NIPASHE
Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani, imewataja vigogo wanaohodhi maeneo makubwa ya ardhi bila ya kuyaendeleza na kuwapa siku 90 kuhakikisha wanayaendeleza, kinyume chake yatachukuliwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Tatu Suleiman, ilisema vigogo hao walinunua mashamba katika eneo hilo na kuyaacha muda mrefu bila kuyaendeleza akiwamo mke wa Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Mama Ester Sumaye ambaye anamiliki mashamba mawili yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 240 eneo la Misufini, Kibaha vijijini.
Taarifa hiyo inawataja watu wengine maarufu ambao wameshindwa kuyaendeleza mashamba hayo kuwa ni, Phillipo Marmo ambaye ni Balozi wa Tanzania Ujerumani anayemiliki shambamaeneo ya Kikongo, Nicodemus Banduka ambaye ni mkuu wa mkoa mstaafu wa mikoa ya Pwani, Iringa na Mtwara anayemiliki shamba eneo la Vikuge ambalo alilipata mwaka 2000 na Kipi Warioba aliyewahi kuteuliwa kugombea Ubunge Jimbo la Kawe ambaye anamiliki eneo Mperamumbi lenye ukubwa wa heka 4000.
Taarifa hiyo inaonyesha kuwa watu wengi walichukua mashamba katika eneo hilo kuanzia miaka ya 1986 na kushindwa kuyaendeleza na kusababisha kuwa mapori hali iliyopelekea halmashauri hiyo kufuata sheria na kanuni zinazohusiana na umiliki wa ardhi.
Kufuatia mashamba hayo kutelekezwa, halmashuri ya wilaya hiyo inapanga kuwasilisha taarifa hiyo kwa wizara husika ili miliki zake zifutwe endapo wahusika watashindwa kuyaendeleza kwa muda waliopewa.
Tatu, alisema mwaka jana waliwataka watu wote waliochukua mashamba hayo kuyaendeleza baada ya kufanyiwa uhakiki na baadhi ya watu walijitokeza kuyaendeleza, lakini watu zaidi ya 40 hawajitokeza.
“Kutokana na kukahidi kuyaendeleza mashamba hayo, tumeshapeleka majina ya wamiliki Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wizara imetutaka tutoe tena siku 90 kama hawatatekeleza kwa kipindi hicho, watajua nini cha kufanya,’’ alisema.
Gazeti hili lilipowasiliana na Waziri Mkuu wa zamani, Sumaye kwa njia ya simu ili kuzungumzia taarifa za mkewe kushindwa kuyaendeleza mashamba hayo kwa kipindi kirefu, alisema hana taarifa zozote za mkewe kushindwa kuyaendeleza mashamba hayo anayomiliki.
‘‘Wewe ndiyo nakusikia, sisi hatujaliona hilo tangazo, wala mke wangu hana hizo taarifa ila baadaye tutakapoziona tutakupigia simu tuwasiliane,’’ Sumaye.
NIPASHE
Marais wa nchi za ukanda wa Kati, wamewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kuangalia miradi 23 ya miundombinu iliyopitishwa kwa ajili ya utekelezaji wa reli, barabara na bandari huku wakitaka ushiriki wa sekta binafsi.
Wamewataka wawekezaji hao kujiwekeza na kujenga miradi hiyo kwa ubia na sekta binafsi za ndani na nje.
Wito huo uliyotolewa jana na marais wa Tanzania, Rwanda, Burundi, na wawakilishi wa Uganda, Kenya na DRC katika mkutano wa wawekezaji na wafanyabiashara wa ndani na nje, kujadili namna ya kushirikiana katika uboreshaji wa miradi iliyopitishwa kwa ajili ya utekelezaji.
Akimkaribisha Rais Paul Kagame wa Rwanda kufungua mkutano huo, Rais Jakaya Kikwete , alisema Rwanda na Tanzania mwaka 2003 zilisaini makubaliano ya ujenzi wa reli ya Dar Isaka hadi Rwanda, lakini kutokana na umuhimu wake Burundi iliunga mkono na baadaye Benki ya Afrika iligharimia upembuzi yakinifu na sasa mradi huo ni miongoni mwa miradi ya ukanda wa kati ya kipaumbele.
“Nawahakikishia wawekezaji na wafanyabiashara mliopo hapa, ukichagua kuwekeza katika ukanda wa kati, hakuna cha kupoteza bali utapata faida nyingi,” alibainisha.
Katika mjadala wa maswali na majibu kutoka kwa wawekezaji na wafanyabiashara kwa wakuu hao wa nchi, baadhi ya wawekezaji aliwaomba viongozi hao kuangalia kwa mapana uwepo wa kitega uchumi kimoja kama Bandari ya Dar es Salaam ambayo inatumiwa na nchi zote kuingia fedha katika uboreshaji na uimarishaji.
Kwa upande mwingine, Rais Kikwete, alisema suala la Bandari ya Dar es Salaam inayotumiwa na nchi zote litaangaliwa na wakuu wa nchi husika, hasa katika utashi wa kisiasa, ili usiachwe kuwa mzigo kwa Tanzania huku manufaa yakiwa kwa wote.
Aidha, Rais Kikwete alisema moja ya mipango mikubwa ya serikali ya Tanzania ni kuwekeza katika reli ili watu binafsi waruhusiwe kuwa na treni zao kama ilivyo kwa usafiri wa mabasi kuwa barabara ni za serikali, lakini wasafirishaji ni sekta binafsi.
“Tunataka iwe kama uwanja wa ndege kwamba ndege ya nchi yoyote na mtu binafsi inaweza kutua alimradi ilipe gharama za kutua na kufuata sheria nyingine…Uganda wana treni zao nasi tunafungua milango kwa watu binafsi kuwekeza kwenye treni,” alisema.
NIPASHE
Rais Jakaya Kikwete, amewateua wabunge wawili wapya wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku ikiwa imesalia miezi minne kabla ya Bunge hilo kuvunjwa.
Walioteuliwa ni Dk. Grace Khwaya Puja na Innocent Sebba, ambao uteuzi wao umeanza Machi 20, mwaka huu.
“Rais amefanya uteuzi huu kwa mamlaka aliyopewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 66 (I) (e), ambapo amepewa mamlaka ya kuteua wabunge wasiozidi 10,” ilieleza sehemu ya taarifa ya iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, jijini Dar es Salaam jana.
Uteuzi huo umekamilisha idadi ya wabunge, ambao Rais Kikwete amepewa kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo kikatiba.
Wabunge, ambao wameshateuliwa na Rais ni pamoja na Prof. Makame Mnyaa Mbarawa; Prof. Sospeter Muhongo na Dk. Asha-Rose Migiro.
Wengine ni Janet Mbene (Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara); Saada Salum Mkuya (Waziri wa Fedha), Zakhia Meghji, Shamsi Vuai Nahodha na James Mbatia (Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi).
Uteuzi wa wabunge hao wapya uliofanywa na Rais Kikwete kipindi hiki, utawafanya wafanye kazi ya ubunge kwa miezi minne tu kabla ya Bunge la 10, lililoanza Novemba, 2010, kuvunjwa Julai, mwaka huu.
Kwa sasa Bunge hilo linaendelea na mkutano wake wa 19, mjini Dodoma kabla ya kuhitimisha wa 20 na wa mwisho, unaotarajiwa kufanyika kwa miezi miwili mfululizo, kuanzia ama mwezi ujao au Mei, mwaka huu.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Elimu na Ushirikiano wa Kimataifa wa Bunge, Jossey Mwakasyuka, alifafanua jana kuwa, jumla ya mikutano ya Bunge moja huwa 20 katika kipindi cha miaka mitano ya uhai wake.
NIPASHE
Siku moja baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kusitisha makundi yanayokwenda kumshawishi kugombea urais, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, amempongeza kwa kutii agizo la chama hicho.
Nape amesema hatua hiyo ya Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli ni nzuri kwa kuamua kusitisha makundi kwenda kumshawishi agombee urais, ambayo kwa siku chache mfululizo yalikwenda nyumbani kwake Monduli na mjini Dodoma kwa nia hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana akiwa katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulahman Kinana wilayani Same, Kilimanjaro, Nape alisema anampongeza Lowassa kwa kuwa amekubali kuheshimu kanuni, taratibu na Katiba ya chama ambayo ndiyo inatakiwa kufuatwa na kila mwanachama wa CCM.
Jumanne wiki hii, Nape alimuonya Lowassa kujiepusha na makundi hayo kwa kuwa kufanya hivyo ni kukiuka kanuni na taratibu za chama na kwamba, hali hiyo inamkosesha sifa ya kuteuliwa kugombea urais kupitia CCM.
Nape alisema walimtaka Lowassa, ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM azuie makundi yanayokwenda nyumbani kwake kwa ajili ya kumtaka agombee urais kwani kilichokuwa kinafanyika ni kuanza kampeni kabla ya wakati.
“Kilichokuwa kinafanyika ni kuanza kampeni kabla ya wakati na kwa mujibu wa chama chetu ni makosa, maana anakiuka taratibu na kanuni za chama. Hatuwezi kukaa kimya wakati kanuni zinavunjwa wazi, hivyo nimpongeze Lowassa kwa kutii agizo la chama,” Nape.
Kuhusu shutuma kuwa kauli anazozitoa siyo za chama bali zake binafsi, Nape alisema yeye ndiye msemaji pekee wa chama na hakuna msemaji mwingine, hivyo kauli zinazotolewa ni za chama na siyo zake.
“Kanuni na taratibu ambazo nazisimamia zipo miaka mingi kabla ya mimi kuzaliwa. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM nchi nzima niko peke yangu, hivyo lazima nisimamie misingi ya itikadi pamoja na kanuni na katiba ya chama chetu. Kwa nafasi yangu siwezi kukaa kimya wakati kuna watu wanakosea,” Nape.
Akizungumzia kuhusu wapambe wa makada wanaotaka urais, Nape aliwataka kuwa makini wasije wakawaharibia sifa wagombea wao.
“Ni vizuri wataka urais wakawa makini na ushauri kutoka kwa wapambe wao kwani wanaweza kuwasababishia kukosa sifa ndani ya chama, nawashauri wote wanaotaka kugombea urais kupitia CCM kutowasikiliza wapambe wao kwa kila wanachoambiwa, maana kuna ushauri mwingine unaweza kuwakosesha sifa za kugombea urais,” Nape.
Alisisitiza kwamba, kwenye hilo si kwa wapambe wa Lowassa tu, bali ni kwa wapambe wote waliopo nyuma ya makada wanaotaka kugombea urais mwaka huu.
“Ni muhimu kwa makada wote kuhakikisha wanaheshimu kanuni, taratibu na miiko ya chama ili wawe salama, kinyume cha hapo watajipoteza sifa,” alisisitiza Nape.
Zaidi ya vijana 100 wakiwamo wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara, wamekutana mjini Moshi na kutoa tamko linalodai kwamba, iwapo Lowassa atapoteza sifa za kugombea urais, CCM kijiandae kisaikolojia kwa sababu kinaweza kupasuka na kushindwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Vijana hao kutoka Jumuiya za Vyuo Vikuu vya Kanda ya Kaskazini na wengine kutoka sekta binafsi, walitoa angalizo hilo jana mjini Moshi kwa waandishi wa habari, ikiwa ni siku moja tangu Lowassa ajibu kauli ya Nape aliyoitoa Jumanne akidai hawezi kuzuia mafuriko kwa mkono.
MWANANCHI
Wakati wenyeviti wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) pamoja na kamati zake za kitaalamu wanakutana Zanzibar kutafuta suluhu kuhusu mgawanyo nafasi za kugombea katika uchaguzi mkuu ujao, kuna uwezekano mkubwa vyama hivyo kuteua mgombea urais kutoka Chadema.
Tovuti hii inaweza kuripoti kwa uhakika kuwa uwezekano huo unatokana na vigezo vinavyotumiwa na vyama hivyo kusimamisha mgombea mmoja kwa kila jimbo na kwenye nafasi ya urais ambavyo vinaipa Chadema nafasi hiyo dhidi ya vyama vingine katika umoja huo ambavyo ni CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
Vigezo hivyo ni matokeo ya uchaguzi 2010, idadi ya madiwani kwa kila chama, matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Desemba mwaka jana, mtandao wa chama nchini na nguvu ya mgombea iwapo Chadema kitamsimamisha katibu mkuu wake, Dk Willibrod Slaa kwa mara ya pili.
Taarifa zilizolifikia Mwananchi kutoka ndani ya kamati ya ufundi ya Ukawa zinasema pamoja na kuwapo mvutano katika baadhi majimbo Tanzania Bara, kwa upande wa Zanzibar hakuna tatizo hilo, jambo linaloipa CUF nafasi ya moja kwa moja kwenye ubunge, uwakilishi na hata urais wa visiwa hivyo.
Kwa mujibu wa habari hizo, nafasi nzuri ya CUF kupita moja kwa moja Zanzibar bila ushindani ndani ya Ukawa, inatoa fursa kwa upande wa Bara, kwa vyama vilivyosalia kupitishwa kuwania urais wa Muungano.
Hata hivyo, kwa vigezo vilivyotajwa hapo juu, Chadema ndiyo inakuwa na nafasi isiyo na kipingamizi kutokana na rekodi vyama vilivyosalia Bara.
Katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, Chadema kilimsimamisha Dk Slaa na aliibuka wa pili baada ya Rais Jakaya Kikwete akiwa na kura 2,271,941 (asilimia 26.34) akifuatiwa na Profesa Ibrahim Lipumba aliyepata kura 695,667 (asilimia 8.06) na Hashim Rungwe wa NCCR-Mageuzi aliyepata kura 26,388 (asilimia 0.31). NLD haikusimamisha mgombea urais.
Kwa upande wa majimbo yaliyotokana na uchaguzi wa 2010, Chadema kiliongoza kikiwa na wabunge 24 (wote kutoka Bara), CUF 23 (wawili kutoka Bara, 21 Zanzibar) na NCCR-Mageuzi wanne (wote wa Bara).
Katika rekodi za uchaguzi wa mitaa zilitolewa na Tamisemi kabla ya chaguzi za marudio, Chadema ilipata mitaa 980, ikifuatiwa na CUF (mitaa 266), NCCR Mageuzi (28) na NLD mtaa mmoja. Kwa upande wa vijiji, Chadema kilishinda vijiji 1,754, CUF (516), NCCR-Mageuzi (67) na NLD vijiji viwili.
Hata kwa upande wa vitongoji Chadema kiliviongoza vyama hivyo kwa kupata vijiji 9,145 kikifuatiwa na CUF (2,561), NCCR-Mageuzi (339) na NLD vitongoji viwili.
MWANANCHI
Mvutano mkali uliibuka jana bungeni wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha Muswada wa Takwimu wa mwaka 2013, baada ya wabunge kuupinga.
Muswada huo una kipengele kinachotoa adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela na faini isiyopungua Sh10 milioni kwa mtu au chombo cha habari kitakachofanya makosa ya kutoa takwimu zisizokuwa sahihi.
Wabunge hao waliufananisha muswada huo na miswada miwili ya habari ya mwaka 2015 ambayo itawasilishwa bungeni Jumanne chini ya hati ya dharura kwa usiri uliopo na mpango wa kuiwasilisha bila wadau kushirikishwa.
Awali, muswada wa Takwimu uliwasilishwa kwenye mkutano wa 17 wa Bunge uliofanyika Novemba mwaka jana na wabunge wakapinga vifungu vinavyobana waandishi wa habari kuhusu eneo la takwimu, ndipo Serikali ilipoamua kuutoa kwa maelezo kuwa inakwenda kuurekebisha hadi ilipourejesha jana na ukapitishwa kwa mbinde.
Jana, Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha muswada huo, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alihoji juu ya kifungu hicho kinachotoa adhabu kali na Serikali kujibu kuwa imeshakifanyia marekebisho.
Hata hivyo, Mnyika hakukubaliana na maelezo hayo, bali alisema kifungu hicho hakijafanyiwa marekebisho yoyote na Serikali na adhabu bado inaendelea kuwa kali.
Mnyika aliungwa mkono na mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya aliyehoji, “Iweje Serikali iweke kinga kwa mtumishi wa Serikali anayetoa taarifa zisizo sahihi lakini ikaacha kuweka kwa mwandishi anayepewa taarifa hizo zisizo sahihi na ofisa huyo wa Serikali?”
Maelezo ya Bulaya yalimfanya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju kusimama na kusema kwa kifupi kuwa “mwandishi atakwenda kujieleza mahakamani au polisi.”
Kabla ya kuondolewa bungeni Novemba 2014 muswada huo pamoja na mambo mengine, ulikuwa ukipendekeza faini ya Sh10 milioni au kifungo cha mwaka mmoja jela au vyote kwa chombo cha habari kitakachotoa taarifa za kitakwimu za uongo au zenye upotoshaji.
“Mtu yeyote, kwa kujifanya anatimiza majukumu yake, iwapo anapata au anaomba kupatiwa taarifa ambayo haijaidhinishwa kuipata na kuichapisha au kuisambaza atakuwa amefanya kosa ambalo adhabu yake ni kifungo kisichopungua miezi 12 au faini isiyopungua shilingi milioni mbili au vyote kwa pamoja,” ilisema ibara ya 37 (d) cha muswada huo.
MWANANCHI
Matumizi ya mitandao ya kijamii kwa sasa ndiyo habari ya mjini, Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaotumia mitandao ya kijamii sehemu mbalimbali duniani.
Hii inatokana na wengi kutumia simu za kisasa maarufu kama smartphone ambazo zina uwezo mkubwa wa mawasiliano ya intaneti.
Inakadiliwa kuwa kwa sasa mtu mmoja kati ya watu wanne duniani kote, anatumia mojawapo ya mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, Instagram na WhatsApps.
Takwimu zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya watumiaji wa mitandao hii, ni vijana wenye umri chini ya miaka 30. Na wengi hutumia simu za mkononi zenye mtandao wa intaneti na wengine hutumia kompyuta kutembelea mitandao hiyo.
Pamoja na faida kadhaa za matumizi ya mitandao hiyo, baadhi ya watafiti wa maswala ya afya ya jamii wanabainisha kuwa matumizi ya mitandao hii yana athari kwa afya ya kisaikolojia na ubora wa maisha kwa watumiaji.
Jambo la kuvutia ni kwamba watafiti wamegundua kuwa watu wengi wanaotumia mitandao ya kijamii hawana utulivu wa kihisia na wengi wanakabiliwa na wasiwasi.
Katika utafiti ulioongozwa na Dar Meshi wa Chuo Kikuu cha Freie cha Ujerumani, inaonekana kuwa watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii wanapata uraibu fulani. Uraibu huo ni wa kutaka kuendelea kuwasiliana na hata kuona fahari kuzidi kuongeza idadi ya wale anaowasiliana nao.
Wengi wao huhangaika ili kuinua kiwango chao cha kujisikia vizuri kihisia.
Mwaka 2012, shirika linalojihusisha na maswala ya hali ya wasiwasi nchini Uingereza (Anxiety UK) lilifanya utafiti kuhusu athari za matumizi ya mitandao ya kijamii na kubaini kuwa asilimia 53 ya washiriki wa utafiti huo walikuwa wamebadilika kitabia kutokana na matumizi ya mitandao ya kijamii.
Na asilimia 51 ya watu wote waliokiri kuwa walibadilika kitabia. Mabadiliko yao yalikuwa yameegemea kuwa hasi kuliko chanya.
Utafiti huo pia ulibaini kuwa asilimia 66 ya washiriki wa utafiti walikosa usingizi na utulivu wa kihisia kila walipomaliza kutumia mitandao ya kijamii.
Asilimia 55 walisema kuwa walihisi wasiwasi na kukosa furaha pale waliposhindwa kupata mtandao ili kuunganishwa na mitandao ya kijamii wanayoipenda.
Akizungumzia matokeo ya utafiti huo, Dk Linda Blair, mtaalamu wa saikolojia anasema kuwa watu wengi hupata athari za kisaikolojia kwa sababu wanashindwa kudhibiti matakwa yao,” anasema akisisitiza: afikiri jambo kubwa ni watu kuanza kutawaliwa na teknolojia, badala ya wao kuitawala,” Dk Blair.
MTANZANIA
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,limemtaka Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kujisalimisha polisi kwa tuhuma za kumkashifu Kiongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Hatua hiyo ya polisi imekuja baada ya jeshi hilo kupokea malalamiko, ambapo inadaiwa Mchungaji Gwajima alitoa lugha ya kashfa dhidi ya Kardinali Pengo ambaye alipinga tamko lililotolewa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) la kuipigia kura ya Hapana Katiba Inayopendekezwa.
Taarifa iliyotolewa janana Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi, Kamishna Suleiman Kova, imemtaka Mchungaji Gwajima kujisalimisha haraka katika Kituo cha Polisi cha Kati kwenye Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda kwa mahojiano kuhusu tuhuma za kashfa na matusi.
Kova alisema jeshi hilo limepokea malalamiko ya kukashifiwa na kutukanwa hadharani Kardinali Pengo.
Alisema matusi hayo yameonekana kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii ya WhatsApp na mingineyo, ambapo kuna sauti iliyorekodiwa na picha za video zikimuonyesha Mchungaji Gwajima akimkashifu na kumtukana kwa maneno makali Kardinali Pengo katika hali ambayo pia imewaudhi watu wengine.
Kova alisema baada ya tukio hilo, juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanyika ili kumpata Mchungaji Gwajima bila mafanikio.
“Ni muhimu sana kwa Mchungaji Josephat Gwajima aripoti mwenyewe badala ya kutafutwa au kukamatwa ili ajibu tuhuma hizo kutokana na nafasi yake katika jamii.“Jalada la uchunguzi limefunguliwa na upelelezi wa shauri hili unaendelea ili sheria ichukue mkondo wake,” aKamanda Kova.
Hivi karibuni sauti iliyorekodiwa na picha za video zilionekana katika mitandao ya kijamii ambazo zilikuwa zikimtukana Kardinali Pengo.
Sehemu ya maneno hayo ambayo yanamwonyesha Gwajima akizungumza kupitia mitandao ya kijamii ya WhatsApp na Facebook ni;“Pengo unaaibisha kama mtoto mdogo aliyevaa pampasi aliyebebwa na mama yake, Pengo ni mjinga asiyefaa, juzi aliokoka kwa kula chakula chake ovyo ovyo, sijui kala maharage ya wapi?
“Pengo awe Mkatoliki amejishushia heshima yake mwenyewe, aache uaskofu awe mkulima wa kawaida, hafai mzee ametudhalilisha kabisa na amewageuka maaskofu wote kwa kile walichopatana .
“Amewadhalilisha maaskofu wote, amedhalilisha CCT, amedhalilisha CPCT, pia amewadhalilisha Watanzania wote.”.
UHURU
Rais Jakaya Kikwete, amesema siku chache zijazo mizigo inayosafirishwa kwenda nchi za Afrika Mashariki na Kati kutoka Bandari ya Dar es Salaam, itabebwa kwa treni na kusafirishwa kwa reli na kuachana na usafirishaji mizigo kwa malori.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa treni za mizigo kwenda nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Uganda, Burundi na Rwanda, alisema kwa sasa mizigo itasafirishwa kuanzia makao makuu ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kwenda nchi husika.
Alisema kwa sasa wataalamu wa TRL wamebuni utaratibu mzuri wa mabehewa yanayotoka nchi moja kwenda nyingine moja kwa moja tofauti na utaratibu wa awali wa kukata bogi ili kushusha mizigo.
“Pamoja na treni za nje ya nchi, lakini kutakuwa na treni za kubeba mizigo ya ndani…utaratibu huu utapunguza ucheleweshaji wa mizigo uliokuwapo, hivyo nchi zenye bandari kuona kama adhabu kusafirisha mizigo kupitia Tanzania,” alisema.
Rais Kikwete alisema mkutano uliowaleta pamoja marais wa nchi za Afrika Mashariki na Kati una lengo la kuimarisha miundombinu ya barabara, reli na bandari ili Tanzania itimize wajibu wake wa kuzisaidia nchi zisizo na bahari.
Rais alieleza kuwa alikwenda Burundi na kuzungumza na wafanyabiashara ambao kilio chao kikubwa kilikuwa ni ucheleweshaji wa mizigo unaoanzia bandarini na vikwazo vingine zikiwamo barabarani kiasi cha nchi hiyo kujilaumu kupakana na Tanzania.
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, alisema kwa sasa inachukua siku mbili kwa mizigo kufika Kigoma kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Burundi, DRC na Rwanda na kwamba kwa sasa kutakuwa na mabehewa kati ya 15 na 20 kwa kila safari.
Alisema mizigo ya kwenda Rwanda itashushwa Bandari Kavu ya Isaka na ya Uganda itashushwa feri ya Mwanza na kuvushwa kwa meli kwa haraka.
“Utaratibu huu ni endelevu, utakuwa kila mfanyabiashara atafuatilia mzigo wake ulipo na atapata kwa muda mfupi…tunawashukuru mafundi wa Tanzania na Malaysia ambao wamezifufua Injini za miaka 40 iliyopita kufanya kazi upya,” alisema.
Rais wa Burundi, Pierre Nkrunzinza, aliishukuru Tanzania kwa jitihada za kuisaidia nchi hiyo katika masuala ya kupata Uhuru, kumaliza vita ya wenyewe kwa wenyewe na sasa kuwa na amani ya kudumu.
Alisema wakati wa vita Warundi milioni moja walipata hifadhi ya muda Tanzania na kwamba kwa sasa wanazisaidia nchi zenye vita zikiwamo Afrika ya Kati na Sudan Kusini.
Ni halali yako kupata kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>> twitter Insta Facebook.