MWANANCHI
Wakati dunia ikiwa na zaidi ya watu 34 milioni wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU), madaktari nchini Hispania wametangaza kugundua tiba ya ugonjwa huo wanayodai ni uhakika.
Kwa kutumia damu ya kupandikiza kutoka kwenye kitovu mwana (umbilical cord) cha mtu ambaye ana vinasaba ambavyo havipokei virusi hivyo vya Ukimwi, wataalamu hao wa tiba wa Hispania wanaamini kuwa wanaweza kutibu ugonjwa huo baada ya mafanikio waliyopata kwa mgonjwa mmoja.
Madaktari hao wa Kitengo cha Taifa cha Upandikizaji (ONT) cha Hispania walichukua damu ya vitovu mwana vya watu wenye vinasaba ambavyo havipokei VVU na kuipandikiza kwa mtu anayeishi na virusi hivyo. Baada ya miezi mitatu, mgonjwa huyo alipimwa na kuonekana hana virusi.
Daktari wa Programu ya Upandikizaji kutoka Taasisi ya Tiba ya Catalan, Barcelona, Rafael Duarte alisema mgonjwa aliyetibiwa kwa njia hiyo, Timothy Brown (37), alikuwa anaishi na VVU tangu mwaka 2009 na madaktari hao walithibitisha kuwa amepona baada ya kupandikizwa damu hiyo.
Mgonjwa mwingine aliyefanyiwa majaribio ya tiba hiyo alipona VVU, lakini miaka mitatu baadaye alifariki kwa ugonjwa wa saratani.
Timu ya madaktari wa Hispania ililiambia gazeti la kila siku nchini humo la El Mundo kuwa wana uhakika kuwa wameleta mapinduzi katika mapambano ya Ukimwi na magonjwa yanayofanana na hayo.
Dk Duarte alisema mwaka 2015 umekuwa wa kujivunia ugunduzi huo mkubwa duniani, ingawa alitahadharisha kuwa tiba kamili haiwezi kupatikana katika siku za usoni.
Kaimu mkurugenzi wa mwitikio wa Taifa wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk Morris Lekule alisema utafiti kama huo hauna budi kufuata taratibu zote na kuthibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kabla ya kutangazwa kuwa ni tiba sahihi.
“Kila mara taarifa zinakuja zikisema tiba ya Ukimwi imepatikana, lakini tiba kupata uthibitisho kwamba ni sahihi, ni mchakato mrefu unaotakiwa kuhakikisha kama kweli dawa hiyo inatibu na ni lazima WHO wathibitishe hilo,” alisema.
Alisema ni vizuri kama wataalamu hao wakapata uhakika kutoka WHO badala ya kuwapa watu matumaini kuwa kuna tiba na baadaye matumaini hayo yanapotea.
Daktari wa kitengo kinachoshughulika na masuala ya Ukimwi cha WHO, Richard Banda alisema hana taarifa za tiba hiyo. Tiba inavyofanya kazi Madaktari wa ONT walitumia damu ya mtu mwenye vinasaba vya ‘CCR5Delta’ ambavyo seli zake haziathiriwi na virusi hivyo vya Ukimwi.
Dk Duarte alisema kwanza huziua seli za damu ya mgonjwa kwa kutumia mionzi halafu seli mpya (kutoka kwenye damu ya mtu mwenye seli zisizoathiriwa na VVU hupandikizwa. Damu hiyo ilipandikizwa kwa mgonjwa mwenye virusi hivyo na saratani ya damu.
Baada ya seli hizo kupandikizwa, Virusi vya Ukimwi vilivyo kwenye damu ya mgonjwa hushindwa kujipenyeza katika seli mpya zilizopandikizwa. “Siku 11 baada ya upandikizaji, mgonjwa wa Barcelona alianza kupata nafuu na baada ya miezi mitatu, tulimpima na kukuta hana VVU,” alisema.
HABARILEO
Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wanne wa taasisi nyeti tofauti kuhusu mambo mbalimbali ya mustakabali wa Serikali yake ya awamu ya tano.
Mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, miongoni mwa viongozi aliokutana nao ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Assad ambaye wamezungumzia kupunguza gharama za matumizi ya kuendesha serikali na kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Viongozi wengine ambao alikutana nao ni Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP), Biswalo Eutropius Mganga; Shehe Mkuu, Mufti Abubakar Zuberi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana, ilisema pamoja na kutakiana heri ya Mwaka Mpya, Rais Magufuli alizungumzia mambo mbalimbali kuhusu mustakabali wa Serikali yake ya awamu ya tano.
Akizungumzia yaliyojiri katika mazungumzo hayo, CAG Assad alisema Rais Magufuli ametaka ofisi yake ihakikishe Tanzania inaongeza ukusanyaji wa mapato kutoka asilimia 14 ya Pato la Taifa (GDP) kwa mujibu wa hesabu zilizofanyika mwaka juzi.
“Hadi mwaka juzi Tanzania ilikuwa inakusanya mapato kwa kiwango cha asilimia 14 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na Kenya ambayo ilikuwa ikikusanya asilimia 19 ya Pato la Taifa, na hakuna sababu za msingi za kwa nini Tanzania iwe nyuma katika ukusanyaji wa mapato hayo,” alisema Assad.
DPP Mganga alisema mazungumzo yao na Rais Magufuli yalijikita katika suala la kupeana mikakati ya namna ofisi yake inavyopaswa kufanya kazi kuendana na kauli mbiu ya serikali ya awamu ya tano ya ‘Hapa Kazi Tu’.
Aidha Mganga alisema wamezungumzia umuhimu wa kuhimiza Watanzania kufuata sheria, na kwamba ofisi yake itatekeleza wajibu wake bila kumwonea mtu. Kiongozi mwingine aliyekutana na Rais Magufuli ni Mufti Abubakar Zuber ambaye pamoja na kumpongeza rais kwa juhudi kubwa alizoanza nazo katika uongozi wake, amesema Waislamu wote nchini wanamuunga mkono na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee na juhudi hizo.
“Na pia kwa niaba ya Waislamu tunataka kumueleza kwamba kazi anayoifanya ni kazi ambayo tunairidhia na tunamuomba aendelee kuifanya wala asiogope, na kauli yake ya Hapa Kazi Tu iendelee, kwa sababu inaonesha kwamba sasa nchi yetu itakaa mahali pazuri,” alisema Mufti.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Bulembo, alimpongeza Rais kwa kasi nzuri aliyoanza nayo katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015-2020 na kutaka kasi hiyo iendelee. Alisema Jumuiya inaunga mkono kazi kubwa inayofanywa na Rais Magufuli.
Bulembo alisema Rais amemhakikishia kuwa ataendelea kufanya kazi hizo zaidi katika kutekeleza Ilani ya chama. “Tunafurahi kwamba yapo mambo mengi ambayo Rais Magufuli ameanza kuyatekeleza kwa haraka, mojawapo likiwa ni kufutwa kwa ada za shule, na hivi sasa wanafunzi watakwenda shule pasipo kutozwa ada.” alisema Bulembo.
HABARILEO
Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde amevitoza faini ya zaidi ya Sh milioni 60 viwanda viwili vya Lodhia Plastic Industries Limited na Sunflag (T) Ltd kwa kukiuka taratibu za kazi na kudharau mamlaka ya usalama mahali pa kazi (Osha).
Mavunde alitoa adhabu hiyo jana jijini hapa wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye viwanda hivyo huku akiongozana na wakuu wa idara ya kazi, idara ya uhamiaji na viongozi kutoka Osha.
Awali alipokuwa katika kiwanda cha Sunflag, alizungumza na baadhi ya wafanyakazi na kugundua kuwa baadhi yao hawana mikataba ya ajira na wamefanya kazi zaidi ya mwaka mmoja lakini pia hawana vifaa vya kutosha vya kuzuia pamba kuingia mwilini.
Pia aliagiza menejimenti ya kiwanda hicho, kuhakikisha inalipa mishahara ya wafanyakazi kwa kima cha Serikali na si kuwalipa Sh 4,424 kwa siku. Aidha akiwa kiwandani hapo aligundua kuwa kuna wafanyakazi raia wa kigeni 41 wanaofanya kazi katika idara mbalimbali zinazopaswa kusimamiwa na raia wa Tanzania.
Akiwa katika kiwanda cha Lodhia, Mavunde alifuta kibali cha mmoja wa wageni kutoka nje ya nchi kutokana na kukiuka kibali cha kufanyakazi na kumwagiza Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Raju Sighn kupeleka vibali 38 vya raia wa kigeni ili vikaguliwe.
Kutokana na kasoro hizo Mavunde alitoza faini ya jumla ya Sh milioni 22.9 kwa kiwanda cha Sunflag na kiwanda cha Lodhia Plastic kilitozwa Sh milioni 10 kutokana na kukiuka masharti ya uendeshaji viwanda na kutoa siku 14 faini hiyo iwe imelipwa.
“Ndani ya siku saba muwe mmepeleka taarifa Osha na hivi vibali vya wageni kutoka nje ya nchi kwa ofisi za kazi jijini Arusha. Maana mnasema mna vibali lakini nilivyoviona havijaniridhisha, pelekeni ili waone na ikithibitika mmekidhi viwango mtapunguziwa adhabu, ila heshimuni sheria za nchi,” alisisitiza.
HABARILEO
Serikali imenunua mashine mpya ya CT-Scan kwa ajili ya kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa mbalimbali katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH). Mashine hiyo yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 1.7 (takribani Sh bilioni 3.6) imeelezwa kwamba ni yenye uwezo wa hali ya juu.
Ununuzi wa mashine hiyo, umefanyika baada ya agizo la Rais John Magufuli alilolitoa hivi karibuni akiutaka uongozi wa MNH kuboresha huduma zake kwa kuhakikisha vifaa tiba na dawa vinapatikana ili Watanzania wapate huduma bora ya matibabu.
Ununuzi wa mashine hiyo ulielezwa jana na Mkuu wa Idara ya Mionzi, Dk Flora Lwakatare, wakati Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kingwangalla alipofanya ziara katika hospitali hiyo kubwa zaidi nchini.
Dk Kigwangallah pia alitembelea Idara ya Magonjwa ya Dharura, Idara ya Mionzi na sehemu mpya ya wagonjwa waliopo chini ya uangalizi maalumu (ICU). Dk Lwakatare alisema kwamba CT-Scan hiyo mpya imetengenezwa na kampuni ya Siemens na kwamba imefungwa siku mbili zilizopita.
Alifafanua kwamba tayari wameshaanza kuifanyia majaribio kwa wagonjwa 26 tangu ilipofungwa na kusaidia sana uchunguzi. Dk Lwakatare alisema mashine ya uwezo huo iko moja tu nchini na kwamba katika nchi za Afrika Mashariki, hospitali nyingine yenye mashine kama hiyo ni Aga Khan ya nchini Kenya.
“Mashine hii inatoa huduma za hali ya juu kwa magonjwa ya moyo, ubongo, tumbo na kifua na ina uwezo wa kupima kifua na tumbo kwa sekunde sita tu,” alisema. Naibu Waziri Kigwangalla alifafanua kwa waandishi wa habari kwamba mashine hiyo imenunuliwa kwa fedha za serikali na sio mkopo.
“Tunatarajia kununua mashine pia kama hii katika hospitali za Dodoma na Mwanza,” alisema Kigwangalla. Naye Kaimu Mkurugenzi wa MNH, Profesa Laurence Maseru alisema mashine hiyo ina sahani 128, mara mbili zaidi ikilinganishwa na iliyokuwepo.
Kuhusu mashine ya MRI, Profesa Maseru alisema kwamba tangu ilipofanyiwa matengenezo makubwa Novemba 26 mwaka jana, imeshahudumia wagonjwa 560 na inaendelea kufanya kazi.
Dk Kigwangalla pia alitembelea Idara ya huduma za dharura na kuangalia jinsi huduma zinavyotolewa, ambapo alielezwa na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura, Dk Juma Mfinanga kwamba wanahudumia wastani wa wagonjwa 300 hadi 400 kwa siku.
Naibu Waziri huyo, mbali na kupongeza maboresho yaliyofanyika na huduma nzuri inayotolewa kwa sasa, alitoa maagizo kwa uongozi wa hospitali hiyo kuboresha huduma zaidi kadri inavyowezekana.
Aliutaka uongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha unawalipa wafanyakazi malipo ya ziada kwa wakati, kutumia mfumo wa kompyuta sehemu zote, kupunguza msongamano wa wagonjwa na kuwa wabunifu.
HABARILEO
Watu wanane akiwemo Msaidizi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Gerald Ryoba pamoja na familia yake, wamekufa maji baada ya gari walilokuwa wakisafiria kusombwa na maji katika mkondo mpana wa mto unaotenganisha Kibaigwa na Pandambili, mkoani Dodoma.
Watu sita ni wa familia ya Ryoba waliokuwa ndani ya gari lililosombwa na maji likijaribu kupita. Pia miili ya watu wengine wawili ambao pia walikufa kutokana na kusombwa na maji, ilipatikana baada ya maji kuisha.
Pamoja na msaidizi huyo wa IGP, wengine waliokuwa kwenye gari hilo lililosombwa na maji, ni mkewe, Fidea Kiondo ambaye ni Mwalimu katika Manispaa ya Temeke, jijini Dar es Salaam pamoja na watoto wao, Gabriel (4) na Godwin; msaidizi wa kazi za ndani, Sarah na dereva, Koplo Ramadhani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime katika taarifa yake alisema kwamba Ryoba na familia yake walikuwa wakitoka mkoani Geita kwenda Dar es Salaam. Mtendaji wa Kata ya Kibaigwa, Gabriel Mganga alimwambia mwandishi wa habari hizi kwamba maiti wawili ambao ni tofauti na waliokutwa kwenye gari, mmoja hakutambulika lakini mwingine amebainika ni Ofisa Kilimo na Mifugo Kata ya Lenjulu, wilayani Kongwa aliyetambulika kwa jina la Eudiji.
Kuopolewa kwa familia hiyo ndani ya gari kuliwezeshwa usiku wa manane baada ya maji kupungua. Mganga alisema kwamba walilazimika kukata kwa gesi gari lililokuwa limebeba familia ya msaidizi wa IGP baada ya kusombwa na maji kwa ajili ya kutoa watu wawili waliokuwa ndani.
Wengine waliokotwa nje na kutambuliwa kutokana na vitambulisho vilivyokutwa katika gari. Alitaja gari hilo ni aina ya RAV 4 yenye namba za usajili T 516 DEP. Kwa mujibu wa mtendaji huyo aliyekuwa kwenye eneo la tukio, dereva huyo wa polisi alionywa asiingie katika mkondo huo kutokana na wingi wa maji lakini hakuwasikiliza.
Alisema baada ya kuingia kwenye mkondo, maji yaliitoa gari barabarani na kuitupa katika korongo la mto kabla ya kwenda kusimama katika eneo lenye bwawa. Alisema mkondo huo ambao wengi hupaita Pasua, ni moja ya sehemu korofi na madereva wengi hushitukizwa na maji kwa kuwa mkondo huo unatoka mbali.
Diwani wa Kata ya Kibaigwa, Kapinye alisema eneo hilo linajulikana kuwa korofi na ni pana na maji yake huja kwa kishindo. Ilielezwa kwamba maji hayo yaliyoanza kuingia barabarani juzi saa 11.30, yalisababisha magari zaidi ya 400 kukwama kila upande katika barabara hiyo kuu ya Dodoma-Morogoro.
Mafuriko hayo ni matokeo ya mvua zilizonyesha katika Kata ya Njoge Kiteto, Hembahemba na bonde la Ndurugumi wilayani Kiteto. Wakati huo huo, Kamanda Misime katika taarifa yake pia alisema kwamba madaktari katika hospitali ya rufaa Dodoma wanaandaa miili ya marehemu kwa ajili ya kusafirishwa ambapo familia ya Ryoba itapelekwa Geita, mfanyakazi wa ndani atapelekwa Mbinga na dereva mwili wake utapelekwa Lindi.
“Huyu koplo ambaye alikuwa ni dereva yeye ni mwenyeji wa Lindi na Mkaguzi (Ryoba) ni mtu wa Geita hivyo tunatarajia kusafirisha mwili wake pamoja na wa mkewe na watoto wake wawili, na msichana wa kazi atapelekwa Mbinga,”alisema Misime. Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Ibenze Ernest amethibitisha kupokea miili sita ya marehemu kutoka eneo la tukio.
HABARILEO
Licha ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoa huduma bure za afya kwa wajawazito, ni asilimia 12.4 tu ya wanawake wanajifungulia katika hospitali za serikali.
Ofisa Mshauri Mwandamizi wa huduma za uzazi salama, Hanuni Waziri Songoro alisema hayo wakati alipozungumza na wafanyakazi wanaotoa huduma za uzazi kwa akinamama huko Mbweni mjini.
Songoro alisema kwa upande wa Pemba asilimia ya wanawake 66 wanajifungulia majumbani kwa sababu mbali mbali ikiwemo masafa ya kupata huduma hizo zaidi vijijini. Aidha kwa upande wa Unguja asilimia 44 ya wanawake wanajifungulia majumbani kwa kupata huduma kutoka kwa wakunga wa kienyeji.
“Utafiti uliofanywa wa wajawazito kuhusu matumizi ya huduma za uzazi salama imebainika wengi bado hawajapata mwamko wa kujifungulia katika hospitali zenye huduma sahihi zaidi,” alisema.
Alisema kwa upande wa kisiwa cha Pemba, moja ya matatizo makubwa linalowafanya wajawazito kujifungulia majumbani ni umbali wa vituo vya afya. Aidha alisema bado baadhi ya wananchi wamekuwa wakiendekeza itikadi na imani za jadi ambazo huwafanya kupenda kujifungua majumbani kuliko hospitalini.
“Zipo sababu mbali mbali zinazowafanya akinamama kujifungulia majumbani ikiwemo umbali wa kupata huduma za afya zaidi vijijini. Lakini lipo tatizo la wanawake kuamini zaidi imani ya itikadi,” alisema.
Mkazi wa Kilimahewa, Asha Saidi, alisema baadhi ya wanawake wanagoma kujifungua katika hospitali kwa sababu ya huduma zisizoridhisha kutoka kwa wauguzi.
Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kufuta ada mbali mbali walizokuwa wakitozwa akinamama waliokuwa wakijifungulia katika hospitali za Serikali, lakini zaidi alitaka kuimarishwa kwa huduma hizo kutoka kwa wauguzi.
“Mimi nimejifungua watoto wanne wote katika hospitali ya Serikali lakini tatizo moja kubwa ni kwamba huduma kutoka kwa wauguzi zinatakiwa ziimarishwe na kuwa bora zaidi kwani watu wanaona bora kuwafuata wakunga wa kienyeji,” alisema.
Muuguzi katika hospitali ya Mnazi Mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Asia Juma, alisema wamejipanga kuhakikisha kwamba wanatoa huduma bora zinazokwenda sambamba na maadili na viapo vya kazi.
“Huduma zinazotolewa katika hospitali zinazowahudumia wajawazito zimeboreshwa kwa kiwango kikubwa kwa lengo la kuondosha malalamiko yote yaliyokuwa yakitolewa awali,” alisema.
NIPASHE
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameutaka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuhakikisha wakulima wa mahindi wanapatiwa magunia ya kuhifadhia mazao yao.
Agizo hilo alilitoa jana katika ziara yake ya siku tatu ya kikazi mkoani Ruvuma na kwamba anatekeleza agizo la Rais John Magufuli kuwa hakuna Mtanzania atakayekufa njaa.
Majaliwa alisema wafanyabiashara wamekuwa wakipatiwa magunia na NFRA kwa ajili ya kununulia mahindi lakini wakulima wanapoomba kupatiwa imekuwa ni tatizo kwao kuyapata kwa urahisi.
Alionyesha kusikitishwa na vitendo hivyo vinavyofanywa na wafanyabiashara wajanja, ambao wamekuwa wakipita vijijini kuwarubuni wakulima na kununua mahindi kwa bei ndogo ambayo hailingani na uzalishaji wa zao hilo.
Alisema kumekuwa na mianya ya rushwa inayofanywa na wafanyabiashara hao kwa kushirikiana na baadhi ya maofisa wa NFRA kwa lengo la kujinufaisha watu wachache huku mkulima wa kawaida akiendelea kuteseka na mazao yake shambani.
“Magunia yanayonunuliwa na serikali kwa ajili ya kuhifadhia zao hili, ninazo taarifa za kutosha kwamba hayamfikii mkulima kule kijijini, badala yake yanaishia kwa watu wachache”, alisema Waziri Mkuu.
Alisema serikali ina wajibu wa kuhifadhi chakula katika mazingira yanayokubalika ili kisiharibiwe na wadudu waharibifu, hivyo ameitaka NFRA Kanda ya Songea kuhakikisha mahindi yaliyohifadhiwa chini ya ardhi yanatafutiwa sehemu nyingine ili yasiharibike.
Alifafanua kuwa uhifadhi wa aina hiyo, usalama wake ni mdogo na kwamba mlundikano huo wa magunia yaliyosheheni mahindi katika hifadhi unasababishwa na wakala kuwa na upungufu mkubwa wa maghala.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alihoji kuwepo kwa msongamano wa malori kandokando ya barabara ya Songea – Mbinga.
Alisema hali hiyo imekuwa ikisababisha malalamiko kutoka kwa wasafirishaji kuwa magari yanayoingia kupakia mahindi, NFRA huwapatia watu wanaojulikana kwanza, ndipo huruhusu wengine kitendo kinachoonyesha kuwepo upendeleo.
Awali, Mbunge wa Songea Mjini, Leonidas Gama, alisema tatizo la soko la mahindi katika mkoa huo ni kubwa, hivyo ameiomba serikali ya awamu ya tano, iangalie namna ya kutafuta masoko ili wakulima wadogo wapate fursa ya kuuza mazao yao.
NIPASHE
Wafanyakazi 350 wa kiwanda cha Sukari Mahonda wapo katika hatari ya kupoteza ajira baada ya shamba la miwa la kiwanda hicho kuchomwa moto kwa mara ya pili ndani ya kipindi cha siku tano, mkoa wa Kaskazini Unguja.
Hayo yalisemwa na meneja wa kiwanda hicho, Tushar Mehta, wakati Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alipofanya ziara ya kukagua mashamba yaliyochomwa moto ya wawekezaji hao.
Alisema kitendo cha kuendelea kuhujumiwa mashamba yao ya miwa kinaweza kusababisha uongozi wa kiwanda hicho kuzuia ajira mpya 450 baada ya kukamilika kwa matengenezo makubwa na kuanza tena uzalishaji wa sukari.
Alisema watu wasiofahamika waliingia katika shamba hilo na kuwasha moto kwa mara ya pili baada ya tukio kama hilo Disemba 30, mwaka jana.
“Moto uliwashwa katikati ya shamba la miwa juzi, kabla ya waliofanya kitendo hicho kuwasha moto huo waliweka kizuizi kwa makusudi ili vikosi vya uokozi vishindwe kuuzima haraka,” alisema.
Mehta alisema hadi sasa eka 200 zimeteketezwa kwa moto kwenye matukio yote mawili katika kipindi cha siku tano na kusababisha hasara ya dola za Marekani 1,176,234.28 sawa na Sh. bilioni 2.3.
Akizungumza baada ya kupatiwa taarifa hiyo, Balozi Seif alisema vitendo hivyo vya hujuma haviitakii mema Zanzibar katika harakati zake za kukuza uchumi na kufanikisha mpango wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini kwa wananchi wake.
Alisema watu wanaofanya vitendo hivyo wanafanya dhambi kubwa na pia wanawavunja moyo wawekezaji walioamua kuwekeza miradi yao ya kiuchumi Zanzibar kwa lengo la kuisaidia serikali pamoja na wananachi kupata maendeleo.
Alisema fikra za baadhi ya watu kwamba hujuma hizo zitatoa fursa kwao kutumia maeneo ya mashamba hayo ya miwa kuendeleza kilimo na mifugo inafaa kuachwa mara moja kwa vile yataendelea kuwa katika mipango ya serikali ya kuhudumia sekta ya viwanda.
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram na YouTUBE wa kubonyezahapa>>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE.