MWANANCHI
Licha ya Rais Jakaya Kikwete kusema hana mpango wa kuongeza muda na kuwa Uchaguzi Mkuu utafanyika Oktoba, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimezidi kuonyesha wasiwasi wake kikieleza kuwa hakuna dalili za uchaguzi huo mwaka huu.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alikieleza kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kuwa uchaguzi huo unaweza kuahirishwa kama ilivyotokea kwenye Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
Kikatiba, uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani unatakiwa kufanyika Jumapili ya mwisho ya Oktoba ambayo itakuwa Oktoba 25, mwaka huu ikiwa ni mwaka wa tano tangu kuchaguliwa kwa Serikali iliyopo madarakani.
Katika kipindi hicho, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitakiwa kurekebisha mara mbili Daftari la Kudumu la Wapigakura lakini haijafanya hivyo hata mara moja na hii ya sasa inayoendelea katika baadhi ya mikoa bado inasuasua.
Kutokana na kusuasua huko, NEC ililazimika kuahirisha Kura ya Maoni iliyokuwa imepangwa kufanyika Aprili 30, hadi tarehe itakayotangazwa baadaye, licha ya awali kuelezwa mara kwa mara na tume yenyewe au viongozi wa Serikali kuwa kura hiyo ilikuwa palepale.
Ni kutokana na hali hiyo, Chadema na vyama washirika vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), vilieleza wasiwasi wa kuwapo uwezekano wa kuahirisha uchaguzi mkuu kwa kisingizio cha kutokamilika uandikishaji wapigakura kama ilivyofanyika kwa kura ya maoni.
Lakini akihutubia siku ya wafanyakazi (Mei Mosi), mjini Mwanza, Rais Kikwete alieleza kuwashangaa wapinzani hao, akisema ni aibu kwao kuzua jambo ambalo halipo, kwa kuwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba uko palepale na hana mpango wa kuongeza muda.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu, Damian Lubuva jana alisisitiza kauli ya Rais akisema uchaguzi huo utafanyika kama Katiba inavyoeleza (wiki ya mwisho ya Oktoba), huku Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama akisema uandikishaji unavyoendelea ni kielelezo kwamba uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa.
Akifungua kikao cha siku mbili cha Kamati Kuu jana, Mbowe alisema: “Wote hatujui kama uchaguzi mkuu upo mwaka huu, waziri mkuu anasema upo, NEC wanasema upo lakini mazingira hayaonyeshi kwamba utakuwapo mwaka huu.”
Alisema bado uandikishaji wapigakura unasuasua na mazingira hayaonyeshi kwamba utakamilika kabla ya siku ya uchaguzi inayoelekezwa na Katiba.
MWANANCHI
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira amewakosoa baadhi ya vigogo wanaojinasibu kuanzisha programu ya shule za sekondari za kata nchini akisema ni ujinga kusema hivyo kwa kuwa miradi yote hufanywa na Serikali na siyo mtu binafsi.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini kwake juzi, Wasira alisema wazo la kujenga sekondari kila kata ni ahadi ya CCM katika ilani ya mwaka 2005 na si wazo la mtu mmoja kama inavyodaiwa.
Huku akitumia nadharia ya uendeshaji Serikali, Wasira alisema miradi yote ya maendeleo inafanywa kwa pamoja na kwamba kama ni kuihusianisha na mtu mmoja, basi mwenye sifa hiyo ni Rais.
Kauli ya Wasira ilikuja baada ya kuulizwa juu ya changamoto mbalimbali zinavyoikabili nchi na masuala ambayo rais ajaye anatakiwa kufanya ili kuiletea nchi maendeleo.
“Mtu anayesema alijenga sekondari za kata anawadanganya Watanzania. Ile kitu ipo kwenye ilani ya CCM… jitihada na sifa za kujenga sekondari huwezi kuzihamisha kutoka kwa rais anayeongoza nchi na kusema waziri mmoja tu ndiyo anahusika, nakataa kabisa na yeyote anaweza kuninunia kwa hilo,” Wasira
Alisema Serikali inapoamua kufanya mradi ni jambo la pamoja na huendeshwa kama familia, hivyo hakuna mtu mmoja katika baraza anaweza kusema ni la pekee yake kutokana na kuangukia katika wizara yake.
Ingawa Wasira hakutaja jina la mtu, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amekuwa akihusishwa kusema mara kwa mara kuwa alikuwa kiungo muhimu katika uanzishwaji wa mpango wa shule za kata nchini.
NIPASHE
Takribani siku 22 zikiwa zimepita tangu madereva wagome kutoa huduma za usafiri nchi nzima, leo wametangaza mgomo mwingine kutokana na ukimya dhidi ya madai yao kwa serikali.
Madereva hao jana walitoa tamko la kuwapo kwa mgomo huo kupitia vyama vyao, huku wakikanusha kwamba watagoma sambamba na kuandamana.
Walisema leo watakuwa kwenye ofisi zao za muungano wao zilizopo Ubungo, jijini Dar es Salaam na hawatatoa huduma za usafiri
Katibu wa Umoja wa Madereva na Chama cha Malori, Rashid Salehe, alisema, mgomo upo pale pale kwa madai kuwa bado kuna mambo ambayo yameendelea kuwa kikwazo kwao.
Alisema iwapo serikali haitatoa majibu ya kuridhisha, leo hawataingia barabarani kutoa huduma za usafiri.
Alisema jana walifanya mkutano wa madereva jijini Dar es Salaam huku ajenda kubwa ikihusu mgomo huo.
Alitaja baadhi ya sababu zinazowafanya wagome kwa mara nyingine kuwa ni serikali kutotekeleza madai yao likiwamo kupewa ajira rasmi na waajiri wao.
“Msimamo wetu upo palepale kwamba kesho (leo) hatutaendesha magari..madereva wanaambiwa wezi, tunataka mikataba iboreshwe…tutakaa hapa hata ndani ya siku saba hadi serikali ije na kutoa majibu yanayoridhisha. Tunataka tupatiwe mikataba inayoeleweka na waajiri wetu mbele ya serikali,”
Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), Enea Mrutu, alisema walipata taarifa zote kuhusu mgomo huo na kueleza kwamba wanaotangaza mgomo huo siyo madereva walioajiriwa.
Kwa mujibu wa Mrutu, madereva hao ndiyo waliosababisha magari yao kutoingia barabarani Aprili 11, mwaka huu na kuitaka serikali kuingilia kati suala hilo, vinginevyo leo magari hayataweza kuingia barabarani.
Mwenyekiti wa Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (DARCOBOA), Sabri Mabrouk, alisema chama hicho kina taarifa kuhusu mgomo huo, lakini akaeleza kusikitishwa kwake kwa namna madereva wa vyombo vya usafiri wanavyowahusisha wao akisema hawahusiki.
Kutokana na hilo, Mabrouk aliomba mgomo huo usiwe wa lazima bali wa hiyari kwani si vyema kuwahusisha wao wanaohusika na daladala tena ndani ya mkoa na kupewa vitisho vya kupigwa mawe endapo gari lolote litakaidi agizo hilo.
NIPASHE
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema kuporomoka kwa Shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani kunakoshuhudiwa hivi sasa, kunaiweka nchi katika shaka kubwa ya maendeleo kiuchumi.
Amesema hali hiyo inatokana na ukweli kwamba, kuporomoka kwa Shilingi kutaendelea kuathiri uwekezaji mkubwa nchini.
Mbowe, ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema hayo wakati akifungua kikao cha Kamati Kuu ya Chadema cha siku mbili, kilichoanza jijini Dar es Salaam jana.
Alisema hali hiyo inatokana na wawekezaji kuwa na wasiwasi kuhusu hali ya kisiasa na hatima ya uchaguzi mkuu.
“Kwa hiyo, uchumi utazidi kuathirika zaidi kwa siku zijazo iwapo kitendawili hicho hakitatatuliwa,” Mbowe.
Alisema anashangazwa kuona namna Rais Jakaya Kikwete anavyoendelea kukaa kimya, huku akishuhudia jinsi uchumi unavyoyumba, uwekezaji unavyozidi kuzorota na sarafu ya Tanzania inavyozidi kuporomoka kwa sasa.
Mbowe alisema taifa liko njia panda kutokana na wakuu wa serikali, akiwamo Rais Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kukimbia kuzungumza ukweli kwamba uchaguzi mkuu uko shakani.
Alisema ni wazi kwamba, mazingira ya nchi kuelekea uchaguzi huo hayako sawa kutokana na kuwapo ishara zote zinazoonyesha unaweza usifanyike.
Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, ameitaka serikali kuchukua hatua za haraka kuokoa Shilingi ya Tanzania, ambayo imeporomoka kwa zaidi ya asilimia 20 dhidi ya dola ya Marekani ili kunusuru uchumi wa nchi.
Mrema, alisema kwa hali ilivyo, serikali bado haijachukua hatua za kutosha kukabiliana na tatizo hilo na hivyo kutia shaka umakini wake katika kushughulikia mambo muhimu yanayowagusa wananchi.
MTANZANIA
Chifu wa kabila la Wazanaki, Japheth Wanzagi ametaja sifa za rais ajaye akisema, anapaswa kuwa ni mtu wa haki.
Hata chifu huyo amesema ni kitendawili kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa na mtu mwenye sifa hiyo.
Chifu Wanzagi alisema kwa kuwa Watanzania walio wengi ni masikini, hivyo rais ajaye anapaswa kutenda haki.
“Kitu kinacholeta taabu kwa sasa ni haki. Haki sasa inanunuliwa, watu wengi ni masikini na utakuta ndiyo wanaoshindana na matajiri na wanashindwa. Hilo ndilo litakalokisumbua chama tawala.
“Ukitembea barabarani utaona vijana wengi wakiuza maji biskuti na bidhaa nyingine. Utakuta kijana anakuuzia bidhaa kwa bei ya chini kwa sababu hawana fedha…Ukifika uchaguzi mkuu vyama vinapita na kuwaaminisha vijana kwamba shida hizo zinaletwa na CCM…kwa hali hii huwezi kusema kuwa CCM itarudi madarakani au wapinzani wataingia madarakani,” Chifu Wanzagi.
Alisema hivi karibuni alipokutana na Rais Jakaya Kikwete, wakati wa uzinduzi wa meli vita mbili za doria katika bahari kuu TNS Msoga na TNS Mwitongo,Chifu Wanzagi alisema alimhakikishia rais bora atapatikana.
“Rais Kikwete alisema hilo ni jukumu lake kupata rais mwenye sifa bora… Aliposema ‘sasa meli zimezinduliwa,” mvua kubwa ikanyesha. Nina imani uchaguzi utakuwa wa amani,”.
Akichambua zaidi juu ya mwenendo wa kisiasa ndani ya CCM, Chifu Wanzagi alisema kwa sasa kinatawaliwa na vijana wengi wasiojua chimbuko lake, huku wapiga kura wengi wakiwa vijana.
Akizungumzia tetesi za mtoto wa Mwalimu Nyerere, Makongoro Nyerere kugombea urais, Chifu Wanzagi alisema kwa sasa familia haina maandalizi yoyote kwa ajili yake.
Alisema hata kama Makongoro atajitosa, bado hajafikia uwezo wa kuvaa viatu vya Mwalimu Nyerere.
“Hatuna maandalizi yoyote kwa Makongoro, kila mtu ana siri yake mwenyewe, lakini hatuna maandalizi rasmi,” .
Hata hivyo, alisema ni jambo jema kwa familia ya Mwalimu Nyerere kuwa na mrithi wa kiti cha urais, huku akieleza jinsi anavyomlinganisha Makongoro na baba yake .
MTANZANIA
Joto la Uchaguzi linazidi kupanda mjini hapa, baada ya vijana takribani 1,000 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), katika Jimbo la Arusha Mjini, kutangaza kutomsaidia Mbunge wao Godbless Lema wakati wa kampeni.
Vijana hao wakiongozwa na aliyekuwa dereva wa kwanza wa Lema ambaye pia alikuwa mratibu wa mawakala katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Rashidi Shuberti, wamekutana mjini hapa na kutangaza kupambana na mbunge huyo.
Wakati kundi hilo la vijana wakitangaza uamuzi wa kumwangusha Lema, Katibu wa Lema, Innocent Kisanyage aliliponda kundi hilo na kudai kuwa ni wahuni waliofukuzwa ndani ya Chadema siku nyingi.
Akizungumza na vijana hao jijini hapa jana Shuberti alidai alikuwa mstari wa mbele kwenye Kamati ya ushindi ya Lema mwaka 2010.
Alisema pamoja na kuongoza mapambano ya ushindi kwa kuwaongoza vijana wa Arusha Mjini sasa umefika wakati wameamua kupambana kuhakikisha Lema hashindi katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktiba mwaka huu.
“Kwa bahati mbaya vijana wenzangu tuliaminishwa na kuanza kuhubiri Injili tusiyoijua ndani ya Chadema, kwani katika Injili hiyo wapo waliokufa, ndoa zao kuvunjika na wengine kupigwa risasi,” Shuberti
Alisema katika kupinga udhalimu huo alipewa jukumu la kuratibu maandamano ya kupinga matakwa ya CCM yaliyofanyika Januari 5, 2011 na kusababisha mauaji ya vijana watatu na majeruhi kadhaa.
Shuberti alisema atahakikisha anashiriki kwa kiwango kile kile alichoshiriki kuhakikisha anamuangusha Dk. Batilda Burian aliyekuwa mgombea ubunge kupitia CCM ili kuhakikisha Lema anashindwa uchaguzi.
Alipomtafuta Lema kwa simu hakupokea na alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu na kuulizwa kama anamfahamu Shuberti alisema.“Fedha ya CCM inaweza kutumika na vichaa wengi lakini haiwezi kuwasaidia CCM, Arusha hakuna CCM ila kuna bendera za CCM na muhimu CCM ifanye jitihada za kumpata mgombea ubunge, atakayeshindwa tena.“… kwani najua hawawezi kushindana na chama changu wala mimi hata kidogo kuna vichaa wengi mitaani,” Lema.
MTANZANIA
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, amesema kuwa akishindwa katika mchakato wa kura za maoni za kusaka urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), atarudi jimboni kuendelea kuwatumikia wapiga kura wake.
Kutokana na hali hiyo January ambaye ni Mbunge wa Bumbuli, amewataka wananchi wake kuwapuuza watu wanaopita na kudai kuwa wanataka ubunge kwa kuwa yeye anatajwa katika kinyang’anyoro cha urais ndani ya CCM.
Kauli hiyo aliitoa juzi jimboni kwake Bumbuli, wilayani Lushoto mkoani Tanga katika mkutano wa hadhara ambapo alikuwa akizungumzia mafanikio na changamoto za utekelezaji wa ilani ya uchaguzi tangu alipochaguliwa mwaka 2010.
January alitumia mkutano huo kuwashukuru wapiga kura wake kwa kumchagua kuwa mbunge mwaka 2010 huku akisema kuwa kama si wao asingeweza kutajwa katika mbio za urais ndani ya CCM.
“kutajwa si dhambi na kwa kuwa fomu za uchaguzi si sumu si dhambi kuchukua…. na kuingia katika kinyang’anyiro hicho.
“Hivi kuna kiu kubwa ya uongozi wa aina mpya na kuna watu wamemwona mtu na kumtaja yeye jambo ambalo si baya. Wapuuzeni watu wanaopita na kusema mimi sitaki ubunge eti kwa sababu natajwa kwenye urais.
Akizungumzia hatua ya kufufua uzalishaji wa Kiwanda cha Chai Mponde, January alisema kuwa Serikali imeridhia kutoa Sh bilioni 4 ambazo ni gharama za kulipa madeni ya malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi.
Alisema mbali na hilo madeni ya malipo ya wakulima, gharama za ukarabati na mtaji wa kuanzia kuendesha shughuli za uzalishaji utaimarishwa.
HABARILEO
Kutokana na kushamiri kwa matukio yenye viashiria vya kigaidi nchini, Kanisa Kuu Katoliki Jimbo la Dodoma limeanzisha utaratibu wa kukagua watu wote wanaoingia katika ibada kwa kutumia kifaa maalumu cha kugundua silaha au kifaa chochote hatarishi na vile vya mlipuko.
Aidha, wito umetolewa kwa waumini wa madhehebu ya Kikatoliki wanaohudhuria ibada zao kwenye Kanisa hilo, kuchukua tahadhari zote kukabiliana na suala la tishio la usalama kwa matukio ya kigaidi, yanayoweza kujitokeza kanisani hapo, kutokana na mkusanyiko mkubwa wa watu wanaohudhuria ibada siku za Jumapili.
Paroko wa Kanisa hilo, Padri Sebastian Mwaja alitoa wito huo jana wakati akiendesha ibada za kawaida za Jumapili.
Alisema kanisa hilo limeanzisha utaratibu wa kuwakagua watu wote wanaoingia katika ibada hizo kwa kutumia kifaa maalumu cha kugundua silaha au kifaa chochote hatarishi na vile vya mlipuko.
Padri Mwaja alisema idadi ya waumini imeongezeka ghafla hususani baada ya Jimbo la Dodoma kumpata na kumsimika rasmi Askofu Mkuu mpya wa Jimbo la Dodoma.
“Pia mji wetu kuwa na desturi ya kupokea wageni wengi wa kiserikali, ni wazi hatuwezi kujisahau na kuacha suala la usalama wa waumini wetu,” .
Alitaja baadhi ya hatua zilizoanza kuchukuliwa kukabiliana na matishio ya vitendo vya kigaidi kuwa ni pamoja na kuundwa kwa kamati ya ulinzi ya kanisa hilo ijulikanayo kwa kifupi “KAUKA”, ambapo baadhi ya taratibu za awali tayari zimeshawekwa na kamati hiyo, ikiwamo tahadhari kwa waumini wote kuhakikisha anamtambua jirani yake aliyekaa naye kanisani, na kama atamtilia shaka yoyote, atoe taarifa mapema katika kamati hiyo.
Hatua nyingine iliyochukuliwa ni pamoja na kuhakikisha kila muumini anayeingia kanisani hapo anakaguliwa ndipo aingie ndani ya kanisa na pia magari yote pamoja na pikipiki kuachwa nje ya ua wa parokia hiyo katika eneo maalumu lililoandaliwa ili kudhibiti usalama.
Paroko huyo ametaja pia changamoto iliyojitokeza wakati wa kutekeleza ulinzi huo, ikiwemo upungufu wa vifaa vya ukaguzi ambapo hadi sasa kipo kifaa kimoja tu kinachotumika kwenye lango (geti) moja na mengine kubakia yamefungwa.
HABARILEO
Jeshi la Polisi mkoani Katavi linawashikilia watu tisa wakiwemo vikongwe wa miaka 80 na 70 baada ya kukamatwa wakiwa na bunduki tatu za kienyeji aina magobole, risasi zake 15, mtambo wa kutengenezea silaha, baruti na sare za Jeshi la Wananchi la Ulinzi na Usalama (JWTZ).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi , Dhahiri Kidavashari alitaja vitu vingine vilivyokamatwa kufuatia msako mkali unaoendelea wilayani Mlele ni vipande tisa vya nondo, vyuma vya kutengenezea risasi na mafuta ya kiboko yaliyohifadhiwa kwenye chupa.
“Mafanikio haya yametokana na ushirikiano mzuri kati Jeshi la Polisi, askari wa Tanapa na raia wema ambapo wamekuwa wakiendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu na kufanikisha katika ukamataji,” alieleza .
Alidai kuwa silaha hizo zilikuwa zikimilikiwa kinyume cha sheria na zilikuwa zikitumika katika visa vya kijangili na uhalifu mwingine wilayani Mlele.
Akizungumza kwa njia ya simu, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni pamoja na Lazaro Zakaria aliyekamatwa akimiliki gobole bila kuwa na kibali, Shaaban Mussa gobole bila kuwa na kibali na Robert Kaumba.
Wengine ni Hamisi Rehani alikamatwa akiwa na mtambo wa kutengenezea silaha aina ya gobole bila kuwa na kibali, Benedict Simon akiwa na risasi 15 za gobole, vipande tisa vya nondo, vipande vya miti, mtutu mmoja na baruti ndani ya chupa na Shaaban Mussa alikamatwa akiwa na risasi moja ya gobole bila kibali.
Kwa mujibu wa Kidavashari, katika msako huo pia jeshi hilo lilimtia mbaroni Esther John akiwa na sare ya JWTZ na vyuma viwili vya kutengenezea risasi na Mashaka George, alikamatwa akiwa na mafuta ya kiboko aliyoyahifadhi kwenye chupa.
HABARILEO
Serikali imesema haitalipa fidia kwa wananchi wanaopisha miradi ya usambazaji umeme vijijini inayotekelezwa na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Hayo yamesemwa mjini Mbeya na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage wakati wa kikao chake na mameneja Tanesco wa mikoa na wilaya katika Nyanda za Juu Kusini Magharibi na makandarasi wanaotekeleza miradi ya REA ya usambazaji umeme vijijini, Awamu ya pili katika kanda hiyo.
Alisema serikali imechukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa suala hilo limekuwa likichelewesha utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijijini pamoja na kuigharimu serikali fedha nyingi ambazo zinapaswa kutumika katika kuongeza kasi ya usambazaji umeme katika maeneo hayo.
Suala hilo la baadhi ya wananchi vijijini kukwamisha miradi ya umeme kwa kudai fidia, lilielezwa pia na baadhi ya makandarasi wanaotekeleza miradi hiyo vijijini ambapo limepelekea usitishaji wa ujenzi wa miundombinu ya usambazaji umeme katika sehemu zenye mapingamizi.
Naibu Waziri aliwaagiza makandarasi hao kuhakikisha kuwa wanatoa taarifa kwa wananchi kabla ya kuanza kazi katika maeneo ya wananchi hao ili kujenga uelewa wa pamoja na hivyo kupunguza changamoto za kupinga miradi hiyo ya umeme.
Aidha, Naibu Waziri aliwataka makandarasi hao kuongeza rasilimali watu katika maeneo waliyopangiwa kusambaza umeme ili miradi hiyo ikamilike Juni mwaka huu kama ambavyo makubaliano kati ya serikali na makandarasi hao yanavyoelekeza.
“Ongezeni wakandarasi katika maeneo mnayofanyia kazi na kama mna changamoto yoyote wasilianeni na Wakala wa Nishati Vijijini ili changamoto hizo zitatuliwe na miradi hii ikamilike kwa wakati,” Mwijage.
Alisema makandarasi watakaozembea katika ukamilishaji wa miradi ya umeme, Awamu ya Pili, hawatapata nafasi ya kushindanishwa katika mchakato wa kuwapata makandarasi watakaopewa kazi ya kusambaza umeme vijijini Awamu ya Tatu.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter,Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.