HABARILEO
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete amesema ujivuni wa fedha sio mali kitu, kwani mtu anaweza kununua watu wachache kwa tamaa na njaa zao, lakini hawezi kukinunua chama chote.
Pia, amesema wana CCM wasihofu kwani mtu anaweza kuwalipa watu wachache na kamwe hataweza kuwanunua Watanzania wote.
Akimtambulisha mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli kwa wanachama wa chama hicho mkoa wa Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema uteuzi wa mgombea huyo umekipa sifa chama hicho.
Alisema uteuzi wa Dk Magufuli ni kama ulipangwa na Mungu na akaeleza kuwa ndio maana hata uchukuaji wake wa fomu, haukuwa na mbwembwe zozote wala hakutaka kuzungumza na waandishi wa habari kama walivyofanya wagombea wengine.
“Siku moja nilizungumza naye nikamuuliza wenzako wanachukua fomu za urais, mbona wewe hujaenda kuchukua, akanijibu hivi na mimi natosha kuwa Rais, nikamweleza wana CCM wenyewe wataamua kama unatosha ama hautoshi.
“Siku moja akasema ana shida ya kuja kuniona, nikamwambia njoo, alivyokuja akaniambia masuala ya madeni ya makandarasi… lakini baadaye akasema mzee nimekuja kukuaga naenda kuchuka fomu, lakini sitazungumza na waandishi wa habari… sasa nikamhoji watu watakujuaje?” Kikwete.
Alisema ndio maana kwenye vikao vya chama wakati wa uteuzi jina la Magufuli kuanzia Kamati ya Maadili, Kamati Kuu na kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa lilipenya kwa sababu ni mtu mwadilifu na akapita pia kwenye mkutano mkuu.
Rais Kikwete pia alitumia mkutano huo, kutaja sifa za mgombea huyo wa CCM kuwa ni mgombea mzuri aliyekamilika kila upande, kwani ni mwadilifu na mwaminifu kwa chama chake.
HABARILEO
Ofisi za serikali na taasisi za Umma zimeagizwa kuacha mara moja kukusanya mapato ya serikali kwa kutumia risiti za kuandika kwa mkono, badala zitumie mfumo wa serikali mtandao.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ameziagiza ofisi kutoa agizo hilo jana wakati akifungua kongamano la siku mbili la serikali mtandao na matumizi ya Teknolojia za Habari na Mawasiliano (TEHAMA) lililoshirikisha makatibu wakuu wote wa Wizara za serikali na Manaibu wao, Makatibu Tawala wote wa Mikoa hapa nchini, Wakurugenzi wa Jiji na Halmashauri kote nchini na wakuu wa idara zore za serikali na taasisi za umma.
Alisema hakuna sababu yoyote ya mapato ya serikali kukusanywa kwa risiti za kuandika kwa mkono katika karne hii na kuwataka wahusika kubadilika.
“Kuanzia sasa sio hiari ni lazima Jiji, Halmashauri, ofisi za serikali na taasisi za umma kote nchini kuacha mara moja kukusanya mapato ya serikali kwa kuandika risiti za mkono,’’ alisema.
“Tukifanikiwa kukusanya mapato ya serikali kwa teknolojia ya TEHAMA kuna uhakika mkubwa wa mapato.’’
Aidha, utengenezaji wa mifumo uzingatie programu ambazo wataalamu wa hapa nchini wanaweza wakatambua kinachofanyika badala ya kuwa na mifumo ambayo hawajui kinachoendelea nyuma ya pazia.
Awali kabla ya kumkaribisha Balozi Sefue, Kaimu Katibu Mkuu ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hab Mkwizu alisema kongamano hilo la siku mbili limeshirikisha wajumbe zaidi ya 200 na wanapatiwa mafunzo ya kisasa kutoka kwa wataalamu kutoka nchini India na Singapore.
HABARILEO
Maofisa Utumishi watatu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashitaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh milioni 3.7.
Washitakiwa ni Anold Shana, Prisca Mangili na Agness Hugo ambao walisomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda.
Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Sophia Ghula alidai walitenda makosa hayo katika tarehe tofauti mwaka 2008.
Katika mashitaka yanayomkabili Shana, anadaiwa kati ya Septemba na Desemba 2008 akiwa Ofisa Utumishi alitumia vibaya madaraka yake kwa kutokutoa maelekezo kwa Mhasibu Mkuu wa wizara hiyo, aondoe jina la mfanyakazi aliyestaafu, Rota Mboya katika orodha ya malipo jambo lililosababisha alipwe Sh milioni 1,194,750 .
Mshitakiwa mwingine, Mangili, anadaiwa kati ya Februari na Juni 2008, alitumia madaraka vibaya kwa kutokutoa maelekezo kwa Mhasibu Mkuu wa Wizara, kuondoa jina la mfanyakazi aliyestaafu, Bibi Kanancia katika orodha ya malipo jambo lililosababisha alipwe Sh milioni 1,682,653.52 .
Naye Hugo anadaiwa Aprili, 2008 alitumia madaraka yake vibaya kwa kutokutoa maelekezo kwa mhasibu mkuu wa wizara kuondoa jina la Eidis Mabu, katika orodha ya malipo na kusababisha alipwe Sh 942,593 na hivyo kuisababishia serikali hasara.
Washitakiwa walikana mashitaka. Upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na imepangwa Septemba 23 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa. Wapo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili waliosaini hati ya Sh milioni mbili kila mmoja.
HABARILEO
Ubomoaji wa jengo pacha lenye ghorofa 16, lililopo mtaa wa Indira Ghandi Dar es Salaam, imeshindikana.
Imeelezwa kuwa mkandarasi aliyepewa kazi hiyo amebadili msimamo wake dakika za mwisho kwa madai kuwa, kazi ya kubomoa ni ngumu na yenye madhara kwa majengo yaliyo jirani.
Hayo yamebainishwa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngurumi wakati akizungumzia hatua zilizofikiwa wa ubomoaji wa jengo hilo, kufuatia kubainika kuwa limekiuka sheria za mipango miji.
Mngurumi alisema mmiliki wa jengo hilo baada ya kupewa taarifa ya kulibomoa alikimbilia mahakamani, na kwamba kesi hivi sasa imesikilizwa na imeisha na maamuzi ni kwamba jengo hilo linapaswa kubomolewa.
Alisema Manispaa ya Ilala ilitangaza zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi atakayeweza kubomoa jengo hilo, na kwamba katika zabuni hiyo, alijitokeza mkandarasi mmoja kampuni ya kichina ya CRJ, ambapo ilikubali kazi hiyo, ila ilijitoa dakika za mwisho.
Aliongeza, wao hawawezi kulibomoa kwa kuwa hawana ujuzi wa kazi hiyo na kwamba kinachofanyika hivi sasa ni Manispaa hiyo inazungumza na Bodi ya Wakandarasi Nchini (CRB), kuangalia kama wanaweza kumpata mkandarasi mwenye sifa na uwezo wa kufanya kazi hiyo ya ubomoaji.
Kubomolewa kwa jengo hilo, kunatokana na kuporomoka kwa jengo lililokuwa jirani na hilo ambalo lilisababisha vifo vya watu 36, na kujeruhi wengine 18, tukio lililotokea Machi 29 mwaka 2013.
Hata hivyo, sababu za kuporomoka kwake zilitokana na kujengwa chini ya kiwango lakini pia ukiukwaji wa sheria kwa kuongeza idadi ya ghorofa kutoka ghorofa nane zilizoidhinishwa kisheria hadi ghorofa kumi na tano.
Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, inatoa maelekezo kwa mwekezaji yeyote anayetakiwa kufanya ujenzi wa mradi wowote ambao ni zaidi ya ghorofa tano, lazima aombe kibali cha tathimini ya mazingira katika ofisi hiyo.
Mara baada ya tukio hilo, la Machi 29, Aprili 5 mwaka 2013, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka aliyeambatana na wajumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira walitembelea eneo hilo na kutoa siku 30 kwa mmiliki wa jengo hilo, Ally Raza kulibomoa baada ya kubainika kujengwa chini ya kiwango na sehemu isiyo zingatia mipango miji.
MTANZANIA
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli pamoja na mwenzake kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa, wamepigana vikumbo mahakamani huku kila mmoja akisaka kiapo cha mahakama kuthibitisha rasmi kuwania nafasi hiyo.
Magufuli na Lowassa kwa sasa wamekuwa mahasimu wa kisiasa tangu waziri mkuu huyo wa zamani alipotangaza kuihama CCM baada ya mchakato wa urais uliofanyika mjini Dodoma Julai mwaka huu.
Wagombea hao walikwenda jana Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kupewa fomu kila mmoja kwa wakati wake ya kumthibitisha kuwania nafasi hiyo ya juu katika uongozi wa nchi.
Wagombea hao walithibitisha fomu hizo mbele ya Jaji Sakieli Kihiyo kwa matakwa ya kanuni za uchaguzi wa Rais na Bunge za mwaka 2015.
Dk. Magufuli alikwenda mahakamani hapo akiwa ameandamana na mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan mbele ya Jaji Kihiyo saa tano na walikaa katika chumba cha mahakama kwa zaidi ya saa moja kwa ajili ya kusaini.
Baada ya kumaliza kuapa na kusaini Dk. Magufuli alitoka nje ya mahakama na kuzungumza kwa kifupi na wanahabari.
“Katika fomu ya kugombea nafasi ya urais inaeleza kwamba mtu anayetaka kushika madaraka makubwa azingatie kanuni na sheria zilizoainishwa .
“Kilichonileta hapa leo (jana) ni kukamilisha sehemu ya kanuni na sheria, kukagua fomu kwa ukamilifu na kusaini kiapo, naomba Watanzania waniombee,”alisema na kuondoka.
Waziri Mkuu Mstaafu, Lowasa alifika eneo la mahakama saa saba adhuhuri na kuelekea moja kwa moja katika chumba cha mahakama kwa ajili ya kuapa na kusaini fomu ya kugombea urais.
Lowassa alichukua nusu saa kumaliza mchakato huo na kutoka na alipotakiwa kuzungumza na waandishi wa habari alisema hawezi kusema chochote.
“Siwezi kusema lolote, tusubiri Tume ya Uchaguzi ikinipitisha nitazungumza,”alisema kwa kifupi Lowassa.
Akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari Msajili wa Mahakama Kuu John Kahyoza, alisema katika fomu za kugombea udiwani, ubunge na urais kuna kipengele cha tamko au kiapo cha kisheria cha mgombea.
“Leo wagombea urais wamekuja kuthibitisha kwa kiapo waliyoyajaza katika fomu ya kugombea nafasi hiyo ni sahihi, wamefanya hivyo kwa matakwa ya kanuni za uchaguzi na Bunge za mwaka 2015.
“Miongoni mwa wanayothibitisha ni kwamba wao ni raia wa Tanzania, wametimiza umri unaohitajika kisheria, hawajawahi kutiwa hatiani na kufungwa kwa kosa lolote ikiwemo kukwepa kodi.
“Fomu ikisharudishwa na kubainika kwamba miongoni mwa waliyoapa walisema uongo ni kosa la jinai hivyo aliyeapa anastahili kuchukuliwa hatua,”alisema.
Alisema madiwani na wabunge wanatakiwa kuapa mbele ya hakimu lakini haikueleza ni hakimu wa mahakama gani hivyo wanaweza kuapa kwa hakimu wa mahakama yoyote.
Alipoulizwa sababu ya Dk. Magufuli kutumia zaidi ya nusu saa, Kahyoza alisema wagombea urais walitakiwa kupita katika mikoa kumi kwa ajili ya kusaka wadhamini hivyo fomu zinatakiwa ziwe 40.
“Kundi la kwanza lililoingia la Dk. Magufuli lilikuwa na fomu zote 40, zikathibitishwa na kusainiwa.
“Kundi la pili la Lowassa waliingia na fomu zao nne, nikawauliza wakajibu ndizo walizoelekezwa, nikawashauri wakaongeze mbili, walifanya hivyo zikathibitishwa na kusainiwa.
MTANZANIA
Maambukizi mgonjwa wa kipindupindu yamezidi kushika kasi mkoani Dar es Salaam, baada ya idadi ya wagonjwa kuongezeka kutoka 34 hadi kufikia 43.
Ongezeko hilo limekuja ikiwa ni siku tano tangu kugundulika kwa ugonjwa huo, ambao tayari umesababisha vifo vya watu watatu.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Dk. Azizi Msuya, alisema kutokana na ongezeko hilo, wamelazimika kutoa huduma kwa wagonjwa wote waliopo kwenye kambi ya Hospitali ya Mburahati.
“Mpaka sasa hatujapokea taarifa ya mgonjwa wa kipindupindu aliyefariki dunia katika wilaya yetu… juzi tumewaruhusu wagonjwa wanne na jana tumeruhusu watatu,” alisema.
Alisema kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo, manispaa imejipanga kutoa elimu ya nyumba kwa nyumba kuhimiza usafi katika familia pamoja na kunyunyizia dawa sehemu za mazalia.
Dk. Msuya alisema ni muhimu jamii itambue kuwa chanzo cha ugonjwa huo ni uchafu unaotokana na mazingira husika, hivyo haina budi kuzingatia usafi na kuepuka ulaji ovyo wa vyakula bila mpangilio.
Naye Muuguzi Mkuu wa Wilaya hiyo ambaye ndiye msimamizi wa kambi ya Mburahati, Nusura Kessry, alisema kambi hiyo imezidiwa kutokana na wagonjwa wanaotoka katika vituo vingine kuhamishiwa kituoni hapo.
“Tuna wagonjwa 21, kati yao 10 wanatarajiwa kuruhusiwa kutokana na afya zao kuimarika. Tatizo kubwa linalotukabili ni ufinyu wa eneo kwa kuwa tuna uwezo wa kuhifadhi wagonjwa 16 tu.
“Kambi hii inatarajiwa kuwa kituo kikubwa cha wilaya na wagonjwa wote walioko hospitali za Sinza na Mwananyamala watahamishiwa hapa,” alisema.
Akizungumzia uwapo wa vifaa tiba kwenye kambi hiyo, alisema mbali na ufinyu wa eneo na kuhitaji mahema hawana tatizo jingine.
Alisema kutokana na ongezeko la wagonjwa wanaohamishiwa katika kambi hiyo, ni muhimu kila mtu achukue tahadhari juu ya ugonjwa huo.
“Familia wanapogundua kuwapo kwa mtu mwenye dalili hizo, ni vyema kuwahishwa katika hospitali iliyo karibu.
NIPASHE
Serikali imezuia matumizi ya uwanja wa Taifa kwa shughuli za mikutano ya kisiasa.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Assah Mwambene, alisema jana kuwa hatua hiyo imechukuliwa ili uwanja huo utumike kwa shughuli za michezo pekee.
“Tumeamua kuufahamisha umma juu ya jambo hili kutokana na taarifa zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii na kuripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pamoja na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) vitafanya mkutano wa uzinduzi wa kampeni keshokutwa katika uwanja huo,” alisema Mwambene.
Alisema walipata barua ya maombi kutoka Chadema Agosti 12 wakiomba uwanja huo kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni zao na kwamba walishawapatia majibu kwamba hakuna chama cha siasa kitakachoruhusiwa kutumia uwanja huo kutokana na mihemuko na hamasa za kisiasa inayoweza kujitokeza miongoni wafausi wa vyama na kusababisha uharibifu.
Alisema walichukua uamuzi huo kwa busara ili kuufanya uwanja wa Taifa ubaki kwa ajili ya shughuli za michezo tu.
Hata hivyo, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene, alisema hawajapata taarifa zozote kutoka serikalini zaidi ya kusikia kupitia vyombo vya habari.
Makene aliongeza kuwa hatua hiyo imechukuliwa kuficha aibu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuhofia wingi wa watu watakaojitokeza kwenye mkutano wa Ukawa kwa kuwa chama tawala kitazindua kampeni zake katika viwanja vya Jangwani eneo ambalo ni dogo ambalo hawawezi kupata watu wengi.
“Serikali inapaswa kutambua kuwa uchaguzi unaamua hatima ya nchi husika kwa kuzingatia demokrasia, hivyo wanachokifanya ni kuvinyima vyama vya upinzani haki ya msingi kwa ajili ya shughuli mhimu kwa kigezo cha kuvunja amani kitu ambacho si sahihi,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Makene, hawatapoteza muda kubishana na Serikali bali watatafuta eneo lingine la kufanyia mkutano huo na watatoa taarifa kwa wananchi na wafuasi wote wa Ukawa nchini.
NIPASHE
Mgombea ubunge wa Chama cha Wananchi (CUF) amedai kutekwa, kutishwa na kuporwa fomu za kugombea katika jimbo la Shaurimoyo, Unguja.
PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos