Viongozi wa mapinduzi ya kijeshi nchini Niger, wamesema wanataka kuafikiwa kwa makubaliano kati yake na Ufaransa kuhusu kuondoka kwa jeshi lake katika taifa hilo la Afrika Magharibi.
Utawala wa kijeshi, uliomuondoa madarakani rais aliyechaguliwa kwa njia ya demokrasia miezi miwili iliyopita kupitia taarifa yake, umesema suala ya kuwaondoa wanajeshi wa Ufaransa nchini humo lazima liafikiwe na pande zote
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Jumapili ya wiki iliyopita alitangaza kwamba nchi yake itamuondoa balozi wake nchini Niger, kisha hatua hiyo ifuatiwe na ile ya kuwaondoa wanajeshi wake jijini Niamey katika kipindi cha miezi ijayo.
Katika taarifa yake, rais Macron alisema ushirikiano wa kijeshi ulikuwa umekamilika na kwamba Paris itawaondoa wanajeshi wake nchini Niger katika kipindi cha miezi chache ijayo kabla ya kumaliza mchakato huo mwishoni mwa mwaka.
Ufaransa imekuwa na wanajeshi 1,500 nchini Niger ambayo walitumwa katika eneo hilo la Sahel kupambana na makundi ya kijihadi.
Wakuu wa kijeshi waliokaribisha tangazo hilo la rais Macron, walisema wanasubiri hatua kuchukuliwa na mamlaka ya Ufaransa.
Ufaransa imesisitiza kuwa haitambui utawala wa kijeshi nchini Niger na kwamba rais Mohamed Bazoum anastahili kuachiwa huru na kurejeshwa madarakani.