Polisi wa Jimbo la Kano, Nigeria wamefanikiwa kukamata kundi la watu waliobobea katika kuwateka nyara watoto na kuwasafirisha hadi majimbo mengine kusini mwa nchi hiyo.
Katika mahojiano na BBC, msemaji wa Polisi, SP Abdullahi Kiyawa alisema polisi wamefanikiwa kuwakamata wanachama kadhaa wa kundi hilo, ambao wanafanya vitendo vya uhalifu katika majimbo ya Kano, Bauchi, Anambra, Imo na Lagos.
Anasema tarehe 15 Disemba, 2023, mwanamke mmoja aitwaye Comfort Amos, mwenye umri wa miaka 45, alikamatwa katika kituo cha basi cha Mariri huko Kano alipokuwa akijaribu kumsafirisha mvulana, Abdulmutallib Sa’ad, mwenye umri wa miaka mitano kwenda Lagos.
Iligunduliwa kuwa Abdulmutallib alitekwa nyara Desemba 12, 2023, huko Quarters Zango katika Jimbo la Bauchi.
Uchunguzi ulipelekea kukamatwa kwa watu wengine wengi akiwemo Chika Ezugbu, Joy Nzelu, Clement Ali na Emeka Ekeidigwe, wote wakazi wa Kano, ambao wanashukiwa kuhusika na shughuli za kikundi hicho.
“Hivi sasa tumekamata watu tisa, na watoto saba walikutwa mikononi mwa watu hao ambao umri wao ni kati ya miaka mitatu hadi minane,” amesema Kiyawa.
Ameeleza kuwa wazazi wa wengi wa watoto waliookolewa wametambuliwa na kwa sasa wako katika afya njema.