Viongozi wa kijeshi nchini Niger, wanasubiri hatua ya Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Magharibi ECOWAS, baada ya kukataa kutii agizo la kurejesha madaraka kwa rais Mohammed Bazoum, kufikia hapo jana.
Vikosi vya kigeni kutoka Jumuiya ya ECOWAS, havijaonekana jijini Niamey, wakati huu viongozi wa Jumuiya hiyo wakisalia kimya, baada ya agizo lao kukaidiwa.
Ripoti zinasema kuwa wakuu wa nchi kutoka ukanda huo wa ECOWAS watakutana tena jijini Abuja siku ya Alhamisi.
Aidha, taarifa kutoka Jumuiya hiyo zinasema kwa sasa, hakuna mpango wa kutuma jeshi nchini Niger, mara moja kumrejesha rais Bazoum madarakani.
Wakati hayo yakijri, Mataifa ya Ulaya ya Italia na Ujerumani, yametoa wito wa kupatikana kwa suluhu kwa njia ya mazungumzo, zikiomba jeshi la Niger kupewa muda zaidi.
Katika hatua nyingine, Mali na Burkina Faso ambazo zimesema zitasimama na Niger, iwapo itashambuliwa kijeshi, zimesema zinatuma ujumbe jijini Niamey, kuonesha kuwa zinasimama na watu wa Niger.
Ufaransa ambayo ina wanajeshi wake 1,500 nchini Niger na inayounga mkono mpango wa ECOWAS, wiki iliyopita, iliwaondoa raia wake nchini humo.