NIPASHE
Wakati zikiwa zimebaki siku 44 kabla ya kufikiwa kwa siku ya kupiga kura Oktoba 25, mwaka huu, mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, ameamua kuweka wazi sifa za watu atakaowajumuisha katika baraza lake la mawaziri pindi akichaguliwa kuwa mrithi wa Rais Jakaya Kikwete katika serikali ijayo ya awamu ya tano.
Akizungumza mbele ya umati katika mkutano wake wa kampeni mjini hapa jana, Magufuli alisema sifa mojawapo kubwa ya mtu atakayemteua katika baraza lake la mawaziri ni kutokuwa bingwa wa kutoa visingizio vya hapa na pale katika kuhalalisha ucheleweshaji wa huduma kwa wananchi.
Kadhalika, alisema sifa ya pili ya mtu atakayemteua kushika nafasi ya uwaziri katika serikali yake ni kuchapa kazi bila kuchoka katika kushughulikia matatizo ya wananchi, huku akigusia kauli mbiu yake ya “Hapa Kazi Tu”.
Magufuli alitaja sifa ya tatu muhimu kwa waziri atakayemteua kuwa ni anayejali matatizo ya wananchi na hata mvumilia ambaye atatelekeza ofisi na kwenda kwenye shughuli zake binafsi.
Alisema sifa ya nne kwa waziri atayekuwamo katika serikali yake ni kujali muda katika kushughulikia kero za wananchi; kwamba kila tatizo likifikishwa kwake alishughulikie kwa wakati na si kinyume chake.
“Nitaweka aina ya mawaziri ambao wao ni kazi tu… wakipelekewa matatizo ya wananchi wanayatatua kwa wakati na sitaki kusikia visingizio kama mchakato unaendelea wala nini… nataka kazi tu,” alisema Dk. Magufuli na kuamsha shangwe kubwa kutoka kwa wananchi waliofika kwa wingi kumsikiliza.
Katika sifa ya tano, Magufuli alisema kila waziri atakayemteua ni lazima aonyeshe wazi kuwa anayo dhamira ya dhati ya kuwatumikia Watanzania na mara zote atafanya kazi kwa kujua kuwa kipaumbele kikubwa ni kuwatumikia wananchi waliowachagua.
Magufuli alitaja sifa ya sita muhimu zaidi kwa mawaziri wake ni uadilifu na wasiotiliwa shaka na wananchi watakaokuwa wakiwatumikia, huku wakijua kuwa wengi wao (wananchi) ni watu maskini wanaohitaji huduma zote muhimu za kijamii ili kujikwamua kiuchumi.
“Mimi ni mwenzenu ni maskini na nimeishi maisha hayo ya kupanda bajaji, daladala na hata baiskeli… msifanye makosa (siku ya uchaguzi) na kama kweli mnataka maendeleo, basi nichagueni mimi muone kwasababu najua ubaya wa umasikini, “ alisema Dk. Magufuli.
Alisema atafunga mianya yote ya upotevu wa fedha za umma ili fedha zitakazookolewa zielekezwe katika kutoa huduma za jamii kama kuhakikisha kuwa hospitali, zahanati na vituo vya afya vinakuwa na dawa na vifaa tiba vya kutosha.
Akihutubia katika Jimbo la Mkinga, Dk. Magufuli alisema akichaguliwa na kuingia Ikulu, ataboresha zaidi maslahi ya watumishi wa umma, hasa walimu na madaktari, ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Nikiwa Rais nitakuwa mtumishi wa Watanzania wote. Uwe CUF wewe ni wangu, ACT – Wazalendo, Chadema, NCCR – Mageuzi wote nitakuwa mtumishi wenu. Hivyo naombeni kura zenu niweze kuwatumikia katika kuleta maendeleo,” alisema Dk. Magufuli.
Aliongeza kuwa katika kampeni zake ameamua kutumia barabara za vumbi na zenye makorongo ili ajue shida za wananchi akiingia madarakani aweze kuzishughulia kwa uhakika.
Akiwa katika Jimbo la Bumbuli, Dk. Magufuli aliahidi kufuta misamaha ya kodi kwa kampuni kubwa ili fedha zitakazookolewa zitumike kusaidia miradi ya maendeleo kama elimu, afya na barabara.
Alisema anazijua kampuni kubwa ambazo zimekuwa zikinufaika na misamaha ya kodi bila sababu za msingi wakati wananchi wa kawaida wakiteseka kwa kukatwa kodi.
Alisema serikali yake haitakubali hata kidogo kuona mamalishe na wamachinga wakikamatwa kila mara na kuteswa na askari mgambo kwa sababu ya kodi ndogo ndogo wakati kuna kampuni kubwa zinazopata faida kubwa lakini hazilipi kodi.
NIPASHE
Polisi mkoani Geita imefanikiwa kuokoa baa moja maarufu iliyopo mkoani humu (jina limehifadhiwa) isiteketezwe na moto na wananchi wenye hasira waliokuwa wakidai inahusika na matukio ya vifo vya kutatanisha vya walinzi watatu waliofariki dunia kwa nyakati tofauti.
Wananchi hao walikuwa na hasira ya kutaka kuteketeza baa hiyo baada ya walinzi hao (majina yao yamehifadhiwa), wakazi wa mkoani Geita, kufariki dunia ikiwa ni miezi minne tangu mlinzi mwingine kuuawa akiwa lindoni.
Vifo hivyo viliwafanya wananchi waamini kwamba vinatokana na imani za kishirikina.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Joseph Konyo, alisema tukio hilo limewafanya wananchi kuhusisha na imani za kishirikina lakini polisi wanaendelea kulifanyia uchunguzi kitaalam.
‘’Upelelezi umefikia hatua nzuri, tupo hatua nzuri ya kuwanasa watuhumiwa waliotaka kuhusika na tukio hilo, lakini tunafanya hivyo kwa kuzingatia sheria kwani matukio hayo yameacha utata mkubwa,” alisema Kamanda Konyo.
Alisema baa hiyo kwa sasa imefungwa kutokana na shinikizo la wananchi na pia mmiliki wake huenda anahofia usalama wake huku akiwataka wananchi kutojichukulia sheria mkononi.
Hata hivyo, Mchungaji Samson Mkamato, wa Kanisa la Muungano wa Makanisa ya Kipentekoste mkoani humu, alisema anasikitishwa na hatua hiyo kutokana na watu wengi kuweka mbele imani za kishirikina na kupoteza hofu ya Mungu.
“Ninashauri ulinzi shirikishi kuimarishwa na kuna haja ya viongozi wa dini kuelimisha jamii ili kuepukana na imani za kishirikina kama ambavyo wananchi walivyopandwa hasira kutokana na vifo vya walinzi hao,” alisema Mchungaji Mkamato.
NIPASHE
Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) umeahidi kuwa kama utashinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwezi ujao, utarejesha serikali ya Tanganyika.
Kauli hiyo ilitolewa mjini Zanzibar jana wakati wa uzinduzi wa kampeni ya mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, katika uwanja wa Demokrasia.
Maalim akihutubia umati wa wananchi katika mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na mgombea wa Ukawa wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa, alisema wakishinda wataunda serikali ya muundo wa serikali tatu kama ilivyopendekezwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Mstaafu, Joseph Warioba.
Tume hiyo iliyokusanya maoni ya wananchi na kuandaa rasimu ya katiba mpya, pamoja na mambo mengine, ilipendekeza muundo wa serikali tatu yaani ya Tanganyika, Zanzibar na ya Muungano.
Hata hivyo, Bunge Maalum la Katiba (BMK) lililokuwa na wajumbe wengi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) lilitupilia mbali mapendekezo hayo na kupitisha katiba inayopendekezwa inayopendekeza muundo wa sasa wa serikali mbili ya Muungano na Zanzibar uendelee kwa maelezo kuwa ndiyo utakaowezesha Muungano udumu zaidi.
Maalim Seif alisema pamoja na wananchi kutaka Muungano wa serikali tatu kupitia Tume ya Katiba Mpya, lakini CCM) ilisaliti maoni hayo na kutengeneza ya kwao ambayo hayakutokana na maoni ya wananchi.
“Ninasema kwamba mimi na Lowassa tukiingia madarakani, tutawahakikishia Watanzania kwamba ni lazima tutarejesha rasimu ya Warioba, Bunge la Katiba litafanyika chini ya serikali yangu na Lowassa ili turejeshe maoni waliyotoa wananchi kwa kuunda Zanzibar inayojitegemea, Tanganyika inayojitegemea na serikali ya Jamhuri ya Muungano,” alisema.
Kadhalika, Maalim Self, alisema jambo la kwanza atakalolifanya ikiwa atachaguliwa kuiongoza Zanzibar, ni kulinda maslahi ya Wazanzibari.
Alisema akiingia madarani atahakikisha Zanzibar inapata mamlaka kamili na kuwa licha ya kwamba Zanzibar inaongozwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini cha inaongozwa na maamuzi kutoka CCM.
Pia aliahidi kuwa atalinda misingi ya utawala bora na kwamba hatakubali kuona utu wa Wazanzibari unadhalilishwa.
Jambo jingine alilosema atalifanya akiingia madarakani ni kujenga uchumi imara na unaokua kwa kasi na kuifanya Zanzibar kama Singapore ya Afrika Mashariki na kwamba hiyo ndiyo ndoto yake.
Kwa upande wake, Lowassa alilaani kitendo cha mahasimu wao kubandua mabango yao na kuyatupa porini.
Alisema kitendo hicho ni ukiukwaji wa haki za raia, na kuwataka waache mara moja.
Aidha, Lowassa alisema pamoja na kufanyiwa yote hayo, lakini aliwahakikishia Watanzania kuwa hakuna atakayewaibia kura Oktoba 25, mwaka huu kwa kuwa uwezo wa kuzilinda wanao.
MTANZANIA
Mgombea mwenza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, amewataka Watanzania kuthamini kura zao na kutokubali kuziuza kwa bei rahisi inayofanana na chumvi.
Samia, aliyasema hayo jana katika Kijiji cha Kingerikiti katika moja ya mikutano yake ya kampeni kwenye Jimbo la Nyasa mkoani Ruvuma.
Akihutubia wananchi wa jimbo hilo, Samia alisema wapo watu wanaopita kuwahadaa kwa kutumia fedha ili wawapigie kura katika uchaguzi mkuu ujao, huku wakiahidi ahadi zisizotekelezeka.
Aliwataka wananchi kuwa makini na watu hao na kuhakikisha ifikapo Oktoba 25, mwaka huu wanafanya uamuzi sahihi.
Akiwa Kijiji cha Tingi, Samia aliwataka wananchi wa Jimbo la Nyasa kutokata tamaa na maendeleo yanayofanywa na Serikali licha ya jimbo hilo kuwa jipya.
Alisema ujenzi wa barabara katika jimbo hilo umeanza na utakamilika baada ya mgombea urais wa chama hicho, Dk. John Pombe Magufuli kuingia Ikulu.
“Dk. Magufuli ameshika wizara nyingi, anajua barabara zote na urefu wake… alipokuwa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, alijua mpaka idadi ya samaki,” alisema.
Alisema ili wananchi wa Nyasa na Mbinga Vijijini waendelee, Serikali imejipanga kuweka ajira kwa vijana kwa kujenga viwanda vikubwa na vidogo vya kubangua na kusaga kahawa na mahindi.
Katika kuwawezesha wananchi kiuchumi, alisema Serikali itajitahidi kuongeza pembejeo za kilimo ili itakapoweka viwanda viweze kuzalisha kwa wingi.
Akizungumzia sekta ya afya, aliwahakikishia wananchi wa Tingi kuwa kituo chao cha afya kitapandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya cha wilaya.
MTANZANIA
Wakazi 89 wa Kijiji cha Rugunga, Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, wamelazwa katika hospitali ya wilaya hiyo, baada ya kunywa juisi ya kienyeji inayosadikiwa kuwa na sumu wakati wa sherehe ya harusi.
Tukio hilo limetokea Septemba 6, mwaka huu, baada ya watu hao kunywa juisi na kula chakula kilichoandaliwa katika sherehe hiyo.
Baada ya muda mfupi, waalikwa hao walianza kuumwa matumbo na kuharisha mfululizo hali iliyofanya kukimbizwa hospitali kwa ajili ya matibabu.
Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Kelvini Chayonga, alisema tukio hilo lilitokea siku hiyo mchana.
Alisema wagonjwa wote walipelekwa kwenye zahanati ya kijiji hicho, lakini hali ilivyozidi kuwa mbaya walihamishiwa Hospitali ya Wilaya ya Kibondo kwa matibabu zaidi.
MTANZANIA jana lilishuhudia mlundikano wa watu wazima na watoto katika wodi za hospitali hiyo, waliofika ili kupata matibabu na wengine wakiwasindikiza ndugu na jamaa zao.
Mmoja wa waathirika wa tukio hilo, Letisia Philemon, alisema baada ya kula na kunywa juisi hiyo, walianza kuhisi maumivu makali.
“Tulikunywa vizuri ile juisi na chakula cha mchana, lakini kadiri muda ulivyozidi kwenda, ndivyo maumivu yalivyokuwa yakizidi kunibana, hadi tukakimbizwa hospitali,” alisema.
Naye bwana harusi, Christian Lugonde alisema amesikitishwa mno na tukio hilo, kwani baada ya kuwa la furaha liligeuka kuwa huzuni.
Alisema juisi hiyo ilitengenezwa na mama yake wa kambo, ikiwa ni sehemu ya mchango wake kwenye harusi hiyo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kibondo, Dk. Kizito Luhamvya, alisema walianza kupokea waathirika saa tano usiku na kufikia jana asubuhi walikuwa wamefikia 89.
Alisema baada ya kuwapima wote, 68 wametibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani, lakini 21 wanaendelea na matibabu zaidi.
MTANZANIA
Mtuhumiwa wa mauaji katika Hoteli ya A Square Belmont jijini Arusha, Elijus Lyatuu , ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tano wa masomo ya falsafa katika Chuo cha Kanisa la Katoliki Segerea jijini Dar es Salaam, amepandishwa kizimbani na kusomewa shtaka la mauaji.
Mtuhumiwa huyo, alifikishwa mahakamani jana saa 4:30 asubuhi akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi ndani ya gari aina ya Toyota Land Cruiser yenye namba za usajili PT 1434.
Mwendesha mashtaka wa Serikali, Lilian Mmasi, alidai mbele ya Hakimu Nestory Baro wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, kwamba mtuhumiwa anadaiwa kutenda kosa la kumuua Alfred Kimbaa maarufu kwa jina la Mandela (18), Agosti 30, mwaka huu ndani ya Hoteli ya Belmont jijini hapa.
Alidai mtuhumiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 196 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Hata hivyo, aliomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutaja kesi hiyo kutokana na madai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.
Kwa upande wake, hakimu Baro alimweleza mtuhumiwa huyo kuwa kesi inayomkabili haina dhamana, hivyo atalazimika kuendelea kukaa mahabusu hadi shauri hilo litakapoanza kusikilizwa.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Septemba 23, mwaka huu itakapokwenda kwa ajili ya kutajwa tena.
MTANZANIA
Mgombea ubunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Jimbo la Bunda Mjini, Ester Bulaya, amesema amemwokoa mtoto wa Waziri wa Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, aliyetaka kuchomwa moto ndani ya nyumba na wananchi kwa madai ya kugawa rushwa.
Bulaya alisema mtoto huyo aliyejulikana kwa jina la Kambarage, alikumbana na mkasa huo juzi kwenye Kata ya Kunzugu eneo la Bukore.
Alisema Kambarage akiwa na baadhi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na viongozi wengine, wakiwamo watumishi wa Serikali, walifungiwa ndani ya nyumba na wananchi na kutaka kuwachoma moto baada ya kugundua kwamba walitaka kuwapa baadhi ya vijana rushwa ili wafanye fojo kwenye mkutano wake.
Bulaya alisema wananchi wa Bukore baada ya kuwafungia watu hao ndani ya nyumba, kabla ya kuchukua uamuzi wa kuwachoma moto, baadhi yao walimpigia simu ndipo alipochukua askari na kwenda eneo hilo.
“Nimewaita leo ili niwaeleze hali ambayo imetokea hapa jimboni, kuna watu ambao tukikaa kimya wanaweza kusababisha hali ya amani ikapotea hapa.
“Jana (juzi), mtoto wa Wasira na wenzake nimewaokoa wakitaka kuchomewa moto ndani na wananchi ambao walipata taarifa zao za kukutana ili wawape watu rushwa waje kufanya fujo kwenye mkutano wangu ninaopanga kuufanya Bukore.
“Mambo haya lazima yaangaliwe na vyombo vya usalama, wananchi hawataki kuona mambo ya ajabu,” alisema Bulaya mbele ya waandishi wa habari.
Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Tanzania (TAKUKURU), Wilaya ya Bunda, Alex Mpenda, alikiri kutokea kwa tukio hilo.
Alisema walipofika eneo walipofungiwa watu hao, walikuta tayari wameshaondolewa na askari polisi waliofika hapo mapema.
Kwa upande wake, Katibu wa Chadema Wilaya ya Bunda, Daniel Charles, alisema zipo taarifa za vijana zaidi ya 15 kutoka nchini Kenya, kuingizwa wilayani humo ili kuweza kufanya vurugu kwenye mikutano yao.
Alivitaka vyombo vya dola vifuatilie taarifa hizo na kuzifanyia kazi kwa sababu hadi sasa vijana wanne wanaokiunga mkono chama chao wameshavamiwa kwenye maeneo tofauti ya jimbo hilo na kukatwa mapanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Philip Kalangi, alikiri kuwapo kwa tukio hilo ambapo alisema walipigiwa simu na wananchi wakieleza kuwa kuna watu walikuwa wamefungiwa kwenye nyumba.
“Tulikwenda eneo la tukio na kuwachukua watu hao, na tulipowafikisha kituoni mtu mmoja ndiye aliyeripoti kushambuliwa na watu wasiojulikana ni wa chama gani.
HABARILEO
Siku moja baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kukemea kitendo kilichofanywa na mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa cha kuomba kura kwa kuwataka waumini wa madhehebu ya Kilutheri, kumchagua yeye kwa kuwa madhehebu hayo hayajawahi kutoa Rais, maaskofu kadhaa nchini wamepongeza karipio hilo.
Aidha, wamewataka viongozi wa dini nchini kutenganisha siasa na udini, lengo likiwa kuendelea kuwafanya Watanzania kuwa wamoja badala ya kuwagawa kwa misingi ya udini au ukabila.
Viongozi hao pia wameeleza kupinga hatua ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kujihusisha na masuala ya siasa, wakisema inakiuka misingi ya dini huku wakimkana Askofu huyo kuwa msemaji wa Maaskofu.
Viongozi hao walitoa maoni yao jana, walipozungumza na gazeti hili kufuatia uamuzi wa NEC unaotokana na Lowassa kudaiwa amewaomba waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) mjini Tabora, kumpigia kura kwa madai kuwa ni zamu kwa Walutheri kutoa Rais.
Rais wa Shirika la Kimataifa la Wapo Mission, Askofu Sylvester Gamanywa, aliitaka NEC kuendelea kuwakumbusha wadau juu ya Sheria ya Maadili ya Marais, Wabunge na Madiwani na pia kuhusu Sheria ya Uchaguzi, kwa kile alichosema uchaguzi wa mwaka huu ni tofauti na ule uliofanyika miaka 10 au mitano nyuma.
“Ni lazima tukubali kuwa uchaguzi wa mwaka huu ni tofauti na uchaguzi mwingine wowote uliopita, kuna mabadiliko mengi na hata maadili ya sasa si kama yale ya zamani, kwani kumekuwepo na utandawazi na upevukaji mkubwa wa masuala ya kidemokrasia,” alisema Askofu Gamanywa, aliyekataa kuzungumzia suala la Lowassa akisema atatoa tamko baada ya kufanya utafiti wa kina kuhusu kile kilichotokea.
Pamoja na ushauri wa kuitaka NEC kuvikumbusha vyama na wagombea wake juu ya kufuata maadili ya uchaguzi, pia alipinga hatua ya Askofu Gwajima kuwa Msemaji wa Maaskofu, kama alivyodai alipozungumza na vyombo vya habari juzi jijini Dar es Salaam.
Kuhusu Gwajima kudai kuwa atawasemea maaskofu, Askofu Gamanywa alisema si sahihi kwa vile kila taasisi ya dini inaye msemaji wake kwa masuala yake, akitoa mfano wa Baraza la Maaskofu (TEC) kwa masuala yanayolihusu Kanisa Katoliki, Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwa Makanisa mengine.
Mwenyekiti wa Mkesha Mkuu wa Kuliombea Taifa (Dua Maalumu), Askofu Godfrey Mallassy akizungumzia suala hilo alisema;” Siwezi sana kuzungumzia masuala ya siasa maana si kazi yangu.
Hata hivyo, Askofu huyo akizungumzia suala hilo alisema; “Mimi kama ninavyofahamika na watu wote kazi yangu ni kuliombea Taifa ili liwe katika amani na utulivu. “Suala la kuzungumzia siasa ni kupingana na kile ninachokifanya.
Siwezi kutoa maoni yoyote kuhusu siasa na wanasiasa, bali nitaendelea kuomba amani kwa taifa ili makundi yote wakiwemo wanasiasa waweze kutimiza majukumu yao, wafanyakazi wafanye kazi na mambo kama hayo.”
Pamoja na hilo, Askofu Mallassy aliwaasa waandishi wa habari nchini kuisaidia nchi kwa kuandika mambo yanayochochea umoja na mshikamano wa kitaifa, badala ya kuligawa taifa, jambo alilosema ni la hatari.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste nchini, Askofu David Batenzi, akizungumzia suala hilo pamoja na kuipongeza NEC, alisema kitendo cha Lowassa kuwaomba Walutheri kumchagua si sahihi, kwa vile kiutaratibu kama taifa, hakuna zamu za dini katika urais.
Askofu huyo ambaye pia alimkana Askofu Gwajima kuwa msemaji wao, alisema si sahihi kwa wanasiasa kutumia makanisa kama majukwaa ya kisiasa akisema kama hilo litaachwa likaendelea kutokea, litaligawa Taifa.
Alisema kwa kawaida makanisa yamekuwa yanatoa huduma za kiroho kwa watu, ambao wana itikadi tofauti za kisiasa na hivyo kuruhusu makanisa hayo kutumika kwa mambo ya kisiasa, kutaingiza nchi katika matatizo makubwa, na aliwataka wanasiasa kuacha kutumia makanisa kwa masuala ya kisiasa.
Askofu wa Kanisa la Kiadventista Wasabato Tanzania ambaye hakupenda jina lake kutajwa gazetini, akidai si msemaji wa Kanisa, alisema msimamo wa kanisa hilo ni kuwepo kwa utenganishi baina ya dini na siasa, na aliipongeza NEC kwa karipio lake.
“Sisi hatuamini katika makanisa kufanya kazi za kidini. Dini zifanye masuala ya kidini, na wanasiasa wafanye masuala ya kisiasa. Ukichanganya haya mambo kuna hatari ya kutokea kwa madhara makubwa sana.”
Kiongozi huyo alisema Kanisa hilo, litaendelea kuwapokea waumini wa vyama vyote vya siasa kwa lengo la kuabudu katika makanisa hayo, lakini kamwe haliwezi kuruhusu makanisa yake kutumiwa kama majukwaa ya kuwajenga au kuwabomoa wanasiasa.
Lowassa anadaiwa kutoa kauli hiyo Septemba 6, mwaka huu, katika Kanisa la KKKT la Tabora, ambapo akihudhuria ibada hiyo alinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari akidai kuwa kwa kuwa tangu nchi ipate Uhuru, hajawahi kutokea Rais kutoka madhehebu ya Kilutheri hivyo mwaka huu ni zamu ya Walutheri.
MWANANCHI
Baada ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kuibua mambo mazito ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa juzi, wanaharakati na wasomi wametoa maoni yao na kueleza kusikitishwa na hatua za kiongozi huyo wa dini kutoa siri za waumini wake.
Wanaharakati hao pia wameiomba Serikali ipige marufuku viongozi wa dini kujihusisha na siasa. Juzi, Gwajima alizungumza na wanahabari Dar es Salaam, alisema Dk Slaa amestaafu siasa kwa sababu ya shinikizo la mkewe, Josephine Mushumbusi.
Kiongozi huyo machachari wa dini katika mazungumzo yake na waandishi wa habari, alipinga kauli iliyotolewa na Dk Slaa, kwamba amejiuzulu siasa kwa sababu chama chake kimekiuka makubaliano kwa kumkaribisha Edward Lowassa.
Kadhalika, Gwajima alikwenda mbali na kudai Mushumbusi alimfukuza na kumrushia Dk Slaa nguo zake, akimtaka ajiuzulu Chadema hali iliyosababisha katibu mkuu huyo wa zamani kulala ndani ya gari.
Gwajima aliyasema hayo wakati Dk Slaa na familia yake wakiwa safarini kuelekea Marekani kwa mapumziko, huku akisema kurejea kwake kutategemea mazingira ya wakati husika.
Dk Slaa aliaga kupitia Televisheni ya Azam katika mahojiano maalumu. Wasomi na wanaharakati Aliyekuwa Mkuu wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Profesa Tolly Mbwete aliwataka Gwajima na Dk Slaa kuachana na masuala ya kupambana kwenye majukwaa, badala yake aliwataka waongelee masuala ya maendeleo.
“Hao wazee waachane na hayo mambo, ni mfano mbaya kwa vijana. Waongee masuala ya kimaendeleo, wanatutia aibu sisi wazee wenzao,” alisema.
Mkazi wa Magumuchila, Masasi mkoani Mtwara, Julius Mazinde alisema vita hiyo ya maneno kati ya watu wawili ambao ni viongozi wa kiroho, inatia shaka na inatishia amani ya nchi.
“Unajua Gwajima ana wafuasi na Dk Slaa ana wafuasi wengi, haya malumbano yao yakizidi, wanaweza kufika pabaya ikaleta machafuko, lakini sisi tunaombea hilo lisitokee,” alisema.
Mazinde alimsihi Gwajima kukaa kimya iwapo Dk Slaa atajibu lolote, pia, alimuomba Dk Slaa asijibu chochote ili kuepusha kuchochea malumbano zaidi. Serikal ipige marufuku Kuhusu viongozi wa dini kutoa siri za waumini wao, kwa mfano Gwajima alipotamka kuwa Mushumbusi ana mapepo, Mkufunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dk Eliamani Sedoyeka aliishauri Serikali kupiga marufuku viongozi wa dini kujiingiza katika siasa. Alisema imekuwa bahati mbaya kuwa viongozi wetu wanachanganya siasa na dini, hali ambayo aliitaja kuwa ni kufilisika.
“Kikubwa mimi sioni kama kutaja zile siri za Dk Slaa kuna mashiko, kwanza Serikali haiamini kuhusu mapepo, haina dini,” alisema.
Alizungumzia pia malumbano ya Dk Slaa na Chadema na kusema hatua zinazofikiwa na baadhi ya viongozi hao, zinawakatisha tamaa wananchi na kuleta taswira mbaya kwa wapiga kura wao.
Alimtaka Askofu Gwajima afute usemi wake kuhusu Dk Slaa na kumsihi Dk Slaa ajisafishe kuhusu tuhuma zake kwa maaskofu.
Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba alisema kutokana na nafasi ya Gwajima nchini, yaani uaskofu, hakutakiwa kutoa siri za Dk Slaa, bali alitakiwa kujikita kujibu hoja za kuitwa mshenga, kujibu kama amehongwa au hakuhongwa na kujibu tuhuma za maaskofu.
“Kimaadili si vizuri kutoa siri hizo, angeweza kujibu bila kutaja mambo mengine kama masuala ya mapepo, kutokana na nafasi yake si vizuri alivyofanya”alisema.
Alisema kuwa Gwajima alikwenda kinyume na maadili ya kazi yake ya utumishi wa Mungu kwani si jambo jema kueleza siri za muumini kuwa ana mapepo. Maswali kwa Gwajima 1. Kwa nini walinzi wa Gwajima wanamlinda Dk Slaa?
MWANANCHI
Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amemaliza kampeni zake mkoani hapa, akiahidi kuwakaba koo wawekezaji wakubwa wanaonufaika na misamaha ya kodi isiyokuwa na tija kwa nchi.
Dk Magufuli alisema anataka Serikali yake iwe rafiki kwa wafanyabiashara wote, lakini wawekezaji wakubwa ni lazima waondolewe misamaha ya kodi isiyokuwa na tija ili fedha zitakazopatikana zikasadie kuendeleza miradi mbalimbali ya Serikali.
Akiwahutubia wakazi wa Bumbuli wilayani Lushoto jana, Dk Magufuli alisema inasikitisha kuona badala ya wafanyabiashara wakubwa kubanwa kulipa ushuru, wafanyabiashara wadogo kama waendesha bodaboda na mama lishe wanaonewa.
“Nitakuwa upande wenu siku zote, sina maana Serikali yangu nitakayounda haitakusanya ushuru, lakini nitayabana makampuni makubwa ambayo hupewa tax holiday (msamaha wa kodi) kwa miaka mitano, ikiisha wanabadilisha jina na kupatiwa mingine mitano. Najua wananisikia huko waliko, ndugu zangu hao mimi nitalala nao mbele,” alisema huku akishangiliwa.
Akionekana kuongea kwa ukali, Dk Magufuli, ambaye amekuwa waziri tangu utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu, alisema: “Ni lazima walipe ushuru na kodi ili fedha zinakazopatikana zisaidie kuwasomesha watoto shule bure na kufidia ushuru kwa wafanyabiashara wa chini usio na kichwa wala miguu.” Katika mkutano huo uliofurika watu na wengine kukaa kwenye miteremko ya milima, mbunge huyo wa Chato anayemaliza muda wake, alisema Serikali yake itakuwa makini kwa ajili ya watu na kutatua kero za masikini.
Mgombea huyo aliyekuwa akimaliza mkoa wa nane kumwaga sera zake, aliwaahidi wakazi hao kutatua changamoto zilizopo katika kiwanda cha chai cha Mbonde ambacho hivi karibuni kilichukuliwa na Serikali baada ya kufungwa kutokana na mvutano baina ya mwekezaji na wakulima.
Hatua hiyo, alieleza kuwa ni moja ya mikakati yake ya kujenga viwanda vikubwa, vya kati na vidogo itakayochangia kukuza ajira kwa asilimia 40 na kuongeza bei ya zao la chai. “Tutawahamasisha watu wenye uwezo ndani ya nchi waanzishe viwanda vidogo vidogo ili vitoe ajira kwa vijana wetu,” alisema.
“Hii ndiyo maana tutaendeleza usambazaji umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) ili usaidie kujenga viwanda vidogo vijijini ambavyo vitapunguza umasikini,” alisema. Kama ilivyo ada, Dk Magufuli aliahidi kujenga kwa lami barabara ya Soni hadi Bumbuli yenye kilomita 22. 89.
Kwa upande wake mgombea ubunge kupitia CCM jimbo la Bumbuli, Januari Makamba alisema kiwanda cha Mbonde kilishachukuliwa na Serikali na fedha zilishatengwa, lakini urasimu umechangia kuchelewesha kuanza kazi. Januari aliwaonya Watanzania kutoharakia mabadiliko yasiyo na tija kwa kuwa kuna baadhi ya nchi kama Zambia ilifanya hivyo, lakini mpaka sasa haijaonja matunda ya mabadiliko bora.
Mkazi wa Sunta mjini hapa, Khatibu Shelutete alisema ahadi nyingi za Dk Magufuli zinatekelezeka kwa kuwa historia yake katika kila wizara inaonyesha hufanya vizuri na huwa hana mchezo.
“Kwetu hapa kero kubwa ni hospitali na barabara ya kutoka Soni hadi hapa Bumbuli. Hii barabara ambayo leo Magufuli ameahidi tena alishawahi kuahidi Rais Kikwete alipoomba kura mwaka 2010, lakini hadi leo bado haijajengwa,” alisema Shelutete.
Dk Magufuli amekuwa akitumia sehemu kubwa ya mikutano yake kuwasihi wananchi kutowachagua wanasiasa wenye tamaa ya madaraka ambao mipango yao ya haraka haraka inaweza kuchochea kuvuruga amani nchini. Alisema anapenda kuiongoza nchi yenye utulivu na amani ambayo wananchi wake hawagawanyishwi kwa dini, kabila au vyama.
“Naomba tuitunze amani yetu ndugu zangu. Hata Kenya wakati wa uchaguzi waliuana wao kwa wao, Rwanda kule watu wasiopungua milioni moja waliuawa, vivyo hivyo, kule Uganda na Burundi. “Niwaombe kura zenu Watanzania bila kujali dini zetu, makabila yetu, vyama yetu kwa sababu nataka kufanya kazi kwenye nchi yenye amani,” alisema.
Akiwa mjini Lushoto, Dk Magufuli aliahidi kuboresha masilahi ya wafanyakazi wote nchini kwa kuwapatia mishahara na kuwajengea nyumba ambazo miradi yake inaweza kufanywa na mifuko mikubwa ya hifadhi za Jamii kama NSSF na mingineyo.
Mwenyekiti wa CCM mkoani Tanga, Henry Shekifu alirusha vijembe kwa Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye kuwa ni “mpiga dili” kuliko mgombea wa urais kupitia mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa akimtuhumu kuwa alikula fedha za Shirika la Taifa la Hifadhi za Jamii (NSSF) na kumiliki maeneo makubwa ya ardhi mkoani Morogoro.
MWANANCHI
Uamuzi wa Papa Francis kulegeza masharti ya utaratibu wa kubatilisha ndoa kwa waumini wa kanisa hilo umepokewa kwa hisia tofauti.
Uamuzi wa kuondoa urasimu katika ubatilishwaji wa ndoa ulitangazwa juzi na makao makuu ya Papa.
Kesi zinazohusu maombi ya ubatilishaji ndoa sasa zitachukua muda mfupi zaidi na mchakato wake hautakuwa na urasimu kama ilivyokuwa awali.
Baadhi ya viongozi wa kanisa hilo na waumini waliozungumza na Mwananchi wameupongeza uamuzi huo kuwa unazingatia mazingira halisi ya kanisa hilo kwa sasa.
Askofu msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini ameueleza uamuzi huo kuwa utaharakisha utendaji wa kazi za kanisa kwa kupunguza muda wa kusikiliza mashauri hayo na kuyapatia ufumbuzi.
“Ni uamuzi mzuri unaoonyesha kwamba kiongozi huyo ana imani na maaskofu wake,” alisema Askofu Kilaini Kwa upande wake, Padri Evodius Nachenga wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam alieleza kuwa kwa uamuzi huo, matatizo baina ya wanandoa yatakuwa rahisi kupatiwa mwafaka.
Mlei mmoja, John Lipingu alisema kuwa ni hatua nzuri kwa kuwa kanisa hilo limeangalia sheria na kanuni ambazo zimetumika karibu miaka 2,000 ambazo zimekuwa haziendani na hali halisi.
Juzi, Papa Francis kupitia jopo la wataalamu wa sheria za kanisa na theolojia alipitisha sheria inayolegeza masharti ya kubatilishwa kwa ndoa, ambayo yamekuwa yakitumika tangu mwaka 1908.
Sheria hizo, ambazo zilipitishwa mwaka 1740 zimekuwa zikitaka masuala hayo kujadiliwa kwa ngazi ya jimbo, kupitia mahakama maalumu ya kanisa hilo, kisha mapendekezo kufikishwa makao makuu ya kanisa hilo, Vatican kwa uamuzi.
MWANANCHI
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Othman Chande, amesema baadhi ya Mahakama nchini bado zinakabiliwa na tatizo la rushwa kutokana na watendaji wake kuendekeza vitendo hivyo na kuwakosesha haki wananchi. Jaji Chande alitoa kauli hiyo wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama mjini hapa jana.
Jaji Chande aliyataja maeneo ambayo bado yanakabiliwa na vitendo hivyo mahakamani kuwa ni kwenye dhamana, hukumu na mwenendo wa mashauri.
Alisema rushwa imekuwa sugu mahakamani licha ya juhudi kubwa za Serikali kuboresha masilahi ya watumishi wa mahakama.
“Tatizo lingine ni suala la haki katika utumishi wa Mahakama. Watanzania wanahitaji kupata haki tena kwa wakati. Watumishi nataka mchape kazi kwa kuwa ndiyo wajibu wenu,” alisema Jaji Chande.
Alitaja changamoto nyingine zinazoikabili mahakama kuwa ni kushuka kwa nidhamu na uwajibikaji wa watendaji wake na kuonya tabia hiyo iachwe.
Jaji Chande alisema vitendo hivyo vinamkera na kulazimika kuipa kazi Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini (Repoa) ya kufanya uchunguzi wa malalamiko ya wananchi kwenye Mahakama za mikoa 13.
“Katika mikoa hiyo tulibaini bado kuna upungufu wa kimaadili uliosababisha tukawafukuza kazi watumishi 21 na wengine tisa tunaendelea kuwachunguza zaidi, haiwezekani watu wakafanya kaziwanavyotaka wenyewe,” alisema Jaji Chande.
PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos