NIPASHE
Serikali mkoani Kilimanjaro, imetoa saa 48 kwa maofisa watendaji kata, vijiji na mitaa, kufanya zoezi maalum la uhakiki wa wageni, wanaodaiwa kutumia mwavuli wa dini kuendesha biashara haramu ya wizi wa watoto.
Agizo hilo limekuja siku chache baada ya kugundulika mahali walipofichwa watoto 29, wanaodaiwa kupotea kwenye mazingira ya kutatanisha katika mikoa 13 nchini na kuhifadhiwa kwenye makazi hayo kinyume cha sheria za nchi.
Mkuu wa mkoa huo, Leonidas Gama alisema unalenga kusaidia kupunguza hofu na hasira ya umma kuhusiana na usalama wa watoto hao; na mahali wanakopelekwa baada ya kupatiwa mafunzo maalum ya kujihami pamoja na elimu ya dini.
“Nimeagiza ndani ya saa 48, kila mtendaji kwenye ngazi za vijiji, mitaa na kata, wawe wamewatambua watu wote na kuwasilisha taarifa za siri kwa wakuu wa wilaya zao. Baada ya zoezi hilo nitatoa taarifa rasmi kwa umma, Jumanne ya wiki ijayo kuhusu hali ya usalama katika mkoa wetu,” Gama.
Watoto walio okolewa hadi sasa, baada ya kugunduliwa kwa matukio hayo ni wenye umri wa miaka miwili hadi 16, ambao walikutwa wamehifadhiwa kwenye nyumba moja, iliyopo karibu na uwanja wa Mandela, Kata ya Pasua, Manispaa ya Moshi, mali ya mfanyabiashara wa nguo nchini Kenya, Abdelnasir Abdurahaman, maarufu kama Karata (33), huku watoto wengine 11, wakiokolewa pia katika kituo cha UMM Sakhail, kilichopo Lyamungo, Wilaya ya Hai.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Tangazo la Serikali namba 280 la mwaka 2002, pamoja na kifungu cha 353 cha Sheria ya Elimu, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002; mzazi yeyote au mlezi atakayeshindwa kuhakikisha mwanae anapata elimu ya msingi kwa wakati husika, atashtakiwa, kulipishwa faini au kupata adhabu ya kifungo, iwapo atashindwa kutimiza matakwa ya sheria hiyo.
Kufuatia taharuki hiyo kuikumba mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Ernest Mangu, juzi alilazimika kukutana na kutetea kwa zaidi ya saa sita na timu ya makachero wa makao makuu ya jeshi hilo pamoja na maofisa wake wa mkoa wa Kilimanjaro, ikiwa ni siku tano baada ya kukamatwa kwa wafanyabiashara wanaodaiwa kuwahifadhi watoto kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Alipoulizwa iwapo watoto hao, wanatokea mikoa ipi ya Tanzania; Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwela, alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa watoto hao ni wakazi wa mikoa ya Tanga, Mtwara, Mbeya, Tabora, Manyara, Arusha, Kagera, Mara, Kilimanjaro, Dodoma na Shinyanga.
NIPASHE
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amewataka wananchi wa Kigoma kuwa wavumilivu wakati akipigania haki za Watanzania hasa anapopambana na mafisadi.
Akihutubia mkutano wa hadhara jana katika Kijiji cha Nyarubanda mkoani hapa, baada ya kushindwa kwenye kesi dhidi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kuvuliwa uanachama, Zitto aliwataka wananchi hao kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha mgogoro na chama chake.
Aliwataka wananchi kutosononeka kwa kuwa yuko kwenye haki na anatetea maslahi ya watu.
Mapema wiki hii Zitto, alishindwa katika kesi aliyofungua ya kupinga kujadiliwa na kuvuliwa uanachama na chama chake kufuatia mgogoro kati yake na Chadema.
“Mimi nina nia njema na watu wote, niko tayari kuwatetea na ninataka nchi hii iendelee, ninataka kupambana kwa dhati na ufisadi kama tunavyofanya bungeni hivi sasa, lakini tunapambana na ufisadi ndani na nje ya vyama vya siasa na hatutaogopa tutasema ukweli daima uongo kwetu ni mwiko,” alisema.
Alisema katika kipindi hiki wananchi wawe wavumilivu kwa lolote litakalo tokea na kuwaomba wamuunge mkono.
Alisema kuna watu wanaotumiwa na maadui zake na kuwaambia suala hilo ni la muda kwani adui akishafanikisha malengo yake au akishindwa anakaa pembeni.
“Lengo letu ni moja ni maendeleo ya mkoa wetu, ni maendeleo ya jimbo letu na ni maendeleo ya nchi yetu bila kujali itikadi za vyama kwa hiyo kesho (leo) nitakuwa na mkutano nitawaelezea kwa kina zaidi nilitaka niwaaambie haya ili muelewe msisononeke, msisikie propaganda mimi bado nawahudumia bado nawafanyia kazi na moja ya kazi ninayofanya ni hii ya kutimiza ahadi yangu ya kumkabidhi mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kigoma, funguo za gari aina ya Toyota Hiace yenye namba za usajiri T 779 DCF kwa ajili ya kituo cha afya cha Nyarubanda, alisema.
Baada ya kukabidhi gari hiyo, wananchi walimbeba huku wakiimba “karibu mkombozi wetu, karibu rais mtarajiwa tunakuombea maisha mema kwa Mungu ili uendelee kutuongoza.”
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Michael Mwandesi, alimshukuru Zitto kwa kutimiza ahadi yake na kuahidi kwamba gari hiyo itafanya kazi za kituo cha afya cha Nyarubanda na si vinginevyo.
NIPASHE
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, William Lukuvi, amemsimamisha kazi afisa ardhi msaidizi wa Jiji la Mwanza, Asubuhi Otieno, kwa udanganyifu wa kubatilisha matumizi ya ardhi kinyume cha sheria.
Alichukua hatua hiyo kufuatia tuhuma zinazomkabili afisa huyo za kusema uongo.
Alitangaza uamuzi huo katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili ambazo anadaiwa kuandika barua na kusainiwa na mtu mwingine na alipotakiwa kuijibu, alijibu kwa kusoma maelezo ambayo hayapo ndani ya barua hiyo.
“Otieno umenidanganya umesoma kitu ambacho hakijaandikwa katika barua hii, hivyo kuanzia sasa nakuwajibisha kwa kukusimamisha kazi kwa muda kwa sababu huna mamlaka ya kubatilisha matumizi ya ardhi kisheria,” Lukuvi.
Hata hivyo, Otieno alipopewa nafasi ya kujieleza hakuwa na maelezo ya kuridhisha zaidi ya kuinamisha kichwa chini kabla ya kusimamishwa kazi na kudai aliandika barua kwa niaba lakini hakubainisha hivyo kwenye nyaraka ya awali.
Hata hivyo, Lukuvi alisema baadhi ya maafisa wa ardhi wamekuwa wakipima viwanja na kuviuza kiholela bila kuwashirikisha wananchi na wakati mwingine kuwalipa wamiliki wa ardhi hiyo fidia isiyo stahiki.
Alisema sheria ya ardhi inabainisha wazi kuwa hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kupima na kugawa kiwanja bila kushirikisha wananchi na kutambuliwa na uongozi wa serikali ya mtaa.
“Wenyeviti wa serikali za mitaa andaeni kitabu cha wageni ili maafisa ardhi wanapoenda maeneo yenu, waweze kusaini na kujitambulisha wamekuja kufanya nini,” alisema.
NIPASHE
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema iko mbioni kuifungia mitandao ya kijamii, redio na televisheni inayokiuka maadili ya Mtanzania.
Meneja Mawasiliano wa Mamlaka hiyo, Innocent Mungy, alisema kuwa mitandao hiyo ni pamoja na facebook, whatsapp na instagram.
Alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu changamoto zinazoikabili mamlaka hiyo kutokana na kuwapo kwa watumiaji wengi wa mitandao hiyo katika kuelekea Siku ya Mawasiliano duniani inayofanyika Machi 15, kila mwaka.
Mungy alisema kuwa Mamlaka hiyo inafanya utafiti ili kubaini mitandao inayoongoza kwa kulalamikiwa na wateja ili hatua zichukuliwe.
“Tangu TCRA iwezeshe kuwa na wingi wa simu na kuwezesha kuwepo kwa mitandao mingi ya kijamii changamoto zimeongezeka, maadili yameporomoka tofauti na miaka ya nyuma wakati kuna redio moja tu maadili yalizingazitiwa, kwa sasa utasikia lugha za matusi kwenye radio ikiwa ni pamoja na vipindi visivyofuata maadili na kanuni za habari, tuna mpango wakuifungia mitandao hiyo na vyombo vya habari visivyokidhi mahitaji,” alisema.
Alisema kuwa Mamlaka hiyo lengo lake ni kuwezesha Watanzania kwenda na wakati na kuelewa mambo mengi kwa wakati mmoja ikiwa ni pamoja na kupata habari ndani na nje ya nchi na kuongeza ajira kwa Watanzania kama ilivyo kwenye makampuni ya simu.
Aliwataka wamiliki wa mitandao kufuata maadili ikiwa ni pamoja na viongozi wa dini, wazazi, kuwafundisha wananchi na waumini wao kuwa na maadili ili kuondoa upotofu huo ambao unaweza kugeuza kizazi kisichofuata maadili na wengine kukosa ajira kutokana na kutumia mitandao vibaya.
MTANZANIA
Serikali imechukua hatua ya dharua ya kuchangisha damu kwa hiari kutoka kwa wananchi ili kubaliana na tatizo la upungufu wa damu katika benki ya damu.
Hayo yalibainishwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mpango wa Taifa wa Damu Salama, katika mkutano na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu shughuli hiyo itakayofanyika kwa siku tano kuanzia Machi 23, mwaka huu.
Kaimu Mkurugenzi wa NHIF, Michael Mhando, alisema, mahitaji ya damu salama nchini ni chupa 400, 000 hadi 450, 000 kwa mwaka ambayo ni sawa na wastani wa chupa 106,000 za damu kwa robo moja ya mwaka.
Alisema hadi sasa takwimu zinaonyesha kuwa kiasi cha chupa 19,000 za damu salama zilikusanywa kati ya Oktoba na Desemba mwaka jana huku chupa 15,000 zikikusanywa kuanzia Januari mwaka huu.
“Hili ni suala la dharura na linahitaji hatua za haraka na ushirikiano miongoni mwa wadau wa sekta ya afya na wananchi kwa ujumla. Hii inaonyesha kuwa upo uhaba mkubwa wa damu kulinganisha na uhitaji uliopo hasa katika vituo vikubwa mfano Muhimbili ambako zinahitajika chupa 50 hadi 60 za damu kwa siku.”
Alisema, NHIF na Mpango huo wa Damu Salama, wameona vyema kuunga mkono juhudi za serikali katika kipindi hicho cha uhaba mkubwa wa damu salama kwa kuendesha shughuli hiyo ya ukusanyaji wa damu kwa hiari kutoka kwa wananchi takriban 6,000.
Aliongeza kuwa, shughuli hiyo pia itaambatana na upimaji wa afya kwa magonjwa yasiyoambukiza katika mikoa sita nchini kwa pamoja kwa siku tano tangu Machi 23 mwaka huu.
Alitaja baadhi ya mikoa hiyo kuwa ni Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Kilimanjaro, Tabora na Mtwara.
Naye Meneja masoko na uhusiano wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Rajabu Mwenda, alisema, changamoto iliyopo ni uhujumu wa damu kwa baadhi ya wahudumu wa afya wasiowaaminifu hospitalini hivyo kuwafanya wananchi kukosa imani na mpango huo.
Hata hivyo, alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo hayo kwa ajili ya shughuli hiyo na damu salama itakayopatikana iweze kusambazwa nchini kuokoa maisha ya Watanzania ambao wana uhitaji mkubwa wa damu.
MWANANCHI
Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahimu Lipumba ameunga mkono tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania kupinga Katiba Inayopendekezwa, akisema hoja zao ni za msingi kwa kuwa kuna mambo mengi yanayopingwa na wananchi.
Kauli ya Profesa Lipumba ni mwendelezo wa kauli tofauti zilizotolewa na watu mbalimbali kuhusu tamko la jukwaa hilo, wakiwamo wasomi, viongozi wa dini, wanaharakati na wanasiasa kuhusu hatima ya Kura ya Maoni na muswada wa Makahama ya Kadhi.
Alhamisi iliyopita, jukwaa hilo linaloundwa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) liliwataka waumini wake kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, kushiriki kikamilifu katika elimu ya Kura ya Maoni, na kisha kuipigia kura ya “hapana” Katiba Inayopendekezwa.
Pia, tamko hilo lililotiwa saini na maaskofu Dk Alex Malasusa wa (CCT), Tracisius Ngalalekumtwa (TEC) na Daniel Awet wa CPCT, lilishauri mjadala unaoendelea kati ya Serikali na vikundi vya kidini kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi kikatiba na kisheria ufungwe na badala yake ziachiwe taasisi husika za kidini kuamua juu ya masuala hayo bila kuihusisha serikali wal
Jana gazeti hili lilimnukuu makamu mwenyekiti wa TEC, Askofu Severine Niwemugizi akisema tayari tamko hilo limeshasambazwa katika majimbo yote ya kanisa katoliki na kwa waumini wa dini nyingine.
Akizungumzia tamko hilo, Profesa Lipumba alisema ni sahihi kuipinga Katiba hiyo kwa sababu wananchi walilalamikia mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya baada ya kubaini kuwa mambo mengi waliyoyapendekeza yaliondolewa wakati wa Bunge Maalumu la Katiba.
“Wananchi walitaka kuwepo na ukomo wa wabunge wao, viongozi wasifungue akaunti nje ya nchi na mambo mengine yote hayamo kwenye Katiba Inayopendekezwa. Hoja yao (maaskofu) ni ya msingi,” Prof. Lipumba aliyeongoza wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka nje ya Bunge la Katiba na kususia mchakato huo moja kwa moja.
HABARILEO
Akiwa katika maadhimisho ya kuanza mwaka wa pili wa utume wake katika kuongoza Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Francis, ametoa kauli kuashiria kuwa huenda asidumu katika wadhifa huo kwa muda mrefu ujao.
Alisema hayo juzi katika mahojiano ya ana kwa ana na kituo kimoja cha televisheni cha Mexico, Televisa News, baada ya kutangaza kuwa Desemba mwaka huu, Kanisa Katoliki litaadhimisha Mwaka Mtakatifu.
Mwaka huo Mtakatifu utaanzia Desemba 8, mwaka huu na kuisha Novemba 20, mwakani.
Inaelezwa kuwa kuzinduliwa kwa Mwaka Mtakatifu au Jubilee, kunaendana na maadhimisho ya 50 ya kufungwa kwa Baraza la Pili la Vatican, ambalo hukusanya maaskofu ambao huzungumzia mambo ya baadae ya kanisa.
Kwa kawaida Mwaka Mtakatifu huadhimishwa kila baada ya miaka 25. Ukomo wake Katika tamko hilo, Baba Mtakatifu Francis mwenye umri wa miaka 78, ameweka wazi kuwa hataadhimisha miaka mingine mitakatifu katika siku zijazo.
“Nina hisia kwamba utume wangu utakuwa wa muda mfupi, kama miaka minne au mitano; sijui inaweza hata kuwa miwili au mitatu lakini miaka miwili imeshapita,” alitabiri katika mahojiano hayo.
Hata hivyo, hakutaka kuweka wazi kama atafuata nyayo za mtangulizi wake, Baba Mtakatifu mstaafu Benedict XVI, ambaye ameweka historia ya kuwa Baba Mtakatifu wa kwanza kustaafu katika miaka 600 iliyopita, baada ya kuchukua hatua hiyo mwaka 2013.
Alipoulizwa swali mahususi kama atafuata nyazo za Baba Mtakatifu mstaafu, Benedict XVI, alijibu; “Huenda Benedict XVI akabakia kuwa Baba Mtakatifu mstaafu pekee kwa miaka mingi ijayo, na huenda akapata mwenzake,” na kuongeza kuwa Baba Mtakatifu mstaafu “ameonesha njia.
” Hii si mara ya kwanza kwa Baba Mtakatifu Francis kuzungumzia ukomo wake, kwa kuwa amewahi kusema kustaafu kwa Baba Mtakatifu Benedict XVI mwaka 2013, kusichukuliwe kuwa tukio la pekee.
Pia, alisema hakuchukia kuteuliwa kuwa Baba Mtakatifu, lakini aliweka wazi kwamba katika wadhifa huo, amejikuta akipoteza uhuru wake.
“Natamani tena kuwa na uwezo wa kutoka nje siku moja bila mtu yeyote kunifuatilia na kunitambua nikajinunulie mahitaji yangu,” alisema na kutabasamu. Lengo la mahojiano hayo na kituo hicho cha Televisa News, lilikuwa kujadili maisha yake ikiwemo mawasiliano yake na baadhi ya watu, ambao wamekuwa wakimwandikia barua kumshirikisha katika huzuni zao na kupata ushauri wake.
MWANANACHI
Rais Jakaya Kikwete amevitaka vyuo vikuu nchini kuwaandaa vijana kuwa wahadhiri badala ya kutegemea wastaafu.
Kikwete alisema hayo juzi usiku, katika harambee ya kuchangia fedha Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini (Tudarco) iliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam ambapo Sh 1.6bilioni zilipatikana.
Alisema kuwa vijana zaidi wanahitajika kutoa elimu katika vyuo vikuu nchini ili kupunguza uhaba mkubwa wa wataalamu wa kada hiyo.
“Ajirini wahadhiri wenye damu changa, tusiwategemee wastaafu peke yao kuwa katika kada hii. Utegemezi wa wahadhiri wastaafu liwe jambo la mpito tu katika vyuo vyenye sifa,” Kikwete.
Hata hivyo, ushauri huo wa Rais Kikwete wa kutaka vyuo viajiri vijana zaidi umepokewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wahadhiri. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ProF. Jamidu Katima, alisema suala hilo lina sura mbili kwani wahadhiri wazee wamefanya mengi kama tafiti, machapisho na wamekaa muda mrefu katika taaluma tofauti na wahadhiri vijana.
“Upande wa pili ni kweli kuwa, ingawa wahadhiri wazee wamefanya mengi, wahadhiri vijana nao wanahitajika ili kuziba mianya ya uhaba iliyopo,” Prof. Katima.
Alisema wakati mwingine vyuo huona gharama kubwa kusomesha vijana, badala yake huwatumia wahadhiri ambao tayari wamestaafu.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Emmanuel Malya alisema ingawa wahadhiri vijana ni wazuri, ni wachache hapa nchini.
“Serikali iwekeze katika kuwasomesha maprofesa, ni gharama lakini ni vizuri kwa sababu kuna uhaba mkubwa wa vijana katika kada hii,” Dk Malya.
Alisema ni vigumu kuwapata wahadhiri vijana wenye shahada za uzamivu (PhD) na hata hao wenye shahada moja ni wachache wenye alama nzuri zinazohitajika katika kufundisha.
Hautopitwa na stori yoyote inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook