwa akiishi mtuhumiwa.
Mauaji hayo yanadaiwa kufanywa Julai, mwaka jana, baada ya mtuhumiwa kudaiwa kushindwa kumlipa rafiki yake huyo Sh. milioni 35.
Inadaiwa kuwa marehemu alimpa mtuhumiwa huyo fedha hizo ili akamnunulie gari na kwamba, baada ya kudaiwa muda mrefu, ndipo alipoamua kufanya ukatili huo.
Habari zinaeleza kuwa kabla ya kufanya mauaji hayo, mtuhumiwa alimpigia simu rafiki yake huyo na kumtaka aende bandarini kuchukua gari hilo kwa madai kwamba, lilikuwa limewasili.
Kwa mujibu wa habari hizo, wakati huo mtuhumiwa alikuwa bandarini akimsubiri rafiki yake huyo. Inadaiwa rafiki yake huyo alikwenda hadi bandarini na kuonana na mtuhumiwa huyo.
Hali hiyo ilimfanya rafiki yake huyo kulazimika kuondoka baada ya kushindwa kuhimili mzunguko waliokuwa wakifanyiwa na mtuhumiwa. Baada ya kushindwa kupata gari alilolitarajia, mtuhumiwa aliamua kurudi na rafiki yake huyo nyumbani kwake (mtuhumiwa), Ilala ambako alitekeleza mauaji hayo na kumzika.
NIPASHE
Serikali ya Tanzania imesema itachukua hatua ya kuwafahamisha watalii na wageni wanaokuja kutembelea vivutio vya kitalii kutumia viwanja vya ndege vilivyopo nchini ili kuepuka kadhia na gharama zisizo za lazima.
Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia Kenya kuendelea kuzuia magari ya kitalii yaliyosajiliwa Tanzania kuingia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta kwa ajili ya kuchukua na kushusha watalii.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema jana kuwa serikali imesikitishwa na uamuzi uliochukuliwa na Kenya kwani uamuzi wake hauendani na dhamira njema ya mkataba wa kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Tanzania haitazuia magari ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki au nyingine yoyote kuingia katika viwanja vyake vya ndege kuleta au kuchukua watalii wanaopitia katika viwanja hivyo na kwenda katika nchi hizo:-Mwakyembe.
Alisema Tanzania itaheshimu na kuzingatia mkataba huo ili kulinda undugu na urafiki uliopo kati ya nchi hizo wakati ikiendelea kutafakari hatua za kuchukua ili kuondoa bughudha kubwa itakayotokea kwa watalii na wasafiri wanaopitia uwanja wa Jomo Kenyatta.
NIPASHE
Wakala wa Vipimo, Mkoa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, imefungia vituo vya kuuza mafuta rejereja viwili kati ya sita baada ya kubainika kutoa huduma kwa njia ya udanganyifu kwa kuwaibia wateja wa huduma hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi, wa Wakala mkoani humo, Stella Kahwa alisema zoezi hilo limeanza jana na kwamba vituo viwili kati ya sita vimefungwa baada ya kubainika vinatoa huduma kwa udanganyifu.
“Matunda ya ziara ya ukaguzi wa mashine katika vituo vya mafuta tumefanikiwa kubaini vituo viwili (majina tunayahifadhi) tumevifungia kwa sababu wanawaibia na kuwapunja wateja … zoezi hilo litaendelea nchi nzima” alisema na kuongeza:
“Kwa wale tuliowakuta na makosa hayo watalipa faini kwa mujibu wa sheria zetu na ikilazima kuburuzwa mahakamani wataburuzwa… hakuna aliye juu ya sheria.”
Alisema kwa kuwa wana mamlaka ya kutoza faini kwa sasa wako macho kuhakikisha vituo vyote nchini vinakidhi vigezo katika utoaji huduma kwa jamii.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Wauza Mafuta rejareja (Tapso) Tino Mmasi, alisema amesikitishwa na tukio la wafanyabiashara hao kupunja mafuta wananchi.
MWANANCHI
Mtafiti mwandamizi wa taasisi ya maendeleo ya kimataifa ‘SID’ Edmund Matotay, amesema kuimarika kwa uchumi wa nchi hakujasaidia kuondoa hali ya umaskini wa wananchi.
Amesema licha ya mageuzi makubwa ya makusanyo ya pato la Taifa na kuongezeka kwa uzalishaji katika sekta mbalimbali bado wananchi wengi wanaishi katika hali ya umaskini mkubwa.
“Bado Tanzania inategemea misaada kutoka nje kwa asilimia 41 kutokana nakutokuwepo usimamizi mzuri wa kukusanya kodi:- Matotay.
Alisema kwa kawaida ukuwaji wa uchumi wa nchi yoyote lazima uendane na mabadiliko ya maisha ya wananchi lakini kinachoshuhudiwa nchini ni tofauti
MWANANCHI
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameuvunja uongozi wa chama hicho kwenye majimbo ya Ukonga na Ilala kutokana na kutoelewana kwa muda mrefu baina ya viongozi na kutofanya vizuri kwa chama hicho kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14 mwaka jana.
Habari zilizothibitishwa na Mbowe zinaeleza kuwa mwenyekiti huyo aliuvunja uongozi huo wiki mbili zilizopita baada ya kikao cha siri na viongozi wa majimbo hayo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Klabu ya Billicanas iliyopo katikati ya jiji.
Pamoja na CCM kuibuka na ushindi mkubwa kwenye uchaguzi huo wa ngazi ya mwanzo ya uongozi, Chadema iliongoza kwa upande wa upinzani ingawa haikuwa na matokeo mazuri kwenye majimbo hayo mawili.
Katika uchaguzi huo, CCM ilishinda kwa asilimia 79.4 katika nafasi ya uenyekiti wa mitaa, Chadema asilimia 15.1 na CUF asilimia 4.6. Vyama vingine kwa ujumla vilipata asilimia 0.9.
MWANANCHI
Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) imembadilishia hati ya mashtaka Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma aliyekuwa akikabiliwa na shtaka la kupokea rushwa ya Sh 323 milioni toka kwa James Rugemalira fedha ambazo ni sehemu ya fedha za Akaunti ya Tegeta Esrow.
Katika hati mpya iliyosomwa na Mwendesha Mashtaka wa Takukuru Leonard Swai mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Emillius Mchauru aioneshi tena kuwa fedha zilizopokelewa na Mujunangoma toka kwa Rugemalira ni sehemu ya fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow.
Swai kupitia hati hiyo mpya alidai kuwa Februari 5, 2014 Mujunangoma akiwa mtumishi wa serikali kama Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma alipokea rushwa ya Sh Sh323 milioni kupitia akaunti yake namba 00120102602001 iliyopo kwenye benki ya Mkombozi .
Alidai kuwa mshtakiwa huyo alipokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa James Burchard Rugemalira, ambaye ni mshauri huru wa kitaalamu, mkurugenzi wa VIP na mkurugenzi wa zamani wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL kama tuzo kwa kushughulikia mambo ya ufilisi wa muda wa kampuni hiyo.
MTANZANIA
MCHAKATO wa kupata Katiba Mpya ya nchi unadaiwa kugubikwa na wingu la ufisadi hali iliyosababisha Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kuhoji tenda ya uchapwaji wa nakala milioni mbili za Katiba Inayopendekezwa kwa gharama ya Sh bilioni 6.
Hatua hiyo inakuja huku Watanzania wakiwa wanasubiri kupiga kura ya maoni inayotarajiwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu, ambapo inaelezwa taratibu za manunuzi zilikiukwa kwa baadhi ya kampuni zilizopewa kazi hiyo kuwa na walakini.
Kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011, taasisi zote za umma zinatakiwa zitangaze zabuni kabla ya kutoa zabuni husika.
Kutokana na sheria hiyo, inaelekeza taarifa za zabuni husika hutangazwa kupitia jarida na tovuti ya PPRA jambo ambalo linadaiwa halikufanywa na Wizara ya Katiba na Sheria.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, kila nakala ya Katiba Inayopendezwa inachapishwa kwa gharama ya Sh 3,000.
“Kwenye hizo kampuni zilizopewa hiyo kazi, nyingine hata uwepo wake una walakini, hii haikuwa kazi ya dharura kiasi hicho, lakini pia kutoa zabuni ya Sh bilioni 6 za umma kwa kujuana tu bila kufuata taratibu ni jambo la kushangaza,” kilipasha chanzo chetu.
HABARILEO
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru) imesema imejipanga kikamilifu kuhakikisha inashughulikia vitendo vya utoaji na upokeaji rushwa katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Akizungumza jana wakati wa ufunguzi wa jengo la taasisi hiyo mkoani Kigoma lililogharimu Sh bilioni 1.2, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hosea alisema anasubiri kuanza kwa ratiba ya Tume ya Uchaguzi ili iweze kuanza kutekeleza jambo hilo kwa kufuata sheria za uchaguzi.
Alisema taasisi yake imeshaanza kuona viashiria vya utoaji rushwa vinavyofanywa na baadhi ya watu walioonesha nia ya kugombea katika uchaguzi mkuu ujao kwa kutoa vitu mbalimbali zikiwemo fulana, chupa za chai na vitu vinavyofanana na hivyo.
Hata hivyo, alisema kwa sasa haitaweza kuwakamata wala kuwahoji watu hao kwa kuwa si wagombea rasmi kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi, lakini alibainisha kuwa vijana wake wanafuatilia kwa karibu nyendo zinazofanywa na watu hao.
Sambamba na kujipanga, Hosea alitoa wito kwa wananchi kuchukia vitendo vya kupokea rushwa wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu kwani vinawapotezea haki ya kuchagua mgombea mwenye sifa badala yake hushawishiwa kuchagua kwa rushwa.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram, na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook