MWANANCHI
Aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa, anatarajia kufanya mkutano wa hadhara kesho jijini Tanga, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kuwashukuru Watanzania waliompigia kura wakati wa uchaguzi mkuu.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene, ilisema katika ziara hiyo Lowassa ataambatana na viongozi wengine waandamizi wa Ukawa, ikiwa ni mwanzo wa ziara ya nchi nzima.
“Watawashukuru kwa namna walivyounga mkono upinzani na ajenda ya mabadiliko katika uchaguzi mkuu uliopita na wanavyoendelea kuweka matumaini yao kwa upinzani kuwa ndiyo nguzo imara wanayoweza kuitegemea kuwaletea mabadiliko ya kweli kwa ajili ya maendeleo yao na ustawi wa taifa kwa ujumla.
“Itakumbukwa mbali ya Watanzania kupiga kura za ushindi katika nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu uliopita, wananchi waliwachagua wabunge wengi wa upinzani wanaotokana na Ukawa na kuongeza nguvu kubwa ndani ya Bunge, hususan kupitia Kambi ya Upinzani Bungeni,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema kuwa kambi rasmi ya upinzani bungeni itakuwa Serikali mbadala ya wananchi.
“Wameviamini vyama vyetu hivyo kusimamia na kuongoza halmashauri zipatazo 34 nchi nzima, ikiwa moja ya misingi imara katika kupigania mabadiliko ambayo Watanzania wanayataka,” inasema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa wananchi wanastahili shukrani kwa imani hiyo ambayo ni ishara ya kuwa matumaini yao kwa miaka mingine mitano yatasimamiwa na kuongozwa na upinzani imara kupitia Ukawa.
MTANZANIA
Wakati vita dhidi ya wakwepa kodi katika Bandari ya Dar es Salaam ikipamba moto, umeibuka utata wa Sh bilioni 80 ambazo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema ni kodi ya makontena 329 kutoka kwa wafanyabiashara 58, walioyatoa bandarini bila kuyalipia kodi.
Akitoa ufafanuzi wa ukusanyaji wa fedha hizo, Desemba 12, Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dk. Philip Mpango, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa wamekusanya Sh bilioni 10.6 kutoka kwa wafanyabiashara 28 na kwamba wamebaki 15 wanaodaiwa Sh bilioni 3.7.
Kutokana na takwimu hizo, wafanyabiashara hao 15 nao wakilipa kodi, zitapatikana jumla ya Sh bilioni 14.3 kwa makontena yote 329, jambo linalofanya kuwe na upungufu wa Sh bilioni 65.7, tofauti na kiasi cha Sh bilioni 80 alichosema Waziri Mkuu Majaliwa.
Juzi Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alipotafutwa na gazeti hili kufafanua utata huo, alisema: “Sikiliza, usituingize kwenye ‘issue’ na waziri mkuu, ninachoweza kusema ni kwamba tumekusanya Sh bilioni 10.6 na zilizo nje bado ni Sh bilioni 3.7.”
Alipotafutwa Msemaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Irine Bwire siku hiyohiyo, alisema waziri mkuu ameshatoka ofisini, lakini takwimu za Sh bilioni 80 hakuzitoa kichwani bali kwenye ripoti iliyotoka TRA.
“Mimi nitamuuliza vizuri kesho asubuhi (jana),” alisema Bwire.
Jana alipotafutwa tena, alisema hajafanikiwa kuzungumza na waziri mkuu kwa kuwa alikuwa na vikao vingi.
“Labda baadaye kama atarudi ofisini kwa sababu sasa hivi amekwenda Ikulu kwenye kikao kingine,” alisema Bwire.
Rais Dk. John Magufuli, alipokutana na wafanyabiashara, alitoa siku saba kwa waliokwepa kulipa kodi kufanya hivyo na watakaokaidi watachukuliwa hatua.
Kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, Desemba 12, Dk. Mpango alisema ni kampuni 28 tu ndizo zilizotii agizo hilo la rais na kufanikisha ukusanyaji wa Sh bilioni 10.6.
Dk. Mpango alisema kuwa muda wa kulipa kodi kwa hiari uliisha Desemba 11, hivyo wafanyabiashara 15 ambao wameshindwa kulipa kodi katika kipindi hicho “wasubiri cha moto” kwa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
“Hata hizo siku saba walizokuwa wamepatiwa tayari walikuwa wameshavunja sheria, hivyo wale waliolipa kwa wakati wamesamehewa kupelekwa mahakamani, lakini ambao hawajalipa watashtakiwa na kupigwa faini,” alisema Dk. Mpango bila kubainisha kiwango cha adhabu.
Alisema baadhi ya wafanyabiashara hao walienda “kulalamika”, lakini TRA haitawasamehe kwa kuwa kodi hizo zinahitajika kufanikisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Dk. Mpango alibainisha kuwa kati ya fedha zilizokusanywa katika kipindi hicho, Sh bilioni 4.16 zimetoka katika kampuni 13 ambazo zimelipa kodi yote iliyokuwa imekadiriwa, huku Sh bilioni 2.2 zikitoka katika kampuni 15 zilizotoa sehemu ya kodi wanayodaiwa.
Alisema bandari kavu (ICD) ya Azam ililipa kiasi cha Sh bilioni 4.17 kama dhamana kati ya Sh bilioni 12.6 ya kodi iliyokuwa imekwepa kulipa katika sakata hilo la upotevu wa makontena 329.
MTANZANIA
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imeridhia kutoa dhamana kwa watuhumiwa watatu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuwataka kila mmoja kutoa fedha taslimu Sh bilioni 2.6.
Akisoma uamuzi huo jana, Jaji Winfrida Koroso, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Tiagi Masamaki (56) ambaye ni Kamishna wa Forodha wa mamlaka hiyo, Burton Mponezya na Habibu Mponezya ambaye ni Meneja wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja.
Alisema kabla ya kutoa dhamana hiyo, mahakama hiyo imepitia maelezo ya pande zote mbili ambazo ni upande wa washtakiwa na wa Serikali ili kuangalia kama watuhumiwa hao wana vigezo vya kupewa dhamana.
Jaji Koroso alisema baada ya kupitia maelezo hayo, mahakama iliridhia kuwapatia dhamana hiyo, huku ikiwataka kutimiza masharti sita ili waweze kukidhi vigezo.
Aliyataja masharti hayo kuwa ni kila mwombaji kulipa fedha taslimu Sh bilioni 2.6 au mali yenye thamani ya fedha hizo na kudhaminiwa na wadhamini wawili ambao ni wafanyakazi wa Serikali wenye bondi ya Sh 20 kila mmoja.
Alisema, kila mwombaji hatakiwi kusafiri bila ya kibali cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambako kesi hiyo inaendeshwa, kuwasilisha vibali vya usafiri ikiwamo paspoti katika mahakama hiyo na kuripoti mahakamani hapo kila baada ya wiki mbili siku ya Jumatatu.
Alisema masharti mengine ni kila mwombaji ahakikishe taarifa zote alizowasilisha mahakamani hapo ziwe zimesainiwa kisheria na kukamilisha taratibu za dhamana ndani ya saa 24 ili waweze kukidhi vigezo vya dhamana hiyo.
Awali, Masamaki na wenzake walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakituhumiwa kufanya makosa mawili ya uhujumu uchumi ambapo shtaka la kwanza ni kutoa makontena 329 katika Bandari ya Dar es Salaam bila ya kulipiwa kodi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 12.7.
Katika shtaka la kwanza, ilidaiwa mahakamani hapo kuwa tarehe tofauti kati ya Juni mosi na Novemba 17 mwaka huu, sehemu isiyojulikana ndani ya Jiji la Dar es Salaam, watuhumiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kuidanganya Serikali kuwa Sh bilioni 12.7 zimetolewa kwa kutoa makontena 329 katika bandari kavu ya Azam baada ya kodi zote kutolewa.
Shtaka la pili, inadaiwa kuwa Juni mosi na Novemba 17, mwaka huu ndani ya Jiji la Dar es Salaam, walishindwa kutimiza majukumu yao kwa namna inavyotakiwa na kusababisha Serikali kupata hasara ya Sh bilioni 12.7.
HABARILEO
Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Saed Kubenea amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashitaka ya kutumia lugha ya matusi dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.
Kubenea ambaye ni Mbunge kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Thomas Simba.
Vitalis alidai juzi katika Kiwanda cha TOOKU Garments kilichoko maeneo ya Mabibo External, Kinondoni, Kubenea alitumia lugha ya matusi kwa Makonda, jambo ambalo lingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, Kubenea alimwambia Makonda; “wewe kibaka, mpumbavu, mjinga na cheo chenyewe cha kupewa tu.” Kubenea ambaye anatetewa na Wakili Peter Kibatala akisaidiana na Dk Rugemeleza Nshala, Nyaronyo Kicheere, Geremia Mtobesia, Omary Msemo na Fredrick Kiwelu, alikana mashitaka hayo.
Wakili Vitalis alidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba kupangiwa tarehe ya usikilizwaji wa awali. Wakili Kibatala aliomba mshtakiwa apewe dhamana kwa kuwa mashitaka yanayomkabili yana dhamana kisheria. Upande wa Jamhuri haukuwa na pingamizi juu ya ombi hilo.
Hakimu Simba alisema mshtakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili wa kuaminika ambao kila mmoja atasaini hati ya dhamana ya Sh 500,000. Kubenea alitimiza masharti ya dhamana, hivyo kuachiwa kuwa nje kwa dhamana na kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 29, mwaka huu kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.
HABARILEO
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu amesema diwani anayefikiri ameingia madarakani kwa lengo la kupata utajiri ni vyema ajiondoe mapema, kwa kuwa serikali haitavumilia mtu atakayebainika kujihusisha na rushwa, watachukuliwa hatua.
Alisema wapo wanaofikiri udiwani ndiyo njia ya kujinufaisha kwa kuendekeza vitendo vya rushwa, ufisadi na kuhujumu miradi ya wananchi. Mwambungu alitoa rai hiyo jana mjini hapa alipokuwa akizindua Baraza la kwanza la Madiwani wa Halmashauri ya mji wa Mbinga.
Akiwasilisha salamu za serikali katika baraza hilo, aliwataka watendaji wa serikali kushirikiana pamoja na madiwani hao kufikia malengo ya kimaendeleo, yaliyokusudiwa kwa manufaa ya jamii.
“Ndugu zangu kiongozi ambaye ni mpenda rushwa au fisadi aliyekubuhu, tukikubaini tutakuchukulia hatua na mwisho wa siku tutakuondoa, tafuteni maisha kwa njia zilizo halali acheni kujihusisha na matendo maovu”, alisisitiza Mwambungu na kuongeza:
“Hapa namaanisha kwamba kila ngazi itekeleze wajibu wake, mapato yatumike kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa, hatutamsamehe wala kujenga huruma kwa mtu ambaye ni mwizi, na mwenye lengo la kutaka kuturudisha nyuma kimaendeleo.”
Alisema lengo la serikali ni kutaka kwenda na kasi ambayo inaendana na weledi, uaminifu na uadilifu wa hali ya juu katika utendaji kazi.
Awali kabla ya Mkuu huyo wa Mkoa kutoa salamu hizo kwa baraza hilo la Madiwani wa Halmashauri ya mji wa Mbinga, ulifanyika uchaguzi wa kumpata Mwenyekiti, Makamu wake na kamati mbalimbali za halmashauri hiyo. Mwenyekiti aliyechaguliwa ni Diwani wa Kata ya Myangayanga, Ndunguru Kipwele kutoka CCM aliyepata kura 24.
Alikuwa akishindana na Diwani wa Kata ya Mbiga Mjini B, Frank Mgeni wa Chadema aliyepata kura mbili. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti ilichukuliwa na Diwani wa Kata ya Kikolo, Tasilo Ndunguru aliyepata kura 23 na kumshinda Aidan Nombo wa Kata ya Utiri, aliyepata kura tatu.
HABARILEO
Polisi mkoani Singida inamshikilia Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Itaja na mkewe kwa tuhuma za kumfungia ndani ya chumba mtoto wao mlemavu wa viungo kwa miaka 12 bila kutoka nje.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni David Mtipa (59) ambaye ni Mchungaji wa Kanisa hilo na mkewe Mariam Philipo (45) wote wakazi wa kijiji cha Itaja katika tarafa ya Mgori wilayani Singida.
Kamanda Sedoyeka alisema tukio hilo liligundulika juzi katika kijiji hicho baada ya Polisi kupata taarifa za siri kutoka kwa wasamaria. Akielezea tukio hilo, Kamanda Sedoyeka alisema watuhumiwa walimfungia ndani ya chumba mtoto huyo, Timotheo David (30) kwa muda wa miaka 12 huku huduma zote za kibinadamu, ikiwemo haja ndogo na kubwa pamoja na chakula zikifanyika humo ndani.
“Baada ya timu ya askari wa Upelelezi na Ofisa Ustawi wa Jamii kufika eneo hilo wakiwa na viongozi wa kijiji na kufanya mahojiano, watuhumiwa walikiri kumfungia chumbani mtoto wao huyo na kwamba ni mlemavu wa miguu na mikono, lakini pia ni mlemavu wa akili,” alisema Kamanda Sedoyeka na kuongeza:
“Wamesema mtoto wao alizaliwa mwaka 1984 akiwa mzima, lakini alipofika darasa la sita 2003 alianza kuugua ugonjwa usiojulikana ikiwa ni pamoja na kuanguka kisha kutoa povu mdomoni huku mwili wake ukibadilika rangi kuwa ya njano na kutibiwa bila mafanikio.”
Aidha, alisema mlemavu huyo alitibiwa maeneo mbalimbali bila mafanikio na ndipo wazazi hao walipoamua kumfungia ndani baada ya kuona wanafedheheshwa mbele ya jamii huku akila chakula, kujisaidia humo chumbani na kutoruhusiwa kutoka nje.
Kutokana na hali hiyo, majirani waliingiwa na hofu kwa kutomwona mtoto huyo kwa kipindi kirefu kiasi hicho hali iliyozua maswali mengi. Wakati baadhi walijua huenda ameuawa, wengine walihusisha kitendo hicho na imani za kishirikina huku Mchungaji akidaiwa kuzidiwa maarifa na mkewe.
Alisema kitendo cha kumfungia mtoto huyo ndani kwa kipindi chote hicho, kumwacha akiwa uchi na kumlaza kwenye kitanda cha kamba kisichokuwa na godoro ilikuwa ni ukiukwaji wa misingi ya binadamu na si cha kiutu.
Alisema amepelekwa Hospitali ya Mkoa wa Singida kwa matibabu na uchunguzi zaidi wa afya yake wakati wazazi hao wakishikiliwa na kuhojiwa ili hatimaye wafikishwa mahakamani kwa ukatili uliovuka mipaka.
HABARILEO
Wafugaji waliovamia maeneo ya wakulima katika kijiji cha Dihinda wilayani Mvomero mkoani Mogorogo na kusababisha mapigano yaliyoua mkulima na ng’ombe 71, wamekimbia kijijini hapo na kutokomea kusikojulikana.
Akizungumzia hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Wilaya ya Mvomero, Mkuu wa Wilaya hiyo, Betty Mkwasa alisema ulinzi bado umeimarishwa eneo hilo, na kwamba wafugaji waliovamia wamekimbia.
“Wafugaji wamekimbia na sisi tutateketeza maboma yao, kwa sababu walivamia eneo hili la wakulima na ng’ombe walioachwa wamepigwa mnada na fedha imeingizwa kwenye mfuko wa serikali ya kijiji hicho,” alisema Mkwasa.
Aidha, katika msako uliofanywa kwa ushirikiano wa Serikali ya Wilaya na Polisi silaha moja ya askari iliyochukuliwa ilipatikana na kwamba wakulima wametolewa hofu na kusisitizwa kuendelea na kazi zao kama kawaida.
Alifafanua kwamba hali kwa sasa kijijini hapo ni shwari na kwamba mifugo iliyouawa kwa kukatwakatwa mapanga yote imeshafukiwa na uongozi wa serikali ya wilaya umepanga kuingia mkataba na viongozi wa vijiji na kata ili kudhibiti, migororo baina ya makundi hayo.
Alisema katika kudhibiti matukio ya mapigano au uvunjifu wa sheria na mpango wa matumizi bora ya ardhi, Mvomero itaanza kuingia mkataba na watendaji wa vijiji na kata na iwapo migogoro itatokea, wao ndio watawajibishwa.
Awali Desemba 12, mwaka huu, kundi la wafugaji wa jamii ya Kibarbaig waliwavamia wakulima na kuanza kuwashambulia kutokana na mmoja wa wafugaji ambaye mifugo yake iliharibu mazao ya mkulima kutakiwa kulipa fidia ya Sh 200,000. Katika tukio hilo.
HABARILEO
Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri nchini wametakiwa kuhakikisha takataka zote zilizolundikwa wakati wa kazi ya usafi iliyofanyika Desemba 9, nchini kote zinaondolewa.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene wakati akizungumza na watumishi wa wizara hiyo mjini hapa, na kuagiza kuwa ifikapo Desemba 20, mwaka huu takataka zote zilizolundikwa ziwe zimeondolewa.
“Naagiza wakuu wa mkoa, wilaya na wakurugenzi kuwa ifikapo tarehe 20 mwezi huu takataka zote ziwe zimeondolewa katika maeneo yao,” alisema Simbachawene na kuongeza kuwa hategemei kusikia baada ya tarehe hiyo takataka kuwa bado zimelundikana kwenye maeneo mbalimbali.
Kumekuwapo na mlundikano wa takataka katika maeneo mbalimbali ya miji nchini na kuwa uchafu baada ya kazi ya usafi ya Desemba 9, nchini kote kutokana na agizo la Rais John Magufuli la kufuta sherehe za sikukuu ya Uhuru na badala yake siku hiyo itumiwe kufanya usafi katika maeneo mbalimbali nchini.
NIPASHE
Kwa mara ya saba sasa viongozi wakuu wa kitaifa wa Zanzibar, akiwamo mgombea urais wa CCM, Rais Dk. Ali Mohamed Shein na mgombea urais wa Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad, wamekutana bila taarifa zozote kwa umma kutolewa juu ya mazungumzo hayo tangu kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa visiwa hivyo uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Zikiwa zimetimia siku 47 sasa tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi huo, vikao hivyo vimekuwa vikifanyika huku umma ukiwa njia panda juu ya kinachozungumzwa kutokana na kugubikwa na usiri mkubwa.
Jana viongozi hao wakuu wa kitaifa walikutana kwa mara ya saba Ikulu mjini hapa, huku waandishi wa habari wakizuiwa kupata taarifa yoyote kuhusiana na mazungumzo ya kikao hicho.
Viongozi waliokutana jana ni Rais Dk. Ali Mohammed Shein, Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Balozi Seif Ali iddi, Makamu wa Pili wa Rais na marais wastaafu, Amani Abeid Karume na Ali Hassan Mwinyi, ambao walikutana kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana.
Alipoulizwa kuhusiana na mazungumzo hayo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai (hashiriki mazungumzo hayo), alisema chama chao hakijui chochote kinachozungumzwa katika vikao hivyo kwani havihusiana na chama.
“Vikao vinavyoendelea kufanyika Ikulu ambavyo vinawakutanisha viongozi wa kitaifa havihusiani na vyama na ndio maana hakuna mwakilishi wa CCM wala Cuf, isipokuwa viongozi wa serikali,” alisema Vuai.
Hata hivyo, licha ya kutopatikana kwa taarifa yoyote kuhusiana na mazungumzo hayo, hali ya amani na usalama visiwani hapa imezidi kuimarika, huku wananchi wakiendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii kama kawaida.
NIPASHE
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, amewaonya vikali mawakili wa serikali wanaokula njama za kuhujumu kesi mahakamani kwa kushirikiana na mawakili wa kujitegemea na kusababisha serikali kushindwa kesi na kuingia hasara za mabilioni ya fedha.
Masaju alisema ili kutenda haki kwa Watanzania, mawakili wa serikali wanatakiwa kutojihusisha na mchezo huo mchafu wala kushiriki kwa namna yoyote kesi za mawakili wa kujitegemea.
Alisema wakati mwingine mawakili wa serikali wanakula njama na wateja wao kuharibu kesi mahakamani au wakati mwingine wakili hao anashirikiana na mteja kuvujisha kesi mahakamani.
“Kuapishwa kwenu leo (jana) kusiwe ni sehemu ya uvunjifu wa sheria za mahakama, kwa sababu mtaungana na kundi jingine la maofisa wa mahakama kwa lengo la kupigania utawala wa haki uliothabiti katika sehemu zote,” alisema.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman, alisema mawakili hao wamefikisha idadi ya mawakili 5,176 nchini, lakini kati yao 55 wanakabiliwa na mashtaka ya nidhamu na kuwataka mawakili hao walioapishwa kufanya kazi kwa uadilifu, pamoja na kulinda siri za wateja.
Alisema kila mwaka serikali inawaapisha mawakili wapya 450 hadi 500, hali ambayo imesaidia kutatua changamoto ya uhaba wa mawakili katika mahakama mbalimbali nchini, pamoja na kupunguza mrundikano wa kesi ambazo zingeweza kusikilizwa kwa wakati.
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram na YouTUBE wa kubonyeza hapa >>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE.