NIPASHE
Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, amejibu tuhuma zilizoelekezwa kwake na Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja, kwamba naye amekuwa akipokea misaada mbalimbali kwa matumizi binafsi kuwa ni upuuzi.
Zitto alijibu tuhuma hizo jana kupitia ukurasa wake wa Facebook, ikiwa ni siku moja baada ya Ngeleja kumtuhumu na kueleza kuwa tuhuma hizo ni za kipuuzi na kwamba ameshawahi kuzijibu huko nyuma na kuziita ni siasa za majitaka.
“Tuhuma zote hizo zimeshawahi kutolewa huko nyuma, hazina msingi wowote na zilikuwa siasa za majitaka, hata hivyo zimekuwa zikijirudia rudia kwa malengo maalumu wanayoyajua wanaotoa tuhuma hizo”.
“Watuhumiwa wa ufisadi wa Escrow hawajazoea kuona taasisi za maadili zikifanya kazi kwa namna ilivyo sasa, hivyo wanajaribu na wataendelea kubwabwaja na kuhangaika ikiwamo kutaka kila mtu aonekane ni mtuhumiwa kama wao.”
“Ndiyo maana Ngeleja ametaja msururu wa watu akiwamo mfanyabiashara kwamba huwapa fedha wabunge bila kuwapo chembe ya ushahidi, hivyo narudia kutamka kwamba ninataka uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo ufanyike mara moja, wenye ushahidi wapeleke katika vyombo vya uchunguzi na niitwe mbele ya Baraza la Maadili kujieleza,” Zitto.
Aidha, Zitto aliunga mkono kazi iliyofanywa na Baraza la Maadili, alieleza kazi hiyo ilipaswa kuwa imefanywa kwa muda mrefu sasa kwa kashfa mbalimbali zilizowahi kuwapata viongozi, kama vile rada, rushwa katika manunuzi ya mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya umeme, kujipatia mikopo katika taasisi za umma bila kulipa na kujilimbilikizia mali tofauti na kipato.
Zitto aliiomba Sekretarieti ya Maadili izichukulie kwa uzito tuhuma za Ngeleje dhidi yake, kwani kwa mujibu wa sheria na kanuni za utumishi wa umma yanapaswa yafanyiwe uchunguzi.
Akijitetea juzi kwenye Baraza la Maadili, Ngeleja alikiri kupata mgawo wa Sh. bilioni 40.2 kutoka kwa mfanyabiashara James Rugemalila wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd na kudai kuwa wabunge wamekuwa wakifadhiliwa na wafanyabiashara na mmoja wa wabunge walionufaika na misaada ya fedha za wafadhili, ni Zitto, ambaye kisheria ni mtumishi wa umma.
NIPASHE
Taifa limekumbwa na msiba mkubwa, baada ya watu 38 kufa na wengine zaidi ya 82 kujeruhiwa vibaya, baada ya kuangukiwa na nyumba zilizobomolewa na mvua kubwa ya mawe iliyonyesha usiku wa kuamkia jana ikiambatana na kimbunga, katika kijiji cha Mwakata, kata ya Isaka, wilayani hapa, mkoa wa Shinyanga.
Kufuatia maafa hayo, Rais Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za rambirambi na pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ali Nasoro Rufunga, kuomboleza vifo vya watu 38 na pole kwa wengine 82 waliojeruhiwa.
“Nimepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya watu 38 waliopoteza maisha na wengine 82 waliojeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama kwa matibabu baada ya nyumba zao kusombwa kabisa na maji kutokana na mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo mkali kunyesha,”.
Rais Kikwete katika salamu zake kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, alisema msiba huo siyo wa wananchi wa Shinyanga pekee, bali ni wa Taifa zima ambalo limepoteza nguvukazi muhimu kwa maendeleo yake na ustawi wa jamii.
Aliwaomba wafiwa wote wawe na moyo wa uvumilivu, utulivu na subira wakati huu wa majonzi makubwa kwao wanapoomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao na wasisahau ukweli kwamba kazi ya Mungu haina makosa.
Aidha, aliwahakikishia wafiwa wote kuwa binafsi yuko pamoja nao katika kipindi chote cha kuomboleza msiba huo mkubwa kwao na kwa Taifa.
Maafa hayo yalitokana na mvua kubwa ya mawe iliyonyesha ikiambatana na upepo mkali na hivyo kuathiri watu 3,500.
Alivitaja vijiji vilivyoathirika kuwa ni, Makata ambako kaya 350 zimeathiriwa, kijiji cha Ngumbi, kaya 100 zimeathirika na katika kijiji cha Magung’hwa, kaya 50 zimeathiriwa.
Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, akizungumzia tukio hilo, alisema idadi ya watu waliokufa wengi wao ni watoto ambao walisombwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua hizo baada ya maji kujaa ndani ya nyumba na kubomoa nyingine.
Kamugisha alisema idadi hiyo inaweza kuongezeka kutokana na waokoaji kuendelea kufukua vifusi vya nyumba zilizobomoka.
Alisema hadi sasa majina ya waliokufa hayajafahamika kutokana na kuendelea kwa kazi ya uokoaji.
“Tunaendelea na uokoaji na kufukua miili ya watu pamoja na madhara mengine yaliyopo, idadi ya watu waliokufa inaweza kuongezeka… Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Shinyanga itakutana baadaye ili kutathmini maafa hayo pamoja na kujua msaada upi unahitajika kwa waathirika,” Kamugisha.
Alisema mvua hiyo ilianza kunyesha saa 4:00 usiku wa kuamkia jana na kudumu kwa saa kadhaa na kusababisha maafa hayo.
NIPASHE
Meneja Miradi ya umeme ya Kinyerezi, Simon Jilima, amesema mtambo wa Kinyerezi 1 unaojengwa na kampuni ya Yakobsen Elektro ya Norway unatarajia kukamilika mapema Juni mwaka huu.
Jilima aliyasema hayo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyofanya ziara katika mtambo huo ili kujionea maendeleo ya ujenzi wake. Kamati hiyo imeanza ziara ya kutembelea miradi ya umeme iliyopo katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Singida, Arusha na Kilimanjaro pamoja na kuzungumza na wadau wa madini aina ya tanzanite katika mkoa wa Manyara.
Jilima alisema kwa sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 80 na kufafanua kuwa kazi inayofanyika kwa sasa ni kumalizia utandazaji wa nyaya, ufungaji wa mabomba ya maji na gesi pamoja na ujenzi wa barabara za ndani.
Alisema ofisi kwa ajili ya watumishi pamoja na karakana kwa ajili ya kuhifadhia mitambo imekamilika.
Jilima alisema mpaka sasa serikali imelipa kiasi cha Dola za Marekani milioni 167.2 na kuongeza kuwa kiasi cha Dola za Marekani milioni 15 kinatarajiwa kumaliziwa kabla ya kukamilika kwa mradi.
Jilima alieleza kuwa awali changamoto kubwa ilikuwa ni ukamilishwaji wa mradi wa bomba la gesi ili waanze kutumia gesi hiyo katika kuzalisha umeme, lakini kutokana na kasi ya mradi huo kuwa ya kuridhisha, wana imani kuwa gesi itaanza kuzalishwa mapema kabla ya kukamilika kwa mtambo wa Kinyerezi 1
“Ndugu wajumbe, awali tulikuwa na wasiwasi wa kupatikana kwa gesi kwa ajili ya kuzalisha umeme kupitia mradi wa Kinyerezi 1 kutokana na mradi wa bomba la gesi kuwa na changamoto nyingi, lakini baada ya kuona mradi wa bomba la gesi uko katika hatua nzuri yaani zaidi ya asilimia 90, tunaamini kuwa mara mtambo utapokamilika, gesi itakuwa imekwishaanza kuzalishwa na hapo ndipo tutaanza kuzalisha umeme mara moja,” Jilima.
MWANANCHI
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli jana aliungana na viongozi wenzake wa Serikali kuwamwagia sifa viongozi wa vyama vya upinzani baada ya kumwelezea Mbunge wa Hai na Mwenyekiti Chadema, Freeman Mbowe kuwa ni mpigania maendeleo ya wananchi na kwamba alitakiwa awe malaika.
Dk Magufuli alimuelezea kiongozi huyo wa upinzani bungeni kuwa ni mtu ambaye anafuatilia maendeleo ya watu bila ya kujali itikadi zao.
Waziri huyo ameungana na Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kusifu utendaji wa viongozi wa upinzani.
Februari 10, Rais Kikwete alisifu utendaji wa meya wa Manispaa ya Moshi, Jaffar Michael wa kuwaletea maendeleo wananchi, na siku 12 baadaye Waziri Pinda alimsifu mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa kwa kuwa kiongozi wa kwanza kuchangia vitanda 30 kwenye Hospitali ya Frelimo.
Jana, Dk Magufuli alimmwagia Mbowe sifa hizo katika mkutano wa hadhara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Kwasadala-Masama-Machame katika Jimbo la Hai inayojengwa kwa kiwango cha lami.
“(Mbowe)Unadhihirisha kwamba maendeleo hayana chama na kwa kweli tukienda hivi Tanzania itakuwa ni nchi ya kutolewa mfano. Sincerely (kwa dhati) nakupongeza Mbowe na Mungu akubariki,” alisema.
Kabla ya Dk Magufuli kutoa pongezi hizo, Mbowe aliwataka wanasiasa kutekeleza ahadi zao kwa vitendo kwa kuwa maendeleo hayana itikadi.
“Mimi naamini maendeleo hayana itikadi. Jambo jema likifanywa na chama chochote cha siasa ama kiongozi wa chama chochote au Mtanzania, kama ni jema anastahili kupongezwa,” :-Mbowe.
Hata hivyo, alitumia mkutano huo wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Masama kumuomba Dk Magufuli atoe maagizo ya kiserikali baada ya viongozi wawili wa CCM kutishia kuchoma moto greda lake.
MWANANCHI
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu amesema kuchelewa kwa uandikishwaji na utoaji wa vitambulisho hivyo katika mikoa mingi hapa nchini kumesababishwa na uhaba wa fedha na rasilimali watu.
Akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Nida, alisema kuwa licha ya mamlaka hiyo kuendelea na shughuli zake, lakini inakabiliwa na changamoto ya rasilimali fedha na rasilimali watu hali inayozoretesha utendaji na mikakati ya kuendelea na usajili katika mikoa ya Tanzania.
“Mpaka sasa Nida imepiga hatua kubwa katika Usajili na Utambuzi wa watu na ugawaji wa Vitambulisho vya Tafa, lakini bado tunakabiliwa na changamoto ya rasilimali fedha na watu hali inayochangia kuzorotesha utendaji,”:-Maimu.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Pereira Ame Silima, ameitaka Nida kuhakikisha changamoto zinazojitokeza kutafutiwa ufumbuzi ili Watanzania wote wenye sifa waweze kupata haki ya msingi ya kikatiba ya kusajiliwa na kupata vitambulisho.
Silima alisema kuwa Serikali itaendelea kusaidia mamlaka hiyo ili kufikia malengo ya Serikali ya awamu ya nne ya kila Mtanzania kusajiliwa na kupata kitambulisho.
“Serikali kupitia Wizara yangu tutaendelea kuongezea nguvu na mamlaka kufikia malengo iliyojiwekea. Lengo ni kuhakikisha tunafanikiwa na Watanzania wote wanapata vitambulisho,”:- Silima..
JAMBOLEO
Askari wa Jeshi la Polisi kikosi cha kutuliza Ghasia FFU Mkoani Mwanza PC Magesa ameuawa baada ya kunyongwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi.
Kamanda wa Polisi Mwanza,kamishna msaidizi mwandamizi ‘SACP’ Valentino Mlowola alithibitisha jana ni kweli askari huyo ameuawa.
Askari huyo akiongozwa na polisi jamii walikwenda eneo la tukio usiku kwa nia ya kuwakamata watu hao wanaodaiwa kuwa ni wezi wa mafuta,lakini baada ya kupata taarifa walijipanga ili kutelekeza unyama huo.
“Inaonyesha askari polisi akisaidiwa na polisi jamii walikwenda kutekeleza jukumu hilo kinyemela na walipofika eneo la tukio ambapo uhalifu ulitokea walifanikiwa kuwakamata baadhi ya wahalifu”:-Mlowola.
“Lakini gafla walijitokeza wengine kasha kuwazingira na wakamuua askari wa FFU kwa kumnyonga shingo”.
HABARILEO
Mnikulu Shaban Gurumo amekiri mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, kwamba alipokea Sh milioni 80.8 kutoka kwa James Rugemalira na kuzitumia kwa matumizi yake binafsi, ingawa amekanusha kuomba fedha hizo.
Gurumo alitoa utetezi huo jana Dar es Salaam mbele ya baraza baada ya kusomewa mashitaka ya kutumia cheo chake cha uongozi wa umma vibaya na kujipatia fedha hizo, jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Alikiri kumfahamu Rugemalira, akisema ni rafiki yake kwa zaidi ya miaka 10. Alisema daktari wake, Fred Limbanga ndiye aliyemtambulisha kwa Rugemalira.
“Kama Mnikulu sijawahi kupokea fedha za kiuchumi kwa Rugemalira wala kuwa na mahusiano naye ya kiuchumi, naitambua akaunti ya Mkombozi kuwa ni ya kwangu na niliifungua baada ya James kunishauri,”:- Gurumo.
Alisema awali hakufahamu nani aliyemwekea kiasi hicho cha fedha kwenye akaunti hadi hapo baadaye alipotambua kuwa ni Rugemalira.
Alidai hadi sasa hajafahamu sababu za kupewa kiasi hicho cha fedha na wala hakuhangaika kumuuliza Rugemalira. Pia, alisisitiza kuwa pamoja na kutofahamu fedha hizo alipewa za matumizi gani, ana uhakika si zawadi kama inavyodaiwa.
“Ila nahisi baada ya kuitwa na Kamati ya Uchunguzi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kujibu tuhuma zinazonikabili, huenda Rugemalira alinitumia fedha hizo baada ya kusikia kuwa nina mgonjwa anayeumwa saratani ya mfuko wa uzazi,” alisema.
Alisisitiza kuwa hajawahi kuzungumza wala kuomba fedha si kwa barua, simu wala kwa mazungumzo ya ana kwa ana na Rugemalira, ila amekuwa akizitumia kwa shughuli zake binafsi kwa kuwa alizikuta kwenye akaunti yake.
“Sijawahi kuomba fedha yoyote kwa Rugemalira wala VIP,” alisema. Alisema pia hata katika tamko la mali na madeni, aliloliwasilisha Desemba 29, mwaka jana kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, akiwa kama kiongozi wa umma, aliziorodhesha fedha hizo kuwa ni mali yake iliyopo katika akaunti yake ya Benki ya Mkombozi alizopewa na Rugemalira.
Alikiri kuwa alikuwa na matatizo ya kuwa na mgonjwa huyo, aliyempeleka India kwa matibabu na hadi sasa ameshatumia dola za Marekani 40,000 ambayo ni sawa na Sh milioni 73.2, hivyo hakuwa na shida yoyote ya fedha. “Mimi nina fedha zaidi ya hizo za Rugemalira ndio maana sikuomba.”
“Nakiri kupokea fedha hizo Sh milioni 80.8, lakini nilishangaa kwa mara ya kwanza niliposikia kwenye redio iliyokuwa ikirusha hewani kipindi cha Bunge, mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alikuwa akisisitiza nilipewa Sh milioni 800 na kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, jambo ambalo si la kweli,”.
MTANZANIA
Mwimbaji wa muziki wa injili, Emmanuel Mbasha, anayekabiliwa na kesi ya kumbaka mtoto wa miaka 17, jana alitoka kwenye chumba cha Mahakama ya Wilaya ya Ilala akibubujikwa machozi.
Hali hiyo ilimtokea mara baada ya shahidi wa pili wa kesi hiyo, aliyejulikana kwa jina la Suzan, kutoa ushahidi wake.
Mara baada ya kesi hiyo kuahirishwa na Mbasha kuondoka kwenye viwanja vya mahakama hiyo akiwa na wakili wake, Ngassa Ganja, Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga, alisema shahidi huyo aliieleza mahakama jinsi binti anayedaiwa kubakwa alivyomsimulia namna alivyotendewa kitendo hicho.
Alisema shahidi huyo alitoa ushahidi wake mbele ya hakimu Flora Mjaya.
“Mnakumbuka ile siku ambayo shahidi namba moja (binti aliyebakwa) alivyoieleza mahakama kwamba walikwenda kwa dada yake kumtafuta Flora ndipo akabakwa na Mbasha? Basi huyu shahidi namba mbili (Suzy) ndiye yule dada yake,” alifafanua.
Katuga alisema shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa alipata taarifa zote hizo baada ya binti anayedaiwa kubakwa kukimbilia nyumbani kwake na kumpa taarifa zote.
“Lakini kwa mujibu wa sheria (CPA) namba 186 kifungu kidogo cha tatu, inanizuia kueleza kwa kina yale ambayo shahidi huyo ameieleza mahakama,” alidai Katuga.
Kwa upande wake, wakili wa Mbasha,alisema licha ya shahidi huyo kueleza kwamba binti anayedaiwa kubakwa alipigwa na Mbasha, yeye shahidi hakumkagua ili kujiridhisha kama ni kweli alipigwa ama la.
“Ni kweli ameieleza mahakama ushahidi ambao Katuga amewaeleza, ila shahidi huyo hakumkagua (binti aliyebakwa) ili kujua kama ni kweli,” aliongeza.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram, na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook