Waathirika wa mvua ya mawe na upepo mkali iliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 40 katika kijiji cha Mwakata wilayani Kahama, Shinyanga, jana walitawanywa kwa mabomu ya machozi na polisi wa kutuliza ghasia (FFU) baada ya kufunga barabara kuu ya Isaka-Kahama kuelekea nchi jirani za Rwanda, Uganda na Burundi,kwa kulala barabarani na kuweka mawe na miti.
Tukio hilo lililotokea alfajiri jana liliathiri baadhi ya wasafiri wa mabasi makubwa yaliyokuwa yakisafiri kwenda mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma na mikoa ya jirani.
Waathirika hao walichukua uamuzi huo baada ya misaada ya chakula, magodoro, mablanketi na maturubai uliotolewa na wasamaria wema, ukiwa umefungiwa ndani ya darasa na wahusika wakishindwa kutimiza agizo la Waziri Mkuu Mizengo Pinda la kuwataka kuwapa msaada huo.
Mwathirika wa tukio hilo, Benjamini Ndege, alisema wananchi waliamua kuchukua hatua hiyo kutokana na serikali kutowajali.
“Hawa waliofanya hivi ni wale ambao nyumba zao zimeharibika upande, zikiwa na mifugo na mali nyingine, lakini tunashindwa kuhudumiwa mahitaji muhimu…wanataka wote tukusanyike shuleni, sasa tunakaa hapo na mifugo yetu,” Ndege.
Alishangazwa na hatua ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, kutumia polisi kuvurumisha mabomu wakati wakiwa katika majonzi ya kupoteza ndugu zao katika janga hilo.
Alisema mabomu yalirushwa na polisi hao, yamesababisha akinamama na watoto kukimbilia porini wakihofia maisha yao na kutowahi kuona hali hiyo.
“Tumeahidiwa misaada mbalimbali, lakini hatupewi na mvua inanyesha tunabaki kulowa nje wakati maturubai yapo…tunaomba tufanyiwe yale aliyoahidi waziri mkuu,”Maganga.
NIPASHE
Hatimaye Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra CCC) limesikia kilio cha wananchi na kuahidi kushusha nauli za daladala na mabasi yaendayo mikoani.
Katibu Mkuu wa Sumatra CCC, Oscar Kikoyo, akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema nauli ya daladala itashuka kwa shilingi 50 na mabasi ya kwenda mkoani itashuka kwa asilimia 15 hadi 24 kutokana na kupungua kwa bei ya mafuta duniani.
“Kwa mikoani basi la kutoa Dar es Salaam kwenda Arusha nauli itashuka toka Sh. 36,000 hadi Sh. 28,325 kwa mabasi ya luxury,” Kikoyo.
Alisema sekta ya mafuta ni muhimu kwa kuwa inachangia kati ya asilimia 20 hadi 30 katika sekta ya usafirishaji na kuwa baraza hilo linaangalia pande zote mbili kwa mtoa huduma na mteja ili kuweka unafuu wa gharama.
Alisema mtoa huduma akipata zaidi ya asilimia 25 ya faida lazima nauli itashuka lakini ikiwa chini ya asilimia tano nauli zitapanda na mapendekezo hayo watayawasilisha Sumatra Jumatatu ili nauli ziweze kushuka mapema iwezekanavyo.
Hata hivyo, alisema kuwa iwapo Sumatra itakataa mapendekezo hayo basi watayapeleka Tume ya Ushindani kwa usuluhishi zaidi.
Hivi karibuni Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imetangaza kushusha bei za mafuta ya taa, petroli na dizeli nchi nzima.
Bei za jumla zimepungua tofauti na ilivyokuwa mwezi uliopita ambapo petroli imeshuka kwa Sh. 148.66 kwa lita sawa na asilimia 7.16, dizeli Sh.118.69 kwa lita sawa na asilimia 6.16 na mafuta ya taa Sh.105.81 kwa lita sawa na asilimia 5.59.\
NIPASHE
Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Inspekta Prisca Komba, ameibuka mshindi wa Tuzo ya Mwanamke mwenye Mafanikio Tanzania kwa mwaka 2014.
Inspekta Komba, ambaye pia anasimamia Dawati la Jinsia kwenye mkoa huo wa kipolisi, pia alishinda Tuzo ya Mwanamke Mwenye Mafanikio katika Sekta ya Umma.
Wengine waliopata tuzo mbalimbali ni pamoja na Debora Mwenda, aliyepata tuzo ya Mwanamke mwenye mafanikio ya maisha, Penina Mlama, Utamaduni na Sanaa, Mary Gitanho, Ustawi wa Jamii, Sharmillah Bhatt, Sayansi na Teknolojia, Jennifer Shigoli, Mwanamke mdogo mwenye Mafanikio, Blandina Sembu, Habari na Mawasiliano.
Pia Dk. Wineaster Anderson, Taaluma, Nahida Esmail, Elimu, Devotha Likokola, Biashara na Ujasiriamali, Jacqueline Mkindi, Kilimo, Mpendwa Chihimba, Afya na Angel Eaton, Michezo.
Tuzo hizo, zilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Taasisi ya Tuzo za Wanawake Wenye Mafanikio Tanzania (TWAA) inayoandaa tuzo hizo zilizokutanisha wanawake zaidi ya 700.
Rais na Mwandaaji wa tuzo hizo, Irene Kiwia, akikabidhi tuzo hizo alisema jumla ya Wanawake 36 waliingia tatu bora katika vipengele 12 vilivyokuwa vinashindaniwa na kati ya hizo jumla ya tuzo 14 zimetolewa.
“Katika kuelekea siku ya wanawake Duniani ambayo inafanyika kitaifa leo tumeona ni vyema tukawapatia tuzo wanawake ambao wameleta mabadiliko chanya ndani ya jamii, kwani mafanikio yao yanaleta hamasa kwa wanawake wengine wenye malengo,” Kiwia.
Alivitaja vipaumbele vya mwanamke ambaye anataka kuleta mabadiliko ndani ya jamii kuwa ni ndoto, uthubutu, kufuatilia ndoto, uvumilivu na ustahimilivu.
Akizungumzia tuzo hiyo, Ispekta Komba, ameishukuru jamii kwa kutambua umuhimu na kazi ambazo amekuwa akizifanya ndani ya jamii na kwamba amepata nguvu ya kuendelea kufanya kazi hiyo kwa ufanisi zaidi.
“Sikutegemea kupata tuzo hii na nimelia kwa chozi la furaha, namuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Ernest Mangu, pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe, kutoa vyeo kwa wakati ili kuongeza motisha wa kufanya kazi,”Komba.
Aliitaka serikali na mahakama kuhakikisha inasimamia kesi za udhalilishaji na ukatili wa kijinsia zinatolewa hukumu mapema ili kumaliza vitendo hivyo ndani ya jamii na pia kupunguza kasi ya udhalilishaji ambayo inatokana na watuhumiwa kutochukuliwa hatua kwa wakati.
MWANANCHI
Rais Paul Kagame amemshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kuhudhuria mkutano wa tisa wa nchi zilizoungana kutekeleza Miradi ya Miundombinu Ukanda wa Kaskazini za Northern Corridor Projects uliofanyika jijini Kigali, Rwanda, akisema ni hatua muhimu katika kufungua utekelezaji wa miradi ya miundombinu katika kanda nyingine za EAC.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana ilisema kuwa Rais Kikwete alihudhuria kikao hicho kwa mwaliko wa Rais Kagame na kwamba mkutano huo ulifanyika kwenye Hoteli ya Serena mjini Kigali.
Naye Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema kuwa ni jambo la kufurahisha kwamba Rais Kikwete ameweza kuhudhuria mkutano wa jana kwa sababu sasa njia imefunguka kuanza kazi ya utekelezaji wa miradi kwenye Ukanda wa Kati wa Central Corridor unaokatisha katikati ya Tanzania.
Marais Kagame na Kenyatta walikuwa wanazungumza wakati wa hotuba za ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika zaidi ya saa mbili baada ya Rais Kikwete kuwasili Kigali akitokea Dar es Salaam.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wakuu wa nchi za Kenya, Uganda na wenyeji Rwanda.
Mbali na nchi hizo, Burundi na Sudan Kusini pia zilialikwa kwenye mkutano huo kujadili hatua za utekelezaji wa miradi mbalimbali kulingana na maelekezo yaliyotolewa katika mkutano wa nane uliofanyika Nairobi, Kenya, Desemba 11, mwaka jana Marais hao wawili wamekuwa wakitofautiana katika suala la waasi wa Rwanda baada ya Rais Kikwete kumshauri Kagame kukaa meza moja na waasi wa Rwanda ili kumaliza tofauti zao zinazosababisha maisha ya watu kupotea.
MWANANCHI
Wakati ikiwa imesalia siku chache kabla ya kipenga cha kuruhusu wananchi kujitokeza kuwania urais, ubunge na udiwani, moto unawaka kwenye majimbo mbalimbali ambako wabunge wanapigana vikumbo na watu wanaoonekana kutaka kuwarithi.
Vita iliyo wazi ni ile inayohusisha wenyeviti wa vyama vya NCCR-Mageuzi na TLP, James Mbatia na Augustine Mrema ambao wameshatoleana maneno ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano, lakini mchuano ni mkali kwenye majimbo mengine, wakiongozwa na mbunge wa CCM, Ester Bulaya ambaye ameeleza dhamira yake ya kutaka Jimbo la Bunda, ambalo linashikiliwa na Waziri wa Chakula na Kilimo, Steven Wassira pamoja Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Ummy Mwalimu ambaye ameonyesha nia ya kwenda Tanga.
Mchuano huo unazidishwa na kitendo cha wabunge walioingia kwenye Bunge la Kumi kwa tiketi ya viti maalumu, ambao sasa wataka kurejea kwenye chombo hicho cha kutunga sheria kwa kuchaguliwa na wananchi.
Wabunge wengi wa viti maalumu wameanza kuonyesha makucha majimboni wakifanya shughuli mbalimbali za kijamii katika kile kinachoonekana ni kujiweka karibu na wananchi.
Wengi wanajishughulisha na kuchangia masuala ya maendeleo pia kuendesha au kudhamini mashindano mbalimbali ya mpira wa miguu.
Kwenye baadhi ya majimbo, mchuano ni mkali zaidi kutokana na ukweli kuwa waliokuwa wanayashikilia na ambao baadhi walikuwa wanaonekana mibuyu, kutangaza kutorudi tena kuomba kura kutokana na kuona imetosha au kufikiria kuwania nafasi nyingine.
Muungano wa vyama vya upinzani, Ukawa, pia umeongeza joto hilo kutokana na ukweli kuwa vyama vya NCCR-Mageuzi, NLD, CUF na Chadema vimepania kusimamisha mgombea mmoja kwenye majimbo mengi.
“Nimetafakari kufuatia maelekezo ya chama changu, nimejipima na nimetazama hali halisi ya maendeleo na kero ya huduma na matatizo, nikaona ni wakati wa kutatua haya,” Abdulaziz Ahmad alipoulizwa kuhusu nia yake ya kuwania ubunge wa Jimbo la Lindi, ambalo kwa sasa linashikiliwa na Salum Barwany wa CUF.
Mwanachama mwingine wa CCM, Joseph Mhagama, ambaye analitaka Jimbo la Peramiho linaloshikiliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Utaratibu wa Bunge, Jenister Mhagama, alisema haoni kama mbunge wa sasa anawatumikia wananchi.
HABARILEO
Kazi anayofanya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana katika ziara zake mikoani, sasa ni dhahiri ameanza kurejesha chama hicho katika misingi ya asili yake ya Ujamaa, iliyoasiswa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Hilo limejidhihirisha katika kauli na hotuba zake kwa wanachama na wananchi, kwenda kinyume na taswira iliyoanza kujijengea mizizi, kuwa chama hicho kimeanza kuondoka katika misingi ya Ujamaa, iliyojengwa tangu kuasisiwa kwake.
Uadilifu Katika moja ya kauli zake alizotoa jana alipohutubia wakazi wa Mkoka katika wilaya ya Kongwa, akiwa katika ziara ya kutembelea mkoa wa Dodoma, Kinana alisisitiza umuhimu wa uadilifu wa wagombea kwa mtindo uliokuwa ukisisitizwa wakati wa Mwalimu Nyerere.
Kwa mujibu wa Kinana, sifa namba moja inayozingatiwa na wananchi katika kumpata kiongozi wa kuwaongoza, hata kama ni mchapakazi wa kiwango cha juu, uadilifu utasimama kuwa sifa namba moja.
Alisema kutokana na kumomonyoka kwa maadili ya uongozi, tofauti na enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere, wananchi sasa hawazingatii suala la uhodari na uchapakazi kama sifa namba moja ya kumchagua mtu kuwa kiongozi wao. “Wananchi sasa wanaangalia nani muadilifu, nani sio mwizi, nani si mlaji, wapo tayari kukusamehe mambo mengine yote, lakini si suala la uadilifu,” Kinana.
Alisema kutokana na kutambua hilo, CCM itakuwa makini na viongozi wake watakuwa wakali, katika kuhakikisha kuwa watu wasio waadilifu wanadhibitiwa wasishike nafasi za uongozi kupitia chama hicho, ili kujenga heshima na imani ya wananchi kwa chama hicho.
Ishara ya ukaidi Kinana aliweka wazi kuwa moja ya ishara ya kutetereka kwa uadilifu katika utumishi wa umma, ni tabia iliyoibuka siku za hivi karibuni, ambapo viongozi wanaokiuka misingi ya maadili ya uongozi wa umma, wanapoombwa kukaa kando kutokana na makosa waliyofanya, wanagoma kuondoka madarakani jambo ambalo halikuwepo zamani.
HABARILEO
Siri ya mafanikio ya Padri feki, Josephat Asenga, aliyekamatwa mkoani Morogoro, katika kuongoza Misa ya Kanisa Katoliki kwa kufuataa ya Kanisa Katoliki kwa kufuata taratibu zote maalumu bila kutiliwa shaka, imebainika.
Asenga aliyetumia vitambulisho feki, alipojitambulisha kwa uongozi wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Maria Madeko mkoani Morogoro, alipopewa fursa ya kuongoza Misa, alitekeleza wajibu huo wa kipadri bila kuacha shaka.
Akizungumza na gazeti hili jana, kiongozi mmoja wa Kanisa Katoliki (jina limehifadhiwa), alithibitisha kuwa Asenga alipofika Parokiani hapo kati ya Mei na Juni mwaka jana, hakutiliwa shaka hata kidogo kuwa si Padri.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, Asenga alifika kanisani hapo akiwa amevaa mavazi ya kipadri na kujitambulisha kuwa yupo nchini kwa mapumziko, akitokea nchini Marekani, alikodai ndipo anakofanyia shughuli zake za upadri katika Jimbo Kuu la New York.
Mbali na kuvalia mavazi ya kipadri, Asenga pia alionesha kitambulisho na kusababisha uongozi uamini kuwa ni Padri na kumpa makaribisho ya Padri mwenzao.
“Alipoonesha kitambulisho tulimwamini na jinsi alivyokuja na mavazi ya upadri na muonekano wake alionao, haikuwa rahisi kumtilia shaka,” alisema kiongozi huyo.
Kiongozi huyo alithibitisha kuwa Asenga aliongoza vyema misa hiyo, kwa kufuata taratibu zote za kanisa hilo kama zinavyofuatwa na mapadri wengine.
Taratibu Kwa kawaida Misa katika Kanisa la Katoliki, huanzia Sakestia, sehemu ambayo mapadri na waministranti, ambao ni wasaidizi wao, huvaa majoho na kusali kabla ya kuingia kanisani wakisindikizwa na nyimbo. Baada ya kuingia madhabahuni, Padri hubusu madhabahu kabla ya kualika waumini katika Misa.
Mualiko huo hufuatiwa na maelezo kidogo na kuanza Ibada ya Kitubio, ambayo waumini hutubu dhambi zao na kujiweka tayari kusikiliza neno la Mungu. Ibada ya kusomwa neno, kwa kawaida masomo matatu kutoka vitabu vya Agano la Kale na Jipya katika kitabu cha Bibilia Takatifu, Padri huanza kutoa mahubiri.
JAMBOLEO
Wakati Serikali ikipambana kutokomeza mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi inasemekana baadhi ya waganga wa kienyeji wanatajirika kwa kiwango kikubwa na biashara hiyo.
Inadaiwa baadhi ya waganga hao hupata takribani dola za Marekani 75,000 sawa na zaidi ya milioni 100 kutokana na biashara hiyo ambayo Rais Kikwete aliikemea vikali kwamba inatia aibu Taifa.
Hayo yalibainishwa katika ripoti ya chama cha msalaba mwekundu kuhusu vitendo hivyo vilivyoshamiri hasa katika ukanda wa Ziwa Victoria.
Ilidai kuwa baadhi ya watu wenye imani za kishirikina huagiza viungo vya albino kwa ajili ya kutengenezea dawa ambayo huamini ina nguvu maalumu yenye kuleta bahati nzuri.
Baadhi ya wanasiasa wanadaiwa kuagizwa na waganga wa kienyeji wasio waaminifu kuwapelekea viungo hivyo ili nyota zao zing’ae wakati wa uchaguzi.
Hautopitwa na stori yoyote inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook