MTANZANIA
Kesi 18 za dawa za kulevya zilizokuwa zikisikilizwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam zinafutwa kwa sababu zilisajiliwa kimakosa katika katika mahakama hiyo na washtakiwa wanapandishwa upya kizimbani.
Hayo yalibainika jana baada ya kesi nne kufutwa na kufanya idadi ya kesi hizo kufikia nane baada ya nne nyingine kufutwa juzi, ambapo washtakiwa walisomewa upya mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Kesi zote zinazofutwa matukio yalitokea kati ya mwaka 2010 na 2011, ambapo upelelezi ulishakamilika na zilipelekwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kuendelea kusikiliza ushahidi.
Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Godfrey Nzowa, alipoulizwa kuhusu kufutwa mfululizo kwa kesi hizo, alisema kesi hizo zinazofutwa zipo katika orodha ya kesi zilizopo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wiki hii kwa ajili ya kusikilizwa.
“Kwa wiki hii tutafuta kesi 18 ambazo zilianza kufutwa nne juzi, na jana nne, ambapo tatu zimefikishwa Kisutu na moja imepelekwa mkoani Pwani.
“Kesi zinazofutwa zimebainika kusajiliwa Mahakama Kuu katika kitabu cha kesi za uhujumu uchumi, ni makosa, zinarudi upya mahakamani ili washtakiwa waweze kusomewa mashtaka, na kwa kuwa upelelezi ulikamilika, watasomewa maelezo ya awali na kurudishwa tena mahakamani,” alisema.
Kamishna Nzowa alisema leo wanatarajia kufuta kesi nyingine nne, kesho zitafutwa tatu na keshokutwa pia zitafutwa kesi tatu.
Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga, alisema kesi za dawa za kulevya zilizosajiliwa kimakosa na Mahakama Kuu katika kitabu cha kesi za uhujumu uchumi zitaendelea kufutwa.
“Zipo kesi nyingi na zitaendelea kufutwa kutokana na Mahakama Kuu kufanya makosa kuzisajili katika kitabu cha kesi za uhujumu uchumi,” Maganga.
NIPASHE
Watendaji wa kata ya Mkolani Mwanza wameagizwa kufanya haraka kuwahesabu watu wenye ulemavu wa ngozi ndani ya kata hiyo ili kubaini idadi yao.
Diwani wa kata hiyo Stansalaus Mabula alisema zoezi hiyo linatakiwa kuanza haraka ili kutengeneza ulinzi shirikishi kwa jamii kuwalinda albino waliopo ndani ya kata yake.
“Ili kuwalinda watu hawa wenye ulemavu wa ngozi, lazima jamii ichukue hatua ya kukomesha mauaji yanayowalenga na kila mmoja awe mlinzi wa mwingine ili kukomesha tabia hii“- Mabula.
Mabula alisema ulinzi huo unatakiwa kuanzia majumbani ili kurahisisha kuwabaini wenye nia ya kuwadhuru watu hao ambao hawana hatia.
NIPASHE
Rais Jakaya Kikwete amesema serikali itaendelea kuboresha mazingira ya walimu nchini, lakini inatofautiana nao katika suala la kuongeza mishahara kutokana na wao kutaka kuongezwa kwa kiwango cha asilimia 100.
Amesema hayo jana katika hafla ya kukabidhiwa vitabu milioni 2.5 vya sayansi, fizikia na hisabati na Balozi wa Marekani nchini, Mark Childress, vilivyotolewa na serikali ya nchi hiyo kupitia Shirika la Misaada (USAID).
Hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Mtakuja, Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwamo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi-Elimu), Kassimu Majaliwa.
“Tutaendelea kuongeza uwekezaji kwenye sekta ya elimu. Tutaendelea kuboresha mazingira ya walimu. Na msanii ameimba hapa suala la maslahi. Tunatofautiana na walimu sababu wanataka waongezwe kwa asilimia 100, lakini yote hayo tunaendelea kuyaangalia na kuongeza taratibu,” alisema.
Kuhusu usambazaji wa vitabu hivyo, alisema kazi hiyo iliyoanza Januari 2, imeshafanyika na imekamilika Januari 25, mwaka huu na ilifanywa na Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuzitaka taasisi za serikali kuangalia uwezekano wa kulitumia jeshi katika kazi za halali.
Naye Balozi wa Marekani nchini, Childress alisisitiza umuhimu wa kuimarisha stadi za msingi kwa wanafunzi, ambazo ni kusoma, kuandika na kuhesabu ili kuwawezesha kuelewa vyema maudhui ya vitabu hivyo na kuyatumia kikamilifu.
NIPASHE
Vurugu kubwa zimeibuka katika Kijiji cha Ilula, Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa baada ya wananchi kufunga barabara kuu ya Iringa-Morogoro, kuchoma matairi, kujeruhi watu na kuharibu magari kadhaa yakiwamo ya polisi kufuatia kifo cha mwanamke mmoja anayedaiwa kuponzwa na operesheni ya polisi ya kuwasaka watu wanaojihusisha na unywaji wa pombe wakati wa saa za kazi.
Mwanamke anayedaiwa kufa katika msako huo wa wanywaji wa pombe mchana na kuwa chanzo cha kuibuka kwa hasira za wananchi ametajwa kwa jina la Shida Mtandi. Inadaiwa alifariki dunia wakati askari walipokwenda kijijini hapo kusaka watu wanaokunywa pombe mchana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mvungi alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alisema yupo nje ya mkoa huo na kutoa maelekezo kwamba atafutwe kaimu wake, Pudensiana Protace. Naye alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi hakupatikana.
Taarifa zaidi kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa katika vurugu hizo watu wanne wamejeruhiwa akiwamo Mkuu wa Kituo cha Polisi Ilula.
Inaelezwa kuwa wananchi walivamia kituo hicho cha polisi na kuchoma moto magari manne na pikipiki moja.
Mashuhuda walisema kuwa vurugu hizo zilianza jana saa 6:45 mchana na kusababisha magari yaliyokuwa yakisafiri kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na nchi jirani kwenda Dar es Salaam kushindwa kuendelea na safari kwa zaidi ya masaa mawili kutokana na barabara hiyo kufungwa.
NIPASHE
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema uandikishaji wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa kutumia mfumo wa Biometric Voter Registration (BVR), haupaswi kuharakishwa, kwani baada ya kazi hiyo, ni lazima Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), ifanye uhakiki wa majina ya wapigakura.
Akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na Independent Television (ITV), alisema kwa uzoefu wake alipokuwa kiongozi wa timu ya waangalizi wa uchaguzi wa Jumuiya ya Madola nchini Malawi miaka 11 iliyopita, alibaini kuwa mfumo huo unaweza kuandikisha mtu mmoja mara mbili hadi nne.
“Tulikuta wanatumia BVR, utaratibu huu ni mzuri kwa kuzuia udanganyifu. Nchi ya Malawi ina takriban watu milioni tisa. Lakini tulikuta watu milioni sita wamejiandikisha. Tunaona haiwezekani zaidi ya theluthi mbili wajiandikishe kwenye uchaguzi,” alibainisha.
Aliongeza: “Tulibaini wengi walijiandikisha mara mbili tatu, nne, utaratibu huu ukijiandikisha majina mawili unafuta unabakiza moja, na hiyo ni muhimu tume ikishaandikisha lazima ihakiki, isipohakiki lazima yatafutwa, mtu atakuja kwenye kituo jina lake halipo na la mwingine lipo mara mbili na kulalamika.”
Alisema baada ya uandikishaji kumalizika ni lazima Nec ihakiki majina hayo kabla ya kuanza kutumika kwa daftari hilo.
Jaji Warioba alirejea kauli yake kuwa kura ya maoni haiwezekani kufanyika Aprili 30, mwaka huu, kama ambavyo serikali imeeleza kutokana na sababu mbalimbali.
Alizitaja sababu hizo kuwa ni Nec kuandikisha wapigakura, ambao pia watapiga kura katika Uchaguzi Mkuu, huku sheria ikiruhusu kuandikisha vijana, ambao hawajafikisha miaka 18, ambao Oktoba, mwaka huu, watakuwa wamefikisha umri huo.
HABARILEO
Watendaji wa Halmashauri waliokaa kwenye vituo vya kazi kwa zaidi ya miaka 10 , wataanza kuhamishwa wakati wowote kuanzia sasa kuleta ufanisi katika utendaji na kukomesha kufanya kazi kwa mazoea.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameagiza ofisi za mikoa ziainishe majina ya watendaji husika, utaratibu wa kuwahamisha ufanyike kunusuru utendaji wa kazi kwenye maeneo walikokaa muda mrefu. Alitoa agizo hilo juzi wilayani Mufindi katika mkoa wa Iringa.
Alisema serikali imebaini watendaji wanaokaa kwenye vituo vya kazi kwa miaka 10 na zaidi kwenye halmashauri, wanakuwa kikwazo cha utendaji kazi wenye ufanisi kutokana na kufanya kazi kwa mazoea badala ya kitaalamu.
Alisema, “Niliwahi kwenda kutembelea halmashauri fulani nikamkuta mzee mmoja amekaa hovyo kwa kujiachia achia tu na kusahau kuwa ni mtendaji wa serikali. Ilibidi nimuulize, mzee nawe umo, akasema , ndio mheshimiwa.
Nikashangaa, hata huyu! Kwa jinsi hivi alivyo atafanya kazi vizuri kweli?” “…Nilipomwuliza nilipata majibu yaliyodhihirisha kuwa alikuwa alivyo na kutenda kazi kwa mtindo aliokuwa akiufuata kwa sababu ya mazoea yaliyotokana na kuwepo kwenye halmashauri husika kwa zaidi ya miaka 10, hii haikubaliki kwa watendaji wa halmashauri”.
Pinda alisisitiza, kuwepo kituoni kwa muda mrefu kwa watendaji katika halmashauri ni miongoni mwa udhaifu unaotoa mwanya wa wizi wa fedha za halmashauri kwa sababu wanakuwa wakifahamu mbinu za kuiba na jinsi ya kukwepa kujulikana uhusika.
“Huu ni ukweli na ushahidi tumeuona katika maeneo ambako watumishi walikuwa wakiiba fedha. Kuwapangua kulisaidia sana kunusuru fedha zisiibwe katika baadhi ya halmashauri zilizokuwa na matatizo ya kifedha kutokana na wizi wakati wa kukusanya kodi na ushuru mbalimbali,” – Pinda
HABARILEO
Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) kitatumia Dola za Marekani bilioni 1 katika kujenga miundombinu ya elimu Afrika Mashariki kati ya hizo Dola za Marekani milioni 700 zitawekezwa Tanzania.
Akizungumza wakati wa mkusanyiko wa wahitimu uliokwenda sambamba na kutimiza miaka 15 kwa chuo hicho tangu kuanza kufanya shughuli zake Afrika Mashariki, Rais wa AKU, Firoz Rasul alisema kiasi hicho kitatumia katika kujenga kampasi Tanzania, Kenya na Uganda ndani ya miaka 15 ijayo.
“Lengo letu ni kuzalisha wahitimu ambao si tu wako tayari kwa ajili ya kupata ajira, lakini ambao wana ujuzi na wanaoweza kujiajiri na kutengeneza ajira mpya. Hivyo, kila kampasi yetu itakuwa ikiwahudumia wanafunzi kutoka nchi zote za Afrika Mashariki,” alisema.
Alisema kuwa uwekezaji huo utakaoanza mwaka 2015 hadi 2029 kwa Tanzania utachangia wastani wa Dola bilioni 6.3 kwenye uchumi na kuongeza udahili wa wanafunzi 10,000 kutoa ajira za moja kwa moja kwa watu 10,000 na ajira zisizo za moja kwa moja zipatazo 30,000.
Akifafanua zaidi, kampasi ya Dar es Salaam itakuwa kitovu cha kuwafundisha walimu bora wa viongozi wa shule kitatoa shahada katika kitivo cha sayansi.
Alisema kampasi ya Nairobi itakuwa kitovu cha sayansi ya afya na kozi ya uandishi wa habari na mawasiliano ambacho kitatoa mafunzo kwa waandishi wa habari na viongozi katika vyombo vya habari wakati Kampala italenga mafunzo ya uongozi na utawala katika sekta binafsi, za umma na kijamii.
MWANANCHI
Mwanamke mmoja ameieleza mahakama ya nchini Kenya kwamba alilazimika kumuuza mtoto wake wa siku tano kutokana na umaskini wa kupinfuka ambao ulisababisha kukosa fedha za kumtunza mtoto huyo.
Mama wa mtoto huyo Virginia Mwangi aliiambia Mahakama ya Nyeri kwamba alilazimika kumuuza mtoto huyo Shilingi 7,00 kwa Eunice Wangeci Kibira ambaye pia alishtakiwa kwa kosa hilo.
Wanawake hao wawili wanakabiliwa na mashtaka manne ya kushirikiana katika biashara ya kumuuza mtoto huyo kinyume na sheria ya watoto.
Mwangi alikiri makosa hayo mbele ya mahakama hiyo lakini Wendi alikanusha mashtaka na kuachiwa kwa dhamana ya shilingi 50,000.
JAMBOLEO
Halmashauri ya Manispaa ya Temeke imeingilia kati tukio la mwalimu wa Sekondari ya Kibasila, Gaudensia Albert kukaa na kinyesi ,mende na funza ndani kwa muda wa miaka miwili na kutaka kumchukulia hatua.
Ofisa Afya Manispaa ya Temeke Willium Mihemu alisema kwa sasa yupo kwenye mikakati ya kujiandaa kushirikiana na na askari polisi kumchukulia hatua mwalimu huyo anayefundisha masomo ya sayansi hapo shuleni.
“Leo sisi na Polisi tutaungana ili kwenda kumkamata,kwani kwa hali ya kawaida inaonekana mwalimu huyo hana akili timamu“-Mihemu.
Kwa upande wa mwenye nyumba Ruben Shayo ambaye wanaishi eneo la Yombo Visiwani alisema kuwa licha ya kufanya tukio hilo kwa miaka miwili mfululizo lakini bado alimruhusu kuendelea kuishi ndani ya nyumba yake na kumtaka kuondoa kinyesi hicho.
Shayo alisema hajawahi kumuona mwalimu huyo akimwingiza mgenindani ya nyumba hiyo badala yake alikua akimalizana nao nje ya chumba chake.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram, na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook