NIPASHE
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, jana alichukua fomu ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisema hakuupata wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), kwa kupewa kama zawadi au urafiki, isipokuwa alikidhi vigezo vya kiongozi aliyetakiwa kutoka Bara la Afrika.
“Ilikuwa ni zamu ya Afrika na ilikuwa lazima atoke Tanzania, bahati ikawa kwa Asha-Rose, lakini si kama inavyofikiriwa kwamba kuna urafiki, zawadi au hisani ilitolewa ndio nikaipata. Uongozi katika UN unapitia mchujo, unachunguzwa kwa muda mrefu na wala hakuna kupewa kazi kwa ujamaa,” Dk. Migiro.
Dk. Migiro alisema alichaguliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutokana na uwezo wake pamoja na sifa alizonazo; ndio maana Katibu Mkuu wa Umoja huo, Ban Ki-Moon, alimkubali pasipo shaka.
Waziri Migiro alisema uamuzi alioufanya wa kutangaza nia ya kugombea urais, unatokana na CCM kupanua wigo wa demokrasia kwa kuwawezesha wanachama wengi zaidi kujitokeza katika mchakato wa kumtafuta kiongozi muhimu wa Taifa.
“Mazingira mazuri na mafanikio yaliyojengwa na kufikiwa na CCM katika awamu zote nne, yamenisukuma mimi kuwa mwanamke wa tatu kutangaza nia ya kugombea nafasi ya urais, kati ya makada wengine 32 waliotangulia; nafarijika sana na wigo wa demokrasia uliopo,” alisisitiza.
Kuhusu vipaumbele vyake akiteuliwa kuwa mgombea urais, Dk. Migiro alisema: “Nasubiri ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayoandaliwa ili niitumie kama nyenzo kuu ambayo itakuwa imetaja maeneo yote muhimu.”
Hata hivyo, Waziri Migiro alisema mafanikio yaliyofikiwa na serikali ya awamu ya nne, yamechochea ukuaji wa uchumi na uboreshaji wa huduma za afya na hivyo kuongeza umri wa kuishi kutoka miaka 45 hadi 60.
Dk. Migiro aliondoka nchini, Januari 5, mwaka 2007 akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, baada ya kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa UN na kuhudumu hadi alipomaliza muda wake, mwezi Januari mwaka 2014.
Baada ya kurejea nchini, aliteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.
Ahadi zilizotolea na Rais Jakaya Kikwete wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 zinawatesa wabunge wengi wa CCM kutokana na baadhi kutokamilika.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wassira amesema yupo tayari kumuunga mkono mgombea yeyote atakayeteuliwa na CCM kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu, endapo nafasi hiyo haitaangukia mikononi mwake.
Pamoja na ahadi hiyo, amesema hawezi kutoa jibu lolote kwa sasa kama atagombea tena au hatagombea ubunge katika jimbo lake la Bunda kwani haijaingia katika kinyang’anyiro hicho cha urais kwa ajili ya kushindwa.
Akizungumza na wanahabari kabla ya kukutana na wadhamini wake zaidi ya 100 waliojitokeza kumdhamini mjini Iringa jana, Wassira alisema; “mimi ni mtu mwenye uzoefu mkubwa wa kuongoza Watanzania, kwa hiyo ninaamini nina fursa kubwa zaidi ya kuwa mgombea.”
Alisema hashangazwi hata kidogo kwani CCM ina hazina ya viongozi wengi wenye sifa za urais japokuwa katika hao waliojitokeza hakuna anayemhofia.
“Tofauti na wale wenzetu, wao wana mtu mmoja mmoja tu katika vyama vyao, ukizungumza CUF utamtaja Lipumba (Ibrahim) na vyama vingine ni vivyo hivyo; ni sasa tu baada ya kuunganisha vyama vyao kupitia umoja usio rasmi angalau unaweza kuona kama wako wengi, lakini kiuhalisia ni wale wale wanaotegemewa na vyama vyao,”alisema.
HABARILEO
Wakati mwili wa Mufti na Shehe Mkuu wa Tanzania, Issa Bin Shaaban Simba aliyefariki dunia jana asubuhi ukitarajiwa kuzikwa leo jioni mkoani Shinyanga, Rais Jakaya Kikweteameungana na Waislamu wote nchini na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA)kuomboleza kifo cha kiongozi huyo wa juu wa kiroho nchini.
Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya familia, Mufti aliyefikwa na mauti akiwa katika Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa sukari na shinikizo la damu, atazikwa leo kutokana na wosia aliokuwa ameuacha kuwa, akiaga dunia mwili wake usiachwe muda mrefu bila kuzikwa.
Hata hivyo, taarifa kutoka Bakwata zinasema kwa upande wao wanatarajiwa kuuhifadhi mwili wa Mufti kesho au keshokutwa, kwani alikuwa mtu wa watu hivyo kuna umuhimu wa kutoa fursa kwa wengi kutoa salamu zao za mwisho kwa mpendwa wao.
Mmoja wa watoto wa marehemu, Selemani Simba alisema mwili utasafirishwa kwa ndege leo saa 3:00 asubuhi kuelekea mkoani Shinyanga, ambako atazikwa katika eneo la Majengo.
“Hali yake ilibadilika siku ya Ijumaa ambapo tulimkimbiza Hospitali ya TMJ ambako baada ya kufanyiwa vipimo ikabainika mapafu yalikuwa yamejaa maji hivyo ilitakiwa afanyiwe upasuaji,” alisema.
Alisema baada ya kufanyiwa upasuaji huo juzi, madaktari waliagiza mgonjwa apewe muda wa kupumzika na asisumbuliwe, hivyo hakuweza kuzungumza na mtu yeyote hadi umauti ulipomfika jana saa 3:45 asubuhi.
Rais Kikwete Katika salamu zake za rambirambi, Rais Kikwete alisema; “Kifo kinaleta huzuni, hata hivyo kifo hakizuiliki, hatuna budi kukikubali na ni wajibu wetu kumuombea Shehe Mkuu kwa Mola wetu ampe mapumziko ya milele”.
“Nawaombea subra wana familia, ndugu, jamaa, Waislamu wote na wana jamii kwani Mufti alikuwa kiongozi katika jamii yetu,” Rais alisema na kueleza kuwa, “Kamwe mchango wake hautasahaulika katika jamii yote kwa ujumla na hakika sote tutamkumbuka.”
Mufti Simba alijiunga na BAKWATA mwaka 1968 na amekuwa mwalimu wa chuo katika mikoa mbalimbali ya Mwanza, Bukoba na mwaka 1970 alikuwa Shehe wa Mkoa wa Shinyanga.
Rais alimwelezea Mufti kama mwalimu katika jamii ambaye alikuwa na uzoefu wa hali ya juu na mwenye kupenda dini yake na kuitumia kwa manufaa ya jamii iliyomzunguka.
“Amekuwa mwalimu imara na mtu wa kutumainiwa na kutegemewa katika Uislamu na jamii kwa ujumla, hakika tutamkumbuka siku zote.”
MWANANCHI
Kambi rasmi ya upinzani bungeni imesema Serikali inatakiwa kukusanya Sh19.6 trilioni kwa mwaka tofauti na malengo iliyojiwekea ya Sh13.4 trilioni, huku ikihoji sababu za miradi ya maendeleo kutegemea mikopo ambayo alisema imeongeza ukubwa wa deni kwa wananchi.
Akiwasilisha Hotuba ya Bajeti Mbadala jana, Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatiaalisema lengo hilo linaweza kufikiwa endepo Serikali itaweka mazingira mazuri na rafiki kwa mlipakodi.
Mbatia, aliyeingia kwa staili ya aina yake akionyesha mkoba uliobeba bajeti, alisindikizwa na Mchungaji Peter Msigwa, ambaye ni mbunge wa Iringa Mjini, Moses Machali (Kigoma Kasulu), Salum Barwani (Lindi Mjini) na Mustapha Akonay (Mbulu).
Mbatia alitaja njia nyingine za kuongeza mapato kuwa ni kupunguza misamaha ya kodi isiyokuwa na tija hadi kufikia asilimia moja ya Pato la Taifa, kuongeza ufanisi Bandari ya Dar es Salaam na kuweka mazingira mazuri na endelevu katika sekta ya utalii.
Mbatia alirejea wito wa kila mwaka wa wapinzani wa kutaka juhudi zaidi kuwekwa katika kupanua wigo wa vyanzo vya mapato katika sekta kama uvuvi, maliasili, nyumba na ardhi.
Alisema Serikali ipanue wigo wa kodi, kuweka sera na viwango vya kodi vinavyotabirika na endelevu, kuongeza ufanisi wa TRA kwa asilimia 50 na kudhibiti ukwepaji wa kodi.
“Tutaweza kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi hadi kufikia asilimia 20 mpaka 25. Washindani wetu wakubwa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki wanakusanya mapato kwa asilimia 22 ya Pato la Taifa, na hawana mazingira mazuri ya uwekezaji na rasilimali nyingi kama Tanzania,” Mbatia.
Mbatia aliendelea kubainisha sura ya bajeti mbadala kuwa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi yatakuwa ni Sh18 trilioni na mapato ya halmashauri kuwa Sh848.1 bilioni.
Alisema mikopo na misaada ya kibajeti ni Sh660 bilioni huku mikopo na misaada ya miradi ya maendeleo ikiwa ni Sh1.6 trilioni.
Msemaji huyo wa Kambi ya Upinzani alilinganisha bajeti ya Serikali na bajeti mbadala na kusema bajeti mbadala haina mikopo ya kibiashara, hivyo inalenga kulipunguzia taifa mzigo wa madeni.
“Bajeti ya Serikali ina mikopo ya kibiashara ya asilimia 10, bajeti hii inawaongezea wananchi mzigo wa madeni,” alisema Mbatia ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa na mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.
Alisema hivi sasa kila Mtanzania anadaiwa Sh873,904.56 kutokana na deni la Taifa kuzidi kukua.
MWANANCHI
Watu 23 wamekufa papo hapo na wengine 34 kujeruhiwa baada ya basi la Kampuni yaAnother G kugongana na lori eneo la Kinyanambo A, Mafinga wilayani Mufindi, ikiwa ni takriban miezi mitatu baada ya ajali nyingine iliyoua watu 50 katika wilaya hiyo.
Basi hilo, lifanyalo safari zake kati ya Iringa na Njombe, lilipata ajali hiyo saa 1:45 usiku wa kuamkia jana wakati dereva alipokuwa akijaribu kuyapita magari mengine kabla ya kugongana uso kwa uso na lori.
Kaimu kamanda wa polisi wa Mkoa wa Iringa, Pudenciana Protas alisema basi hilo lilikuwa likiendeshwa na Nicholaus Mangula na lori la Kampuni ya Bravo Logisticslililokuwa likiendeshwa na Rogers Mdoe na ambalo lililikuwa likitokea Zambia kuelekea Dar es Salaam.
Katika ajali hiyo, dereva wa lori alifariki dunia papo hapo.
Machi 10 mwaka huu, watu 50 walipoteza maisha kwenye ajali iliyotokea Mafinga, Changarawe, wakati kontena lililokuwa limebwa na lori lilipochomoka wakati dereva akijaribu kukwepa mashimo barabarani na kuangukia kwenye lori.
Alisema majeruhi wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Mufindi mjini Mafinga na maiti zimehifadhiwa hospitalini hapo ikiwamo ya dereva wa lori aliyekufa papo hapo.
Alisema chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa basi la Kampuni ya Another G ambaye alikuwa kwenye mwendo kasi na alikuwa akiyapita magari mengine bila tahadhari ndipo alipofika katikati alikutana na lori na kuamua kulichepusha nje ya barabara hali iliyosababisha kupinduka na kisha lori kuligonga basi hilo ubavuni.
Alisema baada ya ajali hiyo, dereva wa basi alikimbia lakini polisi wamemkamata na yupo chini ya ulinzi.
MTANZANIA
Hekaheka za kusaka wadhamini mikoani kwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaowania kugombea urais zimeendelea kushika kasi mikoani.
Wakati hayo yakiendelea, Mwenyekiti Mstaafu na kada mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kagera, Pius Ngeze ametangaza rasmi kumuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika harakati zake za kutafuta kuwa mgombea urais kupitia chama hicho.
Ngeze aliyekuwa miongozi mwa viongozi wa chama hicho mkoani humo waliojumuika katika mapokezi ya Lowassa aliyewasili mjini Bukoba saa 6.00 mchana akitokea Sumbawanga, alisema kama alivyomuunga mkono Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005 na akashinda, pia anamuunga mkono Lowassa.
“Leo ndiyo leo. Kila siku mnaniuliza, Mzee Ngeze uko wapi… Sasa leo nawatangazia rasmi mbele yenu. Kama nilivyomuunga mkono Rais Kikwete mwaka 2005 na akashinda, natangaza Kagera na dunia nzima, namuunga mkono Lowassa… hata kwenye fomu ya udhamini nimekuwa mtu wa kwanza,” alisema Ngeze huku akishangiliwa na umati wa wanachama na wapenzi wa CCM katika ofisi ya chama hicho mkoa.
Akitaja sababu ya kumuunga mkono Lowassa, Ngeze alisema haoni mgombea mwingine wa kumshinda na kwamba ana uamuzi mgumu.
“Ukiangalia wagombea wote walio nyuma yake, yeye ndiye kiongozi pekee anayeweza kuingia Ikulu na kudumisha yale yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete.
“Anajulikana kwa uamuzi mgumu na nchi yetu inahitaji watu wenye uamuzi kama huo. Lowassa hajawahi kuajiriwa na Serikali, tangu alipomaliza chuo kikuu alichukuliwa pamoja na Rais Kikwete na wengine wawili kukitumikia Chama cha Mapinduzi,” Ngeze.
Aliendelea kumwagia sifa Lowassa akisema ndiye aliyejenga shule za sekondari za kata na kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria kwenda mikoa ya Shinyanga na Tabora.
Lowassa akiwashukuru wana CCM waliomdhamini kuwania kuteuliwa kugombea urais kupitia CCM, alisema kupata wadhamini wengi ni kufunga bao la urais.
“Nawashukuru sana kwa mapokezi makubwa mliyonipa. Wadhamini wanaotakiwa kila mkoa ni 30 tu, lakini nikipata 2000, 4000 au 7000 nashukuru kwani inaonyesha imani na upendo wenu kwangu. Imani hujenga imani… Niliwaambia Shinyanga kuwa ukiona watu wengi ujue umefunga bao na ninyi ndiyo mtaniwezesha kufunga,” Lowassa.
Akizungumzia sababu ya kugombea urais, Lowassa alisisitiza kuwa anachukia umasikini hivyo anataka kupambana nao kwa mwendo wa mchakamchaka.
“Nakerwa sana na umasikini. wapo baadhi ya viongozi wanaovaa nguo mbaya wanadhani ni sifa. Ni aibu kuwa masikini, ni aibu kuishi chini ya dola moja kwa siku, nikishinda nitapambana na umasikini kwa mwendo wa mchakamchaka”, Lowasssa.
Alisema ili kufikia maendeleo ya kweli ni lazima kubadilishwa mtazamo wa kazi na watu wafanye kazi kwa bidii.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.