MWANANCHI
Mfanyabiashara wa Moshi Mjini, Lenana Marealle amejikuta matatani baada ya kuwekwa mahabusi kwa saa tatu kwa amri ya jaji baada ya kuvuta sigara eneo la Mahakama Kuu Kanda ya Moshi.
Moshi wa sigara unadaiwa kuingia kwenye vyumba vya mahakama na kusababisha Jaji Mfawidhi, Aishiel Sumari, mawakili na karani wa mahakama kuanza kukohoa mfululizo.
Hili linaweza kuwa tukio la kwanza kwa mhimili wa Dola kutumia mamlaka yake kuzuia uvutaji wa sigara kwenye maeneo ya wazi ya umma licha ya Sheria inayosimamizi bidhaa za tumbaku ya mwaka 2003 kuharamisha.
Tukio hilo limekuja miezi minne tangu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid kutoa agizo la kuzuia uvutaji wa sigara hadharani ikiwamo katika ofisi za umma.
Kwa mujibu wa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Benard Mpepo, Marealle aliwekwa mahabusu iliyopo mahakamani hapo kuanzia saa tano asubuhi hadi saa nane mchana.
Mpepo alisema Marealle aliwekwa mahabusi kwa kosa la kuidharau mahakama chini ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu kifungu 114 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Bunge mwaka 2002.
Mpepo alisema adhabu ya kosa hilo ni kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya Sh500, lakini ilionekana adhabu ya kukaa mahabusi kwa muda huo inatosha kuwa fundisho kwake.
MWANANCHI
Mkurugenzi mkuu wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dk Hassy Kitine, ametangaza nia ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM, akisema “nipeni miaka mitano niirudishe Tanzania ya Mwalimu (Julius) Nyerere”.
Kitine alitangaza nia hiyo jana mjini Dodoma akitumia sehemu kubwa ya hotuba yake kutoa mifano ya utendaji wa muasisi huyo wa Taifa, huku akiwaponda waliotangaza nia wengine na kujisifu kuwa hakuna mwenye sifa za kumfikia, hasa katika elimu.
“Ninataka kuirudisha Tanzania ya Mwalimu Nyerere… sikuwahi kutangaza wala kuonyesha dalili zaidi ya kukaa na kutafakari katika nafsi… najua sitaweza kufanya kama alivyokuwa Mwalimu, lakini nitasimamia katika misingi ya utendaji ya Mwalimu Nyerere,” alisema waziri huyo wa zamani.
Alisema kuwa enzi za uhai wa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema “Ikulu si pa kukimbilia, Ikulu ni shida, Ikulu ni matatizo”, akisisitiza kuwa ofisi hiyo ya mkuu wa nchi ni matatizo na hata yeye anaiogopa.
“Mwalimu alisema ‘ukiona mtu anakimbilia Ikulu kwa namna yoyote ile, na hasa kwa mapesa, mapesa siyo fedha, mapesa, mapesa, mapesa mpaka yanatisha. Huyu mtu akienda Ikulu lazima azirudishe, na (Ikulu) si pa biashara. Sasa anakwenda kufanya biashara gani?’
“Huyu ni wa kuogopa kama ukoma…mimi ninaijua Ikulu kuliko mgombea mwingine yeyote. Nilikuwa Ikulu kama kiongozi, kila mlango wa chumba Ikulu naujua, hata alipolala Baba wa Taifa. Ikulu si pa kukimbilia.
“Nimefanya kazi Ikulu kwa muda mrefu sana, Ikulu ni shida… ninazijua Ikulu zote Tanzania, si pa kukimbilia, Ikulu ni matatizo, matatizo, matatizo. Sasa pamoja na matatizo hayo, nimewiwa kuchukua fomu kwa kuwa sikuona hata anayefaa kati ya waliochukua,” Kitine.
“Wanahangaika kwenda Ikulu, wanahangaika kwelikweli. Wapo waliotangaza nia na kujaza viwanja vya mpira, wanajaza watu, wanafanya mbwembwe. Sasa nikaangalia hivi kweli hawa wanataka kulitumikia Taifa kwa mbwembwe zote hizi au wanataka kurudisha fedha zao?
“Ndiyo maana nikaogopa sana na nimejitokeza mwishomwisho kwa kuwa Ikulu napafahamu sana, si kidogo, sikukimbilia. Naona tabu hata nikichaguliwa, naogopa kwelikweli, kwa sababu najua kuna matatizo sana.”
Alisema akiwa Ikulu na akiwa na miaka 30 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, alikataa lakini Nyerere alimlazimisha, hivyo akamwambia waendelee na watasaidiana.
NIPASHE
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema sheria tatu za makosa ya jinai zilizo mbioni kupitishwa na serikali, zimelenga kuwanyamazisha wapinzani kwenye uchaguzi mkuu ujao, ili wasiweze kuanika madudu ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika taarifa yake iliyopatikana jana jijini Dar es Salaam, Mbowe alizitaja sheria hizo ambazo ama zimesainiwa au zinasubiri saini ya rais kuwa ni pamoja na ile ya Muswada wa Vyombo vya Habari wa Mwaka 2015, Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015 na Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015.
Alisema kuna nia moja tu inayoweza ikaeleza ni kwa nini sheria hizi zimepelekwa mbio mbio, nayo ni kutokana na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
“Uwingi wa sheria hizo mpya kwa pamoja kunaweza kunyamazisha ukosoaji wa kukosekana kwa utawala bora, na kukandamiza kile ambacho kimekuwa ni utamaduni wa vyombo vya habari wa kuchunguza na kuripoti ufisadi, ndani ya serikali,” alisema.
Mbowe alifafanua kwamba, Muswada wa Vyombo vya Habari wa Mwaka 2015, utawazuia waandishi wote na vyombo vya habari kujiendesha, kuwa na baraza lao la habari, isipokuwa waandishi wenye leseni tu.
Aidha alisema muswada huo unalenga kudhibiti machapisho hadi majarida madogo na blogs, na kutoa adhabu kali kwa watakaopatikana na makosa, pamoja na kuyafungia magazeti.
Kwa upande wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015, alisema itaharamisha machapisho ya mtandaoni yanayoonekana na serikali kuwa na habari za kupotosha, udanganyifu au uongo.
Aidha, alisema sheria hiyo inatoa mamlaka kwa polisi ya kukagua nyumba za watuhumiwa, kukamata kompyuta zao na kutaka takwimu zao kutoka kwa watoa huduma wa mitandaoni
“Itakuwa ni kosa la jinai kutuma barua pepe au mawasiliano mengine ya kielektroniki bila ya idhini,” alisema. Kwa upande wa Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015, Mbowe alisema inaharamisha uchapishaji wa takwimu ambazo kwa maoni ya serikali zitakuwa ni za uongo, na adhabu yake itakuwa faini ya Dola 6,000, au hukumu ya miaka mitatu jela.
“Mtafiti au mwandishi anaweza kwenda jela kwa kuchapisha takwimu ambazo serikali haikubaliani nazo,” alisema.
Mbowe alizitaka nchi washirika katika maendeleo na jumuiya ya kimataifa kumsisitiza Rais Jakaya Kikwete kutozisaini sheria hizo, na kuzirudisha tena bungeni ili mambo yote yaliyolenga kuvisambaratisha vyombo vya habari na kukandamiza uhuru wa kujieleza yaweze kuondolewa.
NIPASHE
Wabunge wa vyama vya upinzani mkoani Kilimanjaro wameukoleza mgogoro unaohusu madai kuwa Mkuu wa mkoa huo, Leonidas Gama, anahusika katika uporaji wa ardhi ya wananchi wa Rombo na Vunjo pamoja na kushirikiana na matapeli kutoa hati ya kiwanja cha Mawenzi, baada ya kuamua kuungana na kumwomba Rais Jakaya Kikwete amfute kazi au kumstaafisha kwa manufaa ya umma.
Mbunge wa Vunjo (TLP), Dk. Augustine Mrema, alisema ili kuunusuru mkoa huo kuingia katika mgogoro, anamuomba Rais Kikwete kuingilia kati na kumfuta kazi Gama au kumstaafisha kwa manufaa ya umma kwa madai kuwa ni dalali na mlanguzi anayefanya biashara akiwa mtumishi wa umma.
“Namuomba Rais Kikwete amuondoe Gama Kilimanjaro kwa sababu ya heshima yake na serikali yake. Ni vizuri akamstaafisha kwa manufaa ya umma,” Mrema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, alisema wanachotaka kwa sasa mkuu wa mkoa huo arejeshe Sh. milioni 168 za halmashauri ya wilaya hiyo kwa madai zilitumika kufanya shughuli binafsi wakati wananchi wa Rombo hawakunufaika na shughuli hiyo.
“Lakini pamoja na kumuomba Rais Kikwete amwajibishe mara moja kiongozi huyu (Gama) kwa kutumia madaraka yake vibaya na kujiingiza kwenye biashara chafu; Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imchunguze sambamba na watendaji wote wa serikali waliotumia vibaya madaraka yao kwa kutumia fedha za umma katika kuanzisha kampuni binafsi,” Selasini.
Jumatatu iliyopita, Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Mendeleo ya Makazi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Halima Mdee, alimlipua Gama ikimtuhumu kushiriki katika uporaji Ardhi ya wananchi wa Rombo na Vunjo huku akishirikiana pia na matapeli katika kutoa hati ya kiwanja cha Mawenzi mjini Moshi.
Gama anadaiwa kushirikiana na matapeli hao kwa kutoa hati ya kiwanja cha Mawenzi chenye hati namba C.T 056035 licha ya kumilikiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa zaidi ya miaka 33.
Hata hivyo, Gama jana alikaririwa na vyombo vya habari akikanusha madai yaliyodaiwa na Kambi Rasmi ya Upinzani kwamba anashiriki vitendo vya uporaji wa Ardhi, akisema suala la kuwekeza kwenye ardhi ya Rombo kwa kampuni binafsi ya Jun Yu Investment Internation Company Ltd lilipitishwa kihalali na kikao cha ushauri cha mkoa (RCC) kwa ajili ya kujenga kiwanda cha saruji.
“Kambi ya upinzani ifanye uchunguzi wa madai hayo na kuyatafutia ukweli. Sijawahi kwenda nchini China kwa lengo la kuwatafuta wawekezaji hao, kama inavyodaiwa, hivyo kambi hiyo itafute ukweli juu ya tuhuma wanazozitoa,” Gama.
Alisema mtoto wake, Mayunga Gama, alimweleza kuwa kuna marafiki zake wawili raia wa China wanataka kuwekeza kiwanda cha saruji mkoa wa Dar es Salaam au Bagamoyo.
NIPASHE
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema asilimia 65 ya wanafunzi kwa sasa wanakaa katika madawati huku asilimia iliyobaki wakitarajiwa kumaliziwa tatizo hilo.
Pinda akizungumza jijini Mwanza jana alisema serikali imefanikisha kuwaondoa wanafunzi kukaa mavumbini hadi katika madawati kwa asilimia 65, huku 35 iliyobaki ikitarajiwa kumalizwa wakati wowote.
“Lengo letu ni kutaka kuboresha elimu nchini na kuhakikisha kila shule inakuwa na madawati tofauti na miaka ya nyuma,” alisema.
Aidha, alizitaka halmashauri nchini kuhakikisha kila mwaka zinatenga pesa kwa ajili ya kununulia madawati ili wanafunzi waondokane na kukaa chini ya matofauri ama sakafuni.
Waziri Pinda alisema katika suala la ujenzi wa maabara, lazima ziwe zimekamilika kabla ya Juni 30, mwaka huu kama agizo la Rais Jakaya Kikwete lilivyosema.
Alisema kila halmashauri inatakiwa kuhakikisha shule zote zinamaliza ujenzi wa maabara tatu kabla ya Juni 30 mwaka huu, ili zifanye kazi kuanzia Julai, mwaka huu.
“Kwa sasa serikali imeashaanza kusambaza vifaa kwa halmashauri 75 nchini kwa ajili ya maabara za sayansi katika shule hizo zinazomilikiwa na serikali,” Pinda.
Pia aliziagiza halmashauri za wilaya zote kuhakikisha zinapima maeneo ya shule pamoja na viwanja vyake ili kuepukana na migogoro ya ardhi inayotokea mara kwa mara.
MTANZANIA
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema endapo Kamati Kuu ya CCM haitalipitisha jina lake kuwania urais mwaka huu, kura yake ataipeleka kwa kada wa chama hicho, Profesa Mark Mwandosya.
Amesema atafikia uamuzi huo kwa kile alichodai kuwa yeye na Profesa Mwandosya ndio wanakidhi vigezo 13 vilivyowekwa na CCM kumpata mgombea urais.
Kauli hiyo aliitoa jana mjini Mbeya, alipokuwa akitafuta wadhamini, ambapo alisema Profesa Mwandosya amebahatika kuwa na sifa zote za kiuongozi.
“Sina wasiwasi na mtu huyu, hata kama chama kikiliondoa jina langu, basi kura yangu naipeleka kwake kwani yeye ndiye mwanamume aliyekidhi vigezo vyote vilivyopitishwa na kuhalalishwa na chama,” alisema Membe huku akishangiliwa.
Aliwataka wakazi wa Mkoa wa Mbeya kuhakikisha wanayapitisha majina mawili ya wagombea wa nafasi za urais – jina lake na la Profesa Mwondosya.
Hata hivyo, Membe alionyesha kushangazwa na tabia za baadhi ya watangaza nia kuwa na uchu wa madaraka kwa kutaka nafasi zote mbili za urais na ubunge, hivyo kuwataka wananchi kuwakataa mapema kabla jogoo halijawika.
MTANZANIA
Mkuu wa Operesheni Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, Simon Siro ametoa ushahidi katika kesi inayowakabili Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba na wafuasi wake 30 na kudai mkutano huo ulipigwa marufuku kutokana na taarifa za intelijensia za kuwapo kwa tishio la ugaidi.
Siro aliyaeleza hayo jana mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Cyprian Mkeha, akiwa shahidi wa upande wa mashtaka.
Alidai Januari 23 mwaka huu walipokea barua ya CUF ikiiarifu polisi kuwa Januari 27 mwaka huu wangefanya mkutano na maandamano yenye lengo la kukumbuka watu waliouawa Pemba na kulaani mauaji hayo.
Siro alisema barua hiyo ya CUF ilidai kuwa chama hicho kimekuwa na tabia ya kuwakumbuka watu waliouawa na kuyalaani mauaji hayo kila mwaka, Januari 27.
“Tuliipokea barua hiyo ya CUF Januari 23, 2015 na Januari 24 na 25, timu ya intelejensia ilifanya kazi kuona kama yanaweza kufanyika na kumalizika kwa usalama,” Siro.
Siro alidai pia kuwa kwa kipindi kile yalikuwapo matukio ya unyang’anyi wa silaha katika vituo mbalimbali vya polisi na kwa sababu hiyo jeshi la polisi liliyazuia maandamano na mkutano uliokuwa umepangwa kufanyika, kwa mujibu wa sheria inayoruhusu kufanya hivyo.
Alidai polisi hawakuyaruhusu maandamano hayo ya Januari 27, 2001 na yalikuwa haramu na hata waliouawa hawakuwa wanachama wa CUF pekee bali hata polisi walikuwamo.
Alidai jeshi hilo liliandika barua ya kuyapinga yasifanyike na kumkabidhi Abdul Kambaya kwa niaba ya Katibu wa CUF na walikubaliana kuwa maandamano na mkutano hautakuwapo.
“Niliamini kuwa makubalino tuliyofanya Januari 26 yangetekelezwa lakini Januari 27 majira ya saa 8.00 nilipigiwa simu na Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Kamishna Zakaria ambaye aliniambia kuwa walikuwapo watu wengi wenye mabango katika ofisi ya CUF wilaya ya Temeke.
Tukio la viongozi hao kukamatwa lilitokea Januri 27 mwaka huu wakati Profesa Lipumba na viongozi wenzake walipokamatwa kwa kuitisha mkutano wa hadhara kuadhimisha miaka 14 tangu wafuasi wa chama hicho kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi wakati wakiandamana kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais wa Zanzibar mwaka 2001.
Maandamano hayo ya Januari 27, mwaka huu yalianzia katika ofisi za CUF Temeke yakiongozwa na Lipumba kuelekea viwanja vya Zakhem kwa ajili ya mkutano wa hadhara.
HABARILEO
Leo ni siku ya Bajeti Kuu. Masikio ya Watanzania yataelekezwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano mjini Dodoma wakati Serikali itakapowasilisha Bajeti Kuu ya mwaka 2015/16.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya atasoma hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa kubainisha namna ambavyo Serikali itaweza kukusanya na kutumia kiasi cha Sh trilioni 22.480, ambazo zimeongezeka kutoka zaidi ya Sh trilioni 19 za bajeti ya mwaka jana, ikiwa ni ongezeko la asilimia 13.24.
Kwa siku mbili mfululizo, waziri na maofisa wa wizara ya fedha wamejifungia ndani na Kamati ya Bunge ya Bajeti wakichambua na kupitia kwa kina bajeti hiyo kabla ya kusomwa leo bungeni.
Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima amewataka Watanzania waondoe hofu na kwamba bajeti itakayosomwa leo itakuwa nzuri na kwa manufaa ya wananchi wote.
“Watanzania wategemee bajeti nzuri, tunaweka misingi kwa serikali ijayo kwa kuwa uchui imara zaidi na maisha bora kwa watanzania wote,” alisema.
Aprili 30, mwaka huu, Mkuya alitoa mwelekeo wa bajeti ukiwa ni zaidi ya Sh trilioni 23, huku utegemezi wa fedha za kigeni ukipungua kutoka asilimia 14.8 ya mwaka wa fedha uliopita hadi asilimia 8.4 kwa mwaka ujao wa fedha.
Bajeti ya mwaka 2015/16 inalenga zaidi kupeleka umeme na huduma za maji vijijini, kumalizia miradi ambayo haijakamilika na kutenga fedha kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.
Alisema katika fedha hizo, Sh trilioni 16.71 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh trilioni 5.77 ambayo ni asilimia 25.9 zitatumika kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Alisema serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya Sh trilioni 13.35 sawa na asilimia 90.1 ya mapato ya ndani huku mapato yasiyo ya kodi ni Sh bilioni 949.2 na yale yatokanayo na vyanzo vya halmashauri yanatarajia kuwa Sh bilioni 521.9.
Mkuya alisema Serikali inategemea kukopa kiasi cha Sh trilioni 5.77 kutoka vyanzo vyenye masharti ya kibiashara huku washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh trilioni 1.89 sawa na asilimia 8.4 ya bajeti, ikilinganishwa na asilimia 14.8 ya bajeti ya mwaka 2014/15 ambazo sehemu kubwa ni mikopo ya masharti nafuu.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.