Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeunga mkono kazi za sanaa ambazo zinasimamiwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kutoa fulana 300 kwa washiriki wote wa Tamasha la World Happy Deaf Family Festival 2023.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa Sera ya Huduma kwa Jamii (CSR) ya Shirika hilo ambayo lengo lake ni kuhudumia jamii katika nyanja ya elimu, afya na makundi makundi maalum.
Akikabidhi fulana hizo Novemba 26, 2023 Jijini Dar es Salaam, Meneja wa Habari na Uhusiano wa Shirika hilo Bw. Muungano Saguya amesema kuwa wanaunga mkono juhudi za Serikali za kuitangaza Tanzania kupitia Tamasha la World Happy Deaf Family Festival 2023 ambalo limeshirikisha viziwi wa kiume na wa kike kutoka nchi mbalimbali duniani.
“Tunaamini fulana hizi zitasaidia kutangaza jina la Tanzania na Shirika letu la Nyumba la Taifa katika mataifa yenu mnapotoka ili zisaidie kuwavutia wawekezaji wakubwa watakaoshirikiana na Shirika letu ambao wanapenda kufanya uwekezaji mkubwa nchini Tanzania na muwe mabalozi wema wa nchi yetu huko mnapotoka” amesema Bw. Saguya
Bw. Saguya aliongeza kuwa Shirika la Nyumba la Taifa lina sera ya ubia ambayo inaruhusu sekta binafsi ya ndani na nje ya nchi kuwekeza katika ujenzi wa majengo makubwa katikati ya miji yetu kwa ajili ya makazi na biashara. Hivyo Bw. Saguya ambaye aliwapa washiriki hao sera yao ya ubia ili wakaitangaze katika mataifa yao na kuvutia uwekezaji katika sekta ya nyumba.
Katika mashindano hayo, Nashua Patience kutoka Uganda ameibuka mshindi wa kwanza na kutwaa taji la mrembo kwa mwaka 2023 huku nafasi ya mtanashati katika mashindano hayo ikinyakuliwa na Ariko David kutoka Uganda wakati Mtanzania Caroline Mwakasaka akiibuka mshindi wa nafasi ya pili kwa upande wa shindano la Mwanamitindo Bora “modal”.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt.Emmanuel Ishengoma amelishukuru Shirika la Nyumba la Taifa kwa kuunga mkono juhudi za Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha wanaitangaza Tanzania katika mataifa 40 kupitia tisheti 300 walizowapa washiriki hao.