MWANANCHI
Wabunge jana waliwaweka kitimoto mawaziri wanne wakiwataka watoe maelezo ya kukwama kwa baadhi ya mambo katika wizara zao na kusababisha matatizo kwa wananchi na Serikali kukosa fedha.
Mawaziri hao ni wa Maliasili na Utalii; Lazaro Nyalandu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; William Lukuvi, Waziri wa Maji; Prof. Jumanne Maghembe na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika; Stephen Wasira.
Wakichangia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji na ile ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, wabunge hao walionekana kukerwa na ahadi zisizotekelezeka za mawaziri hao kiasi cha wao kukata tamaa.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola akichangia taarifa hizo aliwashukia mawaziri watatu kwa wakati mmoja akieleza kuhusika kwao kukwamisha baadhi ya mambo huku akisema migogoro ya ardhi nchini haitakwisha kama viongozi ndiyo wanaohusika kulinda baadhi ya watu.
“Wako viongozi wanahodhi ardhi na kusababisha matatizo, mwekezaji wa Oysterbay Villa, Lukuvi ndiye alimsaidia kupata eneo alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,” — Kangi Lugola.
“Sasa leo amekuwa Waziri wa Ardhi, itakuwaje? Mimi nitaichoma moto mbeleko inayombebea huyu mwekezaji kitendo kinachozuia Kinondoni kupata Sh3 bilioni. Huyu mwekezaji ana kiburi alizuia hata kamati kutaka kuingia kwenye eneo hilo lakini nikatumia ubaunsa wangu tukaingia.”
Hata hivyo, hoja ya Lugola kuhusu Lukuvi na mwekezaji huyo ilipingwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe ambaye alisema waziri huyo alisaidia hata kubadilisha mkataba wa umiliki wa Oystebay Villa, hivyo amwache.
Lugola akiendelea kuchangia alimshukia Waziri Maghembe kwamba anapeleka maji katika eneo lake tu wakati wananchi wa jimbo la Mwibara na Bunda wakiteseka kwa mradi wao wa maji kutokukamilika.
MWANANCHI
Madaktari katika Chuo cha Tiba cha Amrita, Kochi huko India wamefanikiwa kufanya upasuaji wa aina yake wa kupandikiza mikono mipya kwa binadamu aliyekatika viungo hivyo.
Upandikizaji huo uliofanyika Januari 12 na 13, ulifanikiwa kwa mara ya kwanza, baada mwanamume mwenye umri wa miaka 30, aliyekatika mikono katika ajali ya treni kuwekewa mingine. Mikono hiyo mipya ilichukuliwa kutoka kwa kijana wa miaka 24 aliyepata aliyefariki katika ajali ya gari.
Mkuu wa kitengo cha upasuaji katika chuo hicho, Prof. Subramania Iyer alisema; “Siku 14 baada ya upasuaji, mikono ilikubaliwa na mwili na ikaanza kujongea, yaani aliyepandikizwa aliweza kuisogeza huku na kule. Mgonjwa alitolewa chumba cha wagonjwa mahututi na huduma nyingine za kumchunguza ziliendelea.”
Daktari katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Hospitali ya Muhimbili (MoI), Prof. John Kahamba alisema hiyo si mara ya kwanza kwa upandikizaji wa mikono kufanyika duniani kwani na tofauti kubwa na upandikizaji wa figo au ini.
Prof. Kahamba alisema upasuaji huo unafanyika kwa kuhakiki mambo mbalimbali ikiwamo uwiano wa kundi la damu, uhai wa seli na misuli na mishipa midogo ya fahamu.
“Upasuaji mkubwa hufanyika, pamoja na kuangalia uwiano wa damu lakini lazima jopo la madaktari wenye kazi tofauti lifanye kazi kwa pamoja. Kwa mfano, wanaounganisha misuli na mishipa midogomidogo na hata wale wa kuhakiki uhai wa seli“– Kahamba.
Prof. Kahamba alisema kama upandikizaji wa figo unavyofanyika, kadhalika upandikizaji wa mikono unahitaji umakini wa muda.
Anasema iwapo utachelewa kuunganisha mikono baada ya kuitoa, seli zake zinaweza kufa na kushindwa kufanya kazi zitakapopandikizwa kwenye mwili.
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete amekabidhi madaraka ya Uratibu wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali za Afrika ya Mazingira (CAHOSCC) kwa Rais wa Misri, Jenerali Abdel Fatteh El Sisi.
Rais Kikwete alibeba jukumu la uratibu wa CAHOSCC miaka miwili iliyopita baada ya kifo cha aliyekuwa mratibu wa kamati hiyo, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu, Rais Kikwete alikabidhi jukumu hilo Januari 31 na kuwatahadharisha viongozi wa Afrika juu ya athari za mabadiliko ya tabia ya nchi kwenye sekta ya kilimo barani Afrika.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa Kikwete aliwapongeza viongozi wengine wa Afrika wakati wa mkutano wa 24 wa Umoja wa Afrika (AU), Addis Ababa kwa kupata mafanikio wakati wa uongozi wake.
Kikwete alibainisha changamoto mbalimbali zinazolikabili bara la Afrika kwenye mabadiliko ya tabia ya nchi na kutaka ushirikiano kati ya nchi zilizoendelea ambao ndiyo wachafuzi wakubwa wa mazingira na nchi zinazoendelea kutoka Afrika.
NIPASHE
Wimbi la uvamizi na uporaji wa silaha kwenye vituo vya polisi limeendelea kushamiri safari hii likiamia mkoani Morogoro kwa kituo kidogo cha Polisi Mngeta, kilichopo Wilaya ya Kilombero, kuvamiwa na kuporwa bunduki moja aina ya SMG na magazine moja yenye risasi 30.
Tukio la Morogoro lilitokea juzi majira ya saa 9:30 usiku na Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linamtafuta kijana mmoja, Emmanuel Shewele (21) kwa tuhuma za kusababisha kuvunjwa kwa kituo hicho.
Mbali ya silaha hizo, wavamizi hao waliiba vielelezo vya ushahidi ili kupoteza ushahidi wa kesi zake kufuatia kushtakiwa mahakamani kwa kesi zaidi ya tano.
Kamanda wa Polisi Morogoro, Leonard Paulo, alitaja vielelezo kuwa ni genereta moja, viti vinne vya plastiki, redio moja aina ya sabufa, betri ya gari moja na spika moja ya redio.
Alisema tayari watuhumiwa watatu wamekamatwa ambao ni Ramadhani Shewele (20), Hamisi Hamidi (45) na Egnas Shewele (34), huku wakiendelea kumtafuta Emmanuel Shewele (21) wote wakiwa ni wakazi wa kijiji cha Nakaguru A, wilayani humo.
NIPASHE
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola amesema atawashawishi wananchi wasikichague Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika nchini Oktoba mwaka huu ikiwa serikali haitatekeleza miradi ya kupekeleka maji katika Wilaya ya Bunda mkoani Mara na hasa jimboni kwake.
Lugola aliyasema hayo jana, wakati akichangia mjadala kuhusu taarifa ya utekelezaji ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na ile ya Kilimo, Mifugo na Maji baada ya kuwasilishwa bungeni jana.
Alisema mradi wa ujenzi wa bomba la maji kutoka Tamau hadi Bunda ambao pia unakusudia kuvipatia maji vijiji vya Bulamba Bizimbwe na Mwisenye umekuwa kizungumkuti kwa muda mrefu sasa.
Alisema inasikitisha kwenye kitabu cha taarifa ya Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Magembe hajaweka mradi huo na badala yake ameweka miradi mingi ya kwenye jimbo lake.
“Na hata kwenye kitabu hiki cha taarifa yake Mheshimiwa Waziri, Hakuna mradi huu wa maji ya Bunda, mradi mkubwa, lakini ukienda kwenye miradi yake ya Same, Mwanga ndiyo imejaa kwenye kitabu hiki, kwa nini nisiamini unafanya kazi kwa kupendelea maeneo yako“–Lugola.
Alisema wakazi wa Bunda wanahitaji maji hayo kutoka Ziwa Victoria lilipo umbali wa kilometa 20 lakini mpaka sasa ni zaidi ya miaka sita tangu mradi huo uasisiwe hawajapata.
Alisema kwa sasa taifa linaelekea kwenye uchaguzi ambao anaamini CCM kitaendelea kushinda kwa kishindo kwa kuwa Rais Kikwete amefanya mabadiliko ya mawaziri ambayo alitaka sasa yawe ni mabadiliko yenye tija.
Hata hivyo alimtaka Maghembe kufanya mabadiliko haraka ya miradi ya maji kwa kuwa wakazi wa Bunda akiwemo mwenyewe hawatakubali kuipigia CCM kura ikiwa hawatapata maji mpaka kufikia kwenye uchaguzi huo.
MTANZANIA
TUME ya Utumishi wa Mahakama imesema suala la majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wanaotuhumiwa kupokea zaidi ya Sh milioni 400 kutoka katika akaunti ya Tegeta Escrow, limefika kwenye tume hiyo na linafanyiwa kazi.
Kwa utaratibu wa tume hiyo, baada ya uchunguzi taarifa hupelekwa kwa rais ambaye baada ya kupitia mapendekezo yaliyotolewa kwenye ripoti ya uchunguzi, hutoa uamuzi.
Hayo yalielezwa jana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Hussein Katanga, katika banda la Tume ya Utumishi wa Mahakama katika maonyesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.
Majaji wanaotuhumiwa kuingiziwa fedha hizo ni Prof. Eudes Ruhangisa (Sh milioni 404.25) na Aloysis Mujulizi (Sh milioni 40.4).
“Huo ni ukweli, inatakiwa uwepo uwazi zaidi…Tunatakiwa kuwa wazi, hivi sasa tunataka kuweka mabango wananchi wajue jinsi ya kupata haki kuepusha rushwa“– Katanga.
Akizungumzia hilo, Mkurugenzi Msaidizi wa Mahakama za Mwanzo, Warsha Ng’humbu aliyekuwapo katika banda la Kurugenzi ya Ukaguzi, Malalamiko na Maadili, alisema kwa kuwa suala hilo limefika kwenye tume, maana yake lilishapita katika Kamati ya Maadili ya Majaji.
Katibu Msaidizi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Enzeel Mtei alisema tume hiyo inaundwa na wajumbe sita na ina jukumu la kumshauri rais juu ya uteuzi wa Jaji Kiongozi au majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram, na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook