HABARILEO
Mwanasiasa mkongwe nchini na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Chrisant Mzindakaya amewataka Watanzania wasikubali kupiga kura kwa ushabiki.
Ameonya kuwa upigaji kura kwa ushabiki, utaligharimu taifa hivyo Watanzania wapige kura wakijua wanachagua kiongozi ambaye atawakilisha nchi kitaifa na kimataifa.
Mzindakaya alisema hayo jijini Dar es Salaam jana katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Alisema ameamua kujitokeza kutoa ushauri kwa Watanzania, kama mwananchi wa kawaida na pia kama kiongozi ambaye anawafahamu kwa ukaribu wagombea wote wanaowania kiti cha Urais.
“Naomba Watanzania, wapiga kura wenzangu wasikubali kupiga kura kwa ushabiki, wapige kura wakijua wanachagua kiongozi wa Mungu, kiongozi ambaye atawakilisha nchi yetu kitaifa na kimataifa, na katika hili mimi sina maslahi yoyote,” Dk Mzindakaya.
Mzindakaya alisema yeye ni mstaafu baada ya kutumikia taifa kwa muda mrefu, hivyo hana maslahi yoyote binafsi katika kutoa ushauri huo kwa Watanzania, ambao ndio wapiga kura watakaomchagua kiongozi.
“Mimi ni mstaafu, sina maslahi yoyote katika hili, sihitaji kuteuliwa uwaziri au ukuu wa mkoa wala nafasi yoyote ile, lakini naipenda nchi yangu na ninayaona mafanikio ya nchi yangu ambayo yako waziwazi,” Mzindakaya.
Dk Mzindakaya alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kuwa na mipango madhubuti ya kuliletea taifa maendeleo na kufanya mabadiliko makubwa, ambayo yanaonekana na kuwanufaisha watu wengi. Lakini, alisema kuna baadhi ya watu hawapendi kuona na kusifu maendeleo ya nchi yao, badala yake wanaendelea kubeza kwamba hakuna kilichofanyika.
Alisema kuna watu wanaingiza ushabiki kwa kisingizio cha kutaka mabadiliko. Aliwashauri vijana wajue kuwa nchi hii ni mali yao, hivyo hata kama wanataka mabadiliko waangalie ni kiongozi gani wanataka kumkabidhi nchi awaletee mabadiliko.
“Vijana chungeni nchi hii ni mali yenu, ni nchi yenu msipige kura kwa ushabiki nawapeni ushauri na ushauri huu hauna gharama, ila usipozingatiwa mtakuja kuona gharama yake baadaye, sisi ni wazee tumetumikia taifa hili na sasa tumestaafu,” alisema.
Dk Mzindakaya alisema Ikulu ni mahali patukufu kwa sababu serikali za dunia zinatambuliwa na Mungu, hivyo Rais anamwakilisha Mungu duniani. Alisisitiza kuwa nchi inahitaji kuwa na Rais, ambaye sio tu atakuwa na uwezo mzuri wa kuongoza nchi, lakini pia awe na mikono safi.
Alisema amekuwa mbunge kwa miaka 44 na viongozi wote wanaotafuta urais, anawafahamu kwa sababu amefanya nao kazi, hivyo anajua vizuri utendaji kazi wao kwa undani zaidi. Mzindakaya alisema mamlaka ya Rais ni makubwa mno, ambayo yanahitaji mtu makini asiye na pupa na mcha Mungu, ambapo yeye alisema ukilinganisha na wagombea wengine, kwa maoni yake, anaona mgombea wa kupitia CCM, Dk John Magufuli anaweza kuwa kiongozi mzuri.
“Tusipige kura ya ushabiki baadaye tukaja kujuta, kura ya rais inatufanya tuchague kiongozi atakayewakilisha nje pia ya mipaka ya nchi, na kwa maoni yangu naona Magufuli anafaa sana,” alisema Mzindakaya.
Alisema katika kipindi cha miaka mitano hadi kumi ijayo, nchi hii itakuwa tajiri barani Afrika kutokana na misingi iliyowekwa na viongozi waliopita kuibua vitu, ambavyo vitapandisha uchumi wa nchi, kama vile uchimbaji wa gesi, kiwanda cha chuma cha Liganga na uzalishaji wa magadi soda.
HABARILEO
Wanafunzi zaidi ya 10,000 walioandikishwa darasa la kwanza mwaka 2009 mkoani hapa, hawatafanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo za utoro na kurudia madarasa.
Hayo yalibainishwa juzi na Ofisa Elimu mkoa wa Dodoma, Juma Kaponda katika mahojiano na gazeti hili juu ya maandalizi ya mtihani huo mkoani hapa, ambapo alisema yanaendelea vizuri huku nyaraka mbalimbali za mitihani zikiwa zinaendelea kupokelewa.
Alisema wanafunzi 36,273 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mkoani hapa Septemba 9 na 10, mwaka huu. Idadi hiyo ni kati ya wanafunzi 46,596 walioandikishwa mwaka 2009 kujiunga darasa la kwanza.
Kaponda alisema kati ya wanafunzi hao watakaofanya mtihani, 15,746 ni wavulana na wasichana 20,527 kutoka shule 733. Alifafanua kuwa wanafunzi 35,363 watafanya mtihani wa kawaida kwa lugha ya Kiswahili, 881 ni watahiniwa kwa mitihani ya lugha ya Kiingereza, 25 wasioona ambao watatumia nukta nundu na wanne wana uono hafifu.
Akifafanua kuhusu wanafunzi ambao wameshindwa kufanya mtihani kutokana na utoro, Kaponda alisema wanafunzi wengi wamekuwa wakiacha shule kati ya darasa la kwanza na la tano na chanzo kikiwa ni mwamko mdogo wa elimu.
Alisema wanafunzi hao wamekuwa wakitoka kwenye familia ambazo hazina mwamko wa elimu na hukimbilia kuchunga ng’ombe ama kuwa wafanyakazi wa ndani. “Wengi wamekuwa wakitoroka wakiwa kwenye madarasa ya chini na ndio maana idadi ni kubwa,” alisema.
Aliongeza kuwa kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi kushindwa kumaliza elimu hiyo ya msingi, licha ya kuitikia wito wa uandikishaji darasa la kwanza na shule za awali, wameanza kuchukua hatua dhidi ya wazazi ambao watachangia watoto wao kuacha shule kwa kuwafikisha mahakamani.
Kwa upande wa kurudia madarasa, Ofisa Elimu huyo alisema hiyo inatokana na wanafunzi kutokujua kusoma na kuandika, hivyo kibali maalumu kimekuwa kikiombwa na hiyo imesaidia kupunguza idadi ya wanafunzi wanaomaliza darasa la saba huku wakiwa hawajui kusoma na kuandika. Mwaka jana jumla ya wanafunzi 38,064 walifanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mkoani hapa.
HABARILEO
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli ameahidi kunyang’any’a mashamba ambayo yamehodhiwa na watu bila kutumiwa kwa ufugaji wala kilimo, na kuyagawa kwa wakulima na wafugaji wasio na maeneo ya kilimo. Alisema hayo alipozungumza na wananchi wa wilaya za Ulanga na Kilombero mkoani Morogoro jana.
Dk Magufuli alisema akiwa rais, kuna mambo mengi anaweza kufanya, kukabiliana na migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji na mojawapo ni kutoa ardhi zaidi kwaajili ya wakulima na wafugaji, ili kuondoa uhaba wa ardhi, unaosababisha ugomvi wa maeneo ya kulishia mifugo na kulima.
Alisema kuna watu wanamiliki maelfu ya eka za ardhi bila kulima na kwamba atanyang’any’a mashamba hayo ambayo yamehodhiwa na watu hao bila kutumiwa kwa ufugaji wala kilimo. Akihutubia maelfu ya wananchi, pia Dk Magufuli alisema kuwa anajivunia uzoefu wa marais wastaafu wa Awamu ya Pili mpaka Awamu ya Nne na wa Zanzibar, kwamba ndio atakaowafuata kwa ushauri akikwama popote.
Alisema hiyo ni moja ya tofauti kubwa kati yake na wagombea wengine wa urais. “Nitaingia Ikulu nikiwa na washauri wazuri, nikikwama mahali nitakwenda kwa Rais Jakaya Kikwete, nikikwama nitaenda kwa mzee Benjamin Mkapa, nikikwama tena nakwenda kwa mzee Ali Hasan Mwinyi.
“Wako wengi, upo ushauri nitauchukua kutoka kwa mzee Salmin Amour (Rais Mstaafu wa Zanzibar), Dk Ali Mohamed Shein na kwa Amani Abeid Karume,” alisema.
Kutokana na fursa hiyo ya kiuongozi aliyonayo ndani ya Chama Cha Mapinduzi, Dk Magufuli aliomba Watanzania wote bila kujali vyama vya siasa, makabila wala dini kumpa kura kwa wingi kwa kuwa atakuwa na washauri wazuri wenye uzoefu.
Alisema wagombea wengine, akiwemo wa Chadema anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Ukawa, Edward Lowassa, hawataweza kupata ushauri wa washauri hao kama ilivyo rahisi kwake.
Kutokana na uhakika huo wa washauri wazoefu, Dk Magufuli alisema ndio maana baadhi ya wagombea hao wanaweza kuja na ahadi za uongo, ikiwemo ya kuondoa nyumba za tembe na za nyasi.
Aliwataka wananchi kuwapima wagombea hao katika ahadi zao, kwa kuwa baadhi walikuwepo ndani ya Serikali kwa muda mrefu, lakini walishindwa kuondoa nyumba hizo katika majimbo walikotokea.
Dk Magufuli alisema yeye hataahidi kuondoa nyumba hizo, bali anaahidi kushusha bei ya vifaa vya ujenzi hasa saruji, mabati na misumari, ili wananchi wanaofanya kazi wajenge nyumba bora.
Katika kuongeza idadi ya Watanzania wanaofanya kazi ili kufikia lengo hilo, Dk Magufuli alisema katika kila mtaa na kijiji, serikali yake itatoa Sh milioni 50 kwa ajili ya kuanzisha na kukuza biashara ndogo za wanawake na vijana.
Alisema atataka kila anayefanya kazi apate kipato kizuri kitakachomsaidia kukabiliana na mahitaji ya maisha yake, ikiwemo kujenga nyumba bora kutokana na kushushwa kwa bei za bidhaa za ujenzi. Kwa wakulima, alisema atahakikisha pembejeo sahihi zinatolewa kwa wakati na mazao yatakayovunwa, itakuwa marufuku kwa Serikali kukopa mazao yao.
MWANANCHI
Katibu mkuu wa zamani wa Chadema, Dk Willibrod Slaa juzi alijitokeza tena hadharani kujibu mapigo ya hoja mbalimbali zilizojitokeza wakati akitangaza kustaafu siasa za vyama, akiweka bayana kwamba hivi sasa analindwa na usalama na amehama nyumbani kwake.
Dk Slaa alitangaza kujiondoa kwenye siasa za vyama Septemba mosi, akieleza kuwa alitofautiana na viongozi wenzake wa Chadema kuhusu namna ya kumpokea Edward Lowassa kutoka CCM ili awe mwanachama na mgombea urais, na akatumia fursa hiyo kumrushia ‘makombora’ mgombea huyo wa urais kwa tiketi ya Ukawa.
Hotuba yake ilizua maswali mengi, ikiwa ni pamoja na gharama alizotumia kurusha moja kwa moja mkutano na wake na waandishi wa habari kwenye Hoteli ya Serena, huku mkewe wa zamani akijitokeza kukanusha kuishi maisha ya shida, huku Ukawa ikisema alikuwa akiutaka urais, tofauti na maelezo yake.
Akihojiwa kwenye kipindi maalumu kilichorushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Star Tv juzi usiku, Dk Slaa alisema sambamba na kuhamia Hoteli ya Serena, ambayo ni ya kiwango cha nyota tano, hata nyumba yake inalindwa na usalama wa taifa.
“Nakaa Serena kwa sababu ninapata vitisho, nilishasema kuwa kipindi hiki nimepata vitisho vingi kuliko nilivyopata wakati nilipotaja orodha ya mafisadi. Watanzania hawajui jinsi mimi na familia yangu tunavyoishi,” alisema.
Katika mazungumzo yake na Star Tv yaliyodumu kwa dakika 85, Dk Slaa alisema amekuwa akipata vitisho vingi, vinavyoiweka familia yake hatarini huku akieleza jinsi mke wake, Josephine Mushumbusi alivyokoswakoswa na risasi akiwa kwenye gari.
“Si ajabu mimi kulindwa na Usalama wa Taifa. Ingawa nilishawahi kuwasema hawa watu wa usalama, sasa wananilinda na ni utaratibu kuwa ukiomba ulinzi kwa utaratibu unaotakiwa, unapewa,” alisema.
Alifafanua zaidi kuwa ameshtushwa na uzushi ulionezwa kuwa amekimbilia Marekani, akisema hajawahi kufanya hivyo, bali aliwahi kwenda nchini humo mwaka jana katika kazi zake za siasa.
“Niliwahi kwenda Marekani mwaka jana katika kazi zangu za siasa na nikatembelea majimbo 13. Gharama hizo nilijilipia mwenyewe, nilikwenda kujifunza mambo fulani fulani ya uongozi,” alisema.
MWANANCHI
Pamoja na Serikali kuzuia kutumia Uwanja wa Taifa kwa shughuli za kisiasa, eneo hilo jana liligeuka uwanja wa kampeni, baada ya mbunge wa Bumbuli (CCM) January Makamba kuruhusu mashabiki walioko nje waingie uwanjani bure.
Tukio hilo lilitokea wakati timu ya Taifa ya soka, Taifa Stars ikimenyana na Nigeria kwenye uwanja huo kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
Wakati wa mapumziko, timu ziliporudi vyumbani kwa mapumziko, sauti kutoka kwenye vipaza sauti ilisema: “Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM amewaruhusu mashabiki wote walioko nje waingie uwanjani bure.
Lakini badala ya mashabiki kupokea tangazo hilo kwa shangwe, karibu uwanja mzima ulisimama na kuanza kupiga kelele ukisema “people’s power, people’s power, people’s power” na kunyoosha vidole viwili, ambayo ni alama ya Chadema.
Baadaye mashabiki hao waliviringisha mikono hewani kuiga ishara inayotumiwa na Chadema na vyama vinavyounda Ukawa kumaanisha mabadiliko.
Mashabiki hao walianza kulitaja jina la mgombea urais kwa tiketi ya Chadema na Ukawa, Edward Lowassa na kuendelea kufanya hivyo hadi timu zilipokuwa zikirejea uwanjani ndipo wakakaa chini kutazama mchezo.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Makamba alisema Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) ndilo linaweza kuzungumzia. “Sijui chochote labda waulizwe TFF,” alisema. Msemaji wa TFF, Baraka Kizuguto pia hakutaka kuzungumzia tukio hilo. “Leo ni nafasi ya kocha kuzungumzia mpira wa leo na matokeo,” alisema.
Mashabiki waliohojiwa na Mwananchi walisema watu wamechoshwa na CCM. “Watu wamekata tamaa na wanataka mabadiliko,” alisema Juma Hamisi, shabiki aliyejitambulisha kuwa anatokea Ukonga baada ya kuulizwa na Mwananchi kuhusu kitendo cha mashabiki kuonyesha waziwazi msimamo wa kisiasa uwanjani hapo.
“Watu wamechoka kwa kuwa kila mwaka hali ni ile ile. Haijalishi Lowassa ni fisadi au si fisadi watamchagua. “MC alisema watu waingie kwa hisani ya CCM. Hizo ni kampeni za moja kwa moja. Ingekuwa si kipindi cha kampeni wangeruhusu watu waingie bure?” Maoni kama hayo yalitolewa na shabiki aliyejitambulisha kwa jina la Anthony Fred wa Tegeta, ambaye alisema watu wameichoka CCM na ndio maana hawataki kusikia lolote kutoka kwao.
“Kama Makamba alitaka watu waingie bure, angesema tangu jana kabla ya tiketi kuanza kuuzwa. Hizo ni njama za kuwageuza watu akili ili waone CCM inawajali,” alisema huku akisisitiza kuwa huu ni mwaka wa mabadiliko.
Shabiki mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mohamed Hassan alikwenda mbali zaidi na kutabiri kifo cha chama hicho kikongwe.
“Hali iliyojitokeza uwanjani hapa inaweza kuwa anguko la CCM, hivyo wanatakiwa kujipanga kwa kuwa wana kazi ngumu kwenye uchaguzi wa mwaka huu,” alisema.
Athuman Sadiq, shabiki mwingine aliyekuwapo uwanjani, alisema watu wamezomea kwa sababu walikasirishwa kwa kuwa CCM wameonekana walitaka kutumia mchezo huo kwa ajili ya kampeni. Shabiki mwingine, Peter Kisavo wa Mbagala, alisema:
“Mimi ni CCM damu, lakini kitendo hiki kimeniudhi, wanataka kutuharibia kuchanganya siasa katika michezo.” Chadema, ambayo inashirikiana na NCCRMageuzi, NLD na CUF kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu, iliomba kutumia uwanja huo wa kisasa wenye uwezo wa kuchukua watu 60,000 kwa ajili ya kufanyia uzinduzi wa kampeni zake, lakini Serikali ikaikatalia
MWANANCHI
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, amesema ndani ya CCM wapo watu wa hovyo, wezi na wanafiki, lakini kama watamchagua Dk John Magufuli kuwa rais, ataisafisha CCM na Serikali yake.
“CCM tumejitahidi kuleta maendeleo, lakini lazima nikiri ndani ya CCM kuna kasoro. Tuna mijitu hovyo, tuna wezi, tuna majambazi humo na kuna watu wanafiki ndani ya CCM,” alisema Kinana.
Kinana alitoa kauli hiyo jana mjini Moshi katika mkutano mkubwa wa hadhara wa kuzindua kampeni za ubunge katika Jimbo hilo, ambapo Davis Mosha anapeperusha bendera ya CCM. “Magufuli atakisafisha chama akiwa mwenyekiti… si mjumbe, lakini anakijua chama…. CCM kuna majungu na ulaji, lakini Magufuli atayamaliza, hajatumia fedha kupata urais, hajaenda wilayani ama mikoani bali alienda matawini.
“Hana makundi… wapo waliochangisha fedha wamekusanya watu baadaye wanakuja kuwa mzigo. Yeye hana makundi wala hana mzigo,” alisema Kinana.
Alisema kuna watu wamefanya uozo ndani ya Serikali na ndani ya CCM na kuamua kukimbia na huko waliko wanasema wataleta mabadiliko wakati wameshindwa kufanya lolote wakiwa madarakani. Kinana alitoa mfano wa Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye ambaye amekuwa Waziri Mkuu miaka kumi, ameshindwa kufanya kitu na kwamba sasa anakuja kuahidi maajabu.
Hata hivyo katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wanachama wa CCM na wananchi, Kinana aliwaomba wamchague Dk Magufuli kwani ndiye anayeweza kubadili mfumo huo.
“Suala hapa ni mfumo. Mkipata mtu mmoja tu mzalendo kama Dk Magufuli atabadili kabisa mfumo huu. Nataka niwahakikishie kuwa Magufuli akiingia madarakani atasafisha CCM na Serikali,”alisema.
Kinana aliwataka Watanzania kutohadaika na ahadi za mabadiliko zinazotolewa na wale aliowaita “makapi” kutoka CCM ambao walishiriki kuharibu mfumo mzuri wa CCM na sasa wamekimbia.
“Halafu watu walioharibu CCM, hawa makapi hawa wanakuja Chadema, wanawapa matumaini na wengine walikuwa mawaziri kwa miaka 40 kwanini hawakufanya hayo wanayoyasema?” Alihoji Kinana.
Kinana alisema endapo wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro na nchi kwa ujumla, watampa kura Magufuli, ataunda baraza dogo la mawaziri lenye tija na litakalowajibika kwa wananchi. Katibu mkuu huyo aliwatahadharisha Watanzania kufanya mabadiliko kwa chuki na hasira akiwataka warejee mifano ya nchi za Libya, Misri na Zambia ambapo mabadiliko hayajawasaidia sana.
Alitumia mkutano huo kumshambulia Waziri Mkuu mstaafu, Sumaye, akisema katika miaka 10 aliyokuwa madarakani kama Waziri Mkuu, hakuna kitu Watanzania wanachomkumbuka nacho.
“Sumaye amekuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 niambieni kitu kimoja tu mnachomkumbuka nacho. Sokoine (Edward) mbona anakumbukwa kwa uchapakazi na ukali katika kuendesha Serikali?” Alihoji.
Kinana alisema endapo Sumaye atapanda jukwaani mjini Moshi, wananchi wamuulize maswali 100 kwamba chini ya utawala wake amefanya nini hadi leo amuombee mtu kuwa rais.
Kwa upande wao, mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka na Livingstone Lusinde wa Mtera, waliwataka wananchi wa Jimbo la Moshi kutochagua viongozi kwa ushabiki wa kisiasa.
Akizungumza katika mkutano huo Sendeka alisema ni lazima Watanzania wawapime wagombea kwa kujua ukweli si kwa kudanganyana na amewaasa kuepuka dhambi ya ubaguzi wa aina yoyote ile.
NIPASHE
Harakati za mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa za kuchanja mbuga mikoani kusaka kura kwa wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu, jana zimefungua ukurasa mpya baada ya kuvunja rekodi ya mahudhurio katika mikutano yake kwa kuiteka ngome ya CCM Tabora.
Lowassa ambaye baada ya uzinduzi wa kampeni jijini Dar es Salaam Agosti 29, mwaka huu alianza kufanya mikutano ya kampeni katika mikoa ya Iringa, Njombe, Rukwa, Katavi na baadaye Kigoma, jana aliendelea kuwaomba ridhaa wananchi Mkoa wa Tabora kumpigia kura Oktoba 25.
Katika mkutano huo wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Town Primary School, ulikuwa wa kihistoria hasa kutokana na maelfu ya wananchi kuhudhuria ukilinganisha na mikutano mingine iliyofanywa katika mikoa ya Iringa, Njombe, Rukwa, Katavi na Kigoma
Baadhi ya wafanyabiashara walilazimika kufunga maduka yao kwa zaidi ya saa sita kumsubiri Lowassa awasili huku waendesha bodaboda na mama lishe nao wakiungana kusitisha kazi zao kumsubiria waziri mkuu huyo wa zamani.
Baadhi ya wananchi walisikika wakisema mahudhurio ya wananchi wa Mji wa Tabora katika mkutano huo yametia fora na kuvunja ngome ya CCM ambayo kwa miaka mingi Jimbo la Tabora Mjini limekuwa likiongozwa na wabunge kutoka CCM.
Akihutubia katika mkutano huo wa kampeni, Lowassa alisema amepata malalamiko kutoka kwa wakulima wa Tumbaku wa Mkoa wa Tabora kuwa hawajalipwa pesa zao walizokopwa na baadhi ya wafanyabiashara na kuahidi kuwa kama wananchi watampa ridhaa ya kuingia madarakani watu hao watalazimika kulipa deni hilo mara mbili.
Alisema amelazimika kugombea urais kwa kuwa amejipima na kuona anatosha katika nafasi hiyo na wananchi wanamatumaini makubwa naye kwa ajili ya kuwaletea maendeleo.
Lowassa ambaye alitumia takriban dakika tano kuzungumza na wananchi, aliwaomba kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili kura ziwe nyingi ambazo hata wapinzani wake ambao ni CCM wakiiba washindwe.
“Natafuta urais ili nibadilishe nchi. Nataka nibadili mfumo wa elimu. Sitaki michango ya penseli wala chaki,” alisema huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi.
Aliongeza kuwa suala la ajira kwa vijana litakuwa agenda muhimu kwake endapo akichaguliwa na kwamba cha msingi ni kuunganisha nguvu kuchagua Ukawa ili mabadiliko yaweze kupatikana haraka.
PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos