MWANANCHI
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeishinda CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika juzi katika kata tatu za Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa ambazo hazikufanya uchaguzi Desemba 14, mwaka jana.
Uchaguzi katika kata hizo uliahirishwa kutokana na kasoro mbalimbali jambo lililosababisha mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, William Shimwela kusimamishwa kazi.
Msimamizi wa uchaguzi huo uliofanyika katika kata za Msua, Chanji na Kizwite na mitaa mingine miwili iliyorudia uchaguzi, Hamid Njovu alisema Chadema ilinyakua jumla ya mitaa 37 kati ya 44 na kuiacha CCM ikiambulia mitaa mitano.
Matokeo hayo mapya yanaibuka sasa wakati Ofisi ya Waziri Mkuu ilishahitimisha kutangaza matokeo ya jumla ya mitaa katika uchaguzi huo ikisema ulikuwa umekamilika kwa asilimia 100.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tamisemi, Kalist Luanda alisema Desemba 24, mwaka jana kuwa mitaa yote 3,875 nchini ilifanya uchaguzi na kukamilika kwa asilimia 100 huku CCM ikipata asilimia 66.66 baada ya kuzoa mitaa 2,583, ikifuatiwa na Chadema iliyopata mitaa 980 (25.3%), CUF mitaa 266 ( 6.9%), NCCR Mageuzi mitaa 28 (0.7%), TLP mtaa mmoja (0.03%), ACT mitaa 12 (0.31%), UDP mitaa mitatu (0.08%), NRA mtaa mmoja (0.03%) na UMD mtaa mmoja (0.03%).
Akitangaza matokeo hayo jana, Njovu alisema katika Kata ya Kizwite kati ya mitaa 15 iliyofanya uchaguzi Chadema ilishinda mitaa 13 dhidi ya CCM iliyoambulia mitaa miwili, Kata ya Msua mitaa yote 13 iliyofanya uchaguzi ilikwenda kwa Chadema na CCM kuambulia patupu.
Alisema kwa Kata ya Chanji ambayo ilikuwa na mitaa 14 iliyofanya uchaguzi, Chadema ilishinda mitaa 10 na CCM mitatu huku mtaa mmoja wa Nankasi kura ziligongana katika nafasi ya uenyekiti, hivyo kuamuliwa uchaguzi utarudiwa Jumapili.
MWANANCHI
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Benno Ndulu amesema hivi sasa sekta ya Utalii ndiyo inayoongoza kwa kuliingizia taifa mapato ya kigeni baada ya kuipita sekta ya dhahabu iliyoshuka kutokana na kuporomoka kwa bei kwenye soko la dunia.
Akizungumza leo kwenye mkutano uliojadili mabadiliko ya kiuchumi Tanzania, Profesa Ndulu amesema sekta ya utalii inaliingizia taifa dola 2bilioni, dhahabu (dola 1.7bilioni), bidhaa za viwandani (dola 1.3bilioni) na huduma za usafirishaji mizigo ni dola 800milioni.
Sekta ya utalii inaingiza Dola za Marekani 2 bilioni kwa mwaka ikifuatiwa na dhahabu inayoipatia nchi Dola za Marekani 1.7 bilioni, bidhaa za viwanda vinazouzwa katika nchi mbalimbali barani Afrika inaingiza Dola za Marekani 1.3bilioni ikifuatiwa na usafirishaji wa huduma za mizigo katika nchi jirani ambapo zinaingiza Dola za Marekani 800milioni.
Profesa Ndulu amesema ongezeko la mapato kwenye viwanda ni sawa na fedha zote za kigeni zinazotokana na mazao sita makubwa ya kilimo nchini kwa pamoja.
“Mfumo wa kuingiza mapato ya fedha za kigeni nchini umebadilika sana, mimi na imani kuwa nafasi yetu kijiografia inatupa fursa kubwa sana ya kuhudumia wengine walioko mbali na bahari,”:- Prof.Ndulu.
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete amemkabidhi Kiongozi wa Madhehebu ya Isimailia ulimwenguni, Mtukufu Aga Khan hati ya usajili wa Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) ikiwa ni hatua muhimu kwa taasisi hiyo kuendeleza utoaji wa elimu nchini.
Mara baada ya kukabidhi hati hiyo, Rais Kikwete alisema ni mara ya kwanza kwa Chuo Kikuu cha kigeni kusajiliwa nchini na kwamba Aku itatimiza matarajio ya wengi katika utoaji wa elimu bora.
Alisema Serikali imekuwa na uhusiano wa karibu na Mfuko wa Maendeleo wa Aga Khan na umekuwa ukisaidia masuala mbalimbali yanayochochea maendeleo nchini.
“Utoaji wa hati hii leo ni sehemu tu ya hatua ya maendeleo hayo. Tunayo imani kuwa Chuo Kikuu hiki kitasaidia kupunguza tatizo la upungufu wa rasilimali watu katika fani za udaktari, sayansi na teknolojia,” alisema Rais Kikwete katika hafla iliyofanyika Ikulu.
Mtukufu Aga Khan alisema upatikanaji wa hati hiyo ni mwanzo wa safari ya utoaji wa huduma za elimu nchini ikiwa ni utekelezaji wa uamuzi wa kukipanua chuo hicho kutoka nje ya Asia na kuimarisha mizizi barani Afrika ili kupunguza umaskini.
Kiongozi huyo, ambaye pia ni mwanzilishi na Mwenyekiti wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), alisema katika kipindi cha maendeleo ya kasi, suala la elimu ni la msingi ili kukuza ugunduzi na uzalishaji.
“Chuo kitakuwa na kozi tisa tofauti maalumu kwa ajili ya masuala ya Afrika ambazo zitakuwa na umuhimu mkubwa na matokeo ya haraka kwa jumuiya ya Tanzania.
NIPASHE
Wanafunzi sita, mwalimu wao, wamekufa papo hapo na wengine 11 kujeruhiwa kwa kupigwa na radi darasani wakati mvua kubwa zilizoambatana na kimbunga zikinyesha.
Tukio hilo lilitokea saa 2:30 asubuhi katika Shule ya Msingi Nyakasanda iliyopo kijiji cha Nyaphenda wilaya ya Kasuru mkoani Kigoma wakati mwalimu huyo na wanafunzi hao wakiwa darasani.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, John Ndunguru, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita wakati mvua hizo zikinyesha.
Alisema mazishi ya mwalimu huyo na wanafunzi hao, yatafanyika leo mchana katika kijiji hicho chini ya usimamizi wa kamati ya ulinzi ya mkoa huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Jafari Mohamed, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo. Hata hivyo Mohamed, alisema majina ya waliokufa yatafahamika leo wakati wa mazishi yao.
Vilevile alisema wanafunzi wengine 10 na mwalimu wao waliojeruhiwa katika tukio hilo, wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa huo ya Maweni kwa matibabu.
NIPASHE
Zoezi la uandikishaji wapigakura katika Daftari la Kudumu la Wapigakura limeanza katika Mkoa wa Njombe, huku likikabiliwa na changamoto nyingi, ikiwamo mashine za Biometric Voter Registration (BVR) kushindwa kutambua watu wenye vidole vyenye michilizi.
Kujitokeza kwa kasoro hizo kumekuja siku tatu tangu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, alipoeleza kuwa amenasa nyaraka zinazoonyesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), ilishauriwa na mtaalam kutoka Marekani kwamba Tanzania haijawa tayari kwa teknolojia ya BVR.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema zoezi la uandikishaji limeanza katika mkoa wa Njombe na kwamba viongozi wa tume hiyo wapo kwa ajili ya kusimamia kuhakikisha kunakuwa na mafanikio.
Jaji Lubuva alipoulizwa kama tume imeanza na BVR ngapi, alisema suala hilo hawezi kulijibu. Hivi karibuni kuriripotiwa kuwa Nec imepata BVR 250 tu kati ya 8,000 zinazotakiwa.
“Nipo Njombe ndiyo tumeanza zoezi la kuandikisha, suala la kwamba tumeanza na BVR ngapi sina jibu, kwanza nipo kwenye kikao,”alisema Lubuva na kukata simu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Nec, Julius Malaba, alisema uzinduzi rasmi wa uandikishaji katika mkoa wa Njombe utafanyika leo.
Kasoro nyingine zilizojitokeza ni uchache wa vifaa,watoa huduma waliopewa jukumu hilo kushindwa kutumia mashine na kulazimika kutumia muda mwingi kumwandikisha mtu mmoja hali inayotia wasiwasi kwamba huenda siku saba zilizopagwa kufanyika kwa kila mkoa kushindwa kufikia malengo.
NIPASHE
Mbivu au mbichi za vigogo 99 wa Tanzania waliotajwa kuficha mabilioni ya fedha kwenye akaunti za siri nchini Uswiss zitajulikana hivi karibuni, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, amesema.
Kwa mujibu wa Zitto, PAC imewaita Gavana wa Benki Kuu (BoT), Prof. Benno Ndulu; Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dk. Rished Bade, ili kuhojiwa na kamati yake Machi 9, mwaka huu.
Zitto alisema majina ya watu au kampuni zinazohusika na mabilioni hayo vitajulikana kwa kuwa serikali imeshachunguza na ripoti iko tayari.
“Tumewaita BoT, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamishna Mkuu wa TRA Machi 9 waje kwenye kamati kujieleza…tunategemea serikali ina taarifa zote kwa sababu sehemu kubwa ya fedha zinazotoroshwa nje ni kwa nia ya kukwepa kodi. Kwa hiyo, TRA watakuwa wanawajua,”:-Zitto.
Aliongeza: “Siwezi kumtaja mtu yeyote kwa sasa. Lakini bila shaka wahusika wakuu watakuwa wafanyabiashara wakubwa.”
Kwa upande wake, Prof. Ndulu alisema ameitwa na PAC, lakini hawezi kuueleza umma taarifa zozote kwa sasa kwa kuwa atajieleza kwenye kamati.
“Subirini, mimi nimeshaitwa kwenye kamati. Nitajieleza huko…unataka niseme nini sasa hivi wakati nitahojiwa huko?” Alihoji Prof. Ndulu.
Tuhuma za vigogo wa Tanzania kuficha mabilioni ya shilingi katika benki za Uswisi ziliibuliwa upya hivi karibuni baada ya ripoti ya mtandao wa Swiss Leaks chini ya Waandishi wa Habari za Uchunguzi wa Kimataifa (ICIJ), kutaja vigogo 99 wenye akaunti za siri nchini humo.
HABARILEO
VIONGOZI wa madhehebu ya dini jijini Mwanza, wakiwamo Maaskofu na Mashehe jana walijikuta wakibubujikwa na machozi baada ya kumtembelea Ester John, ambaye amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Ester amelazwa baada ya kujeruhiwa vibaya na watu wasiofahamika, ambao walimteka mwanawe mwenye ulemavu wa ngozi (albino), Yohana Bahati na kutokomea naye kusikojulikana.
Viongozi hao wakiwemo maaskofu 10 na mashehe 10 walimtembelea Ester hospitalini hapo jana, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kongamano kubwa la amani linalotarajiwa kufanyika Februari 28 mwaka huu kuiombea nchi amani na kulaani mauaji ya albino.
Mashehe na maaskofu hao walimuombea dua na sala Ester aweze kupona haraka na walilaani kitendo cha kinyama, alichofanyiwa na wauaji hao. Waliiomba Serikali ichukue hatua za haraka kukomesha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini.
Akizungumza hospitalini hapo huku akitokwa na machozi katika Wadi Namba 9 alikolazwa Ester, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Mkoa ya Viongozi wa Dini, Shekhe Hassan Kabeke alisema wanaungana kwa pamoja kulaani matukio mawili ya kinyama ya kuuawa kwa mtoto Yohana na kujeruhiwa vibaya mama yake mzazi.
“Maneno ya kusema yananiishia baada ya kumuona Ester, mimi nadhani hakuna sababu ya kuremba maneno dhidi ya ukatili huu wa kinyama, nasikia maumivu makali sana ndani ya moyo wangu kama kiongozi wa kiroho, tunaitaka serikali katika hili isiondoe adhafu ya kifo kwa kisingizio cha haki za binadamu”, alisema.
HABARILEO
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia vijana watano wa kundi la wahitimu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa tuhuma za kufanya uchochezi na kufanya mikusanyiko isiyo halali jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema vijana hao wamekamatwa kwa nyakati tofauti kwa makosa ya kuunda kikundi kisicho halali kwa mujibu wa sheria za nchi na kuwahamasisha wenzao, kuandamana hadi Ikulu kwa Rais Jakaya Kikwete kudai ajira za kudumu.
“Tunawashikilia vijana watano ambao ndio viongozi wa kikundi kinachojiita umoja wa wahitimu wa Jeshi la Kujenga Taifa. Mwenyekiti ndio alikuwa wa kwanza kukamatwa na wengine tuliwakamata juzi mara baada ya kukusanyika eneo la Msimbazi Centre na Muhimbili,”:-Kova.
Akieleza chanzo cha vijana hao kutaka kuandamana kuelekea Ikulu, alidai wahitimu hao wanadai kuahidiwa ajira za kudumu walipomaliza mafunzo yao na hivyo baada ya kukaa kwa muda mrefu bila kuajiriwa, ndipo wakaamua kuanzisha kikundi hicho ili kwenda kumwona Rais Kikwete kumweleza tatizo la ajira linalowakabili.
“Vijana hawa wanadai kuwa waliahidiwa kupewa ajira za kudumu mara baada ya kumaliza mafunzo yao ya JKT. Jambo hili sio la kweli, kwani tumefanya uchunguzi na kubaini hakuna mkataba wowote unaosema wakimaliza mafunzo lazima waajiriwe, bali kila mtu anatakiwa kutumia ujuzi alioupata kujiajiri.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram, na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook