Watu 10 wameuawa kufuatia milipuko ya mabomu ya kutegwa ardhini iliyowalenga wasafiri kwenye barabara kuu kaskazini-mashariki mwa jimbo la Borno nchini Nigeria.
Matukio hayo yalishuhudiwa jana katika kijiji cha Kunibaa nje ya mji wa Gamboru. Barabara kuu ya Gamboru hadi Maiduguri yenye urefu wa kilometa 140, ni njia ya kimkakati kwa mahusiano ya biashara kati ya Nigeria na Cameroon.
Barabara hiyo ilifunguliwa tena Julai mwaka 2016 baada ya kufungwa na jeshi kwa miaka miwili kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya wanajihadi ambayo tangu mwaka 2009 tayari yamesababisha vifo vya watu 40,000.
Magaidi wa kundi la Boko Haram wakishirikiana na wengine kutoka kundi lenye mafungamano na kundi linalojiita Dola la Kiislam IS walifurushwa katika maeneo hayo waliyokuwa wakiyadhibiti hapo awali katika mzozo uliodumu kwa miaka 14,lakini bado wamekuwa wakiendesha mashambulizi ya kuvizia.