Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema chama chake kimeshindwa kumtangaza mgombea wake wa urais kama ilivyotarajiwa jana, badala yake kikawaomba Watanzania kutokuwa na haraka, wasiwasi wala mihemko na kuwa muda ukifika kitamtangaza.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Magomeni Mwanza, Mbowe aliwaomba wananchi kuuvumilia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa sababu viongozi wake wanaendelea na majadiliano na watakapokubaliana watamtangaza mgombea wao.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema ilikuwa wamtangaze mgombea urais kama ilivyoripotiwa na gazeti hili, lakini wenzao wa CUF wamewaomba kuwa wanaendelea na vikao vyao vya chama.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alisema: “Wengi wana hamu ya kutaka kujua mgombea urais wa Chadema, naomba niseme kwamba tumekuja Mwanza kwa mambo mawili, kuja kuwapokea makamanda hawa wawili na kuitokomeza CCM.
“Ukawa itamsimamisha mgombea urais ambaye Oktoba lazima aiondoe CCM madarakani, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Magdalena Sakaya) ametuomba tena tusubiri hadi tarehe 25 (Jumamosi), kwani watakuwa na kikao cha Baraza Kuu la chama hicho, hivyo tunawasubiri wenzetu.”
Mbowe aliyetumia mkutano huo kuwakabidhi kadi wanachama wapya waliotoka CCM na kujiunga Chadema, Mbunge wa Kahama, James Lembeli na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya, aliweka msisitizo:
“Muungano wetu wa Ukawa ni wa msingi sana, kuna changamoto, tunaomba wananchi muwe wavumilivu, tuache mihemko ili tufikie uamuzi sahihi.
“Tunaomba mtuvumilie, hatuwezi kumtangaza mgombea wetu kwa sababu tu CCM wametangaza wa kwao, hapana! Tutamtangaza mgombea wetu na nyote mtafurahi,” alisema Mbowe huku akishangaliwa na maelfu ya wananchi.
Alisema, Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alikuwa ahudhurie mkutano huo lakini kutokana na foleni za Dar es Salaam alishindwa kuwahi ndege na kwamba, viongozi wengine wa CUF na NCCR Mageuzi walialikwa lakini walikuwa na vikao vya vyama vyao.
Mbowe alisema Ukawa ni mpango wa wananchi, siyo wa viongozi na kwamba ulianzishwa Dodoma na viongozi wote wa upinzani na Kundi la Wabunge 201 wa Bunge Maalumu la Katiba walihudhuria, lakini baadhi yao walipenyezewa ‘kitu kidogo’ wakaondoka hivyo kubaki vyama vinne vya siasa.
MWANANCHI
Kasoro za uandikishaji wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura zilizokuwa zikitokea katika mikoa mbalimbali nchini, zimejitokeza pia jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku ya kwanza ya kazi hiyo.
Mwananchi ilipita katika maeneo mbalimbali jana na kushuhudia wananchi wengi wakiwa wamekutana na changamoto kadhaa kwenye baadhi ya vituo ikiwamo ya kukosekana mashine za Biometric Voters Registration (BVR).
Wananchi hao walisema licha ya kwamba Dar es Salaam imepewa siku 10 ya uandikishaji, kama changamoto hizo hazitachukuliwa hatua kazi hiyo inaweza isikamilike kwa wakati.
Miongoni mwa changamoto nyingine ni kuharibika kwa mashine zilizopo, ukosefu wa umeme, uchache wa watendaji na kuelemewa na watu, mtandao usio wa uhakika na nani aanze kuandikishwa kati ya wenye mahitaji maalumu na wasionayo.
Katika kituo cha uandikishaji cha Shule ya Msingi Oysterbay ambako kuna vituo vidogo vitano, wakala wa uandikishaji, Margereth Galway alisema mwitikio wa vijana umekuwa mkubwa kiasi kwamba inakuwa shida kuwapa nafasi ya upendeleo wazee, viongozi, walemavu au wajawazito na wanaonyonyesha.
“Eneo hili lina wazee na viongozi wengi wa chama na Serikali. Mwitiko mkubwa wa vijana unatufanya tushindwe kuwasaidia watu hao,”Galway.
Alisema wasimamizi wote wa kituo hicho wamekubaliana kuwa kuanzia leo, wateue mashine moja na itengwe kwa ajili ya wenye mahitaji maalumu ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi wanaokuwa wamesimama kwenye foleni muda mrefu.
“Tayari wameshakuja Warioba (Jaji Joseph), Msekwa (Pius) na Butiku (Joseph) wakiwa na wake zao na kujiandikisha. Pamoja na kufahamika kwao bado vijana hawakuwa radhi kuwapisha wakitaka wajipange jambo ambalo ni gumu kulitekeleza.
“Kama tutafanikiwa kuwashawishi waandikishaji basi foleni za watu wa kawaida zitakuwa nne na moja itaachwa kwa ajili ya wenye mahitaji muhimu,” alisema.
Katika Kituo cha Shule ya Msingi Kawe A, wazee wengi walikutwa wamekaa kwenye madawati, nje ya madarasa wakisubiri kuandikishwa baada ya vijana kutokubali kuwapisha wakidai waandaliwe utaratibu ambao hautoingilia foleni iliyopoo.
Katika Shule ya Msingi Hekima iliyopo wilayani Kinondoni, kulikuwa na malalamiko kama hayo na wananchi wakaiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuweka utaratibu maalumu.
Mmoja wa waliofika kujiandikisha, Mwanaidi Abdallah alisema katika uandikishaji huo wanawake wamekuwa wakipata shida kutokana na utaratibu mbovu.
Alisema inachukua muda mrefu kupata huduma kwa sababu baadhi ya vijana wamekuwa wakitumia nguvu kubwa kujiandikisha.
Katika kituo cha Mtendaji kilichopo Mtaa wa Mzimuni, Kata ya Kawe, wananchi walikutwa wakiwa nje saa 8:00 mchana wakisubiri mashine ili uandikishaji uanze licha ya kutangaziwa kazi hiyo ingeanza asubuhi.
Kitu pekee kilichokuwa kinaendelea ni wananchi kujiorodhesha kwenye daftari na kupewa namba ya foleni hadi mashine zitakapoletwa.
MWANANCHI
Baadhi ya wabunge wa Chadema wanaotetea viti vyao wameibuka kidedea katika kura za maoni zilizofanyika katika majimbo mbalimbali nchini jana.
Hao ni pamoja na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ aliyejizolea ushindi mnono wa kura 356 akiwaacha kwa mbali wapinzani wake, Joyce Mashine aliyepata kura43 na Tito Mwanjale kura 18.
Wengine waliokuwa wakiwania kuteuliwa na chama hicho ni Lazaro Mwankemwa aliyepata kura 15, Christopher Nyenyembe (12) na Sishe Simbeye (6).
Mbunge mwingine, aliyepata ushindi wa kishindo ni Highness Kiwia wa Ilemela aliyejizolea kura 134 na aliyemfuatia alikuwa Gasper Mwanaliela ambaye alipata kura 28.
Wabunge wengine, Joshua Nassari hakuwa na mpinzani katika Jimbo la Arumeru Mashariki kama ilivyokuwa kwa David Silinde katika Jimbo la Momba.
Awali, kulizuka tafrani iliyotokana na mgombea, Meshack Kapange kuenguliwa. Mgombea huyo alipinga akidai kuwa hakutendewa haki na kwamba kilichofanyika ni kumkingia kifua Sugu.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema Mbeya Mjini, John Mwambigita alisema Kapange alikwishavuliwa uanachama na suala la kuchukua fomu za kuomba ubunge ilikuwa ni haki ya kila mmoja.
Mkutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na vyama vya siasa kwa ajili ya kusaini maadili ya uchaguzi ya mwaka 2015 jana ulivunjika huku viongozi wa vyama wakiitupia lawama tume kwa kukosa umakini.
Mkutano huo ulianza jijini Dar es Salaam jana, lakini muda mfupi baadaye ulishindwa kuendelea baada ya Mkurugenzi wa Nec, Julius Malaba, kumkaribisha Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar, Hamid Mahamoud Hamid,kusoma maadili ya uchaguzi ya mwaka huu.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa kabla Jaji Hamid kusoma makabrasha yaliyokuwa yameandikwa maadili, Katibu wa Chama Cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi, alisimama na kuomba taarifa.
Muabhi baada ya kuruhusiwa alieleza kuwa vyama vya siasa havina imani na Nec kwa sababu imekiuka makubaliano ya awali ya kutakiwa kupeleka nakala zenye taarifa za maadili ya uchaguzi kwa vyama vya siasa ili viongozi wa vyama wasome na kuchambua kabla ya kufanyika mkutano huo.
“Tulikubaliana katika vikao vilivyopita kwamba maadili haya tuletewe kwanza tuyasome, lakini leo hii mmetuita hapa na kutupatia kabla hatujasoma ili tusaini kinyume cha makubaliano yetu,” alisema.
Muabhi alisema kutokana na Nec kukiuka makubaliano hayo, wanahisi kuna ajenda ya siri, hivyo hawatakuwa tayari kusaini hadi wapate fursa ya kusoma yaliyomo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Philip Mangula, alisema hayo ndiyo yalikuwa makubaliano ya vyama na tume na kubainisha mapungufu mengine kuwa ni ukosefu wa kurasa 13 ndani ya kabrasha lenye maadili lililowasilishwa kwa wajumbe.
“Tume mmetudhalilisha, inaonyesha hamjajipanga, mmetuita kusaini maadili wakati hakuna kurasa 13 humu, hii lazima watu wawajibike,” Mangula.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya mkutano huo kilieleza kuwa kutokana na hali hiyo, Mangula alishauri mkutano huo uahirishwe ili kutoa fursa kwa Nec kujipanga vizuri.
Kufuatia hali hiyo, Jaji Hamid aliwaomba radhi wajumbe kuahidi yatafanyiwa kazi mapungufu yaliyojitokeza.
HABARILEO
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli amesema akifanikiwa kuchaguliwa kuwa kiongozi wa juu wa nchi hii, atahakikisha anatekeleza ipasavyo Ilani ya Uchaguzi wa chama hicho.
Alisema hayo mjini hapa jana jioni alipokuwa akisalimiana na mamia ya wananchi, walioenda kumwona akiwa safarini kutoka nyumbani kwake Chato mkoani Geita kuelekea Dodoma. Alisema ni kwa kutekeleza kikamilifu Ilani hiyo, ndipo maendeleo ya kweli nchini yatapatikana.
Hata hivyo, alisema kuwa atahakikisha analeta maendeleo kwa watu wote bila ubaguzi wa dini, rangi, kabila wala itikadi.
“Maendeleo hayana Chama. Nikifanikiwa kuwa Rais nitaleta maendeleo kwa kila mtu… Kwa wana-Chadema, Wana-Cuf na hata kwa wale wasio na Chama,” Dk Magufuli.
Aidha, alisema akifanikiwa kuwa Rais, atakuwa mtumishi wa watu na kuhakikisha anachagua serikali ya watu makini wasioonea wananchi.
“Namwomba Mwenyezi Mungu nisije kuwa Rais wa kujikweza, wa kujivuna na wa kusahau watu wangu” Dk Magufuli.
Dk Magufuli aliwakosha wananchi na kushangiliwa kwa nguvu pale alipotiririka kwa salamu za makabila mbali mbali nchini, kuanzia Kaskazini hadi Kusini, Mashariki hadi Magharibi mwa Tanzania “Huo ndio Utanzania wetu,” aliwaambia wananchi baada ya kumaliza na kuongeza kuwa atahakikisha anazingatia na kudumisha misingi yote mizuri, iliyoachwa na waasisi wa Taifa hili na marais waliopita.
NIPASHE
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lipo katika mchakato wa mwisho wa kuanzisha kampuni ya kutengeneza nguzo za umeme za zege, ikiwa ni mkakati wa uboreshaji huduma kwa wateja wake, kupunguza matumizi ya nguzo za miti na kudhibiti uharibifu wa miundombinu hiyo.
Mkurugenzi wa Tanesco, Felchesmi Mramba, alisema kampuni hiyo ambayo itakuwa chini ya shirika hilo inatarajiwa kuanza kazi mwishoni mwa mwaka huu mchakato wa kuisajili kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) utakapo kamilika.
Alisema hatua ya shirika hilo kuanza kutumia nguzo za zege badala ya za miti ni moja ya mikakati ya shirika ilo kuhakikisha linatoa huduma bora na za uhakika kwa wateja wake kwani mara nyingi nguzo za miti zimekuwa hazidumu na kulazimika kubadilishwa mara kwa mara kutokana na uchakavu.
“Teknolojia inakuwa kila siku na kurahisisha huduma kwa wananchi na hata wakati mwingine kupunguza gharama, tutakapoanza kuzalisha nguzo za zege tutapunguza kero nyingi kwa wateja wetu kwani nguzo za miti huharibika haraka hasa kipindi cha mvua pamoja nyingine kuungua moto unapotokea,” alisema.
Mramba alisema kutumika kwa nguzo hizo za zege pia kutabadilisha mandhali ya miji na kuongeza kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania.
Kuhusu uboreshaji wa huduma ya umeme kwa jiji la Dar es Salaam, Mramba alisema ujenzi wa vituo vidogo vitano vya usambazaji na upozaji wa umeme unaendelea vizuri pamoja na changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika eneo la Mbagala na Vijibweni na kusababisha kazi hiyo kuchelewa kukamilika.
Alisema vituo hivyo vilitakiwa kuwa tayari mwezi ujao lakini kutokana na changamoto hizo sasa vitakamilika mwishoni mwa mwaka huu na kwamba kituo cha Kinyelezi na City Centre vinategemewa kukamilika Agosti, mwaka huu.
NIPASHE
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro Imemkuta na makosa mawili ya uchochezi ya kujibu Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kislamu Tanzania, Shekh Ponda Issa Ponda.
Kutokana na hali hiyo, Agosti 7, mwaka huu, imepanga kuanza kusikiliza utetezi wake.
Sheikh Ponda atajitetea dhidi ya makosa mawili kati ya matatu yaliyokuwa yakimkabili.
Hakimu wa Mahakama hiyo, Mary Moyo, alisema baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka, Mahakama imemuona mshtakiwa huyo ana kesi ya kujibu katika shtaka la pili na la tatu.
Alisema katika kosa la kwanza mahakama hiyo imeona Ponda ana kesi ya kujibu kwa kuwa shtaka hilo lilitolewa uamuzi na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam baada ya kutupa ombi lake la kufutiwa kesi hiyo hivi karibuni.
Alisema maamuzi yanayotolewa na Mahakama za juu hayawezi kupingwa na mahakama za chini yake.
Alisema mahakama hiyo imeridhika na ushaidi wa upande wa mashtaka ambao ulipeleka mashahidi, mkanda wa video uliorekodiwa katika eneo aambako mshtakiwa huyo alidaiwa kutoa maneno ya uchochezi na nyaraka mbalimbali.
Wakili wa upande huo wa utetezi, Juma Nassoro, alikubaliana na uamuzi wa mahakama hiyo na kuahidi kuwasilisha mashahidi siku hiyo.
Kwa upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Sunday Hyera, uliiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine ya kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa utetezi kwa madai kuwa Wakili Kiongozi wa Serikali, Bernard Kongola hakuwapo mahakamani kutokana na dharura.
Ponda alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Agosti 18, mwaka juzi na kusomewa mashtaka hayo matatu na Wakili Kiongozi wa Serikali, Bernard Kongola.
Kongola alidai kuwa Agosti 10, mwaka 2013 alitoa maneno ya uchochezi katika eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro kwa kuwaambia Waislamu wasikubali kuunda kwa kamati za ulinzi na usalama za misikiti kwa kuwa zimeundwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) ambao ni vibakara wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali.
Aliendelea kudai kuwa Ponda aliwaambia Waislamu hao kuwa kama watajitokeza watu hao na kujitambulisha ni kamati za ulinzi na usalama za misikiti, wafunge milango na madirisha ya msikiti na kuwashambulia kwa kipigo.
Alidai mshtakiwa huyo pia alikiuka amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya Mei 9, mwaka 2013 ya kumtaka kuhubiri amani ndani ya mwaka mmoja wakati akitumikia kifungo cha mwaka mmoja nje.
Alidai Agosti 10, mwaka juzi katika eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro, Sheikh Ponda aliwaambia Waislamu kuwa serikali ilipeleka jeshi mkoani Mtwara kudhibiti vurugu zilizotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu, lakini haikufanya hivyo kwa Loliondo walipokataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo.
Alidai maneno hayo ni ya uchochezi kwa sababu yalikuwa yakiumiza imani za watu wengine kinyume cha sheria.
NIPASHE
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema atafuta umiliki kwa maeneo nchini ambayo yametekelezwa kwa zaidi ya miaka 10 bila ya kuendelezwa.
Lukuvi alitangaza mpango huo katika Kijiji cha Tungamalenga kilichopo Wilaya ya Iringa mkoani hapa, alikokwenda kusikiliza mgogoro wa ardhi baina ya wananchi, wawekezaji , wafugaji na wakulima.
Alisema ametoa agizo hilo nchi nzima kwa watu walionunua ardhi za vijiji zaidi ya hekari 50 na kushindwa kuziendeleza hivyo kugeuka mapori.
Alisema amewaagiza maofisa wa ardhi wa halmashauri na wizara yake kufuatilia ili kujua watu hao wamenunua ardhi hiyo kwa malengo yapi, lini na wameendeleza kwa kiasi gani hadi sasa.
Lukuvi ambaye pia ni Mbunge wa Ismani anayemaliza muda wake, alisema kabla ya kufuta umiliki wa maeneo hayo, maofisa hao watatakiwa kuwapa notisi wamiliki waliyoshindwa kuyaendeleza.
“Kazi ya kuweka akiba ya ardhi haiwezi kuwa kazi yenu ninyi lakini haiwezekani ukatoka jijini Dar es Salaam ukanunua ekari 100 Tungamalenga ukasema unajiwekea akiba ya miaka 20 ijayo mimi sitakubali, “ alisema na kusisitiza kuwa:
“Serikali ya kijiji lazima iwe na akiba ya ardhi kwa vizazi vijavyo na sisi kama serikali kuu lazima tuwe na akiba ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa kitaifa.
Akijibu malalamiko ya wakazi wa kijiji hicho, Lukuvi aliwaagiza maofisa Ardhi wa Halmashauri ya wilaya hiyo kwenda kutoa ufafanuzi wa eneo ambalo limepangwa na serikali kuu na lililoachwa kama akiba ya kijiji.
Kwa upande mwingine aliwaonya viongozi wa vijiji wasiuze ardhi yote kwa wawekezaji ili kudonoa migogoro kwenye maeneo yao.
Nitakutumia stori zote ukibonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.