MWANANCHI
Mkazi mmoja wa Kijiji cha Nanja, Kata ya Lepruko, wilayani Monduli, anadaiwa kumuuza mtoto wake wa kumzaa kwa mtu mwingine kwa Sh70,000 kwa madai kuwa ana maisha magumu.
Katika tukio hilo la kushangaza, inadaiwa mwanamke huyo aliamua kumuuza mtoto huyo wa kiume mwenye umri wa miezi minane katikati ya Mei, mwaka huu akiwa ametoka naye mkoani Singida.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nanja, Time Samsoni akizungumza juzi mbele ya Mratibu wa Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA) Tawi la Arusha, Francisca Gaspar alisema walijaribu kumshawishi akamchukue mtoto wake, lakini aligoma.
Mwenyekiti Samsoni alidai kuwa mtu aliyemnunua mtoto huyo anaishi katika Kijiji cha Longonito na ana wadhifa mkubwa kijijini hapo.
“Kwa kweli tulisikitishwa na kitendo hicho cha huyo mwanamke kumuuza mtoto wake kwa Sh 70,000 akisingizia maisha magumu na ameshindwa kumlea,” Samsoni.
Alisema walimwita mwanamke huyo kwenye ofisi ya kitongoji na kumhoji sababu zilizomfanya amuuze mwanaye, lakini aliwaaambia kuwa hana uwezo wa kumhudumia.
Mratibu wa Tawla, Gaspar alisema watahakikisha wanafuatilia suala hilo ili lipatiwe mwafaka. “Lakini tumeambiwa kuwa mama huyo ametoroka baada ya kuhojiwa na viongozi wa hapa kijijini na hajulikani aliko mpaka sasa.”
MWANANCHI
Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini amewajia juu Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Lembrise Kipuyo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya hiyo, Anthony Tesha akiwataka wajiuzulu nyadhifa zao kwa kushindwa kusimamia sheria wilayani humo.
Selasini alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumzia taarifa ya wanawake wa Rombo inayodai kwamba wanakodi wanaume kutoka Kenya ili wafanye nao tendo la ndoa.
Juzi, gazeti hili liliripoti habari iliyomkariri Mkuu wa Wilaya kuwa baadhi ya wanawake wilayani humo, hukodi wanaume kutoka Kenya kwa ajili ya kufanya nao tendo la ndoa baada ya waume zao kupoteza nguvu kutokana na ulevi.
Eneo ambalo limeathirika zaidi na unywaji wa pombe haramu na zinazotengenezwa kiholela bila viwango ni la Kikelelwa lililopo mpakani mwa Kenya na Tanzania.
Taarifa hiyo ilimnukuu Kipuyo wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo na kuitaja Kikelelwa kama eneo linalohitaji kutazamwa kwa jicho la pekee.
“Imefikia mahali wanaume wengi wanashindwa kumudu kufanya tendo la ndoa na kuwalazimu wanawake wao kukodi wanaume kutoka nchi jirani ya Kenya kwa ajili ya tendo hilo,” Kipuyo.
Kauli hiyo iliungwa mkono na baadhi ya wanawake waliozungumza mbele ya mkuu huyo wa wilaya katika operesheni ya kukamata pombe haramu ya gongo kijijini hapo iliyofanyika wiki mbili zilizopita.
Jana, Selasini alikanusha vikali taarifa hizo akidai kuwa siyo sahihi kuwajumuisha wanaume wote wa jimbo lake na ulevi huo au wanawake wote.
“Hiyo kauli haina utafiti wala haijaonyesha ni wanaume wangapi Rombo wana tatizo hilo au ni wanawake wangapi waume zao wana shida hiyo. Siyo sahihi kutoa kauli ya jumla,” .
MWANANCHI
Ushauri unaotolewa mara kwa mara kwa Serikali, taasisi zake na mashirika ya umma umekuwa ukipuuzwa na kusababisha Serikali kuendelea kupoteza fedha nyingi kwa njia ya ufisadi huku Deni la Taifa likizidi kukua, kwa mujibu wa ripoti ya ukaguzi maalumu wa miaka mitano ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Ripoti ya CAG imeweka bayana ufisadi wa takribani Sh600 bilioni zilizochotwa katika matumizi mbalimbali ambayo hayana maelezo ya kutosha na ripoti hiyo maalum inaonyesha kuwa uovu huo umekuwa ukiwezekana kutokana na mapendekezo ya CAG ya kuziba mianya ya upotevu wa fedha, kutofanyiwa kazi.
Kwa mujibu wa uchanganuzi wa Mwananchi, Sh600 bilioni zilizofanyiwa ufisadi, zingeweza kusaidia kupunguza nakisi kwenye bajeti ya Serikali kwa kuelekezwa kwenye wizara tatu ambazo ni Ofisi ya Rais, iliyopangiwa Sh587 bilioni, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi (Sh68.8 bilioni) na Ofisi ya Makamu wa Rais (Sh112 bilioni).
Pia, fedha hizo zingeweza kujenga vyumba 8,000 vya madarasa kwa gharama ya Sh75 milioni kila kimoja au kuwezesha vijana zaidi ya mara 12 ya fedha zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete, au kujenga kilomita 600 za barabara kwa kiwango cha lami.
Ukaguzi huo maalumu ulifanywa ili kuangalia kama rasilimali zilizotengwa zimetumika kwa ufanisi kwa kuzingatia kiwango cha fedha kilichowekezwa, tija na ufanisi kama ilivyotarajiwa na kupitishwa na Bunge kwenye maeneo kadhaa, inaeleza ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mapendekezo ya CAG yalitolewa katika ripoti tano za ukaguzi wa ufanisi za miaka ya nyuma kwenye maeneo ya usimamizi wa udhibiti wa athari za mafuriko kwa Serikali, mikoa na serikali za mitaa uliofanyika kwa kutumia mafuriko yaliyowahi kutokea Babati (2007).
Sehemu nyingi za matokeo ya uchunguzi kwenye ripoti hiyo zinaonyesha kuwa utekelezaji wa mapendekezo ya CAG ulifanywa chini ya asilimia 50.
MWANANCHI
Baada ya vifo vya wakimbizi kutoka Burundi kufikia 40, Serikali imelazimika kuongeza idadi ya kambi za wakimbizi ili kupunguza msongamano Nyarugusu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Isaac Nantanga alisema jana kuwa hali iliyopo kwenye Kambi ya Nyarugusu siyo ya kuridhisha.
Alisema wakimbizi waliopo kambini ni 29,145 na ambao hawajaingia wakiwa katika uwanja wa Lake Tanganyika ni 4,729
Nantanga alisema Serikali imelazimika kuongeza kambi moja katika eneo hilo litakaloitwa Nyarugusu 2.
Alisema wameshaanza kuwahamisha wakimbizi kutoka kwenye uwanja huo chini ya uangalizi mkali.
“Tumebaini wakimbizi wanabanana sana kwenye kambi moja, kuna wengine wajawazito, wagonjwa wa kipindupindu, hivyo tumelazimika kuongeza kambi ya pili,” Nantanga.
Alisema Serikali inashirikiana na Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR) kuhakikisha huduma za chakula na matibabu zinapatikana.
Nantanga alisema kuhusu suala la ulinzi, Serikali imejipanga kuhakikisha hakuna uhalifu wowote utakaotokea kambini hapo.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Steven Kebwe alisema wanashirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhakikisha wanapeleka timu ya wataalamu maeneo ya Kagunga na Nyarugusu kufanya tathmini na kutoa elimu ya afya.
MWANANCHI
Wakazi wa Mji wa Njombe, jana walikumbwa na taharuki kutokana na mabomu ya machozi yaliyopigwa na Polisi kwa lengo la kutawanya waandamanaji waliokuwa wanapinga mauaji ya mkazi mmoja anayedaiwa kupigwa risasi na askari na mwingine kujeruhiwa.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Franco Kibona alisema jana kuwa hawezi kuzungumzia tuhuma hizo wakati hali ya kiusalama haijatulia.
Kamanda Kibona aliyekuwa eneo la tukio, aliwasihi wananchi kutulia kwani madai yao yanashughulikiwa.
Mauaji hayo yaliyotokea juzi usiku wakati wakazi hao wawili walipokuwa kwenye klabu ya pombe ya Nyondo, Mtaa wa Kambarage.
Wakazi wa eneo hilo walisema kuwa aliyeuawa ni Basil Ngole na majeruhi ni Fred Sanga ambaye amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Njombe.
Wakazi hao walikusanyika hospitalini hapo saa moja asubuhi, huku wakipaza sauti za kulitaka Jeshi la Polisi kugharamia mazishi ya marehemu pamoja na matibabu ya majeruhi.
Kutokana na kadhia hiyo, polisi walifika eneo la tukio na kuwatawanya waandamanaji kwa mabomu na kusababisha mmoja ambaye ni dereva wa bodaboda kujeruhiwa.
Kitendo hicho kiliamsha hasira kwa wananchi ambao waliziba barabara, kwa mawe, na kuchoma magurudumu ya gari.
Majeruhi Sanga akizungumza kwa tabu akiwa hospitalini alisema wakati akiwa katika klabu hiyo, askari wa doria ambao walikuwa hawajavaa sare walifika eneo hilo na kuwaweka wateja chini ya ulinzi.
Alisema hali hiyo ilizua mzozo, ndipo walipolazimika kufyatua risasi ambazo zilimpata yeye na mwenzake aliyefariki dunia.
Mkazi mmoja wa Njombe, Emanuel Filangali alisema kitendo cha baadhi ya polisi kutumia nguvu dhidi ya raia ni cha kulaaniwa.
Alisema kuwa inadaiwa kosa la marehemu na majeruhi ni kunywa pombe nje ya muda katika klabu hiyo.
NIPASHE
Mtu mmoja amefariki dunia baada ya kuanguka ghafla akiwa kwenye foleni ya kwenda kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa teknolojia mpya ya Biometric Voters Registration (BVR).
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea juzi saa 6:30 mchana kwenye kituo cha Lusyoto, kata ya Mpuguso katika eneo la Ushirika, wilayani Rungwe, ikiwa ni siku ya kwanza ya kuanza uandikishaji wa wapigakura wilayani humo.
Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo wamemtaja aliyepoteza maisha kwenye tukio hilo kuwa ni Mary Kabejela anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 60, mkazi wa Ushirika wilayani Rungwe.
Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya mashuhuda walisema Mary akiwa kwenye mstari wa foleni ya kuelekea kwenye chumba cha uandikishaji, ghafla alionyesha kudhoofika na kuishiwa nguvu na kisha kudondoka chini.
Amani Mwaipaya, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alisema baada ya mama huyo kuanguka, wananchi walimwinua na kumpeleka Hospitali ya Wilaya ya Rungwe ya Makandana, ambako alipoteza maisha wakati akipatiwa matibabu.
“Tulimwona akianza kulegea na ghafla akaanguka chini, ndipo tulipomwinua na kumpakia kwenye gari tukampeleka hospitali, lakini wakati daktari akianza kumhudumia alifariki dunia,” Mwaipaya.
Baadhi ya wananchi na viongozi wa kisiasa waliozungumzia tukio hilo, walisema kifo cha mama huyo huwenda pia kimechangiwa na kusimama kwenye foleni kwa muda mrefu kutokana na kasi ndogo ya uandikishaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahamed Msangi, hakupatikana kuthibitisha tukio hilo licha ya simu yake ya mkononi kuita kwa muda mrefu.
Mwandishi wa habari hizi alifika kwenye ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya na kuelezwa kuwa Kamanda Msangi amesafiri kikazi na kwamba kaimu wake, Nyigesa Wankyo pia alikuwa nje ya ofisi kikazi.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Mbeya Mjini, David Mwambigija, maarufu kwa jina la Mzee wa Upako, ambaye yupo wilayani Rungwe kama wakala wa chama chake kwenye kazi hiyo, alisema uandikishaji unafanyika kwa kasi ndogo, hali inayosababisha watu kusimama kwenye foleni kwa muda mrefu na hata kusababisha presha kuwapanda.
“Inawezekana huyu mama akawa amekufa kutokana na presha kupanda, kwani alisimama kwenye foleni tangu asubuhi huku akipigwa na jua kali, kutokana na umri wake kuwa mkubwa huenda presha ilimpanda na kumpelekea kupoteza maisha,” alisema Mwambigija.
Alisema kasi ya uandikishaji siyo nzuri kutokana na watumishi wa serikali waliopewa kazi hiyo kuonekana kama wanajifunza hivyo kutumia muda mrefu kukamilisha kumwandikisha mtu mmoja, hali inayosababisha watu kusimama kwenye foleni kwa muda mrefu.
Mbali na tukio hilo la kifo, zoezi la uandikishaji wapigakura kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura lilianza juzi kwa kusuasua wilayani Rungwe kutokana na madai kwamba mtandao ulikuwa na matatizo.
Kufuatia mtandao kuwa siyo mzuri, idadi kubwa ya vituo vya kuandikishia wapigakura vilichelewa kuanza uandikishaji hadi saa 4:00 asubuhi hali ilipoanza kutengemaa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Veronica Kessy, alikiri kuwapo kwa changamoto katika siku ya kwanza ya uandikishaji, ikiwamo tatizo la mtandao kusumbua.
Alisema hata hivyo tatizo hilo lilikuwa la muda mfupi na baadaye hali ilikuwa nzuri na kasi ya uandikishaji ikaendelea vizuri kama lilivyopangwa katika maeneo mengi.
Kessy alisema ni vituo vichache tu ambavyo zoezi la uandikishwaji wapigakura liliingia dosari kwa kukumbwa na changamoto ndogondogo kama vile kuchelewa kufunguliwa, kujitokeza kwa idadi kubwa ya wananchi kuliko uwezo wa waandikishaji na tatizo la mtandao kusuasua.
Katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya zoezi la uandikishwaji lilianza juzi katika kata 10 zilizopo ndani ya Bonde la Uyole, ambako liliendelea vizuri licha ya wananchi kulalamikia kasi ndogo ya waandikishaji.
Katika kituo cha Isyesye kulitaka kutokea tafrani baada ya wananchi kumshtukia mtu mmoja anayedaiwa kuwa kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukaa pembeni mwa kituo cha kuandikishia wapiga kura akiwa na daftari na kalamu akiorodhesha watu wanaojiandikisha.
Wananchi hao walimjia juu mtu huyo wakitaka kumpiga kabla ya askari wa Jeshi la Polisi kuingilia kati na kumwondoa kwenye eneo hilo kabla hajaanza kushushiwa kipigo.
Awamu ya tatu ya uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapigakura ilianza jana mkoani Dodoma na Tabora utaanza leo, huku Katavi ukiwa umeanza tangu Jumatatu iliyopita.
Awamu ya kwanza ilihusisha mkoa wa Njombe ambayo ulikamilika katikati ya Aprili, wakati awamu ya pili inaendelea katika mikoa ya Ruvuma, Iringa, Lindi na Mtwara.
Uandikishaji huo umekuwa ukilalamikiwa kusuasua kutokana na kasoro kadhaa hususani uchache wa vifaa (BVR kit), uchache wa waandikishaji na vifaa hivyo mara nyingi kukwama kufanya kazi.
NIPASHE
Rais Jakaya Kikwete, amesema atahakikisha anasaini miswada miwili ya habari kabla ya kumalizika kwa mkutano wa 20 wa Bunge la Bajeti unaendelea.
Miswada hiyo ni wa sheria ya kupata habari na wa sheria ya vyombo vya habari huku.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo wakati akifungua mkutano wa kimataifa kuhusu uwajibikaji na uwazi katika serikali, jana jijini Dar es Salaam.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo mbele ya washiriki wa mkutano huo takribani 200 kutoka nchi 65 ambazo ni wanachama wa mpango huo wa kidunia wa kuendesha serikali katika uwajibikaji na uwazi (OPG), wakati akielezea mafanikio yake katika kukuza demokrasia na uwazi kupitia maeneo mbalimbali yakiwamo uhuru wa habari na matumizi ya mitandao ya kijamii.
“Tayari miswada ya habari imeshapelekwa bungeni, ilishapelekwa kwa mara ya kwanza. Ni matumaini yangu wabunge wataijadili kabla ya kumalizika kwa vikao vya bunge la bajeti linaloendelea mjini Dodoma ili nami niweze kuisaini katika muda wangu uliobaki,” alisema Rais Kikwete.
Hata hivyo, Rais Kikwete, hakueleza namna wadau wakiwamo waandishi wa habari watakavyoshirikishwa katika utoaji wa maoni kuhusu miswada hiyo kabla ya kusainiwa kuwa sheria.
Miswada hiyo ilipelekwa bungeni kwa hati ya dharura katika mkutano wa 19, lakini wadau walipinga wakisema serikali ilikuwa na nia mbaya.
Hata hivyo, baada ya wadau kukutana na Spika, Anne Makinda, Spika aliirejesha miswada hiyo kwa Kamati ya Huduma za Jamii ili ipitishwe kwa utaratibu wa kawaida ili kuwapa fursa wadau kushirikishwa.
Alipiulizwa Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, ili kuthibitisha iwapo miswada hiyo kwa mujibu wa kanuni za kibunge imo katika ratiba kwa ajili ya kujadiliwa katika mkutano wa bajeti, hakuwa tayari kulizungumzia jana.
Hivi karibuni, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Saidi Mtanda, alisema tangu kumalizika mkutano wa 19, kamati yake haikupokea miswada hiyo kwa ajili ya kuanza utafutaji wa ,aomi ya wadau.
NIPASHE
Wakati vikao vya maamuzi vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) vikianza kesho, mwanasiasa mkongwe, Amina Salum Ali, amekuwa mwanamke wa kwanza wa daraja lake ndani ya chama hicho kutangaza wazi nia ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema wanawake wamekuwa wanyonge kugombea nafasi za juu za uongozi kwa kukosa fedha, lakini sasa ni wakati mwafaka kwao kujiamini katika jamii kwani uongozi siyo fedha bali ni uzalendo, kujikubali na kujiamini.
“Nimeona nina uzalendo, ninajiamini na ninaweza kuifikisha nchi yangu katika uchumi wa kwanza kwa kutumia rasilimali zetu zikiwamo gesi, mafuta, kilimo na utalii. Ninajiamini kwamba wakati wangu umefika kuwaongoza Watanzania wenzangu kwa kushika nafasi za juu,” alisema mwanasiasa huyo mkongwe.
Amina ambaye aliwahi kushika nafasi za juu za uongozi Zanzibar na Tanzania Bara, ukiwamo uwaziri wa fedha Zanzibar, alisema serikali inatambua mchango wa wanawake katika jamii hivyo kupewa nafasi kubwa kama vile ujaji na uhakimu ili kuongeza zaidi ufanisi wao kiutendaji.
“Wanawake wengi wanaogopa kujitokeza wakihofia kugombea nafasi za juu za uongozi kwamba kunahitaji fedha hivyo wanaishia kuwa wanyonge. Siyo kweli, wajitokeze kwa wingi ili kitimiza ndoto za kuwajibika kwa taifa letu,” alisema.
Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, wanawake wamepigana sana dhidi ya mfumo dume na kwamba baada ya miaka 20 ya maazimio ya Mkutano wa Dunia wa Wanawake uliofanyika mjini Beijing, China mwaka 1995, hali kwa sasa imebadilika na wanawake wanapewa nafasi mbalimbali za uongozi.
Alisema sheria hazitoshelezi kumlinda mwanamke, lakini mfumo dume umepungua kwa kiasi kikubwa hata kama haijafikia asilimia 50 kwa 50.
“Jambo kubwa kwa mwanamke ni kujiamini katika mambo yote… wanawake wa Tanzania hatuna utaratibu wa kuchangiana katika harakati za uchaguzi. Utaratibu wa mwanamke kupata fedha za mitaji kwa hapa nchini bado mgumu hasa katika mabenki lakini tusiogope. Mimi nina amini ninaweza kuiongoza jamii yetu,“ Balozi Amina.
Balozi Amina ametangaza ni ya kuwania nafasi hiyo kubwa kuliko zote nchini wakati kesho vikao vikao vya juu vya maamuzi vikitarajiwa kuanza kwa ajili ya maandalizi ya mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa udiwani, ubunge na urais Oktoba, mwaka huu.
NIPASHE
Mashabiki wa ngumi kutoka sehemu mbalimbali duniani wameliita pambano la ngumi baina ya Mayweather na Pacquiao kuwa ni la kitapeli na wametaka warudishiwe pesa zao za ziada.
Kesi zipatazo 32 zimeshafunguliwa nchini Marekani zikieleza kwamba Pacquiao alipaswa kubainisha kuwa ana jereha lake la beka kwa mashabiki wake kabla ya pambano hilo ambalo Mayweather alishinda kwa pointi za majaji wote watatu baada ya raundi 12 ambapo mashabiki wengi wanaona hazikufanana na promosheni ya pambano lenyewe.
‘Pambano la karne? linaonekana kabisa ni utapeli wa karne, mashitaka hayo yameeleza.
‘Halikuwa pambano zuri wala la kuburudisha, halikuwa na ushindani, lilikuwa linaboa, la taratibu mno na halikuwa na mvuto’…
Mashitaka yalifunguliwa kwa niaba ya baa ya Flights beer iliyolipa kiasi cha milioni 5.2 kwa ajili ya kuonyesha pambano hilo, baa iliyokuwa karibu na uwanja wa ndege wa Los Angeles na imesisitiza kitendo hicho ni sawa na wizi wa wazi.
HABARILEO
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amewaomba radhi wanafunzi wote wa vyuo vikuu nchini, kwa kuchelewa kuwafikishia fedha zao za kujikimu. Hata hivyo, aLIsisitiza kuwa tangu juzi fedha hizo zilishatoka Hazina.
Akizungumza bungeni janaalipokuwa akitoa majibu ya mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM), Mwigulu aliagiza taasisi zinazohusika kuacha shughuli zote, ikiwemo vikao ili kuhakikisha fedha hizo zifike kwa wanafunzi hao jana.
“Serikali imeshatoa fedha, naagiza taasisi zipeleke fedha hizo leo hii hii ili wanafunzi wasome tupate wataalamu wazuri…hii haitatokea tena,” Nchemba.
Awali, Bulaya aliomba Mwongozo wa Mwenyekiti wa Bunge, Lediana Mng’ong’o na alipopewa nafasi, alisema wanafunzi 6,000 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wamegoma kwa kuwa hawajapelekewa fedha hizo na hawana ugomvi na kitu kingine.
Kwa mujibu wa Bulaya, wanafunzi hao wanaipenda Serikali yao, lakini kuchelewa kwa fedha hizo, kumesababisha mateso kwa wanafunzi hao ambao wengi ni watoto wa masikini wanaotokea vijijini, huku wanafunzi wa kike wakiathirika zaidi.
Bulaya alisema hata jana alipokuwa akizungumza bungeni, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph cha Dar es Salaam, kilikuwa kimefikia uamuzi wa kurejesha nyumbani wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza, kutokana na uchelewaji wa fedha hizo na kutaka Serikali ieleze kwa nini imechelewesha fedha hizo.
Alisema kwa utaratibu huo mpya, iliamuliwa kuwa fedha zinazotakiwa kwenda katika mifumo rasmi, ziwe zinapewa kipaumbele kwa kupelekwa kwanza kabla ya maeneo mengine ili uchelewaji wa fedha hizo usitokee tena.
Wanafunzi hao waligoma kuingia madarasani kuendelea na masomo juzi na kufanya mkutano chuoni hapo, kushinikiza Serikali kuwalipa fedha zao za kujikimu.
Kwa mujibu wa mkataba kati yao na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, fedha zinatakiwa kulipwa wiki ya 8 baada ya kusainiwa kwa mkataba baina yao na Serikali, lakini mpaka juzi ilikuwa wiki ya 11 bila malipo hayo.
Wanafunzi hao walisema hawana nia ya kufanya fujo za aina yoyote, bali wanachohitaji ni kupata suluhu ya tatizo hilo, ambalo limewaathiri kimasomo na kisaikolojia.
Waziri wa Mikopo wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO), Shitindi Venance, alinukuliwa akisema kuwa matatizo hayo yanatokana na mfumo mbaya wa mamlaka yenye dhamana ya kukusanya fedha za mikopo kwa walioajiriwa.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Rwekaza Mukandala alikiri madai ya wanafunzi hao 7,000 kati ya zaidi ya 10,000 wanaofadhiliwa na Serikali.
Lakini, alisema tayari amezungumza na Bodi ya Mikopo ambayo imemwahidi kuleta fedha hizo haraka, na kuwaomba wanafunzi kurejea madarasani kuendelea na masomo.
MTANZANIA
Baadhi ya wabunge wamezungumzia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wakisema ufisadi unaoendelea nchini ni matokeo ya kupuuzwa kwa ripoti za mkaguzi huyo.
Maoni ya wabunge hao yametolewa baada ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuibua ufisadi mkubwa katika mamlaka za Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma na Serikali Kuu kwa ukaguzi ulioishia Juni mwaka jana.
Wabunge wengi wamesikitishwa na kitendo cha Serikali kufumbia macho ripoti hizo huku wengine wakisema wabadhirifu wote serikalini ni wezi wanaostahili kushtakiwa na kufilisiwa.
Mbunge wa Lindi Mjini, Salum Baruwani (CUF), alisema kwa mfumo wa sasa ni vigumu ubadhirifu wa fedha za Serikali kukomeshwa kwa vile ni watendaji wanaotakiwa kusimamia ripoti hiyo ndiyo wanaohusika na wizi huo.
“Kesi ya mbuzi huwezi kumpelekea fisi, ninachokiona mimi hapa inabidi CAG apewe meno maana kwa sheria ilivyo CAG akikagua anaishia kutoa ripoti tu baada ya hapo kazi ni ya watu wengine.
“Tumeona udhaifu huo, sisi kama Bunge inabidi tuishauri Serikali ilete sheria tuifanyie mabadiliko CAG aongezewe meno haya mambo yatakwisha,” alisema.
Mbunge wa Longido, Lekule Laizer (CCM), aliitaka Serikali kufungua macho juu ya ripoti za CAG na kueleza kuwa bila hatua kali kuchukuliwa dhidi ya watendaji wabadhirifu fedha nyingi zitaendelea kupotea.
“Hawa watendaji wanaoisababishia Serikali hasara inabidi washitakiwe na wafilisiwe. Mgonjwa bila dawa hawezi kupona lakini pia mwizi bila kukamatwa na kuadhibiwa hawezi kuacha kuiba,” alisema.
Alisema inasikitisha kuona kila mwaka mkaguzi huyo anaendelea kufanya ukaguzi na kubaini uchafu lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa. “Fedha hizi ni sawa na bajeti nzima ya wizara moja lakini zinapotea,” alisema.
Mbunge wa Ngara, Deogratias Ntukamazina (CCM), alisema ubadhirifu wa aina hiyo hauwezi kumalizika iwapo rais wa nchi hatakua mkali kupambana na ubadhirifu.
Ntukamazina anayejulikana kama senior citizen (raia mkongwe), alisema CAG hawezi kuongezewe meno zaidi ya hapo na kwamba kinachotakiwa ni mamlaka ya nchi kulitambua hilo na kulisimamia.
“Utekelezaji wa ripoti hizi ni suala la leadership (uongozi), huwezi kupambana na ufisadi kama wewe si msafi. Katika hili Serikali inabidi ichukue hatua, tunaposema Serikali ni rais, yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuajiri na kuwafukuza hawa watendaji.
“Mchezo huu wa kulindana hatufiki mbali. Mimi siku zote nimekuwa nikikosoa ninapoona Serikali inakosea na baadhi ya mawaziri wamekuwa wakinichukia, lakini nasema rais anatakiwa awe serious (dhamira ya dhati) na hizi ripoti za CAG,” alisema.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.