Nchi ya Niger imetangaziwa vikwazo zaidi baada ya viongozi wa mapinduzi nchini humo kukataa kukutana na ujumbe wa ECOWAS kwa mazungumzo ya kurejesha utawala wa kiraia.
Rais wa Nigeria ambaye pia ndiye mwenyekiti wa ECOWAS, ameagiza benki kuu ya ya nchi yake kufunga akaunti za benki za wote ambao wamehusika kwa mapinduzi nchini Niger.
Ni hatua inayokuja baada ya uongozi wa kijeshi nchini Niger kukataa kukutana na ujumbe wa ECOWAS na wale wa umoja wa mataifa ambao walilenga kufanya mazungumazo ya kumrejesha rais Mohamed Bazoum madarakani.
Baadaye leo wakuu wa mataifa ya ECOWAS wanatarajiwa kukutana kujadili hatua gani zitachukuliwa baada ya uongozi wa kijeshi kupuuza maktaa ya ecowas ya kurejesha utawala wa kiraia siku ya jumapili.
Tayari viongozi wa kijeshi wa Ecowas wamesema wako tayari kutumia nguvu iwapo wataangizwa kufanya hivyo.
Haya yanajiri wakati huu Marekani imesema inajaribu kuzuia kundi la wapiganaji mamluki wa Urusi, Wagner, kutumia mapinduzi ya nchini Niger kujipenyeza zaidi kwenye ukanda huo, licha ya juhudi zake za juma hili kugonga ukuta.