MWANANCHI
Kwa mara ya pili, Spika Anne Makinda jana alilazimika kuahirisha kwa muda shughuli za Bunge la Jamhuri ya Muungano baada ya wabunge wa vyama vya upinzani kukataa kukaa, wakishinikiza kitendo cha polisi kumpiga na baadaye kumkamata Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba kijadiliwe kwa masilahi ya Taifa.
Profesa Lipumba, ambaye pamoja na wanachama wengine 32 walikamatwa juzi eneo la Mtoni Mtongani wakati alipokuwa akielekea Zakhem, Mbagala jijini Dar es Salaam kuwataka wafuasi wa CUF kutawanyika kwa amani baada ya Jeshi la Polisi kuzuia maandamano, jana alikamatwa tena akiwa nje ya Kituo Kikuu cha Polisi muda mfupi baada ya kuachiwa kwa dhamana, akidaiwa kuongea na waandishi wa habari wakati akiwa mtuhumiwa.
Wakati akiwa mbaroni, Profesa Lipumba alijisikia vibaya na hivyo kupelekwa hospitali kabla ya kufikishwa Mahakama ya Kisutu jioni, akishtakiwa kwa kufanya maandamano bila ya kibali.
Jana bungeni, Spika Makinda alijikuta akipambana na nguvu ya wabunge wachache wa upinzani ya kuzuia kuendelea kwa shughuli za Bunge kama ilivyokuwa mwishoni mwa mwaka jana wakati walipotumia staili hiyo ya kusimama wakati wote kushinikiza Bunge kusikiliza matakwa yao kuhusu hatua za kuchukua dhidi ya wahusika kwenye sakata la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
MWANANCHI
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema kuwa haina ubavu wa kununua ndege kwa matumizi ya viongozi wake.
Waziri wa Fedha Zanzibar, Omary Yussuf Mzee alisema hayo jana alipojibu swali la mwakilishi wa Jimbo la Muyuni, Jaku Hashim Ayoub katika kikao cha Baraza la Wawakilishi.
Alisema SMZ itaendelea kukodi ndege kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya matumizi ya viongozi wake.
Aliwaambia wajumbe wa baraza hilo kuwa gharama za uendeshaji wa ndege za Serikali ya Muungano wa Tanzania hutolewa na Serikali ya Muungano, hivyo SMZ hulazimika kukodi na kulipia gharama.
“Kuiweka ndege moja Zanzibar ili itumike kwa viongozi wetu wa kitaifa ni jambo linalowezekana, lakini kufanya hivyo ni kuongeza gharama za uendeshaji, kwani wakala watalazimika kuweka vifaa na wataalamu wa kuzihudumia ndege hizo:-Waziri Mzee.
MWANANCHI
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta amesema angependa kuona sheria inayataja makosa ya udokozi bandarini kama ya uhujumu wa uchumi ili watuhumiwa wanapokamatwa na kushtakiwa wasipewa dhamana.
Waziri Sitta alisema hayo jana wakati akizungumza na watendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), katika mfululizo wa ziara zake kwa mashirika, taasisi na mamlaka zilizo chini ya wizara yake kwa lengo la kufahamiana na kujua changamoto na kupanga mikakati yake katika utendaji.
Akizungumza katika mkutano na watendaji TPA, baada ya kusikiliza taarifa ya utendaji kazi iliyohusisha mikakati, mafanikio na changamoto za mamlaka hiyo, Sitta alisema duniani kote bandari ni kitovu cha uchumi wa nchi.
Alisema vitendo vyovyote vya udokozi na hujuma vinavyofanywa na watumishi wasio waaminifu ni kuhujumu uchumi wa Taifa, hivyo angependa kuona wahusika wanashtakiwa na kunyimwa dhamana.
MWANANCHI
Siku mbili baada kukabidhiwa ofisi na aliyekuwa Waziri wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, waziri ambaye ameteuliwa kushika nafasi hiyo, Dk Harisson Mwakyembe amewataka Watanzania kuondoa hofu ya kuhamishwa kwake kutoka Wizara ya Uchukuzi, huku akisisitiza kuwa hana nia ya kugombea urais.
Dk Mwakyembe aliwataka wananchi kuondoa hofu kwa sababu utendaji aliouonyesha akiwa Wizara ya Uchukuzi, atauhamishia wizara yake mpya.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili muda mfupi baada ya kuapishwa na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Daniel Kidega, Mwakyembe alisema utendaji aliouonyesha katika wizara aliyokuwamo awali zamani, ndiyo uliomshawishi Rais Jakaya Kikwete kumhamishia Wizara ya Afrika Mashariki ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa masuala ya jumuiya hiyo.
“Watanzania wanapaswa kuondoa kasumba ya kutaka anayefanya vizuri katika nafasi yake kuendelea kubaki hapo hapo. Hapana! Anayefanya vizuri sehemu moja ni vyema akahamishiwa sehemu nyingine ili akafanye vizuri huko pia:- Mwakyembe
NIPASHE
Serikali imewaondoa hofu wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kuhusu kivuko cha Mv. Magogoni kuwa ni salama na wakitumie bila hofu tofauti na inavyodaiwa kuwa ni kibovu na hakifai kwa ajili ya huduma ya usafiri na kinahatarisha maisha ya wanaokitumia.
Aidha, serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) imesema ipo katika utaratibu wa ununuzi wa kivuko kipya cha Magogoni-Kigamboni kitakachokuwa na uwezo wa kubeba tani 250.
Kauli hiyo iliyotolewa na Kitengo cha mawasiliano Wizara ya Ujenzi kufuatia taarifa vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na wananchi kuwa kivuko hicho ni kibovu na kinahatarifa maisha ya wanaokitumia.
“Wizara inapenda kutoa taarifa kwa umma kuwa kivuko cha MV. Magogoni ni salama kwa kuvusha abiria na magari kati ya upande wa Magogoni na Kigamboni,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Ilieleza kuwa kivuko hicho kina injini nne, injini mbili zinatumika kuendeshea kivuko na injini nyingine hutumika wakati kukiwa na hitaji la ziada (ongezeko la mizigo au hali mbaya ya bahari).
Kadhalika, ilieleza kwa sasa injini tatu za kivuko hicho zinafanya kazi vizuri baada ya kufanyiwa matengenezo pamoja na kurekebisha mfumo wa kupoza injini ulikokuwa unasababisha injini kupata moto.
NIPASHE
Jeshi la Polisi mkoani hapa limeingia katika kashfa, baada ya askari wake kudaiwa kuvamia kambi ya wafanyakazi wa kiwanda cha chai Kibena usiku wa kuamkia Jumatatu wiki hii, na kuwacharaza viboko baadhi ya wafanyakazi walio kuwa wamelala na familia zao na kupora simu za mkononi.
Baadhi ya wafanyakazi walisema askari hao baada ya kuvamia kambi hiyo usiku wa manane, walivunja milango na kuwaamuru watoke nje huku wengine wakiwa kama walivyozaliwa na kuwacharaza viboko, na kuwapa adhabu ya kuruka kichura.
Mmoja wa waathirika, Vumilia Ngewe, alisema alikumbana na mkasa huo alfajiri akiwa anajiandaa kutoka kazini.
Akisimulia mkasa huo kwa shida kutokana na maumivu ya kipigo, alisema askari hao walivamia kambi yao saa tisa usiku na kuanza kufanya uhalifu huo.
“Askari walikuja kazini kwetu usiku wa saa tisa, wengine tulikuwa tunajiandaa kutoka ili tuwapishe wengine, tukawa tumezima na mitambo, lakini walipofika ofisini walituamuru tuiwashe na tuendelee na kazi huku wengine waliokuwa wamekuja kutupokea wakiwa nje wakifanyishwa adhabu na askari hao:-Ngewe
Ngewe alisema polisi waliingia katika kambi za kiwanda hicho kwa king`ora na kuanza kuwatoa ndani kwa amri huku wakiwaamuru wanawake wawatoe waume zao na kuanza kuvunja milango kuingia ndani.
UHURU
Mgomo wa wafanyabiashara wa mduka umesambaa mikoa kadhaa nchini kupinga matumizi ya mashine za kielektroniki (EFDs).
Mgomo huo ulioanzia kwa wafanyabiashara wa maduka Kariakoo, jijini Dar es Salaam kuanzia juzi, kupinga Mwenyekiti wao Johnson Minja, kukamatwa na polisi, sasa umesambaa hadi miji ya Mwanza, Iringa, Songea na Dodoma.
Minja (34), jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mkoa wa Dodoma kwa makosa mawili likiwamo la kuzuia ukusanyaji wa kodi kwa kutumia EFDs na kusomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Rebbeka Mbiru.
Wakili wa Serikali, Godfrey Wambari, alidai kuwa Septemba 6, mwaka 2014, katika ukumbi wa Chuo Cha Mipango Dodoma alitenda kosa la kushawishi wafanyabiashara kutenda kosa la jinai kwamba wasilipe kodi.
Katika shitaka la pili, siku na mahali pa tukio la kwanza mshtakiwa anadaiwa kuzuia ukusanyaji wa Kodi kwa kutumia mashine za EFD.
Hata hivyo, mshtakiwa alitimiza masharti ya dhamana na kesi hiyo itatajwa Februari 11, mwaka huu.
MTANZANIA
TAASISI ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, imepinga tamko la maaskofu kuhusu kuzuia kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na kusema hatua hiyo ni sawa na kuingilia uhuru wa Bunge.
Kutokana na hali hiyo, wametaka maaskofu hao kupitia Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF), kuwaacha wabunge ili waweze kujadili muswada huo kwa uhuru bila kuwapo shinikizo katika suala hilo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa taasisi hiyo, Sheikh Khamis Mataka, alisema tamko lililotolewa na maaskofu ni sawa na kuingilia madaraka ya Bunge na kutaka kuifanya Serikali ichukiwe kwa kuonekana imeshindwa kutimiza ahadi iliyoitoa kupitia Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
“Tamko lililotolewa na maaskofu halina hoja, hawana sababu za msingi za kuikataa Mahakama ya Kadhi, tunawasihi na kuwaomba maaskofu waachie uhuru wa wabunge hasa waumini wa dini ya Kikristo walioko bungeni, ili waweze kuujadili muswada huo bila shinikizo la kiimani”:-Mataka.
“Mbinu zozote za kuwashawishi wabunge kiimani kutekeleza maazimio ya maaskofu chini ya Jukwaa la Wakristo Tanzania zitaleta udini na jaribio la kuligawa Bunge kiimani, jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa taifa letu,” alisema Sheikh Mataka.
Alisema wabunge wanapaswa kuzingatia viapo vyao vya kuwatumikia wananchi kwa uadilifu bila kuathiriwa na shinikizo la kiimani lililotolewa na maaskofu.
HABARILEO
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umeongeza muda wa mwezi mmoja kwa wanachama wake kuweza kuhakiki taarifa zao, kabla ya kuhitimisha utaratibu huo ifikapo Februari 28, mwaka huu.
Kwa mujibu wa mfuko huo, baada ya uhakiki huo, mfuko huo utaweza kuwa na data ya wanachama wake ya uhakika, taarifa zao za uhakika lakini pia kuondokana na wanachama waliopoteza sifa ya kuwa wanachama wa mfuko huo.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa mfuko huo, Eugene Mikongoti, alisema tangu utaratibu huo wa kujaza fomu za uhakiki kwa wanachama wake uanze Oktoba 27, mwaka jana, jumla ya wanachama 491,010 tayari wamehakikiwa sawa na asilimia 72.
“Jumla ya wanachama wetu ni 740,490 lakini lengo letu la kufanya uhakiki huu wa taarifa za mwanachama ni kupata taarifa za uhakika za mwanachama, kusafisha data lakini pia kubaini wale wote wanaonufaika na mfuko huu wakati tayari wamepoteza sifa, kama vile waliopoteza maisha na walioacha kazi:- Mikongoti
Hakuna story itakayokupita mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>> twitter Insta Facebook