Shirika la dharura la Nigeria linasema kuwa limeimarisha ulinzi katika maghala yake baada ya mamia ya watu kupora duka la chakula katika mji mkuu mwishoni mwa juma.
Uvamizi huo kwenye viunga vya Abuja unaashiria machafuko ya hivi punde ya kijamii kuhusu kupanda kwa bei na uchumi unaodorora wa nchi hiyo baada ya maelfu ya waandamanaji kujiunga na maandamano ya vyama vya wafanyakazi wiki iliyopita.
Vituo vya habari vya Nigeria na picha za mitandao ya kijamii zilionyesha mamia ya watu wakivamia ghala katika eneo la Gwagwa siku ya Jumapili, wakibeba magunia ya nafaka kwa miguu na kwa pikipiki.
Shirika la Kitaifa la Usimamizi wa Dharura lilisema halimiliki ghala hilo, lakini lilitangaza “itaimarisha usalama ndani na karibu na ofisi na maghala ya shirika hilo kote nchini” kama tahadhari.