Nigeria inadhamiria kutuma maombi ya kuwa mwanachama wa jumuiya ya G20 ya mataifa yenye uchumi mkubwa zaidi duniani, baada ya kuhitimisha mashauriano kuhusu athari na manufaa ya hatua kama hiyo, msemaji wa rais alisema Jumapili.
Rais Bola Tinubu ataondoka Jumatatu kuhudhuria mkutano wa G20 nchini India kwa mwaliko wa Waziri Mkuu Narendra Modi, msemaji Ajuri Ngelale alisema.
Afrika Kusini ni nchi pekee mwanachama wa kundi hilo la mataifa 20 yaliyoendelea zaidi kiviwanda duniani.
“Wakati uanachama wa Nigeria wa G-20 unastahili, serikali imeanza mashauriano mapana kwa nia ya kujua faida na athari za uanachama,” Ngelale alisema katika taarifa yake.
Mpango wa Tinubu wa kuhudhuria mkutano huo ni sehemu ya mwendelezo wa malengo ya uanachama wa Nigeria, alisema.
Ijumaa, Ngelale alisema Tinubu atahudhuria mkutano wa kilele wa G20 ili kujaribu kukuza uwekezaji wa kigeni nchini Nigeria na kuhamasisha mtaji wa kimataifa kuendeleza miundombinu.