Rais wa Niger Mohamed Bazoum, aliyepinduliwa katika mapinduzi Julai 26, anaingia siku yake ya 80 kizuizini akiwa na mkewe na mwanawe siku ya Ijumaa. Bado anakataa kujiuzulu na ana matumaini ya kushinda kesi yake mahakamani.
Wakati nchi nyingi na mashirika yanaendelea kutoa wito wa kuachiliwa kwake, serikali ya kijeshi inayotawala bado inashikilia kwa sasa.
– Takriban miezi mitatu kizuizini –
Tangu mapinduzi ya Julai 26, Mohamed Bazoum amekuwa mfungwa katika makazi yake katika ikulu ya rais, pamoja na mkewe Haziza na mwanawe Salem.
“Hali yake haijabadilika,” anasema wakili wake wa Senegal Mohamed Seydou Diagne.
Kulingana na wajumbe wa msafara wake waliohojiwa na AFP, bado “amezuiliwa bila umeme”, na anapata maji mara kwa mara.
“Anapokea chakula kibichi kila siku nyingine na kutembelewa mara kwa mara na daktari wake,” kinasema moja ya vyanzo hivi, ambacho kinaongeza kuwa anaendelea vizuri, kama vile mke na mwanawe.
“Ana nguvu kama zamani. Hatajiuzulu,” kinasisitiza chanzo kingine kilicho karibu naye.
Mapema Agosti, Mohamed Bazoum alijieleza kama “mateka” katika makala ya Washington Post, na alielezea jinsi familia yake inavyotendewa kama “kinyama na kikatili” kwa NGO ya Human Rights Watch.