Vyombo vya usalama vya Nigeria vimemzuilia mkuu wa benki kuu aliyesimamishwa kazi kama sehemu ya uchunguzi kuhusu ofisi yake, shirika la usalama la ndani la taifa lilisema.
Kukamatwa kwa gavana wa Benki Kuu ya Nigeria Godwin Emefiele kulikuja muda mfupi baada ya serikali ya Rais mpya Bola Ahmed Tinubu kumsimamisha kazi kufuatia takriban muongo mmoja katika wadhifa huo.
Tinubu, ambaye aliingia madarakani mwishoni mwa mwezi uliopita kufuatia uchaguzi wa rais wa Februari uliokuwa na ushindani mkubwa, alikuwa ameahidi mageuzi kusaidia uchumi mkubwa zaidi barani Afrika kutoka katika matatizo ya kifedha.
“Idara ya Huduma za Serikali (DSS) inathibitisha kwamba Bw Godwin Emefiele, Gavana aliyesimamishwa kazi wa Benki Kuu ya Nigeria (CBN) sasa yuko chini ya ulinzi wake kwa sababu za uchunguzi,” wakala wa usalama wa ndani wa DSS ulisema katika taarifa.
DSS haikutoa maelezo zaidi, lakini mmoja wa wasemaji wa serikali ya Tinubu alisema hapo awali kwamba Emefiele alisimamishwa kazi mara moja kama sehemu ya “uchunguzi unaoendelea wa ofisi yake na mageuzi yaliyopangwa katika sekta ya fedha”.
Naibu gavana wa benki hiyo ataingia katika jukumu la mkurugenzi akisubiri kukamilika kwa uchunguzi, ilisema taarifa hiyo.
Benki kuu haikujibu mara moja simu za kutaka maoni.
Emefiele alikuwa akishutumiwa hivi majuzi, ikiwa ni pamoja na kuhusu sera ya rais wa zamani Muhammadu Buhari ya kubadilisha noti za zamani za naira na kuweka mpya ili kuzuia rushwa wakati wa uchaguzi wa mwaka huu na kupunguza malipo ya fidia baada ya utekaji nyara.
Sera hiyo ilisababisha uhaba mkubwa wa pesa taslimu naira kote nchini Nigeria, nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika, ambapo watu wengi wanategemea malipo ya fedha katika uchumi usio rasmi ili kuishi.
Emefiele pia alikuwa amejaribu kuchuana na Tinubu katika mchujo wa chama tawala cha All Progressives Congress au APC ili kuwa mgombea wa chama katika kiti cha urais. Hatimaye akajiweka kando.