NIPASHE
Serikali imesema kuwa inafanya utaratibu wa kuwalipa fedha takribani Sh. bilioni 19 za waliokuwa wanachama wa Taasisi ya Development Entrepreneurship Community Initiative (Deci).
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, alisema fedha hizo zimehifadhiwa katika akaunti ya Benki Kuu (BoT) na kwamba kinachofanyika sasa ni uangalizi wa kiasi cha michango iliyochangwa na wanachama ili waweze kulipwa kwa usahihi.
“Bado fedha zinashikiliwa BoT uchambuzi unaendelea kufanywa kwa umakini wa hali ya juu, utakapokamilika wanachama wote waliochanga fedha watalipwa,” Mkuya.
Aidha, Waziri Mkuya alisema siyo jambo litakaloweza kuchukua muda mfupi kukamilisha mchakato wa malipo ya wanachama hao, kwani linahitaji muda wa kutosha kufanyiwa kazi kikamilifu, ingawa hakutaja kiasi kilichopo.
Mwaka 2009 serikali ilisitisha shughuli za Deci na kuwafungulia mashtaka wakurugenzi watano wa taasisi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam na Agosti 19, mwaka 2013, walihukumiwa.
NIPASHE
Wabunge wamefichua ufisadi katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, mkoani Kilimanjaro, ambayo watendaji wakuu wa hospitali hiyo wameuziana magari mapya ya serikali kwa bei ya kutupa ya Sh. milioni 8 kila moja.
Ubadhirifu huo ni wa kutisha uliibuliwa jana Bungeni wakati mjadala wa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016.
Mbunge wa Viti Maaalum Chadema, Suzan Lyimo, alisema viongozi wakuu KCMC wameuziana magari aina ya Prado na Nissani Patro kwa bei ya Sh. milioni 8 kila moja mwaka 2013, ambayo yalipelekwa katika hospitali hiyo kwa shughuli mbalimbali.
Alisema kutokana na ubadhirifu huo Mhasibu wa hospitali hiyo, Paulo Muhunya, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Afya (TUGHE), alimjulisha Rais Jakaya Kikwete, kwa kumtumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS) kuhusu ufisadi huo.
Lyimo alisema katika hali ya kushangaza Mhasibu huyo baada ya kutoa taarifa za ubadhirifu huo, Mei 5, mwaka huu, alisimamishwa kazi jambo ambalo linatia mashaka.
“Nchi hii inashangaza inakuweje mtu aliyesaidia kutoa taarifa za kufichua wizi yeye ndiye anaadhibiwa, au ndio utaratibu wa serikali ya CCM kuwalinda wezi,” .
Naye Mbunge wa Viti Maalum Chadema, Congesta Lwamlaza, alisema Serikali ya CCM ni ya kutumbua tu ndiyo maana fedha nyingi zinatengwa kwa mambo ya starehe tu.
NIPASHE
Chama Cha Wapangaji Tanzania, kimeiomba Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kutokubali kuuza nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), zilizopo katikati ya miji hasa Upanga jijini Dar es Salaam, kwa kuwa wanaotaka kuzinunua ni matajiri wachache wenye kiu ya kunufaika na rasilimali za nchi.
Aidha, chama hicho kimeishauri serikali kusitisha upangaji wa muda mrefu kwa nyumba za NHC, ili Watanzania wengi hasa wanaoanza kazi waweze kunufaika na nyumba hizo.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Ndumey Mukama, alisema utafiti wao umebaini kuwa kuna wapangaji wa kudumu NHC ambao sasa wanataka kuuziwa nyumba hizo kwa bei ya kutupa wakati tayari wameshajenga nyumba maeneo mengine.
Alisema wapangaji wa muda mrefu wa NHC hasa maeneo ya mjini kama Dar es Salaam ni watu wenye uwezo ambao wengine wamejenga nyumba nzuri na wanazipangisha kwa dola za Marekani, huku wakiendelea kulipa kodi ndogo NHC.
Alisema wapo wanasiasa wachache na baadhi ya wapangaji wa muda mrefu wanaong’ang’ania kuuziwa nyumba hizo kinyume cha utaratibu.
Aliishauri Serikali iweke sheria ya ukomo wa upangaji wa nyumba za serikali angalau miaka mitano ili kutoa nafasi kwa Watanzania wengi hasa wanaoanza maisha kuweza kupanga nyumba hizo.
Mukama alisema: “Utaratibu wa sasa wa wapangaji kukaa kwa muda mrefu katika nyumba hizo umewajengea kiburi wapangaji hawa na wamefikia hatua ya kutaka kuuziwa nyumba hizi kwa bei chee wakati ni rasilimali ya Watanzania wote. Hawa wanaouwezo wa kununua nyumba zinazojengwa sasa katika maeneo mengine na NHC wakanunue huko.”
Alisema jambo lingine linalowapa kiburi wapangaji wa NHC ni kusikilizwa ‘sana’ na serikali hata pale ambapo wanakiuka masharti ya upangaji.
Chama hicho pia kimeishauri serikali itengeneze sera ya nyumba ambayo itawabana pia wenye nyumba binafsi na kuweka usawa kwenye sekta hiyo.
MWANANCHI
Tofauti na makada wengine Magufuli, jana alichukua fomu kimyakimya bila kutaka kuzungumza lolote.
Badala yake akasema atatafuta muda muafaka wa kuzuwa CCM ambao walianza kwa kutangaza nia kisha baada ya kuchukua fomu kuzungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Ujenzi, Dk John ngumza na vyombo vya habari baada ya kusoma fomu alizopewa na chama chake.
Hata hivyo, kwa kifupi kabisa alisema endapo atapata ridhaa ya kuiongoza nchi atatekeleza Ilani ya CCM na kuwaomba Watanzania wamuombee.
Dk Magufuli ambaye alikuwa amevalia suruali nyeusi na shati la kijani, hakuwa na mbwembwe za wapambe wengi kama ilivyokuwa kwa wagombea wengine.
Alisindikizwa na watu watatu akiwamo, Mbunge wa Nkenge, Assumpter Mshama na wapambe wawili walioshuka katika gari lake.
Kada huyo alichukua fomu yake saa 11.30 jioni na kisha kuondoka zake katika eneo hilo kimyakimya.
MWANANCHI
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja ametangaza nia ya kuwania urais kupitia CCM, huku akiahidi kupambana na mambo sita aliyoyaita maadui wakuu wa nchi ambayo ni umaskini, ujinga, maradhi, rushwa, ufisadi na mmomonyoko wa maadili.
Akitangaza nia hiyo kwenye Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Mwanza jana, Ngeleja alisema anatambua kwamba Watanzania wa leo wanatamani kumpata rais ambaye atapambana kwa dhati na vitendo na maadui hao.
“Nina mikakati madhubuti ya kujibu swali la kiutafiti linaloonyesha kwamba mamlaka, idara na taasisi za umma zenye dhamana kubwa ya maisha ya Watanzania mfano, Polisi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mahakama, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na watendaji wakuu wa taasisi za biashara (CEO) ndiyo wanaoongoza kwa tuhuma za kupokea rushwa,”.
Ngeleja akiwa ameambatana na mkewe, Blandina na Mwenyekiti wa Kamati yake ya Maandalizi, Mbunge wa Magu, Dk Festus Limbu waliingia ukumbini saa sita mchana na kupokewa na makada wa CCM waliohudhuria ambao walitoka maeneo mbalimbali ikiwamo vyuo vikuu, wajumbe wa halmashauri kuu kutoka bara na visiwani, wawakilishi wa wamachinga na wavuvi.
Alisema Watanzania wanatamani kuwa na rais ambaye atasimamia kwa dhati umoja na mshikamano wa kitaifa, Muungano, kulinda amani, kukemea kwa nguvu zote ubaguzi wa dini, kabila, rangi na aina nyingine yoyote ya ubaguzi inayoweza kujitokeza nchini na kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi.
“Historia ya nchi yetu ni ndefu na imepita misukosuko mingi lakini kwa umoja, udugu na mshikamano wetu tumefanikiwa,” .
Hata hivyo alisema hivi sasa rushwa, ufisadi, uvivu na mmomonyoko wa maadili ni maadui wengine walioongezeka kwa kasi.
“Kadri Watanzania tunavyozidi kuongezeka kwa idadi na maadui zetu hawa nao wanazidi kujitanua. Hivyo mbinu, mikakati na silaha za kupambana na maadui hawa lazima zibadilike,” alisema.
Ngeleja alisema baada ya kushauriwa na baadhi ya Watanzania kutoka pande zote za nchi tena wa kada mbalimbali amejitafakari, kujitathmini na kujiridhisha kuwa anayo dhamira ya kweli kuwatumikia Watanzania.
“Nimejitafakari, nimejitathmini na kujiridhisha kwamba ninayo dhamira ya kweli ya kuwatumikia Watanzania kupitia nafasi ya urais. Mbali ya dhamira ya kweli nimejipima kwamba ninao uwezo wa kubeba matarajio ya Watanzania, kupitia utekelezaji wa kaulimbiu yangu isemayo: “Maono Sahihi, Mikakati Thabiti, Matokeo Halisi (MMM),” alisema.
MTANZANIA
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amechukua rasmi fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akisema hana mpango wa kushindwa.
Lowassa aliwasili katika Makao Makuu ya CCM mjini hapa jana saa 10:20 jioni akiambatana na mkewe, Regina huku akisindikizwa na wabunge mbalimbali pamoja na wanachama wa CCM.
Lowassa alisema hawezi kuzungumzia upande wa kushindwa katika safari yake.
“Swali rahisi sana, sina mpango wa kushindwa,” alisema Lowassa alipokuwa akijibu swali aliloulizwa na waandishi wa habari kama atashindwa katika kinyang’anyoro hicho.
Alipoulizwa kuhusu hali ya nchi kuwa na watu wanaoshambuliwa, Lowassa alisema atajenga Serikali itakayojali utu na uhuru wa vyombo vya habari.
“Kwanza nimpe pole yule mwandishi wa MTANZANIA aliyeteswa. Sikubaliani na mambo ya kuingilia uhuru wa watu kuteswa. Serikali yangu itaheshimu uhuru wa vyombo vya habari,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na wanachama wa CCM waliokuwa wamefurika ndani na nje ya ukumbi huo.
Alipoulizwa kwanini anahusishwa na vitendo vya ufisadi, Lowassa aliyekuwa akijibu maswali kwa ufupi, alisema kama kuna mtu ana ushahidi na tuhuma hizo amtaje jina.
“Kama hawakunitaja hawakunihusisha… Mtu anayejiamini aseme, na anitaje. Nachoka na siasa za tuhuma, hatupimi viongozi kwa rekodi za matusi ila tutawapima kwa matendo yao,” alisema.
Kada huyo wa CCM alivitaka vyombo vya habari kutoshabikia tuhuma zisizo na ushahidi, huku akisisitiza kuwa kila mtu apimwe kwa rekodi yake.
Kuhusu uteuzi wa mawaziri, Lowassa hakutaka kulizungumzia akisema bado hajavuka daraja.
Kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa, alisema ni sera ya CCM iliyotekelezwa baada ya kutokea mgogoro kati ya vyama vya CCM na CUF.
“Angalieni kule Marekani, vyama vya Democrat na Republican, vinashindana kwa kura chache sana. Hata sisi tunapishana kwa kura chache, mimi nadhani kama hatupishani sana hivyo hilo ndilo suluhisho,”.
Naelewa matatizo wanayopata watumishi wa CCM, nayaelewa. Mishahara midogo, hawakopesheki, hawana fedha za likizo na hawana uchumi mzuri. Wakati wengine wanajengewa nyumba na mikopo wenyewe hawapati,” Lowassa.
Hata hivyo, alimsifu Rais Jakaya Kikwete kwa kuimarisha uchumi ndani ya chama hicho, lakini akasema akiwa rais atafanya zaidi.
“Tunaweza kufanya zaidi, tusiwe ombaomba. Nilipokuwa mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini tumejenga jengo la ghorofa 22 Dar es Salaam. Tuna viwanja na maeneo mengi. Nikichaguliwa kuwa rais na mwenyekiti nitaangalia hilo…Bila CCM madhubuti nchi yetu itayumba,” .
MTANZANIA
Upelelezi wa kesi inayomkabili Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Mchungaji Josephat Gwajima na wenzake watatu umekamilika na kesi inatarajiwa kuanza usikilizwaji wa awali Julai 2, mwaka huu.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro aliifahamisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana wakati kesi hiyo ilipokuwa inatajwa.
Mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa, Kimaro alidai kesi ilikuwa inatajwa, lakini upelelezi wa kesi hiyo umekamilika hivyo aliomba tarehe nyingine ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.
Hakimu Riwa aliyakubali maombi ya upande wa Jamhuri na kuahirisha kesi hadi Julai 2, mwaka huu.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni msaidizi wa askofu huyo, Yekonia Bihagaze, mfanyabiashara George Mzava na mkazi wa Kimara Baruti, Geofrey Milulu .
Katika kesi ya kwanza namba 85, Gwajima anadaiwa kati ya Machi 16 na 25, mwaka huu katika Viwanja vya Tanganyika Packers Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam alitoa lugha ya matusi dhidi ya Askofu wa Kanisa Katoliki, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kwamba ni mtoto, mpuuzi asiye na akili katika namna ya kwamba ingeleta uvunjifu wa amani.
Katika kesi ya pili namba 84, Gwajima anakabiliwa na shtaka moja la kushindwa kuhifadhi silaha na risasi kinyume cha sheria ya uhifadhi wa silaha za moto.
Anadaiwa kwamba kati ya Machi 27 na 29, mwaka huu ndani ya Jiji na Mkoa wa Dar es Salaam, alishindwa kuhifadhi silaha aina ya Beretta namba CAT 5802 , risasi tatu za pisto na risasi 17 za shotgun.
HABARILEO
Baraza Kuu la uongozi la Chama cha Wananchi (CUF) limemchagua kwa kura zote 56 Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa chama hicho, Omar Ali Shehe alisema maalim amepita bila ya mpinzani katika kinyang’anyiro cha nafasi ya urais wa Zanzibar kutokana na imani kubwa ya wanachama wa chama hicho dhidi yake.
Alisema uamuzi huo sasa utamfanya Maalim Seif kumsubiri mgombea kutoka katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya kinyang’anyiro cha nafasi hiyo.
“Chama cha CUF kimebadilisha utaratibu zamani jina la mgombea wa nafasi ya urais linaamuliwa na mkutano mkuu wa chama, lakini tumebadilisha maamuzi hayo kutokana na gharama kubwa za kuitisha mkutano katika chama kichanga kama hiki,” alisema.
Mapema Shehe alitangaza majina ya mwisho ya wagombea wa nafasi ya Uwakilishi na Ubunge katika chama cha CUF katika majimbo 50 ya Unguja na Pemba.
Katika majina hayo yanaonesha kwamba Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa ambaye aliangushwa katika kura za maoni amerudishwa kuwania nafasi hiyo katika jimbo hilo.
Aidha, Mbunge wa jimbo la Mji Mkongwe kwa tiketi ya CUF, Mohamed Ibrahim Sanya ameondolewa katika kinyang’anyiro hicho na nafasi yake kuchukuliwa na mwandishi mkongwe aliyekuwa akifanya kazi katika Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Ali Saleh.
Sanya aliibuka nafasi ya kwanza katika mchakato wa kura za maoni huku akimuangusha vibaya kwa kupata kura 21 Ali Saleh ambaye alishika nafasi ya tatu.
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi alipoulizwa kuhusu maamuzi ya Baraza la Kuu la Uongozi wa CUF, alisema baadhi ya vigezo muhimu vilipewa kipaumbele cha kwanza ikiwemo suala zima la matokeo ya kura za maoni kutoka katika majimbo ya uchaguzi kwa wanachama.
Aidha, alisema suala la utekelezaji na kukubalika katika jamii ni suala la pili ambalo lilizingatiwa kwa lengo la kuona mgombea anafanikiwa na kukivusha chama hadi kupata ushindi.
“Vipo vigezo tulivipa kipaumbele cha kwanza ikiwemo matokeo ya awali ya kura za maoni za wanachama katika majimbo ya uchaguzi, lakini pia suala zima la utekelezaji na kukubalika katika jamii,” alisema.
JAMBOLEO
Jeshi la Polisi linamshikilia mkazi wa Mabibo, Salma Said kwa kosa la kujaribu kuiba mtoto katika hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es salaam huku akidai amefanya hivyo ili kulinda ndoa yake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es salaam Camillius Wambura alisema mtuhumiwa alikamatwa na polisi baada ya kupata taarifa kutoka kwa uongozi wa hospitrali hiyo.
Wambura alisema mtuhumiwa alifika hospitalini hapo na kuwadanganya wenzake kuwa amejifungua mtoto njiti huku akionekana kujificha wakati wauguxi wakipita kuangalia wagonjwa mbalimbali katika wodi ya wazazi.
“Mtuhumiwa alikamatwa na muuguzi wa zamu wakati akijaribu kuiba mtoto katika wodi ya wazazi, alikamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria” alisema Mganga mkuu wa hospitali hiyo.
Mtuhumiwa huyo alidai kuwa ameamua kufanya hivyo ili kulinda ndoa yake, na hadi sasa ana watoto wawili ambao kila mmoja ana baba yake na wanahudumiwa na mwanaume anayeishi naye kwa sasa, hivyo alifanya hivyo ili kudumisha ndoa yake zaidi.
Hata hivyo mama mkwe wa mtuhumiwa alikana na kudai hamtambui na kudai si mke halali wa mtoto wake licha ya familia yake ma familia hiyo ilikana kumtolea dhamana mtuhumiwa huyo
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.