Utawala wa kijeshi nchini Niger umeidhinisha Mali na Burkina Faso kutuma wanajeshi wao kwenye ardhi ya Niger iwapo kutatokea shambulio, nchi hizo tatu zilitangaza katika taarifa ya pamoja siku ya Alhamisi, zikipendekeza kwamba viongozi wa mapinduzi wanakusudia kupinga shinikizo kutoka nje la kurejesha utawala wa kikatiba.
Tangazo hili linakuja wakati Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) ikitishia kuingilia kijeshi nchini Niger ili kurejesha utawala wa kikatiba baada ya jeshi kumpindua rais Mohamed aliyechaguliwa kidemokrasia mwishoni mwa mwezi Julai.
Nchi hizo zilikumbusha kuwa Mali na Burkina Faso zitachukulia uingiliaji wowote wa kijeshi nchini Niger kuwa tangazo la vita dhidi yao.
Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, ilijaribu kufanya mazungumzo na viongozi wa mapinduzi, lakini ikaonya kuwa iko tayari kutuma wanajeshi Niger kurejesha utawala wa kikatiba ikiwa juhudi za kidiplomasia zitashindwa.
Ongezeko lolote la uhasama au vita linahatarisha zaidi usalama katika eneo hilo linalokabiliwa na waasi kwani majirani wa Niger, Mali na Burkina Faso zinazotawaliwa na wanajeshi kupitia mapinduzi wamesema wataunga mkono Niger katika mzozo wowote na ECOWAS.
Siku ya Alhamisi, mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi hizo tatu washirika, walisema walikutana katika mji mkuu wa Niger, Niamey, kujadili kuimarishwa kwa ushirikiano wa kiusalama na masuala mengine yanayowahusu.