NIPASHE
Baadhi ya wafugaji wa vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Ruaha wilayani hapa Mkoa wa Mbeya, wamedai kupigwa na askari wa wanyamapori na kuwatoza kiwango kikubwa cha fedha kwa kosa la mifugo yao kuingia kwenye maeneo ya hifadhi hiyo.
Wakizungumza na waandishi wa habari wilayani hapo, wafugaji hao, walidai kuwa imekuwa kawaida kwa askari hao kukamata mifugo na kuwatoza faini kubwa na wakati mwingine kuwashambulia kwa vipigo.
Mmoja wa wafugaji hao, Igembe Mahola, Mkazi wa Kijiji cha Iyala, alidai hivi karibuni ng’ombe wake 143 walikamatwa na askari hao wa wanyamapori wakidaiwa kukutwa ndani ya hifadhi na alipofuatilia, alishushiwa kipigo kisha kutozwa faini ya Sh. milioni 9.
Mahola alidai kuwa kwenye stakabadhi yake, aliandikiwa kuwa amelipa faini ya Sh. milioni 5 badala ya Sh. milioni 9 alizoamriwa kulipa na askari hao.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Wilaya ya Mbarali, Makeresia Pawa, alisema askari hao wanatumia udhaifu wa serikali juu ya migogoro ya mipaka iliyopo kujinufaisha.
“Tumepaza sana sauti zetu sisi wafugaji na inaonekana serikali imekuwa ngumu kutuelewa katika hili hivyo basi tunaiomba kutusikiliza kilio hiki vinginevyo tutakuja na maazimio magumu sana, ”:-Pawa.
Akijibu malalamiko hayo, Mkuu wa Hifadhi ya Ruaha, Christopher Timbuka, alisema hajayapata ila anachofahamu askari hao kuendelea kutekeleza wajibu wao ili kuhakikisha hakuna mifugo inayoingia ndani ya hifadhi hiyo ili kutunza mazingira.
NIPASHE
Mtu mmoja ambaye anadaiwa kuwa kinara wa utapeli wa viwanja jijini Dar es Salaam (jina linahifadhiwa kwa sasa), leo anatarajiwa kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, kujibu tuhuma zinazomkabili.
Mtuhumiwa huyo ambaye aliwahi kufanyakazi katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, anadaiwa kutapeli zaidi ya viwanja 30, kikiwamo cha familia ya Mwalimu Julius Nyerere na cha Katibu Mkuu wa Wizara Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, pamoja na cha mwanamke mmoja ambaye alikuwa akifanya kazi Umoja wa Mataifa (UN).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, amethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.
Habari za ndani zinadai mtuhumiwa huyo,amekuwa akitapeli viwanja mbalimbali katika maeneo nyeti ya Mikocheni, Mbezi Beach na Oysterbay, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili kwa masharti ya jina lake lisiandikwe gazetini, wakili mmoja alisema kuna baadhi ya vigogo ambao wanamlinda na jambo la kushangaza amekuwa akipata hati kutoka Wizara ya Ardhi wakati siyo mmiliki halali wa viwanja hivyo.
“Kuna kiwanja amekidhulumu cha Mbezi Beach mmiliki kaenda kufungua kesi lakini akamtishia kumuua, yaani mwenye kiwanja hana amani na maisha yake na huyo mtu huwa anashirikiana na polisi,”:-
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Alphayo Kidata, alisema ni kweli mtuhumiwa huyo amekuwa akidhulumu viwanja vya watu na kwamba walikuwa wanakusanya taarifa zake kwa umakini ili kumfikisha kwenye vyombo vya dola.
NIPASHE
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ametoboa siri sababu za Rais Jakaya Kikwete kumhamisha Dk. Harrison Mwakyembe katika Wizara ya Uchukuzi kwenda Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Akizungumza juzi na mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Kyela, alisema Rais Kikwete alimhamisha Dk. Mwakyembe katika Wizara ya Uchukuzi kwa sababu anaifahamu vyema Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuwa alishawahi kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Masharika na pia mwanasheria.
“Dk. Mwakyembe amehamishiwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutokana na kuwa anaielewa vizuri na pia ni mwanasheria aliyebobea hivyo Rais Kikwete aliona atakuwa msaada mkubwa katika kuisaidia nchi,” :- Pinda
Hatua ya Waziri Mkuu Pinda kutoa ufafanuzi huo kulifuatia kuwapo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi walihoji kwanini Dk. Mwakyembe amehamishwa Wizara ya Uchukuzi ambayo aliimudu vyema kwa kudhibiti vitendo vya wizi hususani katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na upitishwaji wa dawa za kulevya katika viwanja vya ndege.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), walifanya mkutano Jijini Nairobi na Rais Kikwete alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa EAC huku Waziri Mwakyembe akichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa jumuiya hiyo.
NIPASHE
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), inakabiliwa na uhaba wa damu kwa kiasi kikubwa, hali inayosababisha kitengo cha damu kuhudumia wagonjwa wa dharura zaidi, kuliko walio na magonjwa sugu.
Kitengo cha damu hospitalini hapo, kimekuwa kikipokea maombi yapatayo 100 kwa siku, na uwezo wake ni kutoa chupa 50 hadi 65, sawa na asilimia 60.
Maombi hayo ya damu ni kutoka idara ya dharura, kwa ajili ya akina mama wajawazito, watoto waliopo kwenye matibabu ya saratani, pamoja na vyumba vya upasuaji.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja, Aminiel Aligaesha, alisema hali hiyo inatokana na mahitaji makubwa na ukusanyaji mdogo wa damu, ikiwamo mwamko mdogo wa jamii wa kuchangia damu.
“Hatuna damu ya kutosheleza kwa asilimia 100, hospitali hii ni ya Taifa, tunapokea wagonjwa wengi na mahitaji ni makubwa zaidi na tofauti na benki ya damu iliyopo,”:- Aligaesha.
Alisema kati ya maombi yote kwa siku, MNH hutoa chupa 50 za damu, kupitia kitengo cha ukusanyaji damu hospitalini hapo.
“Tunaendelea kuwasihi watu kuchangia damu ili kuweza kuokoa maisha ya wagonjwa wa dharura, ajali na wengineo, tunapendekeza kuwa turuhusiwe kwenda kufanya kampeni nje ya hospitali tuweze kuwasaidia wagonjwa zaidi na si kutegemea sana Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS),” aliongeza.
MWANANCHI
Msiba wa Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba jana uligeuka uwanja wa siasa, baada ya makada wa CCM wanaotajwa kugombea urais pamoja na wapambe wao kupigana vikumbo na kurushiana vijembe, ikiwa na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Ilikuwa kama walijipanga kwani kila mgombea aliyekuwa anafika katika msiba huo alionekana kuwa na wapambe waliompokea, kumpeleka kutoa pole kwa wafiwa na kumuonyesha eneo la kukaa.
Ukiacha kauli mbalimbali walizotoa kumwelezea marehemu Komba (61), wapambe wa wagombea hao walionekana mara kwa mara kuwa karibu nao wakizungumza, hali iliyoonyesha kuwa kila kundi lilitaka mgombea wao kuonyesha uwepo wake.
Wanaotajwa kuutaka urais ambao walihudhuria msiba wa mbunge huyo uliotokea juzi jioni ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, wote kutoka CCM, pamoja na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibroad Slaa.
Membe ndiyo alikuwa wa kwanza kufika nyumbani kwa marehemu eneo la Mbezi Tangi Bovu na baada ya muda aliwasili Rais Jakaya Kikwete na kukaa naye.
Mara baada ya Rais Kikwete kuondoka, Membe alilakiwa na kundi kubwa la makada wa CCM ambao mbali na kumsalimia walimvuta pembeni na kuomba kupiga naye picha huku wakisika wakisema kuwa “Tunataka kupiga picha na mheshimiwa rais”.
Watu hao ambao walikuwa wakiongozwa na Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage ambaye hata hivyo hakupiga picha na waziri huyo, walisema kuwa kama mambo yakienda vyema, Membe anaweza kuwa rais na hata alipokuwa akiondoka walimsindikiza hadi kwenye gari lake.
MWANANCHI
Kanisa la Pentekoste Tanzania Usharika wa Tandika, Manispaa ya Temeke limenusurika kuteketezwa kwa moto. Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita na mtuhumiwa alikamatwa na kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi Chang’ombe.
Kaimu Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Kamishna Msaidizi (ACP), Zacharia Sebastian alisema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani leo baada ya taratibu kukamilika.
Akizungumza na gazeti hili katika ofisi yake, ambako ndiko moto huo ulianzia, Askofu wa Kanisa Jimbo la Temeke, Raymond Noya alisema tukio hilo ni la kushangaza, kwani halikulenga kuiba mali zilizokuwamo kwenye ofisi hiyo.
“Hili siyo suala la uhuni…naona inaweza kuwa ni vita dhidi ya imani. Lengo lilikuwa ni kuchoma kanisa na siyo kuiba vilivyomo. Kama unavyoona hakuna kilichoguswa wala jaribio la kuvunja ama mlango au dirisha. Hili ni jaribio la pili kutokea,”:- Noya.
Kuhusu jaribio la kwanza alisema lilitokea Novemba mwaka jana, lakini hakukuwa na madhara makubwa na kesi ilifikishwa kituo cha polisi ingawa hadi leo haijafikishwa mahakamani kwa maelezo kuwa upelelezi bado unaendelea.
Noya alisema kwa miaka miwili iliyopita kumekuwa na matukio tofauti yanayokwaza huduma ya kanisa, kwani wakati mwingine wamekuwa wakirushiwa mawe wakati wa ibada.
“Kanisa lina mlinzi, lakini kuna wakati huwa anazidiwa. Tangu kanisa hili lilipoanzishwa mwaka 1997 ni miaka miwili tu iliyopita ndipo mambo yameanza kubadilika. Tumekuwa na ushirikiano mzuri na watu wanaotuzunguka kwa muda wote tuliokuwapo hapa,” alieleza.
Alphonce John, mkazi wa eneo lilipo kanisa alishangazwa na tukio hilo na kusema hakutegemea vitendo vya uharifu wa aina hiyo vinaweza kufanyika wakati huu.
MTANZANIA
Wakati Tume ya Maadili ya Utumishi wa Umma ikiendelea na mvutano wa sheria na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, amesema mbunge huyo alistahili kufungiwa kushiriki kwenye uongozi wa umma muda mrefu.
Zitto alisema tangu izuke kashfa ya rada ambayo pia Chenge alihusishwa, tume ya maadili ilipaswa kumuhoji na kumchukulia hatua kali za sheria.
“Chenge kwa mara ya pili sasa anaonekana kuwa ana makosa ya maadili. Kwenye rada taratibu kama hizi za sasa hazikufanyika. Ilipaswa zifanyike aeleze alipata wapi fedha alizoziita vijisenti, alizoweka huko kwenye visiwa vya Jersey.
Jambo hilo lilipita tu bila Baraza la Maadili kulifanyia kazi, wanachofanya sasa Baraza la Maadili kwenye Escrow ndiyo ilipaswa ifanyike kabla kiasi kwamba Chenge asingekuwa kwenye uongozi wa umma.
Katiba ipo wazi inasema mtu anaweza kupoteza ubunge kwa makosa ya maadili.
Zitto alisema kinachoendelea kwenye baraza hivi sasa ni funzo kubwa na kufumbua macho kwamba mfumo wa kushughulikia maadili upo isipokuwa haukuwezeshwa kufanya kazi.
Sasa tuuwezeshe uweze kushughulika na kesi za utovu wa maadili.
MTANZANIA
Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani cha Ubungo, (UBT), kilifunguliwa Desemba 6 mwaka 1999, lengo likiwa ni kutoa huduma nzuri kwa wasafiri na kuongeza mapato ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Baada ya kufunguliwa kwa kituo hicho, kati ya mwaka 2004 mpaka 2008, ziliibuliwa tuhuma mbalimbali za ufisadi zikiwamo upotevu wa mapato, zilizokuwa zikiihusu Kampuni ya Smart Holdings ya familia ya kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kingunge Ngombale Mwiru. Tuhuma hizo baadaye zilikanushwa na Serikali.
Tofauti na ilivyokusudiwa, mapato mengi yaliyokusanywa kwenye kituo hicho yaliishia kunufaisha watu wachache.
Machi 15 mwaka 2009, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliagiza ufanyike ukaguzi maalumu kwenye kituo hicho kutokana na tuhuma mbalimbali zilizokuwa zimeibuliwa.
Julai 28 mwaka 2009, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali wa wakati huo, Ludovick Utouh, alikabidhi ripoti yake kwa Waziri Mkuu ikieleza ukusanyaji mbaya wa mapato ikiwa ni pamoja na tuhuma za ubadhirifu wa mapato ndani ya kituo hicho cha mabasi.
Baada ya ripoti hiyo, Kampuni ya Smart Holding iliyokuwa ikikusanya mapato kwenye kituo hicho, ilisimamishwa na jukumu lake likachukuliwa na halmashauri ambayo iliweka watumishi wake kukusanya mapato.
Ili kubaini hali ya kituo hicho, uchunguzi umebaini matatizo mbalimbali yakiwamo ubadhirifu wa fedha unaofanywa na waliopewa majukumu ya kukusanya mapato.
Kwa kiasi kikubwa, kituo hicho kwa sasa kimefanywa kama mradi wa watu wachache wanaokusanya mamilioni ya fedha kila siku huku wananchi wanaokamuliwa fedha hizo, wakiwa hawana hata sehemu ya kujisitiri kwa jua ama mvua.
Katika kituo hicho, mabasi ya abiria takriban 400 hadi 650 huingia na kutoka kila siku na kila moja hutozwa ushuru wa Sh 2,000. Idadi hiyo inatofautiana kutokana na msimu wa biashara.
MTANZANIA
Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), ametangaza rasmi kwamba hatagombea tena ubunge wa jimbo hilo wakati wa uchaguzi mkuu mwaka huu.
Amesema ingawa alikuwa na nia ya kuendelea kuongoza jimbo hilo, amelazimika kuacha kwa kuwa baadhi ya viongozi wa chama chake wilayani Kasulu wanachafua jina lake bila sababu.
Machali alitangaza msimamo huo juzi mjini Kasulu alipohutubia mkutano wa hadhara.
“Kuna baadhi ya viongozi wachache wenye mawazo ya kijinga wanaotoka Jimbo la Kasulu Vijijini wanashirikiana na Diwani wa Kata ya Kasulu Mjini, Issack Rashid maarufu kama Mkemwema, kunitangaza kwamba nimechukua uamuzi huu kwa sababu Mkemwema anataka kugombea ubunge katika jimbo langu.
“Hiyo siyo kweli, ugomvi wangu mkubwa na hao watu umekuja kwa sababu ninapiga vita ufisadi na mafisadi waliopo Wilaya ya Kasulu wanaojali masilahi yao badala ya wananchi.
“Mimi sipendi usumbufu na wananchi ingawa wengine wanatembea huku na huko wakisema ‘Machali hatujali’… hivi mnafikiri atatokea mbunge atakayemaliza shida zenu zote?
“Kama atatokea huyo mbunge basi njooni mniombe silaha yangu mnipige risasi nife kwa sababu naamini mbunge huyo hayupo na hatatokea katika dunia hii.
“Watu wananipiga vita bila sababu kwa vile napingana nao, yaani wanataka na mimi nipige madili kama wao, hiyo haiwezekani kwa sababu siko tayari kuchafua jina langu”-Machali.
Hata hivyo, baada ya mbunge huyo kutoa kauli hiyo, alikumbana na upinzani mkali baada ya baadhi ya wananchi kupingana naye huku baadhi wakilia.
Baadhi ya wananchi hao walisikika wakisema hawako tayari kukubaliana na mbunge huyo kwa kuwa wanaridhishwa utendaji kazi wake.
HABARILEO
Wazazi wa mtoto mwenye umri wa miaka 10 aliyeozwa kwa siri wilayani Bahi, katika Mkoa wa Dodoma, wanafikishwa mahakamani leo kujibu mashitaka yanayowakabili.
Mtoto huyo aliokolewa kutoka kwenye ndoa aliyokuwa amelipiwa mahari ya mbuzi 12 na Sh 100,000. Kijana, Joshua Mnamba (25) aliyekuwa amemuoa, inadaiwa alifikishwa mahakamani Februari 24, mwaka huu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime alithibitisha wazazi wa mtoto huyo ambao walikuwa wakishikiliwa na polisi, Stephano Mkuta (baba) na Juliana Gideon (mama), wanafikishwa mahakamani leo kujibu mashitaka ya kuozesha mtoto.
Inadaiwa mtoto huyo aliozwa kwa shinikizo la mama na bibi yake kabla ya kuokolewa kutoka kwenye ndoa hiyo na kuishi nyumbani kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Bety Mkwasa.
Taarifa kutoka kwa majirani zinadai, kijana aliyemuoa mtoto huyo, awali, alikuwa akidai binti huyo ni ndugu yake.
Hata hivyo, ilidaiwa majirani wa kijana huyo, katika kijiji cha Ibihwa, walitilia shaka kutokana na vilio vya mtoto huyo nyakati za usiku ambaye amedumu kwa mwanaume huyo kwa wiki mbili kabla ya kuokolewa.
“Cha kushangaza walikuwa wakiishi peke yao kama mume na mke,” alisema mmoja wa majirani.
Akizungumza na mwandishi akiwa nyumbani kwa Mkwasa ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, mtoto huyo alisema hajui kusoma wala kuandika kwani wazazi wake hawakumpeleka shule na alikuwa akikaa nyumbani kulea wadogo zake.
“Sijapelekwa shuleni…nina wadogo zangu sita, mimi ndio mkubwa na wazazi wangu na bibi ndio walikuwa wakitaka niolewe lakini nilikuwa nikikataa… mimi ni mdogo,” alisema.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram, na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook