Aliyekuwa balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley atasitisha kampeni yake ya urais siku ya Jumatano, kwa mujibu wa chanzo kinachofahamu mipango yake, kuhakikisha kwamba Donald Trump atashinda uteuzi wa chama cha Republican na kwa mara nyingine atakabiliana na Rais wa Democratic Joe Biden katika uchaguzi wa Novemba.
Haley atatoa hotuba kuzungumzia mustakabali wake katika kinyang’anyiro hicho, chanzo kilisema, lakini hatatoa ridhaa wakati huo.
Atamtaka Trump kujaribu kupata uungwaji mkono wa wafuasi wake, ambao ni pamoja na idadi kubwa ya Warepublican wenye msimamo wa wastani na wapiga kura huru, chanzo hicho kiliongeza.
Uamuzi wa Haley wa kusimamisha kampeni yake unakuja siku moja baada ya Super Tuesday, wakati Trump alimshinda vikali katika mashindano 14 kati ya 15 ya uteuzi wa Republican.
Haley alidumu kwa muda mrefu kuliko mpinzani mwingine yeyote wa chama cha Republican dhidi ya Trump lakini hakuwahi kuwa tishio kubwa kwa rais huyo wa zamani, ambaye ushikiliaji wake wa msingi wa chama unabakia kuwa thabiti licha ya mashtaka yake mengi ya jinai.