Utawala wa kijeshi nchini Niger, umefuta zaidi ya vyeti vya usafiri 990 vinavyoshikiliwa na raia wa taifa hilo na wake wa kigeni wanaohusishwa na utawala ulioangushwa wa rais Bazoum.
Wizara ya mambo ya kigeni katika taarifa yake, imewaarifu wawakilishi wa kidiplomasia nchini Niger kwamba vyeti vyao vya usafiri vimefutwa kwa mujibu wa nakala zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii.
Hati hizo za kidiplomasia zilikuwa zinashikiliwa na viongozi wakuu wa zamani katika taasisi na wizara pamoja na wabunge wa zamani na washauri wakiwemo rais na waziri mkuu, shirika rasmi la habari la ANP lilisema Alhamisi.
Takriban hati 50 kati ya hizo zilikuwa zimetolewa kwa raia wa Marekani, Uingereza, Ufaransa, Libya na Uturuki pamoja na raia wengine wa Afrika.
Rais Mohamed Bazoum alipinduliwa Julai 26 na tangu wakati huo amezuiliwa katika makazi yake.
Mwishoni mwa mwezi Agosti, utawala huo mpya ulifuta hati za kusafiria zilizokuwa na wanachama kadhaa wa serikali waliokuwa nje ya nchi, akiwemo waziri mkuu, waziri wa mambo ya nje na balozi wa Niger nchini Ufaransa.