NIPASHE
Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), umesema utakuja na stahili mpya wakati Rais Dk. John Magufuli, atakapokwenda kuzindua na kuhutubia Bunge Novemba 20, mwaka huu.
Umesema staili watakayoitumia ni tofauti na ile waliyoitumia wakati Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, alipozindua Bunge la 10 mwaka 2010 ya kutoka nje ya ukumbi kuonyesha kutotambua serikali yake.
Aliyekuwa Mnadhimu wa Bunge la 10 Kambi la Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, alisema safari hii hawatatoka nje ya ukumbi wa Bunge hata kama hawamkubali Rais Magufuli, kwa kuwa ni wajibu wao kushiriki vikao vya chombo hicho cha kuwakilisha wananchi.
“Sisi ni wabunge, tumo humu kwa ridhaa ya wananchi, tuna haki ya kuingia bungeni, hivyo siku hiyo tutaingia lakini kitakachotokea tutajua siku hiyo, bali haitakuwa kama walivyotuzoea tunatoka nje,” alisema na kuongeza..“Subira yavuta heri, bado siku tatu tu, Watanzania watajua msimamo wetu tukiwa ndani ya Bunge,” alisema.
Hivi karibuni aliyekuwa mgombea urais wa Ukawa kupitia Chadema, Edward Lowassa, alisema hawatambui matokeo yaliyotangazwa naTume yaTaifa ya Uchaguzi (NEC) na kumpa ushindi Rais Magufuli na kwamba hawatashirikiana na serikali yake kutokana na kile alichoeleza kuwa uchaguzi mkuu uligubikwa na wizi wa kura na kuporwa ushindi.
NIPASHE
Baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, leo yatakumbwa na bomoabomoa ya nyumba ambayo ujenzi wake umekiuka matumizi yaliyokusudiwa ikiwamo kujenga bila kibali, bila kufuata michoro ya mipango miji na matumizi ya ardhi.
Kazi hiyo inafanywa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni.
Maeneo yatakayobomolewa nyumba hizo kwa siku tatu mfululizo kuanzia leo hadi keshokutwa huu ni Mbezi Beach, Tegeta, Bunju, Mwenge na Kinondoni eneo la Biafra.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana na Msemaji wa wizara hiyo, Hassan Mabuye, wizara hiyo inakusudia kubomoa nyumba hizo zilizokiuka Sheria na taratibu za Ardhi.
“Maeneo yaliyotengwa mijini kwa matumizi ya umma ikiwa ni pamoja na maeneo ya wazi, njia za miundombinu na huduma nyinginezo za umma, mara kwa mara hutumiwa vibaya au kuvamiwa na waendelezaji binafsi hivyo kuukosesha umma manufaa yaliyokusudiwa. Nyumba hizo tutazibomoa,” alisisitiza Mabuye katika taarifa yake hiyo.
Taarifa hiyo ilirejea tamko namba 6.6.1 la Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995, serikali inahakikisha kwamba maeneo yote ya mijini yaliyotengwa kwa shughuli za umma yanatumika kwa shughuli zilizokusudiwa na yanalindwa ili yasivamiwe.
“Tamko namba 8.2.1 la Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995, linasema serikali za mitaa zitawajibika kushirikiana na Wizara ya Ardhi kuhakikisha usimamizi mzuri wa ardhi katika maeneo yao,” ilisema taarifa hiyo.
Ilibainisha kuwa Sera ya Taifa ya Ardhi inaeleza sababu inayofanya Wizara kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni kuendesha kazi ya ubomoaji huo.
NIPASHE
Serikali imeupa uongozi wa Kiwanda cha Urafiki hadi Desemba mosi, mwaka huu kutekeleza kwa vitendo maagizo yaliyotolewa na Mahakama ya Usuluhishi ya kuanza kuwalipa nyongeza ya mishahara wafanyakazi wake kama sehemu ya kumaliza mgogoro wa wafanyakazi uliodumu kwa zaidi ya wiki moja sasa.
Wiki iliyopita, wafanyakazi wa kiwanda hicho walifanya mgomo endelevu wakidai nyongeza ya mshahara.
Agizo hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, alipotembelea kiwanda hicho na kuzungumza na viongozi na wafanyakazi.
Alisema kila mfanyakazi katika kiwanda hicho ana haki na mamlaka ya kudai anachostahili bila kupingwa na mtu yeyote na vile vile ana haki ya kusikilizwa na kutimiziwa mahitaji yake yote muhimu na kwa muda unaostahiki.
Licha ya kutoa agizo hilo, pia DC Makonda aliutaka uongozi wa kiwanda hicho na Chama cha Wafanyakazi kukaa kwa pamoja ili kubaini deni sahihi la wafanyakazi kwani kiwango cha deni la sasa kinaonekana kuwa na utata.
“Kabla ya kuwalipa madai wafanyakazi hawa, nahitaji pande zote mbili zikae pamoja kwa majadiliano ili kupitia madai upya hatimaye kujua wafanyakazi wanadai kiasi gani,” alisema.
Aidha, Makonda ameagiza kila mfanyakazi husika kupata malipo yake uwe wazi.
Baadhi ya wafanyakazi hao walisema wamepata matumaini ya mgogoro kufikia mwisho na kumpongeza Mkuu wa Wilaya kwa jitihada alizofanya.
MTANZANIA
Aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila kupitia Chama cha NCCR – Mageuzi, amefungua kesi Mahakam Kuu Kanda ya Tabora kupinga ushindi wa Hasna Mwillima wa Chama Cha Mapindunzi (CCM), aliyetangazwa mshindi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Kafulila amewasilisha pingamizi hilo jana kupitia kwa wakili wake, Daniel Lumenyela, huku akiwa ameambatanisha nakala za fomu za matokeo ya kura ya vituo vyote 382 vya jimbo hilo ambazo zilisainiwa na mawakala wa vyama vyote zinazoonesha alishinda uchaguzi huo.
Akiwa mahakamani hapo, umati wa wanachama wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ulifurika tangu majira ya saa mbili asubuhi.
Kafulila alisema ameiomba mahakama ipitie nyaraka hizo na kisha imtangaze yeye kuwa mshindi wa uchaguzi wa jimbo hilo.
Alidai msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Reuben Mfune, alipewa shinikizo na viongozi wa Serikali amtangaze mgombea wa CCM, Hasna Mwilima, kuwa mshindi kwa kura 34,000 dhidi ya kura 32,000 alizopewa yeye.
Kafulila alisema toka siku hiyo Oktoba 28, mwaka huu yalipotangazwa matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo chini ya ulinzi mkali, msimamizi huyo bado hajaonekana hadharani.
Hata hivyo awali matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo yalikuwa yakitarajiwa kutangazwa Oktoba 27, mwaka huu lakini alisitisha utangazaji huo kwa madai kuwa ameshauriwa na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kuagizwa kusitisha zoezi la utangazaji hadi hapo baadaye.
Msimamizi huyo alikaririwa kuwa uamuzi wake huo wa kuwasiliana na ngazi za juu ulitokana na mgombea wa CCM Hasna Mwilima kugomea matokeo baada ya zoezi la kuhakiki kukamilika wakiwa pamoja.
“Haki ya wapiga kura wa Jimbo la Kigoma Kusini itapatikana lakini kinachofanyika ni kunichelewesha kunitangaza mimi kuwa mbunge,” Kafulila.
Alibainisha katika kile kinachoonyesha ni kuficha unyang’anyi waliofanya hata nakala za majumuisho ya matokeo ya kura za wagombea hawakupewa wala kuonyeshwa fomu zake.
Kwa upande wake Wakili Lunyemela anayemwakilisha Kafulila katika shauri hilo alisema uchaguzi mzima haukuwa na utata na ndiyo maana mteja wake anadai mahakamani kutangazwa kuwa ndiye mshindi halali wa jimbo hilo.
“Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo alichofanya ni kuchukua matokeo ya kura ya mteja wake na kumpa aliyekuwa mgombea wa CCM Hasna Mwillima na ndiyo maana walilazimisha kuwepo kwa ulinzi mkali ili watangaze matokeo batili,” alisema.
Lunyemela alisema sheria ya uchaguzi na 343 imeweka vigezo muhimu vya kumpata na kumtangaza mshindi wa uchaguzi ikionyesha wazi kuwa aliyepata kura nyigi ndiye anastaili kuwa mshindi.
HABARILEO
Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani hapa leo inatarajiwa kutoa hukumu ya kesi ya jinai inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shehe Ponda Issa Ponda.
Hukumu hiyo iliahirishwa kutolewa Oktoba 19, mwaka huu baada ya Hakimu Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Mary Moyo kushindwa kukamilisha kuiandika kutokana na matatizo ya kiafya yaliyokuwa yakimkabili.
Kutokana na kushindwa kutolewa kwa hukumu hiyo, Ponda ameendelea kukaa rumande hadi leo ambapo hatima yake itajulikana. Wakati akiahirisha kesi hiyo, Hakimu alisema, sheria inataka hukumu hiyo isomwe ndani ya siku 90 baada ya kukamilika kwa taratibu za kesi hiyo.
Alisema, kutokana na sababu zake za kiafya alishindwa kukamilisha kuandika hukumu hiyo na kutokana na sheria hiyo anayo mamlaka ya kuahirisha kwa vile atakuwa bado ndani ya siku 90 zilizotajwa kisheria.
Kutokana na sababu hizo, aliwafahamisha mawakili hao kuwa hukumu hiyo ameipanga kuitoa Novemba 18, mwaka huu kulingana na matakwa hayo ya kisheria.
Ponda alifunguliwa kesi namba 128/2013 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro awali akikabiliwa na mashitaka matatu anayodaiwa kuyatenda Agosti 10, mwaka 2013 katika eneo la Kiwanja cha ndege Manispaa ya Morogoro.
Alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Agosti 19 mwaka 2013 kwa makosa hayo matatu na baadaye alifutiwa shitaka moja na kubakia mawili ambayo ni kutoa maneno yenye kuumiza imani za dini na kushawishi watu kutenda kosa.
HABARILEO
Rais John Magufuli amewasili mkoani Dodoma kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuongoza Tanzania akiwa ametumia njia ya barabara huku akiwa na siri moyoni ya nani atakuwa Waziri Mkuu wake.
Njia aliyotumia kufika Dodoma imewashangaza wengi kutokana na ukweli kwamba marais waliotangulia wamekuwa wakitumia usafiri wa ndege.
Baada ya kuwasili Ikulu Ndogo ya Rais iliyopo Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma akitokea jijini Dar es Salaam, alipokewa na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Chamwino Ikulu, Joseph Seganje, wananchi wamefarijika kuona Rais huyo akiishi kwenye Ikulu hiyo kama alivyokuwa ameahidi. “Tayari tumempokea Rais wetu na wananchi wana furaha isiyo na kifani,” Seganje.
Wakizungumza mapema wiki iliyopita, baadhi ya wakazi wa Chamwino Ikulu walisema itakuwa ni faraja kubwa kwa Rais kuishi kijijini hapo.
Alice Chidong’oi alisema Dk Magufuli ni kiongozi anayeonesha nia ya dhati ya kuwatumikia watu wake kwa kujali zaidi wanyonge kama ilivyokuwa kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
“Tunaamini akiishi hapa atakuwa sehemu ya jamii ya Wana Chamwino na hilo litasaidia hata kuboreshwa kwa huduma za jamii ikiwemo maji,” alisema Chidong’oi.
Alisema hiyo itakuwa fursa nzuri kwa wakazi wa eneo hilo kufanya biashara, kwani uwepo wake ndani ya wilaya hiyo utaongeza idadi ya wageni.
Mkazi mwingine, Stanley Richard, alisema vijana wa Chamwino wanapenda kazi na Dk Magufuli akiwa hapo itakuwa ni kazi tu. “Ni mtu ambaye anapenda kazi na sisi vijana tunapenda kufanya kazi, tutampa ushirikiano mkubwa katika kipindi chote atakachokuwa madarakani,” alisema.
Alisema alifurahi alipochaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani alijua nchi imepata kiongozi ambaye yuko tayari kuwaletea wananchi wake mabadiliko. Tayari Serikali mkoani hapa imepiga marufuku kufanyika kwa mikutano ya hadhara na maandamano wakati wa vikao vya Bunge vikiendelea.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa, alisema amri hiyo ya kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa bado inaendelea ili kuweka utulivu muda wote wa vikao vya Bunge.
Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Bunge, kesho Alhamisi, Bunge litapokea na kuthibitisha kwa kupiga kura jina la Waziri Mkuu wa 11 wa Tanzania ambalo Dk Magufuli atakuwa ameliwasilisha kwa Spika Job Ndugai.
Kwa hiyo, Dk Magufuli atakuwa ametua mjini hapa akiwa na siri yake moyoni ya nani atakuwa Waziri Mkuu wake kwa miaka ya mwanzo ya utawala wake inayokoma mwaka 2020.
Mbali ya kutoa jina la Waziri Mkuu, Dk Magufuli anatarajia kulihutubia Bunge, Ijumaa alasiri baada ya kuwa amemwapisha Waziri Mkuu asubuhi. Hotuba yake itakuwa dira ya utawala wake kwa miaka mitano ijayo.
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram na YouTUBE wa kubonyeza hapa>>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE.