NIPASHE
Moto ambao chanzo chake hakijafahamika, umewateketeza ndugu sita wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi Maalum, Profesa Mark Mwandosya usiku wa kuamkia jana eneo la Kipunguni A, Dar es Salaam katika nyumba waliyokuwa wakiishi familia hiyo pamoja na kuteketeza kila kitu kilichokuwepo ndani ya nyumba hiyo.
Waliofariki katika tukio hilo, dada wa Profesa Mwandosya, Celine Egela (50), mume wake Kapteni mstaafu wa Jeshi, David Mpira (60) mdogo wake Samuel Egela (30), wengine ni mtoto wa dada yake Mwandosya, Lucas Mpira (20) pamoja na wajukuu wawili, Celine Emmanuel (9) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili na Pauline Emmanuel (5).
Walioshuhudia tukio hilo, wamesema moto huo uliibuka wakati familia hiyo ikiwa imelala ambapo
Josephat Mwakasita, amesema alikuwa mtu wa kwanza kufika eneo hilo baada ya kusikia sauti ya vilio vya watoto wakiomba msaada kutoka ndani ya nyumba hiyo, alipofika eneo hilo alikuta moto ukiwa tayari umetanda nyumba hiyo.
“Nilishindwa kuingia kuwaokoa majirani zangu, niliomba msaada kwa majirani wengine ambao walifika hapo tukaanza jitihada ya kuwanasua ndani,”– Mwakasita.
Mwakasita amesema almkuta marehemu Mpira akiwa amesimama dirishani akisali.
“Alikuwa akisema Yesu wangu, Yesu wangu, lakini sikuweza kumuokoa kwa sababu moto ulikuwa tayari umetanda eneo kubwa la nyumba,”– Mwakasita.
Mmoja anusurika
Yusuph Lima amesema katika tukio hilo, Emmanuel Mpira ambaye ni baba wa watoto wawili waliofariki, alinusurika kutokana na wakati wa tukio alikuwa amelala nje ya nyumba hiyo kutokana na kulalamika joto, kwa sasa yupo hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiendelea na matibabu ya maradhi yake pamoja na mshtuko.
Mwakasita walikuta maiti za watu hao zikiwa zimelala pamoja kwenye vyumba vitatu tofauti.
Waziri Mwandosya ni miongoni mwa viongozi waliofika eneo hilo kushuhudia tukio hilo pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki.
Wananchi wa eneo hilo wamelalamikia kikosi cha zimamoto kwa kitendo cha kuchelewa licha ya kupewa taarifa mapema.
Kamanda wa Polisi Ilala, Mary Nzuki amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini chanzo cha moto huo.
NIPASHE
Baadhi ya viongozi wa taasisi zinazotuhumiwa kuwa vinara wala rushwa wameshangazwa na ripoti ya utafiti wa AFROBAROMETER na kuhoji vigezo vilivyotumika.
Juzi AFROBAROMETER wakitangaza utafiti wao huku wakitaja taasisi hizo na asilimia zake kwenye mabano kuwa ni Polisi (50), Mamlaka ya Mapato TRA (37), Majaji na Mahakimu (36), TAKUKURU (29), Maofisa wa serikali za mitaa (25), Watumishi wa Umma (25), Wabunge (22) na Rais na Maofisa wa Ikulu (14).
IGP Ernest Mangu amesema kuwa bado hajaipata ripoti ya utafiti huo na kuahidi pindi utakapomfikia atazungumzia japo amesema hawajajua ni vitu gani vilivyobainishwa kwenye utafiti huo na kuifanya Polisi kuwa kinara.
“Tukiupata tutauzungumzia kwani mpaka wamefikia maamuzi haya inawezekana kuna vitu wameviona na sisi hatuvijui,” IGP Mangu.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dk. Edward Hoseah alisema kuwa hayupo tayari kujiingiza katika malumbano yoyote na kwamba yaliyosemwa dhidi ya taasisi yake hayamuumizi kichwa kwa kuwa anajua anachokifanya.
“Katika kundi la watu hawakosekani wabaya wapo ambao hawatafanya vizuri hakuna aliye malaika hata unapokuwa na watoto siyo wote watafanana kwa tabia,” Dk. Hoseah.
Dk. Hoseah ametahadharisha kuwa ifike pahala nchi iheshimike na siyo kila wakati ionekane kuwa ni chafu ama haina maana.
Mkurugenzi wa Elimu TRA, Richard Kayombo amesema utafiti huo haujawafikia zaidi ya kuusikia kwenye vyombo vya habari, huku akisema kuwa kwa upande wa TRA wana idara ya maadili ambayo inafuatilia masuala ya tuhuma pale zinapotajwa na hatua kuchukuliwa, wakiipata ripoti hiyo wataifanyia kazi.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alipohojiwa kuhusu wabunge kutajwa katika ripoti hiyo amesema ni vigumu kujua kwa haraka na inawezekana mazingira hayo kuwapo, kama wabunge wametajwa itabidi wakutane na watafiti hao ili wawaeleze jinsi wabunge wanavyoingia katika rushwa .
MWANANCHI
Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani kipo katika hatua za mwisho kuanzisha mfumo wa kulipa faini zote za makosa ya barabarani kupitia benki na mitandao ya simu za mkononi ili kupunguza malalamiko ya wananchi kuhusu vitendo vya rushwa na vitabu bandia vya faini vinavyotumiwa na baadhi ya askari hao.
“Nina uhakika na ninachokisema mpaka Julai mfumo huu utaanza kutumika, tunataka kuboresha mfumo wa ulipaji faini na kuondokana na mianya ya rushwa inayofanywa na baadhi ya askari wetu kama inavyolalamikiwa na wananchi,” alisema Kamanda Mpinga.
Kamanda Mpinga amesema mfumo huo ulitakiwa kuanza kazi mwaka jana ulishindikana kutokana na ukosefu wa fedha za kununulia vifaa na maandalizi kwa ujumla.
MTANZANIA
Ikiwa imebaki kipindi cha mwezi mmoja kabla ya kuanza zoezi la kuchukua fomu za kugombea Urais, Ubunge na Udiwani, Waziri John Pombe Magufuli naye ametajwa kushawishiwa kuchukua fomu ya kugombea Urais huku akihakikishiwa kuungwa mkono na viongozi wa juu wa CCM.
Magufuli hakuwa na mpango wa kugombea nafasi hiyo lakini inasemekana kuwa amepata ushawishi huo kutoka kwa wakubwa hao ambaolengo lao ni kumzuia Edward Lowassa.
Rekodi nzuri ya utendaji wa Magufuli inatajwakuwa na nguvu kubwa ya kumkaribia Lowassa tofauti na wengine.
Mtu mmoja wa ndani kutoka makao makuu ya chama hicho Dar ameongea na gazeti la MTANZANIA kwamba mwanasiasa huyo ameanza kujipanga baada ya kuhakikishiwa kuwa jina lake litapitishwa katika vikao vya uteuzi ndani ya chama.
Nape Nnauye alikaririwa kuwa uteuzi utakaofanywa na vikao vya chama hicho kumpitisha mgombea wake wa Urais utazingatia umakini wa hali ya juu na kuwataka Watanzania kujiandaa kwa kile alichokiita mshangao.
MWANANCHI
Mwanamke mmoja Sophia Nyabohe wa Serengeti mkoa wa Mara amekutwa amefariki kwa kujinyonga siku mbili baada ya kukamatwa kwa ugoni na mumewe nyumbani kwake.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji, Emmanuel Baro amesema baada ya kufumaniwa mwanamke huyo alikimbia kusikojulikana na baadaye kukutwa amejinyonga ndani ya chumba chao.
Mashuhuda wa tukio hilo wamesema baada ya tukio hilo mume wa mwanamke huyo hakumsemesha wala kumuuliza kitu, akawa hali chakula chake wala kuingia ndani ya nyumba hiyo ambapo wanahisi kitendo hicho kilimzidishia mawazo mwanamke huyo akaamua kujinyonga ili kuikwepa aibu hiyo.
Jeshi la Polisi limekirikupokea taarifa hiyo, kwa sasa wanaendelea na uchunguzi.
Nitaendelea kukusogezea kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook