MWANANCHI
Mvua kubwa iliyonyesha kwa siku mbili mfululizo tangu juzi imesababisha vifo vya watu watano huku mamia wakikosa makazi baada ya nyumba zao kubomolewa.
Mvua hiyo iliyofikia kipimo cha milimita 132.5 kwa mujibu wa vipimo vilivyofanywa katika kituo cha Shule ya Msingi ya Maktaba, ilisababisha barabara kujaa maji na nyingine kuharibika na madaraja kadhaa kukatika.
Mkurugenzi Mkuu wa Hali ya Hewa, Dk Agnes Kijazi alisema jana kwamba kipimo hicho cha mvua ni cha juu mno kulinganisha na kile cha wastani ambacho ni kati ya milimita 16 na 30.
“Kwa takwimu za mwezi Mei, kiwango hiki hakijawahi kufikiwa kwa miaka 10 iliyopita.” Alipotakiwa kufafanua miezi mingine, Dk Kijazi alisema hakuwa na takwimu kwa kuwa alikuwa nje ya ofisi.
Awali, Dk Kijazi alitoa taarifa ikisema mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kuwa “hali ya mvua inatarajiwa kuendelea katika baadhi ya siku hadi Mei 20, mwaka huu”.
“Mamlaka inaendelea kushauri wakazi wa maeneo hatarishi pamoja na watumiaji wa bahari kuchukua tahadhari,” Dk Kijazi.
Kutokana na mafuriko hayo, watu watano wakiwamo watoto wawili, walipoteza maisha baada ya kusombwa na maji.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alisema waliopoteza maisha ni watoto wawili na mzee mmoja ambao majina yao hayajafahamika.
Hata hivyo, habari zilizopatikana wakati tunakwenda mitamboni zilisema kuwa waliopoteza maisha ni watu watano.
MWANANCHI
Kada wa CCM Ahmed Ismail aliyerusha risasi hewani katika ofisi za Chadema wilayani Bariadi amehukumiwa kwenda jela miezi sita au kulipa faini Sh2,000 baada ya kukutwa na hatia.
Ismail alikuwa akikabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya silaha.
Mwendesha Mashtaka, Yamiko Mlekano alidai mahakamani hapo kuwa Aprili 22, mwaka huu, saa 10 jioni mshtakiwa huyo alikwenda kwenye mkutano wa hadhara wa CCM katika Mtaa wa Isanga akiwa na bastola.
Alidai kuwa siku hiyohiyo, akiwa kwenye msafara wa Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge alitoa silaha hiyo hadharani kisha kufyatua risasi tatu karibu na ofisi za Chadema wilayani humo kinyume cha sheria.
Mshtakiwa alipotakiwa kujitetea kabla ya hukumu, aliomba Mahakama imuonee huruma kwa kuwa hakujua kama ilikuwa ni makosa.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bariadi, Aidon Mwilapwa alitoa hukumu hiyo baada ya kuridhishwa na ushahidi. Mshtakiwa huyo aliachiwa huru baada ya kulipa faini.
Siku ya tukio Ismail alizua taharuki baada ya kufyatua risasi tatu wakati msafara wa Chenge ulipokutana na ule wa Chadema mjini Bariadi, Simiyu.
MWANANCHI
Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), limesema majina ya wapiganaji wa Tanzania waliofariki dunia kwa kushambuliwa na waasi wa ADF huko Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) yatatajwa baada ya miili hiyo kuwasili nchini.
Msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Masanja alisema jana kuwa kwa sasa wanasubiri maelekezo na taratibu za kuleta miili hiyo zikamilike.
Masanja aliwatoa hofu Watanzania kuhusu usalama wa askari wake walioko DRC, wanaoshiriki operesheni ya kulinda amani chini ya vikosi maalumu vya Umoja wa Mataifa.
Meja Masanja alisema kikundi cha wanajeshi 46 ambao ni walinzi wa amani kilisafiri kwa helikopta kutoka Mji wa Abialose kuelekea Mavivi na baada ya kufika walikwenda Mayimoya kwa gari.
“Wakiwa njiani walishambuliwa na ADF kwa silaha za kivita na gari moja kuteketezwa na kusababisha vifo vya askari wetu na wengine 16 kujeruhiwa,”.
Tukio hilo linafanya idadi ya wanajeshi wa Tanzania waliouawa nchini humo kufikia watatu baada ya askari mwingine, Khatibu Mshindo kuuawa Agosti 2013 katika shambulio la bomu lililofanywa na waasi wa kikundi cha M23 kwenye Mji wa Goma ulioko Mashariki mwa DRC.
Msemaji wa Mpango wa Kulinda Amani kutoka Umoja wa Mataifa, DRC, Felix Basse alikaririwa na Shirika la Habari la AFP akisema mashambulizi ya juzi yalifanyika katika Kijiji cha Kikiki kilichoko kilomita 37, Kaskazini-Mashariki mwa mji wa Kivu.
Habari nyingine zilizopatikana jana, zilisema kuwa askari wa Tanzania wameingia msituni kusaka waasi wa Uganda wa ADF walioshiriki mauaji hayo.
Hata hivyo, alisema UN haitakubali kuona suala hilo likijitokeza tena na tayari vikosi vimeongezwa katika eneo lilipotokea mauaji hayo yaliyoacha askari wengine 13 kujeruhiwa.
Wanachama wa Baraza la Usalama la UN, wamelaani mauaji hayo wakisema hatua hiyo inazorotesha jitihada za kuleta amani Mashariki mwa DRC.
MWANANCHI
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe juzi alikutana na Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza na kumwachia maswali manne atakayoyajibu katika kikao cha dharura cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kilichoitishwa na Rais Jakaya Kikwete ili kuokoa hali ya machafuko yanayohofiwa kutokea Burundi.
Kikao hicho kinatarajiwa kufanyika Dar es Salaam, Mei 13, mwaka huu na kuhudhuriwa na marais wa jumuiya hiyo, kitajadili hali ya kisiasa Burundi.
Hofu ya machafuko imejitokeza baada ya Rais Nkurunziza kutaka kugombea tena katika uchaguzi ujao, jambo linalopingwa na vyama vya upinzani na wanaharakati nchini humo.
Juzi, Waziri Membe aliwaongoza mawaziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Balozi Amina Mohammed na Rwanda, Louise Mushikiwabo kuzungumza na Rais Nkurunziza ili kujua ni jinsi ya kutatua mgogoro huo.
Maswali hayo ni kuhusu uchaguzi ujao kama utakuwa wa haki, amani, huru na endapo nchi itatawalika baada ya uchaguzi huo.
“Hatupendi vurugu na ndiyo maana tunataka kukutana kutatua tatizo lililopo,”.
MTANZANIA
Jumuiya ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umeitaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuacha kuendeshwa na wanasiasa na badala yake itangaze mipaka ya majimbo ya uchaguzi kwa mujibu wa sheria.
Imesema kitendo cha kushindwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria na utaratibu unaotaka mipaka ya majimbo itangazwe kila baada ya miaka 10.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar jana, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka, alisema ZEC imepewa jukumu hiyo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ambayo inaipa uwezo tume hiyo ya uchaguzi.
Akisema hatua ya ZEC kukaa kimya hadi na kushindwa kutangaza mipaka mipya ya majimbo inatokana na woga na vitisho vya siasa kutoka kwa vyama vya upinzani.
“Tunapata shaka huenda wamekubaliana au kupata vitisho vya wanasiasa wasiotaka majimbo ya uchaguzi kupitiwa upya, ila ZEC inachotakiwa ni kutimiza wajibu wake wa sheria na si kuzubaishwa na miluzi ya wanasiasa mapepe,”Shaka.
Alisema taarifa za ndani zinaeleza kuwa kazi ya kukagua mipaka ya majimbo iliyokuwa ikifanywa na ZEC imekamilika siku nyingi jambo ambalo UVCCM inajiuliza kwa nini viongozi wake wamekaa kimya hadi sasa.
“Hatua ya kuweka mipaka ya majimbo siyo ya kwanza kufanywa na Tume ya Uchaguzi, ilifanyika hivyo mwaka 2005 lakini mwaka huu tunaona kuna mchezo wa kuigiza unataka kufanywa.
“Maalim Seif ameanza kutoa vitisho kwamba safari hii hatakubali kunyang’anywa urais wa Zanzibar kama ilivyozoeleka katika uchaguzi uliopita… anajua wazi kauli zake hizi zinakwenda kinyume na miiko ya demokrasia huru na zinaweza kusababisha ghasia tena hapa kwetu Zanzibar,” .
MTANZANIA
Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu (CCM), amesema hana muda wa kulumbana na wanasiasa wanaotafuta ubunge kwa kutumia jina lake hasa kwa Ilala.
Amesema hatarudi nyuma kuwatumikia wapiga kura wake na sasa amejikita kuhakikisha anasimamia kutekelezaji Ilani ya Uchaguzi wa CCM na si kubishana na watu wanaotafuta ubunge kwa kutumia mitandao ya jamii ikiwamo facebook.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Zungu alisema kwa siku kadhaa watu watu wasioitakia mema Ilala wamekuwa wakitumia mitandao ya jamii kuchapisha vijarida kwa lengo la kumchafua mbele ya wapiga kura wake jambo ambalo amesema hawawezi kufanikiwa.
“Hizi fedha huwa zinatolewa kwa kigezo na hata matumizi yake huwa yanapangwa na kamati maalumu ambayo mbunge ni mwenyekiti tu na huwezi kuzikuta katika akaunti ya mbunge ila zinaingia katika halmashauri.
“…matumizi ni pamoja na kupanga matumizi ya miradi ya maendeleo lakini mwisho wa siku Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) huzikagua. Je, ni wapi Zungu anahusika, huu ni wakati wa uchaguzi Watanzania watarajie kuyaona mengi kutoka kwa wasaka tonge,” Zungu.
Alisema pamoja na hatua hiyo lakini hatayumba kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa wapiga kura wake.
Zungu aliwataka wanasiasa wanaomezea mate jimbo la Ilala wasiwe na hofu muda ukifika wakutane uwanjani kwa sababu waamuzi wa mwisho ni wapiga kura.
JAMBOLEO
Serikali imeandaa zaidi ya mashahidi 15 kwa ajili ya kutoa ushahidi kwenye kesi ya uchochezi inayomkabili Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Johnson Minja.
Minja alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma jana na kusomewa maelezo ya awali ya kesi inayomkabili. Alikana mashtaka yote mawili ya uchochezi mbele ya Hakimu Rhoda Ngimilanga.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Paul Kadushi alidai kuwa Septemba 6, 2014, mshtakiwa akiwa katika Chuo cha Mipango kilichopo Kata ya Miuji, Manispaa ya Dodoma, alitoa kauli zilizochochea kutendeka kwa kitendo cha jinai kinyume na sheria.
Katika kosa la pili siku hiyohiyo, mshtakiwa alitenda kosa kwa kuzuia ukusanyaji wa kodi kwa kuwachochea wafanyabiashara nchini kutotumia mashine za kielektroniki za kukusanya kodi (EFDs).
Hata hivyo, Minja alikubali baadhi ya maelezo yaliyotolewa baada ya kusomewa na wakili huyo wa Serikali.
Alikubali mahakamani kuwa anatambua kuwapo na sheria ya matumizi ya mashine za kielektroniki kwa ajili ya kukusanyia kodi, sheria ya kukusanya kodi na utambulisho wake uliotolewa mahakamani.
“Ni kweli kuwa Septemba 6 mwaka jana, tulifanya mkutano katika Chuo cha Mipango kwa lengo la kuwapa wafanyabiashara mrejesho wa maendeleo ya mazungumzo yetu na TRA kuhusu matumizi ya EFD ili kuiongezea Serikali mapato bila kuua uchumi wa nchi na mfanyabiashara mwenyewe,” Minja.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 8 na itasikilizwa kwa siku tatu mfululizo hadi Juni 10.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.