Mbunge wa Bariadi Andrew Chenge na mwenzake wa Sengerema Willium Ngeleja ni miongoni mwa vigogo waliolipa mamilioni ya shilingi kwa mamlaka ya kodi nchini ‘TRA’ kutokana na mgawo wa fedha zilizochotwa katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Habari kutoka ndani ya Wizara ya fedha zinasema wanufaika wachache akiwemo aliyekuwa Wsaziri wa nyumba na maendeleo ya Makazi Anna Tibaijuka na Mtendaji mkuu wa usajili na ufilisi ‘RITA‘ Philip Saliboko wamegoma kulipa kodi.
Wanufaika hao ambao walipokea mgawo huo kutoka kwa mkurugenzi wa VIP Engineering and Marketing James Rugemarila aliyepata mgawo wa dola 75 kutoka kwenye fedha zilizokuwemo kwenye akaunti hiyo na kuzigawa kwa watu mbalimbali kupitia akaunti zao zilizopo benki ya Mkomboziya Jijini Dar es salaam.
Hata hivyo Mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipa kodi wa TRA Richard Kayombo hakuwa tayari kuzungumzia akisema kuwa sheria haiwaruhusu kuzungumza suala hilo hadharani.
Baadhi ya walionufaika na mgawo huo wengi wao wameweza kulipa kodi hiyo akiwemo Chenge ambaye amelipa milioni 300 na Ngeleja ambaye amelipa milioni 10, Chenge alipata mgawo wa bilioni 1.6 na Ngeleja alipata mgawo wa milioni 40.
NIPASHE
Ni Takribani tangu sakata la uchotwaji wa fedha zaidi ya Sh. bilioni 200 katika akaunti ya Tegeta Escrow kutikisa nchi huku mawaziri wawili na mwanasheria mkuu wa serikali wakiondoka madarakani na katibu mkuu mmoja akichunguzwa,
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, amefichua kuwa wajumbe wote wa kamati hiyo wataadhibiwa vibaya kwenye majimbo yao kama njia ya kulipiza kisasi kutokana na kuwaumbua wote walionufaika na fedha hizo.
Katika mahojiano na kituo cha ITV kwenye kipindi cha Dakika 45, kilichorushwa jana usiku, Zitto amesema kuwa wakati PAC wakiendelea kuchambua ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) juu ya Escrow, mjumbe mmoja wa kamati hiyo aliitwa na ‘wakubwa’na kuelezwa kwamba akifika bungeni awageuke wenzake na aseme kuwa mgogoro wa ripoti ya Escrow iliandikwa kwa shinikizo la mfanyabiashara mmoja.
“Mmoja wa wajumbe wangu aliitwa kuombwa aingie bungeni aseme kwamba kuna mfanyabiashara mmoja mkubwa amewapa wajumbe wa PAC fedha ili watengeneze hiyo ripoti ya PAC,” Zitto.
Aliongeza kuwa mjumbe huyo alipokataa aliambiwa: “ Umekataa kutekeleza hili? Sasa tumetenga Sh. milioni 500 kwa kila jimbo kwa kila mjumbe wa PAC ili kuhakikisha hawarudi bungeni.”
Hata hivyo, Zitto hakutaka kumtaja mfanyabiashara huyo.
Zitto alifafanua kwamba maana ya fedha hizo ni kwamba watu hao watatafuta wagombea wa kupambana na waliokuwa wajumbe wa PAC kwa nguvu ya fedha ili wahakikishe wanakwama kutetea majimbo yao katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Aliongeza kuwa kitendo cha kutaja wanufaika wa Escrow wazi wazi, kama vile majaji, mawaziri na wengine wote alijua kuwa hawawezi kukubali jambo hilo lipite hivi hivi tu.
“Kuna watu wana fedha nyingi bwana. Kwa mfano IPTL kwa mwezi wanalipwa capacity charge Sh. bilioni nne,” alisema.
Wajumbe hao ni Zitto, Deo Filikunjombe, Desderius Mipata, Asha Jecha, Lucy Owenya, Ester Matiko, John Cheyo, Zaynabu Vulu, Ally Keissy, Zainab Kawawa, Kheri Ali Khamis, Faida Mohammed Bakar, Ismail Aden Rage na Modestus Kilufi.
NIPASHE
Wakati Serikali ikijiandaa kuwasilisha muswada wa Mahakama ya Kadhi katika mkutano wa 19 wa Bunge unaotarajia kuanza leo, Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila amefungua kesi ya madai Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, akipinga hatua hiyo.
Mtikila anapinga kuanzishwa Mahakama ya Kadhi, kwamba ni kinyume cha Katiba ya nchi.
Kadhalika, Mtikila ameiomba mahakama itoe amri kwamba wale walio kwenye mamlaka ya Serikali akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Dk. Mary Nagu; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira na wenzao watoe sababu kwa nini wasifungwe kifungo kisichopungua miaka mitano endapo watashindwa kujieleza.
Pia, Mtikila kupitia hati yake ya madai iliyopewa usajili namba 14 ya mwaka huu, ameomba Mahakama itoe amri vigogo hao kufungwa kifungo hicho kutokana na kuchezea Katiba ambayo ni sheria mama ya nchi.
Katika hati hiyo, Mtikila pia anaiomba, mahakama itoe amri kwamba Mahakama ya Kadhi na Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC), zitangazwe kuwa ni haramu nchini.
Pamoja na mambo mengine, Mchungaji Mtikila anadai kuwa hatua serikali kuandaa muswada wa Kiislamu na kuuwasilisha bungeni na kitendo cha Bunge kukubali badala ya kuukataa ni sawa na uhaini, kinachofanywa na wale walioupeleka muswada huo.
Anadai kuwa kitendo hicho ni sawa na uvunjifu mkubwa wa viapo vya viongozi hao. “Viapo ambavyo Pinda na wenzake waliapa wakati wa kushika madaraka ya umma vinakiuka ibara ya 19 ya katiba ya nchi inaosisitiza kwamba masuala ya dini na kuabudu yatakuwa ni ya mtu binafsi na kwamba uendeshaji wa mambo au taasisi za kidini hazitakuwa sehemu ya mamlaka ya nchi,” anaeleza katika madai yake.
Hati hiyo inaeleeza kuwa mamlaka ambazo zimepigwa marufuka na Katiba kujiingiza, kujihusisha au kuchezea mambo kama ya kadhi na uanachama wa taasisi za kidini au uanachama wa uislamu ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri Mkuu au viongozi wote wa kiserikali ambao baada ya kula viapo hujifunga kulinda katiba ya nchi na si vingevyo.
Mtikila anaendelea kueleza kupitia hati hiyo kwamba muswaada wa mahakama ya kadhi na uanachama wa OIC havikubaliki katika ardhi ya Tanzania kwa sababu zinabagua na ni ukiukaji mkubwa wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alieleza kuwa sababu nyingine ya kufungua kesi hiyo ni kwa ajili ya kuilinda katiba ya nchi kwamba ibara ya 26 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, inasema kwamba kila mtu ana haki kwa mujibu wa taratibu zilizoanishwa na kuchukua hatua za kisheria kwa lengo la kuhakikisha kwamba Katiba ya nchi inalindwa.
NIPASHE
Wasichana 2,003 wamezokimbia familia zao na kwenda kuishi katika kituo cha Masanga Wilaya ya Tarime mkoani Mara kwa hofu ya kukeketwa na wazazi wao.
Hayo yalibainishwa na Mlezi wa kituo hicho, Germaine Baibika, wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa kupinga ukeketaji ulioandaliwa na Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) uliowashirikisha wadau wa kupinga ukeketaji na ndoa za utotoni.
Baibika alisema takwimu hizo ni tangu mwaka 2008 na idadi hiyo ni tangu walipoanza kupokea wasichana wanaokimbia ukeketaji.
Alisema wasichana wengi wanaokimbilia kwenye kituo hicho wanatoka wilaya za Tarime, Serengeti, Rorya, Loliondo na wengine nchi jirani ya Kenya.
Alitaja changamoto wanazopata katika kupambana na ukeketaji kuwa ni upinzani mkali kutoka kwa viongozi wa kimila ambao wangependa kuona mila hizo zinadumishwa.
Alisema umaskini wa kupindukia kwenye baadhi ya kaya ndiyo husababisha kulazimika kukeketa watoto wao kwa matarajio kuwa watapata mahari watoto wao watakapoolewa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Watoto katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Benedict Misani, alisema wasichana na wanawake milioni 7.9 nchini wamekeketwa licha ya kuwapo sheria ambayo inazuia vitendo hivyo na kwamba hali hiyo inachangiwa na baadhi ya watendaji wa serikali kutokuwa tayari kumaliza tatizo hilo.
Alipongeza juhudi za wanaharakati binafsi ikiwamo CDF kwa kupinga ukeketaji na kuziomba asasi hizo kuendelea kushirikiana na serikali kubuni mikakati mipya ya kijamii itakayoleta suluhisho la kudumu kuhusiana na tatizo hilo.
NIPASHE
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeibuka na ushindi dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi wa marudio wa Serikali za Mitaa katika mtaa wa King’azi B, Kata ya Kwembe, jijini Dar es Salaam.
Uchaguzi huo uliofanyika juzi katika mazingira ya amani na utulivu, ulishirikisha wagombea wa nafasi ya mwenyekiti, wajumbe wa serikali ya mtaa na wa viti maalum kutoka vyama vya Chadema na CCM.
Akitangaza matokeo hayo, Msimamizi wa uchaguzi huo, George Lupia, alisema kuwa Chadema kimeshinda nafasi zote hizo dhidi ya wapinzani wake CCM na hivyo kuwa viongozi wa mtaa huo.
Msimamizi huyo alisema kuwa mgombea wa Chadema, Donath Mtemekele, alishinda kwa kupata kura 585 huku wa CCM, Daud Ngaliba, akipata kura 376 na kwamba kura 18 ziliharibika.
Lupia alisema wananchi ambao walikuwa wamejiandikisha katika daftari wa wapigakura walikuwa ni 1352, lakini waliojitokeza kupiga kura ni 979.
Mtaa wa huo ulirudia uchaguzi baada ya uchaguzi wa Desemba 14, mwaka jana kuvurugika na kuahirishwa mara mbili kutokana na sababu mbalimbali.
Uchaguzi huo ulivurugika kutokana na vurugu ambazo zinadaiwa kufanywa na wafuasi wa vyama hivyo ambavyo vilikuwa vinachuana kuongoza mtaa huo.
Katika uchaguzi huo wa mwaka jana, ilidaiwa kuwa mgombea wa nafasi wa mwenyekiti kupitia Chadema alikuwa ameshinda kwa kura 312 huku wa CCM akipata kura 207.
Kufuatia ushindi huo, Chadema kimesema kitawatumikia ipasavyo wananchi wa eneo hilo ili kuwaletea maendeleo.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema chama chao kimeupokea wa furaha ushindi huo akissema ukombozi umeanza kuonekana kutokana na wananchi kufanya uamuzi shahihi.
“Tumeupokea ushindi kwa furaha kwa mataokeo haya ni jinsi gani ukombozi umeanza kuonekana, wananchi wamemchagua kiongozi sahihi wananyemtaka kwa ridhaa yao,” Dk. Slaa.
MWANANCHI
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva amesema ofisi yake ilijaribu kuazima vifaa vya kielektroniki vya Biometric Voters Registration (BVR) katika nchi ya Kenya na Nigeria kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura, lakini nchi hizo zilikataa.
Uamuzi wa NEC wa kutaka kuazima vifaa hivyo ni kutokana na mchakato wa uandikishaji kukwama kwenda kama ulivyopangwa kutokana na BVR 250 zilizopo kutokuwa na uwezo wa kuandikisha wapiga kura wote nchini.
Kitendo hicho kinaweza kusababisha Kura ya Maoni iliyopangwa kufanyika Aprili 30 mwaka huu kushindikana kwani mpaka sasa ni mkoa wa Njombe pekee uandikishaji unaendelea kufanyika ambako utamalizika Aprili 12, 2015.
“Tulitaka kuazima Kenya lakini wakasema wanavitumia hata kama wamemaliza uchaguzi lakini mchakato wao wa uandikishaji unaendelea kutokana na kwamba watu wao wanapofikisha umri wa kuandikishwa wanawaingiza katika daftari lao,” alisema Jaji Lubuva na kuongeza:
“Tulikwenda Nigeria nako walitueleza wanazitumia. Kuazimana siyo jambo geni kwetu na huu ndiyo ukweli wake.”
Kuhusu mchakato wa uandikishaji mkoani Njombe alikoweka kambi alisema: “Uandikishaji huku unakwenda vizuri licha ya kauli mbalimbali na mimi nimekuwa nikiwahamasisha kujitokeza na tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa.”
Katika uchaguzi wa Ghana uliofanyika mwaka 2013 mfumo wa BVR ulitumika na kuonyesha mafanikio makubwa. Hata hivyo, Malawi iliukataa mfumo huo katika uchaguzi wa mwaka 2014 baada ya kuonyesha udhaifu mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 2005.
MWANANCHI
Jengo la ‘Block B’ la Hostel za Mabibo, za wanafunzi wa kike wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), jijini hapa limeungua kwa moto na kuteketeza vifaa na mali kadhaa za wanafunzi waliokuwa wakiishi kwenye jengo hilo.
Tukio hilo lililotokea leo majira ya 2:35 asubuhi linadaiwa kusababishwa na hitilafu ya umeme katika jingo hilo.
Makamu Mkuu wa UDSM, Prof. Rwekaza Mukandala aliyekuwa eneo la tukio akiahidi kubeba dhamana ya kushughulikia hasara ya mali, nyaraka na fedha kwa wanafunzi walioathiriwa na tukio hilo.
“Kwanza kuhusu vyeti vilivyoungua ,tutashughulikia vipatikane vyote.Pili tutashughulikia hata bajeti za kujikimu kwa wale walioathirika, lakini pia kuanzia leo wanafunzi wote ambao walikuwa kwenye jengo hilo watahamishiwa jengo lingine wakati huo uchunguzi ukifanyika kufahamu chanzo cha moto,” Prof. Mukandala.
Kwa upande wake, Kamanda wa Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alitoa tahadhari ya usalama kwa mali za wanafunzi walioathiriwa na tukio hilo huku akisisiza utulivu wakati uchunguzi wa chanzo hicho ukifanyika.
Taarifa kutoka miongoni mwa wanafunzi hao zimebainisha kuwa, wakati wa tukio hilo wanafunzi wawili wa kike waliruka kutoka gorofa ya pili mpaka chini na kujeruhiwa vibaya.
Askari wa Zima Moto walifika eneo la tukio hilo saa 3:45 asubuhi na kukuta moto ukiwa umeshapungua hatua iliyosababisha wanafunzi hao kuwashambulia huku wakiwazomea na kuwataka waondoke.
Viongozi wawili wa zima Moto, Omary Katonga kutoka Ilala na Mboke Msami wamesema changamoto kubwa iliyojitokeza ni kutopata taarifa mapema.
“Moto umetokea saa 2:35 asubuhi kwa nini watujulishe tena kupitia Tanesco saa moja baadaye, tumefika hapa kwa kutumia dakika 23, wanakosea kutulaumu ila kinachotakiwa ni taarifa mapema,” Katonga.
MTANZANIA
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro amewajibu maaskofu akisema Serikali haiko tayari kuona wananchi wanafundishwa jinsi ya kupiga kura kuhusu Katiba Inayopendekezwa.
Amesema ni muhimu wananchi waachwe waamue kwa utashi wao wenyewe.
Dk. Migiro amesema Serikali inaunga mkono tamko lililotolewa na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kuhusu mustakabali wa Katiba na si makundi ya watu na viongozi wa dini waanze kuingilia uamuzi wa wananchi.
Ametoa kauli hiyo siku tatu baada ya Jukwaa la Kikristo Tanzania kutoa tamko la kuwataka Wakristo wote Tanzania kujitokeza kwa wingi na kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kisha kuipinga Katiba mpya kwa kupiga kura ya hapana.
Waziri alikuwa akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, ambao walitaka kujua msimamo wa Serikali kuhusu mchakato wa Katiba Inayopendekezwa baada ya kukabidhi nakala ya Katiba hiyo kwa taasisi na wadau mbalimbali nchini.
Dk. Migiro alisema katu hakuna kiongozi mwenye mamlaka ya kumchagulia mtu namna ya kupiga kura kwa sababu kila Mtanzania ana akili timamu na ana uwezo wa kuamua kwa utashi wao.
Alisema wanapaswa kufanya uamuzi wao wenyewe bila ya kulazimishwa na kiongozi yeyote wa dini au siasa.
“Sisi tamko lile tumeliona, lakini tulishangazwa kuona viongozi wa dini wanakuwa sehemu ya kuwafundisha waumini wao jinsi ya kupiga kura katika Katiba Inayopendekezwa.
“Tumeshtushwa … tukasema kuwa wananchi ni watu makini ambao hawawezi kushawishiwa na mtu bali wanapaswa kufanya uamuzi kwa utashi wao wenyewe,” Dk. Migiro.
Akizungumza huku akinukuu kauli ya Kardinali Pengo, alisema kauli ile imetolewa na kiongozi makini mwenye kupenda maendeleo kwa Taifa lake.
“Naomba nimnukuu Kardinali Pendo katika kauli yake, alisema kuwa; ‘wananchi wapewe fursa ya kufanya uamuzi wao wenyewe bila ya kushinikizwa na mtu yeyote kwa sababu hata Mungu hawezi kukuamulia baadhi ya mambo unayotaka kufanya.”
HABARILEO
Tanzania inazidi kupiga hatua katika sekta ya afya, na sasa inatarajia kuachana na usafirishaji wa sampuli za magonjwa ya uambukizi mkali yenye virusi visababishavyo damu kutoka mwilini, ikiwemo ebola na dengue.
Hali hiyo inatokana na kuanza ujenzi wa maabara ya magonjwa hayo, unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Maabara ya kwanza ya magonjwa hayo, inajengwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, ambapo zaidi ya Sh milioni 109 zimeshatumika.
Maabara hiyo itakayoanza kutumika hivi karibuni, itakuwa imeboreshwa kutoka iliyokuwepo awali ya upimaji maambukizi ya kifua kikuu.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Steven Kebwe alisema ukarabati wa maabara hiyo, ulianza Februari mwaka huu na utakamilika mwishoni mwa mwezi huu baada ya mkandarasi kutia saini mkataba na Serikali Februari 6, mwaka huu akipewa wiki nne.
Alisema hayo baada ya kutembelea hospitali hiyo na kuzungumza na watumishi hivi karibuni. Dk Kebwe alisema maabara hiyo inatarajiwa kuanza kutumika kabla ya mwezi Julai mwaka huu, ambapo sekta ya afya itaingia katika mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na hivyo kusaidia urahisi wa upatikanaji wa huduma kwa kiwango cha juu.
Alisema kukamilika kwa maabara hiyo, kutapunguza maambukizi ya magonjwa ya milipuko kama vile dengue, ebola na homa ya bonde la ufa.
Pia, maabara hiyo itatumika kufanyia utafiti, kufundishia na vipimo kwa watu walioambukizwa na wasioambukizwa.
Hautopitwa na stori yoyote inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook