Takriban watu sita wamethibitishwa kufariki baada ya jengo moja kuporomoka kusini mashariki mwa Nigeria siku ya Jumatatu.
Jengo la maduka linaloendelea kujengwa katika jimbo la Anambra kusini mashariki mwa Nigeria liliporomoka Jumatatu, na kuua takriban watu sita, huku wengine wakihofiwa kukwama kwenye vifusi, shirika la dharura lilisema.
Jengo hilo, lenye maduka zaidi ya 120, liliporomoka katika jiji la Onitsha, Shirika la Kitaifa la Kudhibiti Dharura (NEMA) lilisema Jumanne.
“Baadhi ya watu waliookolewa wamepelekwa katika hospitali tofauti za Onitsha kwa matibabu,” NEMA ilisema.
Msako unaendelea kuwatafuta manusura wengine, ilisema.
Kuporomoka kwa majengo ni mara kwa mara katika nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika na mzalishaji mkuu wa mafuta kwa sababu ya ulegevu wa kanuni na vifaa vya ujenzi ambavyo havina viwango.