MWANANCHI
Mwenyekiti wa CCM, Simiyu Musa Ntimizi amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumlawiti kijana mmoja mkazi wa Manispaa ya Tabora.
Mwenyekiti huyo alisomewa mashtaka mbele ya hakimu na kudaiwa kufanya koda hilo nyumbani kwake kwa kumrubuni kijana huyo kwa kumnunulia bia mbili kwenye baa moja mjini Tabora kabla ya kutenda kosa hilo.
Wakili Jocktan Rusherwa alidai kuwa baada ya kijana huyo kulewa na kupoteza fahamu, mshtakiwa alimpeleka nyumbani kwake na kufanya kitendo hicho.
Hata hivyo mshtakiwa alikana tuhuma hizo na yupo nje kwa dhamana na wakili kuahirisha kesi hiyo hadi itakaposomwa tena kesho.
MWANANACHI
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amewataka wananchi kuwapima wanaotangaza nia ya kugombea nafasi za urais kama wana maadili ya dhati katika kutokomeza rushwa.
Akizindua Tamasha la Ulamaa la Qaswida katika shule ya Benjamen Mkapa jana, Membe alisema uongozi wa heshima ni ule wenye kuzingatia maadili na unaochukizwa na vitendo vya rushwa.
Alisema rushwa ni kero kubwa kwa wananchi, hivyo viongozi waadilifu pekee ndiyo wanaoweza kumaliza tatizo hilo.
“Wachujeni viongozi wanaotangaza nia ya kuwaongoza, muwapime kama wana maadili ya kutosha, wapimeni kama siyo wala rushwa,..“Rushwa ni tatizo kubwa, viongozi wasio na maadili hawawezi kumaliza tatizo la rushwa. Angalieni ni viongozi gani wenye sifa na maadili.”
Membe alisema watangaza nia hao wanapaswa kupimwa na wananchi hadi kwenye dini zao kama ni watu safi ambao wanafaa kuwaongoza.
Alisema ni vyema wananchi wakatumia muda wa kuwapima viongozi hao katika mambo mbalimbali na kuepuka kuwa wepesi wa kusikiliza kauli na kuzikubali.
“Uongozi wa heshima ni ule wenye maadili. Viongozi bora ni wale watakaochukia vitendo vya rushwa kwa nguvu zote, jamii imechoka kushuhudia vitendo hivi vinavyonyima haki,” .
Kuhusu ndoto yake ya urais, Membe alisema Juni 7, mwaka huu wananchi wakae kwenye runinga zao kwani atatangaza nia ya kugombea urais na kuomba ridhaa kwa CCM. Tayari makada wengine wa CCM wameshaweka hadharani dhamira yao ya kuwania kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu baadaye mwaka huu.
MWANANCHI
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba ametangaza nia yake ya kugombea urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba akieleza jinsi atakavyoivusha Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati utakaopatikana kwa kutoa haki kwa watu wote.
Akitangaza nia hiyo jana kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere katika Chuo cha Mipango Dodoma, Nchemba alisema: “Ahadi yangu kubwa kwenu ni kwamba nitawavusha. Nitawavusha wanaCCM wenzangu pamoja na Watanzania kwa ujumla… wakati ni sasa tunataka Taifa letu lifike kuwa nchi yenye uchumi wa kati,” alisema Nchemba na kuongeza:
“Ninachoomba kutoka kwenu, mniamini na mniunge mkono katika hili… nitawavusha. Lakini tukumbuke kwamba kila mmoja lazima atimize wajibu wake katika utendaji kazi ili tufikie huko tunapotaka kufikia.”
Nchemba aliyekuwa ameongozana na mkewe, Neema na watoto wake watatu, Isaack, Grecious na Joshua pamoja na ndugu jamaa na marafiki, alisisitiza kuwa ili kufikia malengo hayo, lazima nchi iwe na mfumo wa uwajibikaji utakaowezesha kulinda rasilimali za Taifa na kuongeza Pato la Taifa.
Huku akitumia kauli mbiu ya ‘Mabadiliko ni Matendo, Wakati ni Sasa’, ambayo ataitumia katika safari yake ya kuelekea Ikulu, Nchemba aliyetumia dakika 115, kuanzia saa 10.10 jioni hadi saa 11.25 jioni, alisema atapambana na tabia za watu kufanya kazi kwa mazoea, rushwa, ufisadi na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano atakayoiongoza endapo atachaguliwa, itakuwa ya uadilifu na uaminifu.
Alisema iwapo atachaguliwa, ataifanya nchi kuwa ya kipato cha kati sambamba na watu wake, kujenga Taifa linalojitegemea kibajeti na kuwajengea uwezo wananchi kumiliki uchumi wao wenyewe.
Jambo la kwanza na la msingi ni kuitambua ajenda ya Watanzania, Watanzania watamuunga mkono kiongozi kwa kuitambua ajenda yake,” alisema.
Alisema wakati akijitathimini kutangaza nia ya kugombea alikuwa akifahamu ajenda ya Watanzania, huku akisisitiza kuwa umaskini hakuusoma katika vitabu, bali amekulia katika maisha ya kimaskini.
NIPASHE
Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wameishauri serikali ya Burundi kusogeza mbele mwezi mmoja na nusu uchaguzi mkuu nchini humo.
Uchaguzi wa wabunge ulitarajiwa kufanyika Ijumaa wiki hii na wa urais ukipangwa kufanyika mwezi huu.
Hatua hiyo imetokana na kutoimarika kwa hali ya amani na utulivu kufuatia baadhi ya vyama vya upinzani na mashirika yasiyo ya kiserikali kuendelea na maandamano kupinga hatua ya Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza, kutangaza kuwania urais kwa muhula wa tatu.
Taarifa ya kuomba kusogezwa mbele kwa uchaguzi huo ilitolewa jana na wakuu wa nchi hizo katika mkutano wao uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Richard Sezibela, alisema wakuu hao waliishauri serikali ya Burundi kusogeza uchaguzi huo kutokana na nchi hiyo kutotengemaa kisiasa.
Alisema wakuu hao pia walitoa wito kwa makundi yenye silaha kuziweka chini. Pia, waliishauri serikali ya Burundi kuwarejesha raia wake wote waliokimbilia nchi jirani.
Dk. Sezibera alisema wakuu wa EAC pia walitoa wito kwa wadau wa amani ukiwamo Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU), kuingilia kati mgogoro huo.
Waliohudhuria mkutano huo ni Mwenyekiti wa AEC, Rais Jakaya Kikwete (Tanzania); Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta; Rais wa Uganda, Yoweri Museveni huku Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, akihudhuria kama mlezi wa Burundi.
Rwanda iliwakilishwa na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Valentine Rugwaiza huku Burundi ikiwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Allen Nyamizwe.
NIPASHE
Shirika lisilo la Kiserikali la Sikika limewaasa wabunge kuishinikiza serikali iongeze bajeti ya dawa muhimu na vifaa tiba kwa mwaka 2015/16, ili kuhakikisha upatikanaji wa dawa nchini unaongezeka kufikia asilimia 80, kama inavyotarajiwa na mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Aidha, imewataka waishinikize itoe fedha zote zinazoidhinishwa na Bunge kwa wakati, ili kuviwezesha vituo vya huduma za afya vya umma kuondokana na uhaba wa mara kwa mara wa dawa muhimu na vifaa vya tiba, na hivyo kuimarisha afya za wananchi walio wengi.
Wito huo ulitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Sikika, Irenei Kiria (pichani) na kuongeza kuwa wabunge wanapaswa kulichukulia suala hili kwa umuhimu wa kipekee na kuachana na itikadi za vyama, ili kuokoa maisha ya Watanzania, hasa wanaotegemea kupata matibabu katika vituo vya huduma za afya vya umma nchini.
“Ukiangalia bajeti iliyotengwa kwa ajili ya dawa muhimu na vifaa tiba kwa mwaka wa fedha wa mwaka 2015/16, kwenye bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inayosomwa kesho, ni Shilingi bilioni 37 tu kati ya mahitaji halisi ya zaidi ya Shilingi bilioni 500, fedha ambazo ni kidogo sana,” alisema.
Alisema bajeti hiyo imepungua kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na bajeti ya miaka ya nyuma kwa mfano kuanzia mwaka 2011/12, kuonyesha namna serikali isivyotoa kipaumbele kwa eneo hilo lililo muhimu kwa ustawi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kiria alisema mwaka 2011/12, mahitaji halisi ya bajeti ya dawa muhimu na vifaa tiba yalikuwa Sh. bilioni 188, lakini jumla ya bajeti iliyopitishwa ilikuwa Sh. bilioni 123.4, na serikali ikatoa Sh. bilioni 98 (79.4%) ya fedha iliyoidhinishwa.
Alisema mwaka 2012/13 mahitaji halisi ya fedha kwenye eneo hilo yalikuwa Sh. bilioni 198, lakini bajeti iliyopitishwa ilikuwa Sh. bilioni 80.5 na serikali ikatoa fedha zote hizo.
“Japo tatizo likabaki kuwa ni fedha kuchelewa kutolewa kwa wakati na hivyo kuzorotesha utoaji wa huduma kwa wananchi, ikizingatiwa kuwa upatikanaji wa dawa muhimu na vifaa tiba katika vituo vya huduma za afya vya umma, ni moja ya viashiria vya huduma bora za afya katika nchi yoyote ile,” alisema.
Aidha alisema mwaka 2013/14, mahitaji halisi ya fedha yalikuwa Sh. bilioni 549, lakini bajeti iliyoidhinishwa ilikuwa Sh. bilioni 64, na serikali ikatoa Sh. bilioni 50 (78.9%).
Kwa mujibu wa Kiria, mahitaji halisi ya fedha kwa mwaka 2014/15, yalikuwa Sh. bilioni 577, lakini fedha iliyoidhinishwa ilikuwa Sh. bilioni 70.5, na fedha iliyotolewa hadi sasa ni Sh. bilioni 23.5.
NIPASHE
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imesema ilichelewa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kutokana na sababu mbalimbali, zikiwamo kuchelewa kwa fedha kutoka serikalini, marejesho madogo ya mikopo na uchache wa fedha zilizokusanywa.
Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa, alisema HESLB ilishindwa kupeleka fedha kwa wakati kutokana na vyanzo vilivyotegemewa kutoa fedha kuchelewesha huku akisisitiza kuwa fedha iliyokwisha kusanywa haikuweza kutosheleza idadi ya wanafunzi wenye mahitaji.
“Siyo kama inavyoelezwa na vyombo vya habari, mikopo katika mihula yote ya kwanza ilitolewa kwa wakati, katika kipindi hiki cha muhula wa mwisho wa masomo mikopo imechelewa kwa sababu ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya mikopo kuchelewa na urudishaji wa mikopo usioridhisha, Mwaisobwa.
Aidha, alisema mikopo haikuchelewa kupelekwa katika vyuo vyote vyenye wanafunzi wenye mahitaji na kuongeza kuwa hata vyuo vilivyofanya migomo, baadhi ya vitivo vilikuwa vimepatiwa mikopo.
Alisisitiza kuwa HESLB imeshapeleka fedha za mikopo kwenye vyuo vyote na kuwa vyuo ambavyo wanafunzi hawajapokea, vina utaratibu wake wa kuwapatia fedha hizo.
Hivi karibuni, wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini vikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph, Chuo Kikuu cha Iringa na Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu cha Dar es Salaam (DUCE) waligomea masomo kuishinikiza serikali kupitia HESLB kuwapatia fedha za kujikimu.
NIPASHE
Serikali imeombwa kuangalia upya tatizo la ukubwa wa kodi kwa hospitali binafsi kwani lengo kuu ni kutoa hudumu bora kwa gharama nafuu kwa kila Mtanzania.
Ombi hilo lilitolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Regency ya jijini Dar es Salaam (RMC), Dk. Amish Kanabar, wakati wa ujio wa Mwenge wa Uhuru kwenye hospitali hiyo ambao ulizindua jengo jipya la ghorofa 10 la hospitali hiyo.
Alisema hospitali binafsi na za serikali zina lengo la kuwahudumia Watanzania kupata afya bora, hivyo hakuna haja ya kutoza kodi kubwa kwani hali hiyo inazidumaza na kushindwa kukua kwa kasi.
Alisema katika kuhakikisha wanaendelea kutoa huduma bora, RMC imechukua mkopo ghali kutoka benki na hata kuweka rehani hisa za wanachama wake ili kufanikisha ujenzi wa jengo jipya.
“RMC inafanya jitihada kuhakikisha inakuwa chuo cha mafunzo ya uuguzi na utaalam wa tiba na afya ili kupunguza pengo la nguvu kazi katika sekta ya afya Tanzania. Mara zote RMC imekuwa ikishirikiana na sekta ya umma, Manispaa ya Ilala na Lions Club ya Dar es Salaam Host na Shirika La Nyumba La Taifa, “ alisema.
Alisema hospitali inatoa huduma kwa wastani wa wagonjwa 500 kwa siku na kwamba upanuzi wa jengo una maslahi mapana kitaifa kama vile kuwezesha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa gharama nafuu, kutekeleza kwa vitendo sera za Mkukuta II na Dira ya Taifa 2025 na kuongeza wigo wa ajira na mafunzo kwenye sekta ya afya Tanzania
MTANZANIA
Utangazaji nia ya kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) umeanza kwa kishindo, huku machifu wote wa Mkoa wa Mbeya wakitarajiwa kumuunga mkono Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Prof. Mark Mwandosya, ambaye leo anatarajiwa kutangaza nia mkoani Mbeya.
Miongoni mwao ni Chifu wa Rungwe, Mbozi na Chifu wa Jiji la Mbeya, Mwashiga ambaye atawaongoza pia wazee wote wa jiji hilo.
Wakati hayo yakijiri, wakazi wa Jiji la Mbeya wakiwamo vijana, pia wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi kumsindikiza Profesa Mwandosya kutangaza nia.
Hafla hiyo inayotarajiwa kufanyika saa nne asubuhi, itafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkapa uliopo eneo la Soko Matola jijini Mbeya.
Katika hafla hiyo, viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa vilivyo nje ya Ukawa wanatarajiwa kuhudhuria ikiwa ni pamoja na kupata nafasi ya kutoa msimamo wao wa kumuunga mkono Profesa Mwandosya.
Vyama hivyo ni TLP, ACT-Wazalendo, APPT- Maendeleo, UDP, PP, SAU na UPDP.
Wakati Mwandosya akiwa Mbeya, Mbunge wa Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere naye anatarajia kutangaza nia ya kuwania urais kijijini kwao Mwitongo wilayani Butiama.
Wakati hayo yakijiri, Mbunge wa Sengerema mkoani Mwanza, William Ngeleja pamoja na Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. Titus Kamani wao wakitarajiwa kutangaza kesho jijini Mwanza.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema siku saba zijazo kuanzia sasa atachukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea urais wa Tanzania.
Alitoa kauli hiyo jana jijini Arusha baada ya kumalizika ibada ya kwanza aliyoshiriki katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Usharika wa Arusha mjini.
“Nimekuja kanisani kuabudu, nimefarijika kwa neno la Mungu. Nataka kusema, nilishatangaza nia miezi saba iliyopita, Desemba mwaka jana,” Nyalandu
Kwa upande waje Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema atatangaza nia ya kuwania urais Juni 6, mwaka huu jimboni kwake Mtama mkoani Lindi.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.