Serikali ya Tanzania imetangaza kuanza kusajili Mifugo yote inayofugwa Nchini Tanzania kwa njia ya kielektroniki kwa kuwavisha hereni maalum ili kufahamu idadi ya mifugo hiyo, kuzuia utoroshwaji wa mifugo hiyo kwenda nje ya Tanzania na kukabiliana na magonjwa ya milipuko.
Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za ukaguzi na ustawi wa Wanyama kutoka Wizara ya Mifugo na uvuvi Dr. Annette Kitambi amesema “Hii itatusaidia kufahamu idadi ya mifugo iliyopo kwenye maeneo yetu kwenye Halmashauri, Mkoa, Kata husika, Kijiji na hata Kitongoji, usajili huu utasaidia pia kukabiliana na magonjwa ya mlipuko”
“Usajili huu utapoanza utawezesha pia mifugo iliyopotea kupatikana na kudhibiti wizi, hereni hizi zina namba ya Nchi, namba ya Mkoa na namba ya Wilaya kwahiyo Mifugo tunategemea usiweze kutoka sehemu moja kwenda nyingine, palepale uliposajiliwa ndio hapo watatakiwa kuwepo kwa wakati wote, ile biashara ya kuhamahama sasa itakua ni mwisho”
“Usajili huu wa Wanyama kieletroniki bila shuruti utaendelea mpaka mwezi wa nane mwaka 2022 lakini baada ya hapo mfugo wowote ambao haujasajiliwa hautoruhusiwa kuonekana mnadani, machinjinioni na sehemu nyingine kama kwenye utolewaji wa mahari, ambao watakua hawajasajiliwa watashindwa kuuza mifugo yao” ——— Dr. Annette.