Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ameutaka Uongozi wa Benki ya Biashara ya Mwalimu (MCB BANK) kuboresha huduma za kifedha ikiwemo kuweka vivutio na masharti rafiki ambayo yatawawezesha walimu nchini kukopa fedha ili kukuza vipato vyao.
Prof. Ndalichako ametoa wito huo wakati akifunga Kongamano la Walimu
wilayani Kasulu mkoani Kigoma na kusisitiza kuwa matarajio ya serikali ni kuona benki hiyo inakuwa rafiki kwa walimu nchini kwa kuondoa adha na vikwazo ambavyo kwa muda mrefu walimu wamekuwa wakikabiliana navyo katika taasisi mbalimbali za kifedha.
“Benki ya Biashara ya Mwalimu iwe na ahueni kwa mwalimu anapokuwa ni mteja katika kufanya hivyo walimu wengi watahamasika kujiunga na benki hii, kupitishia mishahara pamoja na hata kuchukua mikopo”
Aidha ameutaka Uongozi wa benki hiyo kusimamia vizuri fedha iliyokwisha wekezwa na walimu ili kuwavutia walimu wengine ambao bado hawajajiunga na kusisitiza kuwepo na kasi ya uanzishwaji wa ofisi za benki hiyo katika mikoa yote nchini iongezeke ili kuwavutia wateja.
“Nafahamu kwamba tayari mnatoa huduma kidijitali na mnashirikiana na Benki ya Posta kutoa huduma katika maeneo ambayo hamna ofisi, lakini ni muhimu mkaharakisha uanzishwaji wa ofisi zenu kila mkoa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma,” Ndalichako.
Waziri Ndalichako pia amewaasa walimu nchini kuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba pindi wanapopata mishahara yao ili iwasaidie kuanzisha miradi mingine ya kiuchumi ambayo itakuwa mkombozi wa maisha yao pindi wanapostaafu.
“Walimu tambueni akiba ni kile kitu unachokiweka kwanza kabla ya kuanza matumizi, lakini watu wengi wanadhani akiba ni bakaa baada ya matumizi kwa utaratibu huo kamwe hakutakuwa na kitu kinachobaki,” amesema Ndalichako.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Mwalimu, Richard Makungwa
amesema benki hiyo imeendelea kujiimarisha katika kusogeza huduma kwa wateja wake na kwamba tayari imeanzisha ofisi zake katika baadhi ya mikoa nchini ikiwemo Mbeya, Morogoro na Mwanza huku ikishirikiana na Benki ya Posta kutoa huduma kwa wateja ambao bado mikoa yao haijafikiwa.
Amesema katika benki hiyo mwalimu mmoja anamiliki hisa takribani asilimia 35.28 huku chama cha walimu na kampuni yao wakimiliki takribani asilimia 16.17.
“Ukiangalia utakubaliana nami kuwa chombo hiki ni cha walimu na madhumuni yake ni kuwaletea maendeleo wao wenyewe ndiyo maana tukasema lazima tuwafikia walimu popote walipo,” Mkurugenzi Makungwa
Naye Mkuu wa wilaya ya Kasulu, Kanali Simon Anange amesema mara nyingi watumishi wanakosa nidhamu ya fedha na kutumia zaidi ya kile anachopata na kusisitiza kuwa ni vizuri walimu wakawa na utaratibu wa kujiwekea akiba ili pindi wanapostaafu waweze kuishi maisha ambayo wameishi wakiwa kazini.
Naye mwalimu mstaafu aliyeshiriki kongamano hilo, Kalist Tarimo ameishukuru Benki ya Biashara ya Mwalimu kwa kufanya Kongamano hilo ili kutoa elimu kwao lakini pia ameishauri benki hiyo kuwa na ofisi katika kila Wilaya ili walimu waweze kutumia huduma za benki hiyo.
Kongamano hilo limeandaliwa na Benki ya Biashara ya Mwalimu na limeshirikisha walimu kutoka mkoa wa Kigoma.
FULL HD VIDEO: HARMONIZE ALIVYOMCHEZESHA MAGUFULI KWANGWARU, JAMAA ALIELETA FUJO