Serikali ya kijeshi nchini Niger, imelazimika kukata bajeti yake kwa asilimia 40 kufuatia athari zinazotokana na vikwazo vilivyotangazwa dhidi yake baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Julai tarehe 26.
Kuna hofu kwamba vikwazo hivyo vinaweza kuathiri pakubwa hali ya uchumi ya Niger, mojawapo ya mataifa maskini zaidi duniani.
Katika taarifa yake, utawala wa kijeshi umetangaza kupunguzwa kwa bajeti yake ya mwaka wa 2023 kutoka kwa Dola bilioni 5.3 hadi Dola bilioni 3.2, japokuwa maelezo zaidi kuhusu hatua hiyo hayajaekwa wazi.
Karibia asilimia 40 ya bajeti ya baadhi ya nchi za Afrika Magharibi inatarajiwa kutoka kwa wafadhili na washirika wa ndani.
Mapinduzi hayo yalioangusha utawala wa rais Mohamed Bazoum, yalikashifiwa vikali kutoka kwa mataifa ya ukanda na yale ya kigeni.
Licha ya mapinduzi hayo kukashifiwa, viongozi wa kijeshi wa Niger wameonekana kupata uungwaji mkono kutoka kwa nchi jirani kama vile Mali na Burkina Faso, ambayo nayo pia yameshuhudia mapinduzi ya kijeshi.