Idara ya taifa ya kuratibu dawa ya Nigeria Jumatatu imeidhinisha chanjo ya Malaria iliyotengezwa na chuo kikuu cha Oxford, ikiwa nchi ya pili kuchukua hatua hiyo baada ya Ghana iliyofanya hivyo wiki iliyopita ambapo Idara hiyo ya Nigeria inayosimamia ubora wa chakula na dawa, maarufu NAFDAC, imesema kwamba chanjo hiyo ya R21 ya Malaria itatumika kwa kufuata maagizo ya shirika la afya duniani WHO.
Hata hivyo hatua hiyo inasemekana kuwa isiyo ya kawaida kutokana na kuwa imetangazwa kabla ya kumalizika kwa awamu ya mwisho ya majaribio ya chanjo hiyo.
Ugonjwa wa Malaria unaosababishwa na mbu huuwa zaidi ya watu 600,000 kila mwaka, wengi wao wakiwa ni watoto wachang na wadogo barani Afrika. Nigeria ambayo ina idadi kubwa sana ya watu barani humo ndiyo iliyoathiriwa zaidi na Malaria, ikiwa na asilimia 27 za maambukizi na asilimia 32 ya vifo kutokana na Malaria ulimwenguni, kwa mujibu wa ripoti ya WHO ya 2021.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kitaifa wa Usimamizi na Udhibiti wa Chakula na Dawa Mojisola Adeyeye wakati wa mkutano na waandishi wa habari hii leo alisema “uidhinishaji wa chanjo ya Malaria ya R21 umewasilishwa kwa waziri wa afya na wakala wa taifa wa maendeleo ya afya ya msingi kwa ajili ya hatua zinazofaa za chanjo kwa watu husika.”
“Chanjo imeonyeshwa kwa ajili ya kuzuia malaria ya kimatibabu kwa watoto wenye umri wa kuanzia miezi mitano hadi miezi 36 na joto la uhifadhi wa chanjo hiyo ni 2-8 °C.”