Utawala wa kijeshi nchini humo iliondoa kinga ya kidiplomasia ya Sylvain Itté, wanabaini katika barua ya tarehe 29 Agosti iliyotumwa kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa (Quai d’Orsay). Lakini kwa sasa, Paris inakataa kujibu matakwa ya jeshi ya kufukuzwa kwa balozi wake.
Licha ya makataa ya saa 48 yaliyomalizika Jumatatu, balozi wa Ufaransa, aliyeteuliwa kwa wadhifa huu zaidi ya mwaka mmoja uliopita, bado yuko Niamey. Pia, kwa mujibu wa barua kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Niger iliyotumwa kwa serikali ya Paris, huduma za polisi tayari “zimeagizwa kuanzisha utaratimu wa kumtimua balozi wa Ufaransa nchini Niger”.
Barua iliyotumwa kwa Quai d’Orsay inaeleza kwamba kuondolewa kwa idhini ya balozi wa Ufaransa, hatua iliyotangazwa Ijumaa ya wiki iliyopita, “hakuwezi kubatilishwa na uchunguzi wowote juu ya suala.”
Katika hati ya ukurasa mmoja, inarifiwa kwamba “mhusika hana haki na kinga zinazohusiana na hadhi yake kama mwanadiplomasia”. Lakini pia kwamba visa vya balozi na watu wa familia yake zimefutwa. Hii inapelekea, kulingana na mamlaka ya Niger, kufukuzwa kwake kwani hana tena haki ya kukaa nchini Niger.
Kwa upande wa Ufaransa, mamlaka ilisisitiza tena Alhamisi hii kwa wenzetu wa France 24 kwamba “jeshi halina mamlaka ya kufanya ombi hili”, kwa kuwa idhini ya balozi inatoka tu kwa “mamlaka halali za Niger zilizochaguliwa”. Kwa upande wa Ufaransa, Sylvain Itté, ambaye kazi yake ilisifiwa Jumanne na Rais Macron, alikuwa bado yuko ofisini Alhamisi jioni.