MWANANCHI
Gavana wa Jimbo la Siaya, nchini Kenya, Cornel Rasanga ameingia matatani akidaiwa kutumia Sh20 milioni za nchi hiyo (karibu Sh400 milioni) kutoka katika mfuko za Serikali kwa ajili safari ya kuhudhuria sherehe za kumwapisha Rais John Magufuli.
Dk Magufuli alipishwa Novemba 5, kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kumtangaza mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Oktoba 25. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kenya (PAC), Nicholas Gumbo amemtuhumu Rasanga kwa kutumia fedha hizo kutoka kwenye mfuko wa Serikali wa safari.
“Gavana wa Rasanga lazima awaambie wananchi wa Siaya, imekuwaje akatumia Sh20 milioni kwenda Tanzania kwa ajili ya shughuli ya Dk Magufuli? “Sidhani kama Dk Magufuli ana uhusiano wowote na wananchi wa Kaunti ya Siaya kiasi cha Gavana kutumia fedha hizo za umma kwenda Tanzania,” Gumbo.
Gumbo alisema Dk Magufuli anafahamika kuwa ni rafiki mkubwa wa kiongozi wa Cord, Raila Odinga ambaye pia alihudhuria sherehe hizo. Sherehe hizo pia zilihudhuriwa na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na viongozi wengine wa Afrika. Akizungumzia tuhuma hizo, Rasanga alisema madai yalitolewa na Gumbo ambaye ni Mbunge wa Rarieda, ni uzushi na alikuwa anataka kujikweza kisiasa.
“Hii ilikuwa safari binafsi. Hatukutumia fedha za Serikali kama inavyoelezwa,” alisema alipohojiwa na gazeti la Daily Nation. Gavana huyo alisema alikwenda kuhudhuria kuapishwa kwa Dk Magufuli kwa mwaliko binafsi wa Rais hiyo wa Tano wa Tanzania. Hata hivyo, alisema ziara yake Tanzania itasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza ushirikiano katika Ukanda wa Ziwa Victoria.
“Ukweli ni kwamba Rais wa Tanzania aliwahi kutembelea Siaya na tulijadiliana masuala mbalimbali ikiwamo usafiri hasa katika Ziwa Victoria,” alisema Rasanga na kuongeza:
“Dk Magufuli anatokea Kanda ya Ziwa na mpango wake mkubwa ni kuimarisha bandari katika Ziwa Victoria na kuchaguliwa kwake kuwa Rais kutarahisisha zaidi utekelezaji wa mipango yake.
“Hakuna sababu ya kuingiza siasa katika safari hii. Tuko katika mipango mizuri tu ya kibiashara na Tanzania ambayo kwa sasa imeanza kupanuka.” Mwenyekiti huyo wa PAC Kenya alisema safari hiyo ya Novemba 5, ni matumizi mabaya ya rasilimali za umma.
Hata hivyo, Naibu Gavana, Wilson Ouma alipinga madai ya Gumbo akisema alikuwa na lengo la kumharibia bosi wake.
“Ukweli Gavana Rasanga alitumia fedha zake kwenda Tanzania na uzushi wowote unatakiwa ukomeshwe,” alisema Ouma alipozungumza na Nation. Akisisitiza, Gumbo alisema ataendelea kupambana na matumizi mabaya ya fedha za umma unaofanywa na maofisa wa Serikali kwa kutumia vyeo vyao.
Magufuli kivutio nchi jirani Madai hayo yameibuka wakati kasi ya utendaji wa Rais Magufuli tangu aapishwe ikizidi kuwa kivutio katika mitandao mbalimbali ya kijamii nchini Kenya na katika nchi nyingine jirani.
Kwa kipindi cha takriban siku 20 alizokaa ofisini, Rais Magufuli amechochea utendaji katika utumishi wa umma na kupunguza gharama akianza kwa kukata safari za nje kwa watumishi wa umma na sherehe za uhuru.
MWANANCHI
Utekelezaji wa ahadi za Rais John Magufuli unazidi kushika kasi baada ya kuanza kwa mchakato wa kuanzisha mahakama maalumu ya kuwashughulikia mafisadi.
Jaji Kiongozi, Shaban Lila alisema jana kuwa tayari wadau mbalimbali wa haki jinai wameanza kukutana kuangalia namna ya kuanzisha mahakama hiyo kama sehemu ya utekejezaji wa ahadi ya Rais.
Akizungumza katika hafla ya kuhitimisha mafunzo ya kushughulikia mashauri nyeti ya jinai kwa majaji 12 wa Mahakama Kuu ya Tanzania, alisema juzi walikuwa na mazungumzo na Wizara ya Katiba na Sheria kuangalia mfumo wa uendeshaji wa mahakama hiyo.
“Tunaangalia tuianzishe kama mahakama huru au ifanywe ndani ya muundo wetu wa mahakama kwa kuipa kipaumbele maalumu. Lakini tunafikiria zaidi kama ingekuwa ni kitengo maalumu ndani ya Mahakama Kuu kitakachokuwa kikishughulikia mafisadi,” alisema Jaji Lila.
Hata hivyo, Jaji Lila hakutaja muda maalumu utakaotumika kumaliza mchakato wa kuanzisha mahakama hiyo, huku akisema unahusisha wadau wengi na unyeti wake unahitaji maandalizi makubwa. Jaji huyo bila kutaja takwimu, alieleza kuwa kesi za makosa makubwa ya jinai zinaongezeka nchini ukilinganisha na miaka ya nyuma hasa zile zinazohusu utakatishaji fedha, ugaidi, usafirishaji wa dawa za kulevya, usafirishaji wa nyara za Serikali hasa wanyama hai na mazao yake na ufisadi.
Balozi wa Uingereza nchini, Dianna Melrose alimpongeza Rais Magufuli kwa kuonyesha msimamo wa kupambana na makosa ya jinai yakiwamo ya dawa ya kulevya, usafirishaji wa nyara za Serikali na utakatishaji fedha.
“Nilikuwa nimeketi bungeni namsikiliza Rais siku alipokuwa akilihutubia Bunge, japo hotuba yake ilikuwa kwa Kiswahili lakini nilipata faraja kubwa nilipomuona akiwa mkali katika masuala hayo,” alisema Balozi Melrose.
MWANANCHI
Kigogo mmoja wa CCM wilayani Rombo anadaiwa kumnajisi mtoto wake mwenye umri wa mwaka mmoja. Mama mzazi wa mtoto huyo alidai kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 17, usiku nyumbani kwao Mwanga walipokuwa wamelala na alishtuka baada ya kusikia sauti ya mtoto akilia kutokea chumba kingine.
“Nilipoamka nilikwenda kwenye kile chumba na kumkuta mwanangu akitokwa na damu sehemu zake za siri, nilimchukua na kumpeleka Kituo cha Afya cha Mwanga,” alidai mama huyo.
Alidai kuwa daktari aliyemtibu alithibitisha kuwa alikuwa amenajisiwa. Hata hivyo, alisema baada ya mumewe kufanya kitendo hicho, aliondoka na kwenda kwenye kituo chake cha kazi alichohamishiwa hivi karibuni cha wilayani Rombo.
“Daktari alipompima na kukuta kalawitiwa alimtibu na kumpa dawa za maumivu na kuniambia nikatoe taarifa polisi ili mume wangu akamatwe, lakini hadi sasa hajakamatwa,” alidai na kuongeza: “Tangu amefanya kitendo hiki hajawasiliana na mimi na tayari nilishafungua jalada polisi. Nadhani alidhamiria kufanya kitendo hiki, amemuumiza mtoto,” alidai mama huyo.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Flugence Ngonyani alisema mtuhumiwa bado anatafutwa na polisi kisha afunguliwe mashtaka ya ubakaji.
“Ni kweli tukio hilo nimelisikia na utaratibu unaendelea ili akamatwe na kutoa maelezo dhidi ya tuhuma zinazomkabili. Pia, kama kuna mtu anajua alipo, atusaidie ili tuweze kumkamata na kumfikisha mahakamani,” alisema Kamanda Ngonyani: “Tunawaomba wananchi mtusaidie katika hili, kitendo alichokifanya huyu baba si cha kufumbiwa macho, lazima atafutwe na akamatwe.”
NIPASHE
Chama cha Wananchi (CUF) kimesema hakuna mwenye ubavu wa kutengua maamuzi ya Baraza Kuu la Chama hicho ya kupinga kufutwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa chama hicho, Ali Omar Shehe, alipokuwa akizungumzia mgogoro wa uchaguzi huo, mjini hapa jana.
Alisema pamoja na mazungumzo yanayoendelea kufanyika ya kutafuta muafaka, lakini msimamo wa Baraza Kuu la Uongozi la Cuf bado uko palepale wa kumtaka Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) atengue uamuzi wake wa kufuta matokeo ya uchaguzi kurudi kazini kukamilisha kazi ya kutangaza matokeo na mshindi wa uchaguzi huo.
“Baraza Kuu la Uongozi la Cuf lilikutana Zanzibar na kuweka msimamo huo, hakuna kiongozi yoyote ndani ya Cuf mwenye ubavu wa kwenda kinyume na maamuzi hayo,” alisema. Alisema maamuzi yoyote ambayo yatafanyika lazima yapate baraka za baraza hilo lakini kwa sasa CUF haikubaliani na Zec kutaka kuitisha uchaguzi mpya wisiwani humo.
Msimamo huo wa Cuf umekuja huku kukiwa na tetesi kuwa, mazungumzo kadhaa yaliyofanyika kuhusiana na mgogoro huo na kuwashirikisha viongozi wa ngazi za juu Zanzibar wakiwamo wagombea urais kwenye uchaguzi huo, Rais Mohamed Shein (CCM), Maalim Sharif Hamad (Cuf) na marais wastaafu imefikia muafaka na kutoka na pendekezo la kurudiwa uchaguzi huo ambalo litawasilishwa katika kila chama kilichokuwa kinashiriki mazungumzo hayo.
Hata hivyo, Msemaji wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar, Waride Bakar Jabu, alisema hadi jana chama chake kilikuwa hakijapokea mapendekezo yoyote kutoka katika meza ya mazungumzo hayo alisema yamewaweka njiapanda kwa sababu hawafahamu kinachoendelea. Zec ilifuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar Oktoba 28, mwaka huu kwa madai kufanyika vitendo vya udaganyifu kinyume na sheria na kanuni za uchaguzi.
NIPASHE
Wakati kukiwa na taarifa kwamba Rais Dk. John Magufuli, anatarajia kupunguza karibu nusu ya wizara zilizokuwapo kwenye Serikali ya Awamu ya Nne, imefahamika kuwa wizara zinazolengwa ni zile zilizopo Ofisi ya Rais, Makamu wa Rais na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Chanzo kimoja kutoka serikalini kimeiambia Nipashe jana kuwa wizara hizo zitaunganishwa kwenye wizara mpya zitakazoanzishwa na Rais ambaye ameweka mkakati wa kuwa na baraza dogo la mawaziri.
Wizara zinazotajwa kufyekwa ni Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Kazi Maalum, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Wizara Ofisi ya Waziri Mkuu na Sera, Uratibu na Bunge.
Nyingine ni Wizara Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, Wizara ya Nchi, Ofisi Makamu wa Rais Mazingira na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Kadhalika, katika mabadiliko hayo, wizara nyingine zitaguswa ili kufikia malengo ya kubakia na wizara chache kutimiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano kubana matumizi na kuinua maisha ya Watanzania.
Chanzo hicho kimebainisha kuwa Rais Dk. Magufuli atalitangaza Baraza la Mawaziri ndani ya wiki hii ingawa bado kumekuwa na usiri wa siku halisi atakayotangaza.
Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete, ilimaliza muda wake Novemba 5, mwaka huu ikiwa na wizara 30. Vile vile, alipoingia kwa mara ya kwanza mwaka 2005, Rais Kikwete alikuwa na serikali kubwa yenye mawaziri na naibu wao zaidi ya 60.
Rais Magufuli aliyeapishwa Novemba 5, mwaka huu, tayari ameshamteua Mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa, kuwa Waziri Mkuu wa serikali yake na Ijumaa iliyopita alizindua rasmi Bunge la 11.
Juzi, chanzo kimoja kililiambia Nipashe kuwa tayari Rais Magufuli kwa kushirikiana na wasaidizi wake, ameshakamilisha sehemu kubwa ya mchakato wa kuunda baraza lake la mawaziri na kwamba kinachosubiriwa sasa ni kulitangaza wakati wowote kuanzia sasa.
NIPASHE
Kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi iliyofunguliwa na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, kupinga matokeo ya uchaguzi itaanza kusikilizwa leo na Jaji John Utamwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora.
Kafulila aliyekuwa Mbunge kinara katika kuibua ufisadi wa sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 306 katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), anakutana ‘uso kwa uso’ na Jaji Utamwa, ambaye ndio alitoa hukumu tata iliyosababisha kuibuka kwa kashfa ya ufisadi wa fedha hizo.
Jaji Utamwa aliitoa hukumu hiyo, Septemba 8, 2013 kwa kumwamuru Kabidhi Wasihi, kukabidhi mtambo wa Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kwa mmiliki wake mpya ambaye ni kampuni ya Pan Africa Power Solutions Tanzania Limited (PAP) baada ya kukubaliana na maombi ya aliyekuwa mbia wa IPTL, kampuni ya Engineering and Marketing Limited (VIP) iliyoondoa kesi yake kwa lengo la kuifilisi IPTL.
Hukumu hiyo ndio ilikuwa chanzo cha Kafulila kuibua kashfa hiyo bungeni kwa kuwahusisha vigogo mbalimbali wa serikali na ufisadi huo.
Hatua hiyo ya Kafulila ilisababisha serikali kumuelekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza kashfa hiyo.
Takukuru na CAG ziliwasilisha matokeo ya uchunguzi huo kupitia Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Taarifa ya uchunguzi huo iliyowasilishwa bungeni mwishoni mwa mwaka jana na aliyekuwa Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, iliwahusisha vigogo kadhaa wa serikali wakiwamo waliopewa mgawo wa mamilioni ya Shilingi kupitia benki mbalimbali nchini.
Kashfa hiyo ilisababisha kujiuzulu kwa Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Serikali, Jaji Frederick Werema na pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alifutwa kazi na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.
Pia wabunge kadhaa waliondolewa katika nafasi za uenyekiti wa kamati za Bunge na baadhi ya watendaji wa serikali walifunguliwa mashauri katika Baraza la Maadili huku wengine wakifunguliwa kesi mahakamani.
Jaji Utamwa atasikiliza leo ombi la malipo ya dhamana ambalo Kafulila atatakiwa kulipa kwa kufungua kesi ya kulalamikia matokeo.
Kafulila anaomba apunguziwe kiasi cha dhamana ili asilipe Sh. milioni 15 kwa kuwalalamikia walalamikiwa watatu.
Walalamikiwa hao ni aliyekuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Husna Mwilima, aliyeshinda katika uchaguzi wa ubunge wa Oktoba 25, mwaka huu kwa kupata kura 34, 453 dhidi ya kura 33,382 alizopata Kafulila.
Mlalamikiwa mwingine ni aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Uvinza, mkoani Kigoma, Ruben Mfune, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju.
NIPASHE
Wakati safari holela za nje ya nchi zikidhibitiwa, janga lingine limewashukia vigogo baada ya serikali kutangaza kufuta safari za ndani kwa ajili ya mikutano na vikao vya kazi.
Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, ilitangaza jana kuwazuia watendaji wake kutumia fedha za umma kugharimia safari, kukodi kumbi za vikao na mikutano ya kazi kokote nchini kuanzia sasa.
Badala yake, watendaji hao wa serikali wametakiwa kutumia mfumo wa kisasa wa upashanaji habari kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehema) kufanikisha mikutano hiyo.
Kwa mantiki hiyo, kuanzia sasa serikali haitaingia tena gharama za kuendesha vikao vya kazi na watendaji wake kwa kuwa hayo yatatafanikishwa kupitia mfumo wa mikutano ya video mtandaoni.
Mkakati huo mpya na endelevu ulitangazwa jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Florence Temba, alipozungumza na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa serikali imeanza kusimamia utekelezaji wa mpango huo.
Alisema walengwa wakuu wa vikao kazi ni Wakurugenzi, Makatibu Tawala wa Mikoa na Maofisa Utumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kote.
Temba alitaja gharama ambazo serikali haitaingia tena kuwa ni pamoja na kukodi kumbi, usafiri na muda utakaotumika nje ya vituo vya kazi, hivyo Tehama ndiyo itatumika katika kuendesha vikao kazi vinavyowahusu watendaji wake katika utekelezaji wa majukumu kwenye maeneo ya kazi.
“Menejimenti ya Utumishi wa Umma, inasisitiza kuwa Tehama itatumika kuwa chombo muhimu cha kuboresha utendaji serikalini kwa kuongeza ufanisi, kupunguza gharama za utendaji na kuboresha utoaji huduma kwa wananachi,” alisema Temba.
Alisema kuwa mfumo huo wa kuendesha mikutano ya serikali kupitia mfumo wa picha za video, ni salama kwa sababu miundombinu yote itakayotumika imeratibiwa na kukaguliwa na serikali.
Temba alitaja mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa maandalizi na uendeshaji wa mikutano hiyo kuwa ni pamoja na uhakiki wa mfumo kabla ya matumizi, utunzaji na matumizi ya mifumo ya mawasiliano kwa njia ya video kwa kuzingatia mwongozo wa matumizi bora, sahihi na salama.
Akizungumzia mpango huo utakavyotekelezwa, Mkurugenzi wa Tehama, Priscus Kiwango, alisema katika mikoa yote nchini, ni mikoa mitatu tu mipya ndiyo haijaingizwa katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Hata hivyo, Kiwango alisema mikoa hiyo itashiriki vikao hivyo kwa kutumia mikoa jirani ambapo gharama zitapungua.
Aliitaja mikoa ambayo haijaingizwa katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kuwa ni Geita, Simiyu na Njombe, huku akisisitiza kuwa itaingizwa kwenye utaratibu kadiri serikali inavyoendelea kujipanga.
“Teknolojia hii itawezesha mawasiliano kutoka vituo mbalimbali kuwasiliana kwa njia ya sauti na picha,” alifafanua na kongeza kuwa hivyo inawezesha wahusika kuwasiliana moja kwa moja kwa njia ya kielektroniki bila kuhitaji kukutana pamoja,” alisema.
Utaratibu wa Tehama nchini umeanza mwaka mmoja uliopita na tayari umefanikisha mikutano takriban 10 kwa njia hiyo.
Lengo kuu ni kupunguza gharama za mikutano na kuna uwezekano pia wa kufanya mkutano unaoweza kutumia kwa saa tano mfululizo huku mikoa minane ikiwa imeunganishwa pamoja.
Agizo hili la serikali limekuja siku chache tangu Rais Dk. John Magufuli, atangaze kusitisha kwa muda safari za nje ya nchi kwa maofisa wa serikali akisema itasaidia kubana matumizi ya serikali.
Katika maelezo yake hivi karibuni, Rais Magufuli alisema serikali imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha kwa ajili ya safari za nje kwa maofisa wake wa kada mbalimbali na kuisababishia serikali mzigo mkubwa wa gharama.
HABARILEO
Serikali imedhamiria kuanza utaratibu utakaoweka mazingira ya wanafunzi waliopata mimba wakiwa shule kurudi shuleni kwa lengo la kuhakikisha hawakosi elimu.
Aidha, katika kutekeleza Sera ya Elimu ya Mwaka 2014, kuanzia mwakani inayoeleza kutoa elimu bure, Serikali imewataka wazazi na walezi kwenda kuandikisha watoto kwani ada na michango yote imeondolewa ili kuwezesha watoto wote wapate elimu ya msingi.
Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Paulina Mkonongo alisema hayo jana Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia zilizoandaliwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF).
Mkonongo aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Sifuni Mchome, alisema katika maadhimisho ya mwaka huu yana kaulimbiu “Funguka, Chukua Hatua, Mlinde Mtoto Apate Elimu,” inayosaidia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014.
Alisema sera hiyo inatoa fursa ya elimu kwa watoto wote kuanzia elimu ya awali mpaka sekondari kwa elimu ya msingi kuwa ya lazima na itatolewa bila ada katika mfumo wa umma.
“Aidha, Serikali inazuia utitiri wa michango shuleni ili kuwawezesha watoto wote wapate elimu na kujenga usawa wa kijinsia shuleni, hivyo tunatarajia kupata ushirikiano wa wazazi na walezi ili kuinua udahili na mahudhurio ya watoto shuleni,”Mkonongo.
Alisema mahudhurio kwa wanafunzi na uandikishaji unashuka kwa chini ya asilimia 95 kwa sababu mbalimbali ikiwemo ukatili wa kijinsia pamoja na michango. Hivyo alitoa mwito kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote wenye umri stahiki wa kuanza darasa la kwanza wanaandikishwa kwani hakuna kikwazo cha ada wala michango.
Pia alisema wanafunzi watakaochaguliwa kuanza kidato cha kwanza wazazi na jamii ihakikishe wanaripoti kwa kuhudhuria darasani ambapo watandaa viongozi wa kusimamia udahili na kuhakikisha kila aliyechaguliwa anahudhuria darasani.
Akizungumzia vikwazo mbalimbali vinavyofanya watoto hasa wa kike kukatisha masomo, Mkonongo alisema ni pamoja mimba na ukatili wa kijinsia kwani wanafunzi wengi wa darasa la kwanza mpaka kidato cha nne wana umri chini ya miaka 18.
Alisema kwa takwimu za mwaka 2013, wanafunzi wa kike walioacha shule kutokana na ujauzito kwa shule ya msingi ni 297 na sekondari ni 3,045. Kutokana na hali hiyo, alisema Serikali inaangalia utaratibu wa wanafunzi hao kuendelea na shule baada ya kujifungua kwani elimu ni msingi wa kila kitu.
“Katika utekelezaji wa sera hii mpya suala hili litawekwa vizuri na halitakuwa na shida katika utekelezaji wake huku tukihakikisha wale waliowapa mimba wanachukuliwa hatua stahiki ili isijeonekana sasa ni wakati wa kuzalisha watoto wa kike,” alisema Mkurugenzi huyo.
Alisema hata wakirejeshwa shuleni baada ya kujifungua watakuwa wameathirika kisaikolojia pamoja na kuchelewa muda wa kumaliza shule na hivyo kuwataka wadau kusaidia katika kupeleka mawazo yao juu ya utekelezaji wa suala hilo kama walivyokuwa wakiiomba serikali.
Alisema hatua hiyo itasaidia kupanua fursa ya elimu kwa kuzingatia usawa wa kijinsia katika ngazi zote za kielimu. Akizungumzia ukatili wa kijinsia, alisema ni moja ya visababishi vya utoro shuleni na kudhoofisha taaluma, na kwa takwimu za mwaka 2013, wanafunzi wa shule ya msingi 54,596 na wa sekondari 62,590 waliacha shule kwa sababu ya utoro.
MTANZANIA
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, jana aliwaweka ndani maofisa ardhi zaidi ya 10 kwa saa sita.
Imeelezwa kuwa Makonda alifanya hivyo kwa kile kilichoelezwa kukaidi agizo lake la kuwataka wawahi katika eneo la mkutano kusikiliza migogoro ya ardhi.
Tukio hilo lilitokea katika eneo la Nakasangawe Kata ya Wazo, Dar es Salaam, baada ya maofisa hao kuchelewa kufika tofauti na walivyotakiwa.
Makonda alisema walikubalina kuwahi katika kikao cha pamoja.
Alisema lakini katika hali ya kushangaza ingawa yeye alifika katika eneo hilo kwa wakati, maofisa hao walifika saa 5.00 asubuhi kitendo ambacho hakiendani na nidhamu ya kazi.
“Hivi sasa wamewekwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Wazo na tumelazimika kuahirisha shughuli hii kwa muda,” Makonda.
Alisema hatua aliyoichukua kwa maofisa hao itakuwa fundisho kwa watendaji wengine kuwafanya wawajibike wakati wote kwa ajili ya masilahi ya wananchi na si yao binafsi.
HABARILEO
Kiongozi wa Kanisa la Katoliki Duniani, Papa Francis, amewasili nchini Kenya jana jioni huku akitoa baraka kwa nchi hiyo kwa lugha ya Kiswahili.
Baada ya hotuba yake, Papa Francis, alimaliza kwa kusema “Mungu Ibariki Kenya” jambo lililowafanya watu waliokuwa katika ukumbi wa Ikulu ya Nairobi kulipuka kwa furaha.
Katika ziara yake hiyo ya ya siku tatu nchini Kenya, alipokewa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta, ambapo moja ya mambo ya kukumbukwa ni ujumbe alioutoa kwa Kiswahili akilibariki taifa hilo baada ya kulihutubia taifa Ikulu jijini Nairobi.
Pamoja na mambo mengine, alisisitiza umuhimu wa amani, maridhiano, kusameheana na uponyaji katika taifa hilo lililogawanyika kwa misingi ya ukabila.
Baada ya mazungumzo yao Ikulu, Rais Kenyatta akagusia kwamba leo ni siku ya maombi ya taifa la Kenya na baadaye akamkaribisha Papa Francis kulihutubia taifa.
Papa alianza kutoa hotuba akishukuru kwa makaribisho mema kwenye ziara yake ya kwanza Afrika.
Kuhusu matarajio ya ziara yake, Papa alisema Kenya ina vijana wengi, na hivyo katika siku zake za kuwa humo anasubiri kwa hamu kubwa kukutana na kuzungumza nao na kuwapa matumaini katika ndoto zao za siku za usoni.
Aidha alisema Kenya ni taifa change, linalokua na lenye jamii mseto na ambalo limekuwa likitekeleza jukumu muhimu katika kanda hii na kupitia changamoto nyingi katika uundaji wa demokrasia kama ilivyo kwa mataifa mengi Afrika.
Akihimiza amani na maridhiano Papa Francis alisema: “Jamii zetu zinapoendelea kukumbwa na migawanyiko ya kikabila, kidini au kiuchumi, binadamu wote wenye nia njema huitwa kufanyia kazi maridhiano, msamaha na uponyaji.
“Yote ni katika juhudi za kuunda mfumo wa demokrasia, kuimarisha utangamano na uwiano, kuvumiliana na kuheshimiana, lengo kutenda mema linapaswa kuwa kipaumbele kikuu.”
Aidha alisema kwamba historia inaonyesha kuwa ghasia, mizozo na ugaidi huchochewa na kuogopana na kutoaminiana ambako husababishwa na umaskini na kupoteza matumaini.
“Vita dhidi ya maadui wa amani na ustawi vinapaswa kuendeshwa na wanaume na wanawake wanaoamini katika kushadadia, maadili makuu ya kidini na kisiasa ambayo yalisababisha kuasisiwa kwa taifa,” alisema.
“Wakenya wamethamini zawadi hizi kutoka kwa Mungu na wanajulikana kwa utamaduni wao wa kuhifadhi mazingira. Mgogoro wa kimazingira unaoikumba dunia kwa sasa unahitaji kutambua zaidi uhusiano kati ya binadamu na maumbile.”
Alihimiza taifa kuwajali masikini, ndoto za vijana, na kugawana vyema maliasili na nguvu kazi ambazo Mungu ameibariki Kenya na ameahidi kuendelea kwa juhudi za Kanisa Katoliki, kupitia kazi zake za elimu na kusaidia jamii, kutoa mchango katika hilo.
Akimalizia hotuba yake kabla ya kuondoka katika ukumbi wa Ikulu, baada ya kusalimiana na baadhi ya wageni waalikwa alisema: “Nawashukuru tena kwa kunikaribisha vyema, na kwenu na familia zenu, na watu wote wa Kenya, ziwe baraka tele za Mwenyezi Mungu.” Kisha akamalizia kwa Kiswahili akisema: “Mungu Ibariki Kenya”.
JAMBOLEO
Kikosi cha Polisi wa Usalama Barabarani liko mbioni kuanza kutekeleza mpango wa kuhesabu makosa ya madereva kwa kutumia idadi ya pointi.
Chini ya mpango huo, dereva atakayefanya makosa na kufikisha pointi zitakazoainishwa kisheria, atafutiwa leseni yake.
Aidha, mamlaka itafuatilia kwa makini mwenendo wa dereva husika na kama atataka kurejea tena barabarani, atalazimika kusoma upya sheria na kanuni za usalama barabarani ndipo arejeshewe leseni yake.
Hayo yalisemwa na Wakili wa Serikali na Mwanasheria Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani Taifa, Inspekta Deus Sokoni, wakati wa mafunzo ya weledi na Sheria ya Usalama Barabarani kwa madereva zaidi 100 jijini Dar es Salaam yaliyoratibiwa na kampuni ya Afrexa International Limited.
Inspekta Sokoni alisema kuwa kabla ya kuanza rasmi kwa mpango huo, serikali ilijipa muda wa kutosha kuufanyia utafiti na kubaini kuwa utaleta tija katika kupunguza matukio ya ajali yanayofanywa na madereva wengi kwa sababu wanajua mifumo ya sasa haiwatambui kirahisi.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Afrexa International Ltd, inayojishughulisha na utafutaji wa ajira kwa madereva hapa nchini, Martin Gabone, aliwaeleza washiriki hao kuwa mfumo kama huo umekuwa ukitumika hapa nchini kwa madereva wa baadhi ya kampuni hususan ya simu za mkononi ya Tigo na kufanikiwa kupunguza na kudhibiti makosa mbalimbali.
“Mpango huo unajulikana zaidi kama ‘dring passport & demerit point system’ ambapo mwenendo wa dereva kitaaluma unaonekana kupitia mfumo wa mawasiliano ya kompyuta,” Gabone.
Madereva ambapo wengi wao wameajiriwa kwa mikataba rasmi ya kisheria katika kampuni mbalimbali kwa msaada wa kampuni yake. “Kwa kutambua umuhimu wa fani ya udereva, Afrexa International Limited imeona kuna umuhimu wa kuwaandalia mafunzo madereva angalau mara nne kwa mwaka ili kuwaongezea uwezo wa kutafsiri sheria, kanuni za usalama barabarani na kujiamini,” alisema.
Kadhalika, Gabone alisema kampuni yake ipo katika hatua za mwisho kutekeleza mpango wa mafunzo kwa madereva wanawake nchini, mafunzo ambayo yatakapoanza yatahusisha madereva wengi kwa lengo la kuwaibua na kuwajengea uwezo wa kitaaluma.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, mtoa mada ambaye pia ni Mwanasheria wa idara hiyo Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Inspekta wa Polisi Mussa Manyama, aliwaambia washiriki kuwa dereva mwenye taaluma huwa anajiamini wakati wote anapokuwa barabarani.
“Dereva aliyepata mafunzo, huwa ni kipenzi cha trafiki barabarani kwa sababu anaelewa karibu kila kitu ikiwamo sheria na kanuni za usalama barabarani, kinyume chake wengi huwa wanababaika kila wanapoulizwa jambo,” alisema.
Mmoja wa washiriki mafunzo hayo, Issa Milambo, alisema kuwa moja kati ya mambo waliyojifunza ni kuanza kwa zoezi la ulipaji faini kwa njia ya kielektroniki na kanuni za usalama barabarani.
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO‘ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram naYouTUBE kwa kubonyeza hapa >>> INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE