MWANANCHI
Hatimaye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu itatoa hukumu katika kesi inayowakabili mawaziri wa zamani wa Fedha, Basil Mramba na wa Nishati na Madini, Daniel Yona pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Monja, Juni 30, mwaka huu.
Kesi hiyo inasilikilizwa na jopo la mahakimu watatu, John Utamwa, Sam Rumanyika na Saul Kinemela. Viongozi hao wanakabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.7 bilioni.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya mashahidi saba wa upande wa mashtaka kutoa ushahidi na kuwasilisha vielelezo vyao vilivyopitiwa na mahakama na kuwaona washtakiwa wana kesi ya kujibu hivyo kuwataka watoe utetezi wao dhidi ya mashtaka yanayowakabili.
Katika maandalizi ya kuwasilisha hoja za kushawishi mahakama iwaone washtakiwa hao wana hatia ama la, Jumatatu ijayo mahakama itazipatia pande hizo mbili mwenendo wa kesi nakala ya mwenendo wa kesi ili waweze kuandaa hoja zao za kuishawishi na kuziwasilisha mahakamani.
Kwa mujibu wa kesi hiyo iliyofunguliwa mwaka 2008, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuisababishia Serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha kutokana na kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya M/S Alex Stewart ya Uingereza.
Katika utetezi wa Mgonja, alidai kuwa yeye ndiye aliyemshauri Waziri Mramba kuisamehe kodi kampuni hiyo iliyokuwa ikifanya kazi ya kukagua madini ya dhahabu nchini, kwa sababu kulikuwa na mkataba uliosainiwa Juni, 2003 kati ya kampuni hiyo na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) uliokuwa unaonyesha malipo yafanyike bila ya kukatwa kodi.
MWANANCHI
Mbio za urais zimezidi kupamba moto kwa upande wa upinzani baada ya Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba kutangaza nia ya kugombea nafasi hiyo ya juu kisiasa nchini, akisema ana sifa zote lakini hatakuwa na kinyongo iwapo hatapitishwa na umoja wa vyama vya upinzani.
Profesa Lipumba, ambaye anakuwa mwanasiasa wa tatu kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutangaza nia hiyo baada ya mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi na Dk George Kahangwa wa NCCR-Mageuzi kujitokeza kutaka kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano.
Mwanasiasa mwingine aliyejitokeza kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano ni Maxmillan Lyimbo wa TLP, wakati Hamad Rashid wa Alliance for Democratic Change (ADC na Maalim Sharrif Hamad wa CUF wametangaza kuwania urais wa Zanzibar.
Lipumba, ambaye atakuwa akiwania urais kwa mara ya tano, iwapo atapitishwa na Ukawa ambayo imeamua kusimamia mgombea mmoja atakayeungwa mkono na vyama vinne, alitangaza nia yake juzi mjini Tabora wakati wa mikutano yake ya hadhara ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kupiga kura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25.
“Ninachoomba ni ushirikiano wenu katika safari yangu hii ya kuwania tena urais,” alisema Profesa Lipumba alipokuwa akihutubia wananchi kwenye uwanja wa mpira wa Shule ya Msingi ya Town School mjini hapa.
“Ninajua safari hii, urais (kwa upande wa upinzani) utasimamiwa na Ukawa, lakini naamini mimi ni mwadilifu na nina uwezo wa kuongoza nchi,” Lipumba.
Profesa Lipumba aliwaomba wapenzi na wanachama wa CUF pamoja na Watanzania kwa ujumla, kumuunga mkono katika safari yake hiyo ya kuelekea Ikulu.
Mwenyekiti huyo wa CUF ambaye kitaaluma ni mchumi, alisema ana uwezo na sifa za kuwa rais na kwamba madhumuni makuu ya kutaka kushika madaraka ni kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi na kupambana na ufisadi.
MWANANCHI
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ameliaga rasmi Bunge na kusema kuwa kama atapata nafasi anayoidhamiria basi ataingia kwa mbwembwe ndani ya ukumbi huo.
Membe ni miongoni mwa makada wa CCM wanaotajwa kuwania nafasi ya kuchaguliwa na chama chake kugombea urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25.
Waziri huyo alifanya hivyo jana mara baada ya kujibu hoja zilizotolewa na wabunge kuhusu bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
“Sitaingia ndani sijui nitakuwa nani, labda nikipata hicho ninachodhamiria nitaingia huku kwa mbwembwe,” alisema Membe ambaye amekuwa mbunge wa Mtama kwa miaka 15.
Membe alisema Bunge linaweza kutuhumiana, kunaweza kuwa mabishano lakini inapokuwa maslahi ya Taifa, wanakuwa kitu kimoja.
“Kama nitakosa na nyie ambao mtakaokosa tutaonana huko nje…Chombo hiki ni cha hekima, heshima na elimu,”.
Baada ya kumaliza Naibu Spika, Job Ndugai, alisema Bunge ni elimu na kwamba wanajifunza mengi.
Membe ambaye alisema anasimama kwa mara ya mwisho na bajeti yake kupitishwa jana, awali alipangua hoja mbalimbali za wapinzani.
Mapema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilieleza kuutilia shaka uhusiano wa ‘ghafla’ kati ya Tanzania na Msumbiji uliofikia hatua ya kuondoa malipo ya viza baina ya nchi hizo mbili, kudai kuwa imebaini mbinu chafu za raia wa Msumbiji kupewa vitambulisho vya mzanzibari mkazi ili wapige kura katika Uchaguzi Mkuu Zanzibar.
MTANZANIA
Nyumba za kulala wageni katika Jiji la Arusha na viunga vyake zimeanza kufurika kutokana na makundi ya watu yanayowasili jijini hapa kushuhudia mwanzo wa ‘Safari ya Matumaini’ ya Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, anayoianza rasmi leo.
Mwanasiasa huyo mwenye ushawishi mkubwa miongoni mwa makada wa CCM walioonyesha nia ya kugombea nafasi ya urais kupitia chama hicho, anatarajiwa kutangaza nia leo kuanzia saa 8 mchana katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Kaluta, jijini hapa.
Mtanzania Jumamosi limeshuhudia pilikapilika katikati ya Jiji, Mitaa ya Kaloleni, Makao Mapya, Levolosi na maeneo ya pembezoni ambako kuna nyumba za kulala wageni, baadhi ya watu wakiulizia vyumba ambapo katika nyumba nyingi kuna kibao kinachosomeka ‘vyumba vimejaa’.
Baadhi ya wageni hao ambao walizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotaja majina yao, walisema pamoja na kukosa vyumba, wako tayari kulala nje hadi watakapoianza ‘Safari ya Matumaini’ pamoja na Lowassa.
“Kukosa vyumba si tatizo kwetu, tutalala hata uwanjani, tumesubiri sana siku hii ambayo Mzee (Lowassa) alianza kuitaja tangu mwaka 2013, tunamshukuru Mungu imefika na tutaanza safari ya matumaini pamoja naye,” alisema mmoja wa wageni hao.
Kujaa huko kwa nyumba za kulala wageni, hoteli baadhi ya watu usiku wa kuamkia jana na leo walilazimika kulala kwenye magari.
Taarifa kutoka kambi ya Lowassa zinaeleza kuwa, watu wengi kutoka kada mbalimbali, wanatarajia kushiriki mkutano huo ambao Waziri Mkuu huyo wa zamani pamoja na mambo mengine, atautumia kueleza matarajio yake endapo chama chake kitamteua kugombea urais.
Wazee maarufu, akiwemo Kingunge Ngombale Mwiru, Pancras Ndejembi, Kanali Mwisongo na Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Mirisho Sarakikya, nao pia wanatajwa kushiriki tukio la leo.
Mbali na kufurika kwa wageni katika Jiji la Arusha wanaosubiri kwa hamu hotuba itakayotolewa na Lowassa hii leo, pia mavazi, ikiwamo sare za CCM zenye utambulisho maalumu kwa ajili ya siku hiyo nazo zimepanda bei maradufu.
Maandalizi katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa yalianza tangu juzi mapema asubuhi.
Mkutano huo wa kutangaza nia wa Lowassa kama ambavyo umekuwa ukitangazwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari unatarajiwa kurushwa moja kwa moja pia na vyombo vya habari kutoka ndani na nje ya nchi.
MTANZANIA
Idadi ya makada wanaotajwa kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) sasa inaweza kufikia 30, baada ya wengine wengi kutarajia kujitokeza kuanzia wiki ijayo.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka katika vyanzo mbalimbali vya habari ndani na nje ya CCM zinadai kuwa idadi hiyo inaweza kuongezeka na pengine hata kufikia wagombea 35, kutokana na baadhi ya makada waliohudhuria vikao vya juu vya chama hicho vilivyofanyika wiki iliyopita mjini Dodoma kuonyesha nia ya kuingia katika kinyang’anyiro hicho baada ya kipenga kupulizwa.
Mtoa taarifa mmoja ambaye pia anaongoza kitengo nyeti ndani ya CCM (hatutamtaja jina ili kulinda kibarua chake), alilidokeza gazeti hili kuwa hadi sasa kuna makada 25 ambao wameonyesha nia, miongoni mwao wakiwa ni wale waliokwisha kujitangaza kuwania nafasi hiyo kubwa nchini.
“Tutegemee idadi kuongezeka zaidi baada ya kipenga kupulizwa, wapo waliokuwa na nia muda mrefu na walibaki na siri ya kusubiri kipenga, wapo walioshindwa kujizuia kutokana na shauku ya kutaka nafasi hiyo, ndiyo maana wengine walionyesha nia ya wazi na wengine walijitangaza,” alisema.
Kati ya makada hao 30 wanaotajwa kujitosa kuwania urais, 25 tayari walionyesha nia kwa muda mrefu na wengine kujitangaza kwa nyakati tofauti.
Hata hivyo, kati ya Juni mosi hadi Juni tano, inatarajiwa makada wengi watajitokeza kutangaza nia zao za kuwania urais kupitia CCM.
MTANZANIA
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema kuna haja ya kuwa na sheria itakayowezesha uandikishaji wosia kuwa wa lazima ili kuondokana na migogoro ya kugombania mali za marehemu na unyanyasaji wa wajane na watoto.
Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana, katika maadhimisho ya miaka 25 ya Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) na uzinduzi wa kampeni ya uandishi wa wosia.
Alisema migogoro hiyo kwa kiasi kikubwa inaathiri wanawake na watoto pindi wazazi wa kiume wanapofariki.
“Kama inawezekana nawaomba TAWLA muanzishe mchakato wa kutengeneza sheria ya wosia ili iwe lazima kwa kila mtu kuandika wosia na mimi nitawapa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha suala hilo linafanikiwa,”.
Alisema kuna dhana potofu kuwa kuandika wosia ni kujitabiria kifo, huku wengine wakihofia kuwa wakiandika wosia watauliwa na wanufaika wa wosia ili wamiliki mali walizoachiwa.
“Wananchi watambue kuandika wosia kunasaidia kuondoa matatizo pale mzazi mmoja anapofariki na si uchuro kama wengi wanavyodhani ni kujitabiria kifo,” Pinda.
Alisema wosia huwa ni siri ya anayeandika na hautakiwi kuwekwa wazi kwa wanufaika, isipokuwa kwa mwanasheria na mashahidi wawili ambao huweka bayana mgawanyo wa mali pindi mwandika wosia anapofariki.
NIPASHE
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) , amehoji ziara za viongozi nje ya nchi zinasaidia vipi kukuza uchumi wa nchi kulinganisha na gharama zinazotumika.
Akichangia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuhusu Makadirio, Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2015/2016, jana bungeni, Msigwa alisema, tofauti na ziara za viongozi wa mataifa mengine ambao wanapokwenda nchi za nje wanatangaza uchumi na kutafuta masoko, Tanzania haifanyi hivyo.
“Alipokuja Rais Oboma hapa na ujumbe wake hakuja kushangaa shangaa, alikuwa na watu kutafuta sehemu za kuwekeza kwenye uchumi,” alisema.
Aidha, alisema balozi za Tanzania hazina utangazaji wa uchumi, na kutoa mfano wa ubalozi mmoja wa Tanzania nje ya nchi ambao umeiweka khanga kama kutangaza utalii badala ya kuweka mambo yanayoweza kutangaza fursa za biashara.
“Sisi utalii wetu ni kutangaza khanga na vitenge, hatuna utangazaji wa kiuchumi,” alisema.
Akizungumzia hali za balozi hizo nje ya nchi alisema zinasikitisha kutokana na kuwa hoi na zingine zinakosa hata magari, majengo yamechakaa na mengine yanatoa harufu.
Akichangia wizara hiyo, Mbunge wa Ole (CUF), Rajab Mbarouk, alizungumzia ufisadi unaofanywa na wizara hiyo kwenye safari za viongozi na manunuzi ya tiketi.
Aidha, alisema baadhi ya watumishi waliomaliza muda wao kwenye balozi za Tanzania nje ya nchi wanaendelea kulipwa posho na mishahara.
Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwani Kikwete, alitaka wizara hiyo kuzungumia hali inayojitokeza kwenye mataifa mengine ya nje ya unyanyasaji wa wageni.
Alisema Tanzania imekuwa ikishiriki katka ukombozi wa nchi za Afrika na kutoa mfano nchi ya Afrika Kusini, lakini chakushangaza Watanzania walioko huko wananyanyasika.
NIPASHE
Sakata la vitendo vya mauaji, udhalilishaji na unyanyasaji unaofanywa na askari wa hifadhi za taifa limewaunganisha wabunge bila kujali itikadi zao za vyama kulitaka bunge kuunda kamati ya kufuatilia mgogoro huo na kauli ya serikali kuhusu sakata la utoroshaji wanyama nje ya nchi.
Wabunge hao walitoa hoja hiyo juzi wakati wa kupitisha vifungu vya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, ambapo walisema wafugaji wamekuwa wakiuawa, kudhalilishwa na kunyanyasika huku mifugo yao ikikamatwa na askari wanaolinda hifadhi hiyo kutokana na migogoro ya mipaka.
Walitaka pia serikali iseme ni lini itatoa fidia kwa wananchi walioathirika kutokana na Operesheni Tokomeza.
Akitoa hoja kuhusu suala hilo, Mbunge wa Rombo, Mheshimiwa Joseph Selasini (Chadema), alisema alikuwa kwenye kamati iliyoundwa kuzuia migogoro hiyo na kupata taarifa ya mwanamke mmoja wa Kijiji cha Maweni, aliyebakwa na askari wa tokomeza na kufariki.
“Mheshimiwa mwenyekiti suala hili likiachwa bila kuchukuliwa hatua, litaleta aibu kwa taifa,” alisema. Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema, alisema askari hao wamekuwa wakikamata ng’ombe wa wafugaji na kuwazuia bila kuwalisha kitendo kinachosababisha kufa na wafugaji kutolipwa fidia.
“Tunataka wizara ilaani uzuiiaji wa mifugo ambayo yanaleta mahusiano mabaya kwenye mipaka hiyo,” alisema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (Chadema), alilalamikia tozo kubwa na tabia kandamizi zinazotekelezwa na askari wanyamapori.
Aliitaka wizara hiyo pia kueleza ni lini fidia zitatolewa kwa watu waliothiriwa kutokana na oporesheni tokomeza.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM), alipendekeza kuundwa kwa kanuni ya kukomesha ukatili na kutoa fidia kwa waathirika.
Alisema vitendo vya unyanyasaji wa wanyama kupigwa risasi na askari hao ni kunyume na wanaohusika lazima wachukuliwe hatua. Kwa upande wake , Mbunge wa Longido (CCM), Michael Lekule Laizer, alitaka wabunge wanaotoka eneo la wafugaji na wizara kukaa ili kumaliza jambo hilo kudumisha ujirani mwema.
Aidha, Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo, Livingstone Lusinde (CCM), Pauline Gekul (Chadema) na Ridhiwani Kikwete (CCM), walitaka kujua fidia zitatolewa lini kwa watu walioathirika na migogoro hiyo na kulaani vitendo vya askari hao kupiga mifugo na kuiua.
NIPASHE
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibroad Slaa, leo anatarajiwa kuanza ziara ya siku sita katika mikoa mitatu kwa ajili ya kukagua mwenendo wa uandikishaji wa wapiga kura kupitia mfumo wa kielekroniki wa Biometric Voters Registration (BVR).
Katika taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Tumaini Makene, alitaja mikoa hiyo kuwa Mbeya, Rukwa na Katavi, ambapo pamoja na kukagua zoezi hilo, atafanya mikutano na wananchi kwa lengo la kuwaeleza masuala yanayohusu taifa.
Kupitia mikutano hiyo Dk. Slaa, ataendelea kuwahamasisha Watanzania wenye sifa za kupiga kura, kujiandikisha kwa wingi katika Daftari la kudumu la wapiga kura kutumia mfumo wa BVR.
“Katibu Mkuu atatumia fursa hiyo kukagua shughuli mbalimbali za chama zinazofanywa na viongozi na watendaji katika kanda ya Nyanda za Juu Kusini,” .
Akitoa ratiba kamili ya ziara hiyo, Makene alisema kwamba leo Dk. Slaa atakuwa Mkoa wa Mbeya Wilaya ya Mbozi eneo la Vwawa na kisha kufanya mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Ichenjezya.
Alisema siku ya Jumapili atakuwa mji mdogo wa Tunduma, siku inayofuatia atakwenda mkoa wa Rukwa, huo atakuwa na mkutano kwenye kiwanja cha Stendi ya Chanji mjini Sumbawanga.
Ziara ya kiongozi huyo itahitimishwa juni 2 atakapokuwa Mkoani Katavi, ambapo pamoja na shughuli ya kukagua zoezi hilo atahutubia wananchi.
HABARILEO
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe, amependekeza mfumo wa kupata wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki kutoka Tanzania, ubadilishwe.
Alisema hayo jana mjini hapa, wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa Mwaka wa Fedha wa 2015/2016 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana.
Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, ipo haja ya kubadili mfumo wa kupata wabunge hao kutoka Tanzania, hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa Bunge la Afrika Mashariki ndicho chombo kikuu cha kutunga sheria za Jumuiya.
Alifafanua kwamba sheria hizo kwa mujibu wa Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya, zinapewa nguvu juu ya sheria za nchi wanachama katika masuala ya utekelezaji wa mkataba huo.
Alisema wajumbe wa Bunge hilo wanaruhusiwa kimkataba kuwasilisha hoja na miswada binafsi bungeni kwa majadiliano na uamuzi, lakini fursa hiyo imetumiwa vizuri na wawakilishi wa baadhi ya nchi wanachama kwa maslahi mapana ya nchi zao kuliko ilivyo kwa wawakilishi wa Tanzania.
Kutokana na hali hiyo, alisisitiza umuhimu wa Watanzania kuacha mfumo wa sasa wa kuwapata wabunge hao na kuangalia mfumo utakaopeleka watu watakaokuwa wazalendo na watakaotetea maslahi ya Tanzania, katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kiingereza Waziri huyo aliongeza kwamba kwa kuwa lugha rasmi ya Jumuiya ni Kiingereza na uamuzi ndani ya Bunge hilo unatokana na ushawishi wa hoja unaotokana na ujuzi wa kutosha wa lugha rasmi ya majadiliano, ni vyema Bunge libadili mfumo kabla Taifa halijaharibikiwa kabisa.k
“Tubadilishe mapema iwezekanavyo utaratibu dhaifu na mbovu tuliouendekeza kwa muda mrefu wa kupata wawakilishi wa Taifa letu kwenye chombo hiki adhimu.
“Mfumo huu hauzingatii kabisa uzito wa majukumu yao, uwezo mkubwa kielimu/kiuelewa wa wawakilishi wenzao, na mvutano mkali wa kimaslahi baina ya nchi wanachama unaotaka wawakilishi makini, imara, wazalendo wenye ujuzi, uzoefu na weledi mtambuka na umiliki wa kuridhisha wa lugha ya majadiliano bungeni,“ alisisitiza.
Alisema bila ya uamuzi huo wa makusudi, taifa haliwezi kukwepa sifa ya kuwa wasindikizaji katika mchakato unaoendelea wa mtangamano, ambao umeingia ngazi za kiweledi zaidi ambazo ni Himaya Moja ya Forodha, Soko la Pamoja, Umoja wa Fedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.
Hati za kusafiria Akizungumzia hati kusafiria ya Afrika Mashariki ambayo ilikuwa inatumika ndani ya jumuiya pekee, Dk Mwakyembe alisema kuanzia Novemba mwaka huu itaanza kutumika kimataifa.
Alisema hati hiyo iliyopandishwa hadhi itaanza kutolewa baada ya uzinduzi wake ukataofanywa na wakuu wa nchi wanachama katika mkutano wao unaotarajiwa kufanyika Novemba, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, hatua hiyo inakamilisha juhudi zilizoanza kufanywa tangu Novemba 2013, baada ya maelekezo ya wakuu wa nchi wanachama waliotaka nchi hizo kukamilisha majadiliano ya kuipandisha hadhi Hati ya Kusafiria ya Afrika Mashariki kuwa ya Kimataifa ifikapo mwezi Novemba, 2015.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.