NIPASHE
Wakati hali ya kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, ikiwa tete kwa siku mbili mfululizo, Jeshi la Polisi na waumini wa Askofu huyo wanadaiwa kuvutana hospitali inayofaa kumpa matibabu.
Askofu Gwajima, alizimia ghafla juzi majira ya saa 2: 45 usiku akiwa kwenye chumba cha mahojiano katika Kituo cha Polisi Kati, baada ya kutuhumiwa kumkashifu na kumtukana kiongozi wa kanisa la Katoliki Jimbo kuu la Dar es Salaam, Mwadhama kadinali Polycap Pengo.
Hata hivyo, mara baada ya kutokea tukio hilo, Askofu huyo alichukuliwa akiwa katika hali ya kuzirai na kuanza kuzungushwa katika hospitali tofauti wakati waumini walitaka apelekwe Hospitali ya TMJ Mikocheni, Jeshi la polisi lilitaka apelekwe hospitali za Jeshi na Muhimbili.
Tukio hilo lilianza majira ya saa 3:00 usiku alipopoteza fahamu hadi majira ya saa 8:00 usiku ambapo walikubaliana apelekwe Hospitali ya TMJ ambako anaendelea kupatiwa matibabu.
Baada ya kuwasili kituoni hapo majira ya saa 8:15 alasiri, alikwenda moja kwa moja katika chumba maalumu kilichoandaliwa kwa ajili ya kuhojiwa tuhuma zinazomkabili.
Ilichukua muda wa saa saba ndani ya chumba hicho, na ilipofikia saa 1.05 usiku, hali ya Askofu Gwajima ilibadilika ghafla.
Baadhi ya askari na viongozi wenzake walionekana kujaribu kutumia njia mbalimbali ikiwamo kumpeleka chooni ili kumrudisha hali yake ya kawaida, lakini ilishindikana.
Aliporudi ndani, aliishiwa nguvu na kupoteza fahamu kitu ambacho kilizusha taharuki ndani ya ukumbi huo.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho kilieleza, hali yake ilibadilika ghafla baada ya kuanza kuhojiwa kuhusu mali anazomiliki ikiwamo helikopta aliyoinunua hivi karibuni.
Aidha mambo mengine aliyotakiwa kueleza ni uhusiano wake na wanasiasa mashuhuri pamoja na akaunti anazomiliki na njia anazopata pesa.
NIPASHE
Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara, David Kafulia ameanika kasoro zilizojitokeza wakati wa manunuzi ya mabehewa 25 ya mizigo, ambazo zimo ndani ya ripoti ya awali ya uchunguzi uliofanywa na Mamlaka ya Udhibiti na Manunuzi (PPRA) ambayo pia inazungumzia ununuzi wa mabehewa 274.
Kwa mujibu wa Kafulila, kasoro za msingi katika manunuzi zilizobainishwa kwenye ripoti hiyo ni namna zabuni ilivyotangazwa na hata upangaji wa viwango ulikuwa na mapungufu hivyo kuathiri ubora.
Kafulila aliwaeleza waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa, amelazimika kuzungumzia kasoro hizo kwa sababu leo anasafiri kuelekea Dubai na kuwa serikali iliyopo madarakani, imebaki hatua za lala salama.
Alisema uchunguzi wa PPRA uliangalia iwapo taratibu za manunuzi zilizoainishwa katika sheria na kanuni za manunuzi kama zilizingatiwa na kubainika kuwa mchakato wa ununuzi wa mabehewa uliofanywa na Shirika la Reli Tanzania (TRL), ulitumia fedha iliyotengwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2012/13.
Alisema ripoti hiyo inaonyesha kuwa, kanuni na taratibu chini ya sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 ilifutwa na Sheria namba 7 ya mwaka 2011 ambazo ndizo zilitumika katika manunuzi hayo.
Pia alisema uchunguzi huo umebaini kuwa nyaraka za zabuni zote mbili zinaelekea kuwa kabla ya kutoa tuzo ya mkataba kwa mzabuni atayeonekana kukidhi masharti yaliyoainishwa kwenye nyaraka za zabuni, mzabuni huyo atatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa kina ambao TRL haukuufanya.
“TRL waliingia mkataba na kampuni ya Hindusthan Engineering and Industries ya India bila kujiridhisha kuhusu uwezo wake, hivyo ilikiuka kifungu cha 53 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma na matakwa ya nyaraka za zabuni ambazo zilitaka uchunguzi ufanyike,” alisema.
Kafulila alisema PPRA ilibaini kuwa zabuni hizo zilitangazwa kwenye magazeti ya ndani pekee bila kuyahusisha na yale ya kimataifa kama inavyoelekezwa kwenye nyongeza ya kwanza ya sheria ya manunuzi.
Kadhalika, alisema uchunguzi ulibaini kuwa mikataba yote miwili ilisainiwa Machi 21, mwaka juzi ambapo kwa mujibu wa mikataba hiyo kifungu namba 3, kinaonyesha mabehewa yalitakiwa kuwasilishwa katika kipindi cha miezi 12 baada ya kusainiwa mikataba lakini TRL walichelewa.
Alisema PPRA ilibaini kuwa, menejimenti ya TRL haikuwa makini kushughulikia maombi ya kuongezewa muda yaliyokuwa yanawasilishwa na kampuni hiyo.
“Katika mkataba wa zabuni namba PA/113/2012-13/ME/G/OE/014 kampuni hii iliwasilisha maombi Juni 13, mwaka jana kuomba kuongezewa muda wa mkataba hadi Desemba 14, mwaka huo, TRL iliyaidhinisha Juni 16 na muda wa mkataba uliongezwa hadi Septemba 30,” alisema.
NIPASHE
Mwakilishi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Kanda ya Kati, Charles Ambele, amesema uzimaji wa mitambo ya analojia ya utangazaji wa televisheni mkoani Kigoma, utafanyika Machi 31, mwaka huu.
Ambele aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waaandishi wa habari kuwa vigezo vinavyotumika kuzima mitambo ya analojia ni pamoja na kuwepo utangazaji wa mifumo ya analojia pamoja na kidijitali kwenye eneo husika, upatikanaji ving’amuzi na uwepo wa chaneli tano za kitaifa kwenye mfumo huo mpya.
Alisema elimu ya umma kupitia njia mbalimbali kuhusu kuhamia katika teknolojia ya mfumo wa utangazaji wa dijitali imekuwa ikitolewa kwa kiwango cha kuridhisha. Matangazo ya dijitali yamewafikia watu asilimia zaidi ya 20 kati ya asilimia 24 waliyokuwa wanapata matangazo ya televisheni ya analojia.
Aidha alisema utaratibu wa kuzima mitambo ya analojia utakuwa kwa maeneo yenye matangazo ya dijitali tu. Maeneo ambayo hayana miundombinu ya dijitali hayatazimwa kwa sasa hadi yapate dijitali.
Alisema mabadiliko hayo hayahusu matangazo kwa njia ya utangazaji wa satelaiti, waya, kebo na redio. “Tunawataka wananchi Mji wa Kigoma wasizitupe Tv zao za analojia bali wanunue ving’amuzi ili kupata matangazo ya dijitali”.
Ambele alisema Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeagiza watoa huduma za usambazaji wa ving’amuzi waliyoko Mkoa wa Kigoma, kuhakikisha kuwa kuna ving’amuzi vya kutosha.
Aidha, alisema serikali inatarajia kupata ushirikiano wa karibu kutoka kwa wadau wa sekta ya utangazaji na wananchi kwa ujumla katika kipindi cha uzimaji wa mitambo ya utangazaji wa televisheni wa mfumo wa analojia hapa ili kufanikisha zoezi hili.
Alisema kulingana na ratiba iliyotolewa na serikali Februari 2014 awamu ya pili ya uzimaji wa mitambo ya analojia ulianza kwenye miji ya Singida na Tabora, wakati ambapo miji mingine iliyofuata katika uzimaji wa mitambo ya analojia ambayo ni Musoma, Bukoba na Morogoro,
Kahama na Songea ilihusuka katika uzinduzi wa mitambo ya dijitali ikizingatiwa kuwa haikuwa ya matangazo ya televisheni ya mfumo wa analojia.
NIPASHE
Baraza la Maadili ya Umma, linatarajia kuwasilisha mapendekezo yake kwa Rais Jakaya Kikwete baada ya kuwahoji viongozi waliohusishwa kwenye sakata la Tegeta Escrow linahusu uchotwaji wa Sh. bilioni 300, wiki mbili zijazo.
Fedha hizo zilitolewa kama mgawo kwa viongozi mbali mbali na mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing, James Rugemalira, aliyekuwa mmoja wa wanahisa wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania (IPTL).
Baadhi ya viongozi wa umma waliopata mgawo huo na kuhojiwa na Baraza hilo ni pamoja na Mbunge wa Muleba Kusini, Prof. Anna Tibaijuka ambaye alipokea Sh bilioni 1.6 kutoka kwa mkurugenzi wa VIP Engineering iliyokuwa ikimiliki asilimia 30 ya hisa za IPTL.
Wengine ni Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja aliyejinyakulia zaidi ya Sh. milioni 40.4 na Mkurugenzi Mdhibiti Uchumi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Dk. James Benedict Diu aliyepokea mgawo wa zaidi ya Sh. milioni 80.8.
Mwingine ni Kigogo wa Ikulu (Mnikulu), Shaban Gurumo, ambaye alipata mgawo wa Sh. milioni 80.8.
Watuhumiwa ambao walikimbilia mahakamani ni pamoja na mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge ambaye kwenye mgao huo aliingiziwa kiasi cha fedha kama cha Tibaijuka kwenye akaunti yake.
Mwingine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usajili Uzazi na Vifo (Rita), Philip Saliboko aliyejipatia Sh. milioni 40.4.
Alisema uchambuzi huo unafanyika chini ya Mwenyekiti wa Baraza la Maadili Jaji Mstaafu na Balozi Hamis Msumi akisaidiana na wajumbe wawili.
Alisema timu hiyo hadi juzi ilikuwa ikiendelea kuchambua kesi zilizosikilizwa mwezi uliopita na baraza hilo .
MWANANCHI
Wakati Rais Jakaya Kikwete akisema msimamo wa Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) wa kuwataka waumini wao kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa ni wa hasira pia usiokuwa na tija kwa maendeleo ya Taifa, baadhi ya maaskofu wameshikilia msimamo huo.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa kamati ya amani ya Mkoa wa Dar es Salaam iliyoshirikisha wajumbe kutoka mikoa mbalimbali nchini unaowajumuisha viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo akilenga kuzungumzia tamko hilo la TCF walilolitoa Machi 12, mwaka huu.
Katika tamko hilo lililosainiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Daniel Awet liliwataka waumini wake kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura na kuipigia kura ya hapana Katiba hiyo.
Jukwaa hilo lilitaja sababu mbili za uamuzi wake huo kuwa ni Muswada wa Mahakama ya Kadhi kukiuka misingi ya Taifa kuwa na Serikali isiyo na dini na Kura ya Maoni kusababisha mgawanyiko.
“Hivyo basi, Jukwaa linawataka waumini wake wote wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, waisome Katiba Inayopendekezwa na kushiriki kikamilifu vipindi vya elimu juu ya Katiba Inayopendekezwa na kisha wajitokeze kwa wingi kupiga kura ya hapana,” lilisema tamko hilo.
Katika hotuba yake iliyodumu kwa saa 1.16, Rais Kikwete alianza kwa kuwaomba radhi viongozi hao kwa kuchelewa kwa akisema alikuwa na majukumu mengi. Mkutano huo ulikuwa uanze saa 3.00 asubuhi lakini Rais Kikwete alifika saa 6.30 mchana.
Alisema “Taifa linapitia hali isiyokuwa ya kawaida, tusipokuwa makini kuidhibiti itakuwa ni tatizo, ni kazi kubwa inayohitaji moyo, uvumilivu na viongozi wenye kujali masilahi ya Taifa.”
“Mwelekeo wa mambo hauhitaji uwe bingwa kujua hali hairidhishi sana na kama hatutachukua hatua hatuwezi kufika na tutasababisha uvunjifu wa amani za kidini na moto wake ni mkali sana,” aliongeza Rais Kikwete aliyekuwa akizungumza kwa umakini na taratibu.
Kuhusu tamko la Jukwaa la Wakristo, Rais Kikwete alisema wakati Taifa likisubiri kuona mchakato wa Katiba unakwenda hatua za mwisho kumekuwapo na matamko kadhaa ambayo hayakumfurahisha.
“Nimeyasoma matamko hayo yote kwa umakini, imenishangaza, imenisikitisha na kunihuzunisha. Siamini kwa nini wamefikia huko kwa kuunga au kutokuunga mkono,” alisema Rais Kikwete aliyekuwa akizungumza kwa sauti ya chini wakati wote wa hotuba yake.
“Kinachonisumbua ni kuipa sura na mtazamo wa kidini Katiba Inayopendekezwa, kama ingekuwa inakinzana na uhuru wa kuabudu hapo ingekuwa sawa lakini ibara ya 41 inatambua uhuru wa kuabudu na kuitangaza dini, sasa katika mazingira hayo kuwaeleza waumini kuikataa inanipa tabu sana,” aliongeza.
MWANANCHI
Mbunge wa Pangani (CCM), Saleh Pamba amezilipua wizara tatu kwa kutumia fedha zaidi ya bajeti iliyotengewa ikiwamo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambayo ilitengewa Sh35 bilioni lakini ikatumia Sh154 bilioni.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo jana, wakati akichangia mjadala wa muswada wa Sheria ya Bajeti wa mwaka 2014 iliyopitishwa na Bunge jana.
Wizara nyingine alizozitaja ni Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Nishati na Madini.
Katika mjadala huo wabunge wengine waliopata nafasi ya kuchangia muswada huo wameitaka Serikali ijipange upya na kuja na mikakati thabiti ya kujiongezea mapato ikiwa ni pamoja na kuwabana wafanyabiashara wakubwa walipe kodi ili nchi iache kutegemea wahisani.
Walisema nidhamu ya matumizi ya bajeti kwa Serikali hairidhishi kutokana na ukweli kuwa, taasisi nyingi pamoja na wizara zimekuwa zikitumia fedha bila kujali uzio ulioweka na Bunge (budget fence).
Hata hivyo, Pamba ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti alisema kabla ya mwaka haujaisha wizara hiyo ilitumia Sh154 bilioni kwa safari.
Alisema Wizara ya Ujenzi kwenye bajeti yake ya mwaka 2014/15 ilitengewa Sh445 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara lakini hadi sasa wizara hiyo imevuka kiwango hicho na ina madeni ya Sh998 bilioni.
Wizara ya Nishati, Pamba alisema katika mwaka wa fedha wa 2014/15 walitengewa Sh20 bilioni kwa ajili ya kununulia mafuta machafu ili kuendesha mtambo wa kuzalisha umeme wa IPTL lakini hadi sasa bado hawajamaliza mwaka huo wa fedha, tayari wameshatumia Sh400 bilioni.
Juzi Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, wakati akiwasilisha muswada huo alisema mambo muhimu yaliyozingatiwa ni kubainisha majukumu kati ya Serikali na Bunge ya kiutendaji na usimamizi katika mfumo wa uandaaji na utekelezaji wa bajeti.
“Kuweka misingi ya bajeti katika maeneo makuu matatu ambayo ni mipango, mapato na matumizi ya Serikali. Kurasimisha kisheria mzunguko wa bajeti.” alisema.
Alisema mambo mengine yanayozingatiwa katika muswada huo ni kutambua kisheria majukumu ya kibajeti ya Kamati ya Bunge ya masuala ya bajeti na Ofisi ya Bunge.
Pia alisema jambo jingine ni kuitambua kisheria kamati ya kitaifa ya uandaaji mwongozo wa mipango na bajeti.
MWANANCHI
Nyaraka nyeti za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zilizokuwa zimehifadhiwa katika Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu za Taifa, zimeibwa na mmoja wa watuhumiwa ni ofisa mwandamizi wa Ubalozi mdogo wa Omani uliopo Zanzibar.
Akiwasilisha ripoti ya Kamati Teule ya kuchunguza upotevu wa nyaraka za serikali katika Baraza la Wawakilishi, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mahamoud Mohammed Mussa alisema tukio la wizi huo lilianza kujulikana kuanza Julai mwaka 2013 na Baraza kulazimika kuunda kamati ya uchunguzi.
Mahamoud alisema nyaraka hizo zilikuwa zimehifadhiwa katika chumba maalumu na kuhifadhiwa katika masanduki lakini watu walifanikiwa kula njama za kuiiba nyaraka hizo kwa kuwatumia baadhi ya wafanyakzi wa Taasisi hiyo.
Aliwambi Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wezi hao walitumia mbinu mbalimbali ikiwemo ushawishi wa fedha na zawadi za vyakula zikiwemo tende wakati mpango wa kuibiwa nyaraka hizo ukiendelea kufanyika kwa siri kubwa kabla ya kufanikiwa.
Mahamoud alisema miongoni mwa nyaraka zilizoibiwa ni pamoja na nyaraka za kumbukumbu za Utawala wa Sultani Sayydid barghash Bin Said kabla ya Mapinduzi na waraka uliyotumika kupinga marufuku biashara ya Utumwa kufanyika Zanzibar mwaka 1873 pamoja na kumbukumbu za ujio wa wamisionari Zanzibar ambao walifanya kazi ya kueneza ukiristo Afrika Mashariki.
Hata hivyo alisema kwamba baadaya Kamati kufanya uchunguzi umegundua mpango wa wizi wa nyaraka hizo umeratibiwa na Ofisa Mwandamizi wa Ubalozi wa Omani Humoud Abdallal Rashid na hatua za kumkamta na kumfugulia mashitaka zimekwama kutokana na kuwa na kinga ya kutoshitakiwa ya Kidiplomasia.
Alisema kwamba Humoud kabla ya kufanikisha wizi wa nyaraka hizo alikwa akienda kila mara akiwa na vizawadi vya vyakula na kujenga uhusiano mkubwa na watendaji wa Taasisi hiyo kwa madhumuni ya kuendeleza hifadhi za kumbukumbu visiwani humo.
Aidha alisema pamoja ofisa huyo wa ubalozi kufungulikiwa kesi katika Kituo cha Polisi Mazizini Jeshi la Polisi limekwama kumkamata kutokan na mkataba wa Vienna.
wa kidiplomasia wa mwaka 1961 na sheria namba tano ya kinga na fursa 1986 kuweka kinga ya wanadiplomasia kukamatwa na kufunguliwa mashitaka.
Mohamoud alisema kwamba Uchunguzi pia umegunduwa Waziri mwenye na Kazi na Utawala Haroun ali Suleiman amelidaganya Baraza la Wawakilishi (BLW) kutokana na kauli yake aliyotoa kuwa Humoud hakuwa ofisa mwanadamizi wa ubalozi bali alikuja Zanzibar kama mfanyakazi kufanikisha shughuli za ukarabati wa Jengo moja la historia visiwani humo.
MWANANCHI
Wakati alipoingia madarakani, Rais Jakaya Kikwete alieleza mara kwa mara dhamira yake ya kutenganisha biashara na siasa na kwamba angeunda sheria ya kuzuia jambo hilo, lakini hali inaonekana kuwa tofauti ndani ya chama chake cha CCM, ambacho wafanyabiashara wanazidi kufurika kwa mgongo wa makamanda wa vijana.
Kama ilivyo kawaida ya chama hicho wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) katika ngazi za wilaya na mikoa, huteua makada wa CCM kuwa makamanda, ambao baadhi huchukua nafasi hizo ili kujijengea mazingira mazuri ya kugombea ubunge, lakini wanaopewa wengi ni wale wenye uwezo wa kifedha na hasa wafanyabiashara.
Taarifa zilizokusanywa na gazeti hili katika mikoa mbalimbali, makamanda wengi walioteuliwa ni wafanyabiashara.
Miongoni mwa makamanda ni mfanyabiashara maarufu Kilimanjaro, Seleman Mfinanga anayemiliki vitega uchumi kadhaa, vikiwamo vituo vya kuuza mafuta.
Kabla ya kuwa Kamanda Kilimanjaro, alikuwa akishikilia wadhifa Wilaya ya Mwanga.
Kamanda wa UVCCM Mkoa wa Dodoma ni Haidel Gulamali, ambaye pia ni mlezi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Dodoma.
Kiongozi huyo aliyewahi kuwa mchumi wa CCM Mkoa wa Dodoma kati ya mwaka 2007 na 2012 ni wakala wa usambazaji sukari. Pia ni Mkurugenzi wa Kiwanda cha Magodoro Asili.
Kamanda wa vijana wa Mkoa wa Tanga ni Omari Abdallah Kigoda, Mbunge wa Jimbo la Handeni na Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko. Kamanda msaidizi wa mkoa huo ni Mohamed Salim anayemiliki Kampuni ya Mabasi ya Ratco.
Mkoani Iringa hali siyo tofauti, kwani kamanda wa Vijana wa CCM mkoa ni mfanyabiashara maarufu na Mkurugenzi wa Kampuni ya Asas, Salim Abri.
HABARILEO
Rais Jakaya Kikwete amefafanua msimamo wa Serikali katika mjadala unaoendelea wa Mahakama ya Kadhi, na kuweka wazi kuwa Serikali haina mpango wa kuianzisha, wala kuiendesha.
Mbali na hiyo, Rais Kikwete ambaye jana alizungumza na Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini mkoani Dar es Salaam, pia alielezea kusikitishwa kwake na tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania, lililowaelekeza waumini wao kupigia Katiba Inayopendekezwa kura ya Hapana.
Mahakama ya Kadhi Akifafanua suala la Mahakama ya Kadhi, Rais Kikwete alisema Serikali ina msimamo wa mambo mawili katika mahakama hiyo. Kwanza, alisema Serikali haina mpango wa kuianzisha na kuiweka katika Katiba na pili, haihusiki kuiendesha na badala yake, Waislamu wenyewe ndio watakaoiendesha.
Alisema kimsingi, mahakama hiyo ilikuwepo kabla ya Uhuru na kinachotakiwa kuzungumzwa ndani ya Bunge, ni Sheria ya Kutambua Uamuzi Unaofanywa na Kadhi.
Alifafanua zaidi kuwa Mahakama hiyo ya Kadhi, haihusiki na mambo ya jinai, isipokuwa mambo ya kijamii ikiwemo talaka, mirathi na mengine ya aina hiyo. Alitoa mfano wa Sheria ya Kiislamu, iliyokuwepo tangu zamani, ambayo inatambua chombo hicho na kusisitiza kuwa kinazungumzwa, ni uamuzi unaofanywa na Kadhi utambulike tu.
Katika mfano huo, alisema Muislamu ukigombana na mke wake, kuna mabaraza ya usuluhishi ambayo huyo mwanamke atapaswa kwenda, ila wakishindwa na ataomba talaka ambayo inaidhinishwa na Kadhi, ambaye ndiye msajili wa vyeti vya ndoa kwa Waislmau.
Baada ya kutoa ufafanuzi huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Shehe Alhad Musa, alimshukuru Rais Kikwete kwa ufafanuzi alioutoa na kusema Wakristo na Waislamu siku zote ni wamoja na wataendelea kuishi kwa amani, furaha na ushirikiano.
Katika hilo, Shehe Alhad alinukuu Biblia katika Kitabu cha Mathayo tano, mstari wa 25, ambao unasema; “Patana na mshitaki wako, mngali njiani, asije akakupeleka kwa Kadhi na Kadhi akakukabidhi kwa polisi na polisi akakutupa korokoroni”
HABARILEO
Nchi za bara la Afrika zimeendelea kulilia kiti cha uwakilishi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) ili ziweze kujiwakilisha vyema katika kuzungumzia matatizo yao kuliko ilivyo sasa ambapo nchi hizo zinasemewa pasipo uwakilishi wake.
Kilio hicho kilitolewa jana na mwakilishi wa vijana kutoka nchi ya Niger katika kongamano linalofanyika mkoani Arusha la kuzungumzia mambo mbalimbali, zikiwemo fursa za ajira na mengineyo kwa vijana wa nchi za bara la Afrika.
Kufuatia kilio hicho, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alipotolea tamko jambo hilo na kuiomba nchi ya China ambayo ni mwanachama katika baraza hilo na rafiki wa nchi za Afrika kufikisha kilio hicho kwa nchi zingine wanachama.
Membe alisema mchakato wa maombi ya uanachama katika baraza hilo ulianza muda mrefu, lakini kumekuwa na vikwazo mbalimbali kwa nchi za Afrika, jambo ambalo limekuwa likisababisha mikwamo lakini hata hivyo nchi hizo hazijakata tamaa na kwamba zinaendelea kuomba.
Alisema awali lilikuwepo ombi la kupatiwa jambo nafasi mbili za uwakilishi kwa nchi mbili za Afrika, lakini bado imeonekana kuwa ngumu lakini bado wameendelea kuwasilisha maombi hayo japo kwa hata nafasi moja ili kuweza kusemewa mambo yao sawa sawa.
Alitaja moja ya kikwazo kikubwa kwa nchi hizo za Afrika kuwa ni lazima ziwe zinatumia nyuklia ambapo suala hilo ni gumu kwa nchi hizo za Afrika lini waliwasilisha ombi la kuruhusiwa kutumia na kutengeneza nyuklia ili kuweza kumudu kuingia katika baraza hilo lakini hadi sasa maombi hayo hayajajibiwa.
Alisema kinachofanyika kwa sasa katika baraza hilo si sawa kwa kuwa baraza limekuwa likitumia muda mwingi kujadili masuala ya nchi 54 za bara la Afrika huku likikosa majibu sahihi kutoka kwa nchi za bara hilo kutokana na kukosa uwakilishi wa nchi hizo.
Alisema zipo taarifa kuwa baraza hilo liliahidi kutoa nafasi hiyo ya uwakilishi wa nchi za Afrika kuwa mzunguko ili kutoa nafasi kwa nchi hizo lakini bado hata ahadi hiyo haijatekelezwa hadi sasa pasipo na maelezo yoyote.
Ni halali yako kupata kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>> twitter Insta Facebook